Kujikabidhi kwa Bwana
Anza mchakato sasa wa “kujikabidhi kwa Bwana” kwamba Roho Wake awe nawe kwa wingi.
Habari za asubuhi, akina kaka na akina dada. Kama mfuasi wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo, nimekuwa nikitazamia kukusanyika takribani kutoka kona zote za ulimwengu kwa ajili ya mkutano huu.
Huu umekuwa mwaka usio wa kawaida kwa kiasi kikubwa. Kwangu mimi ulianza kwa jukumu kutoka Urais wa Kwanza la kuweka wakfu hekalu takatifu kwa Bwana huko Durban, Afrika Kusini. Kamwe sitasahau utukufu wa jengo. Lakini zaidi ya mazingira, daima nitathamini utu wa watu ambao walijiandaa vyema kuingia kwenye jengo lile takatifu. Walikuja wakiwa tayari kupokea moja ya taji la baraka za Urejesho; uwekaji wakfu wa nyumba ya Bwana. Walikuja wakiwa na mioyo iliyojaa upendo Kwake na kwa Upatanisho Wake. Walikuja wakiwa wamejawa shukrani kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa kutupatia ibada takatifu ambazo zingeongoza kwenye kuinuliwa. Walikuja wakiwa wenye kustahili.
Mahekalu, bila kujali popote yalipo, yanainuka juu ya njia za ulimwengu. Kila hekalu la Siku za Mwisho ni ulimwengu—yote 168—yanasimama kama ushuhuda kwenye imani yetu katika uzima wa milele na shangwe ya kuuishi pamoja na familia zetu na Baba yetu wa Mbinguni. Kuhudhuria hekaluni kunazidisha uelewa wetu wa Uungu na injili ya milele, msimamo wetu wa kuishi na kufundisha ukweli, na utayari wetu wa kufuata mfano wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Nje ya kila hekalu la Kanisa kuna maneno yaliyokaa vyema, “Utakatifu kwa Bwana.” Hekalu ni nyumba ya Bwana na kimbilio kutoka kwenye ulimwengu. Roho Wake huwafunika wale ambao wanaabudu ndani ya kuta hizo takatifu. Yeye huweka viwango ambavyo kwavyo tunaingia kama wageni Wake.
Baba mkwe wangu, Blaine Twitchell, mmoja kati ya watu wema ambao nimewahi kuwajua, alinifunza somo kuu. Mimi na dada Rasband tulikwenda kumtembelea wakati alipokuwa amekaribia mwisho wa safari yake ya maisha ya duniani. Tulipoingia chumbani kwake, askofu wake alikuwa akiondoka. Tuliposalimiana na askofu, niliwaza, “askofu mwema sana. Yuko hapa kufanya uhudumiaji wake kwa muumini mwaminifu wa kata yake.”
Nilimwambia Blaine, “Je, si ya kupendeza sana kwa askofu kuja kutembelea.”
Blaine alinitazama na kujibu, “Ilikuwa ni zaidi ya hilo. Nilimwomba askofu aje kwa sababu nilitaka mahojiano yangu ya kibali cha hekaluni. Ninataka kufa nikiwa nimejikabidhi kwa Bwana.” Na yeye alikuja!
Kirai hicho, “kujikabidhi kwa Bwana,” kimebaki nami. Kimeweka mtazamo mpya kabisa juu ya kufanyiwa mahojiano mara kwa mara na viongozi wetu wa Kanisa. Kibali cha hekaluni ni muhimu sana kiasi kwamba katika Kanisa la mwanzo, mpaka 1891, kila kibali cha hekaluni kilikuwa kikiidhinishwa na Rais wa Kanisa. 1
Iwe ni kwa vijana au watu wazima, mahojiano yako ya kibali cha hekaluni si kuhusu mambo ya kufanya na kutokufanya. Kibali si orodha ya kuweka vema, ruhusa ya kuvunja sheria, au tiketi ya kikalio maalum. Kina lengo la juu zaidi na takatifu zaidi. Ili kustahili heshima ya kibali cha hekaluni, lazima uishi sawasawa na mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Katika mahojiano yako unayo nafasi ya kuichunguza nafsi yako kuhusu imani yako binafsi katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Unapata baraka ya kuelezea ushuhuda wako wa injili iliyorejeshwa, utayari wako wa kuwaidhinisha wale ambao Bwana amewaita kuongoza Kanisa Lake, utimizaji wako wa majukumu ya familia, viwango vyako vya uaminifu, usafi wa kimwili, usahihi, utiifu, kushika Neno la Hekima, sheria ya zaka, na utakatifu wa siku ya Sabato. Hizo ni kanuni za msingi za maisha yaliyotolewa kwa Yesu Kristo na kazi Yake.
Kibali chako cha hekaluni kinaakisi kusudi la dhati, la kiroho kwamba unajitahidi kuishi sheria za Bwana na kupenda kile Anachopenda: unyenyekevu, upole, uthabiti, hisani, ujasiri, huruma, msamaha, na utiifu. Na unakubali kuwajibika kwa viwango hivyo wakati unapoweka sahihi yako kwenye nyaraka hiyo takatifu.
Kibali chako cha hekaluni hufungua milango ya mbinguni kwako na kwa wengine kwa haki na ibada za umuhimu wa milele ikiwa ni pamoja na ubatizo, endaumenti, ndoa, na kuunganishwa.
“Kujikabidhi kwa Bwana” ni kukumbushwa juu ya kile kinachotarajiwa kwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho anayetunza maagano. Baba mkwe wangu, Blaine, aliliona kama matayarisho muhimu kwa ajili ya siku ambayo kwa unyenyekevu angesimama mbele za Bwana.
Fikiria wakati Musa alipopanda Mlima Horebu na Bwana Yehova akamtokea katika kichaka kilichokuwa kinaungua. Mungu alimwambia, “Vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni ardhi takatifu.” 2
Kuvua viatu vyetu kwenye mlango wa hekalu humaanisha kuacha matamanio ya ulimwengu au starehe ambazo zinatuvuruga kutoka kwenye ukuaji wa kiroho, kuweka kando mambo yale ambayo yanavuruga maisha yetu ya duniani yenye thamani, kuinuka juu ya tabia ya mabishano, na kutafuta muda wa kuwa mtakatifu.
Kwa mpango mtakatifu, mwili wetu ni uumbaji wa Mungu, hekalu kwa ajili ya roho yako, na unapaswa kutendewa kwa heshima. Kama yalivyo ya kweli maneno ya wimbo wa Msingi, “Mwili wangu ni hekalu ambalo linahitaji uangalizi mkubwa.” 3 Wakati Bwana alipowatokea Wanefi, Yeye aliwaamuru, “Muweze kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu, ili msimame mbele yangu bila mawaa.” 4 “Mnapaswa kuwa watu wa aina gani?”5 Bwana aliuliza na kisha akajibu, “Hata vile nilivyo.” 5 “Tukijikabidhi kwa Bwana,” tunajitahidi kuwa kama Yeye.
Ninakumbuka kumsikia Rais Howard W. Hunter katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa 14 wa Kanisa. Alisema: Ni shauku ya ndani kabisa ya moyo wangu kuwa na kila muumini wa Kanisa anayestahili kuingia hekaluni. Itamfurahisha Bwana kama kila mshiriki mtu mzima atastahili—na kubeba—kibali chake cha sasa cha hekaluni.” 6 Ningeongeza kwamba kibali chenye ukomo wa matumizi kitafungua njia kwa ajili ya vijana wetu wa thamani.
Rais Nelson alikumbuka maneno ya Rais Hunter, “Siku ile, Juni sita, Elfu moja Mia Tisa Tisini na Nne, kibali cha hekaluni ambacho tunabeba kilikuwa kitu tofauti kwenye pochi yangu. Kabla ya hilo, kilikuwa ni jambo tu la kuleta matokeo. Kilikuwa ni njia ya kuniruhusu kuingia nyumba takatifu ya Bwana; lakini baada ya kutoa tangazo lile, hilo lenyewe likawa matokeo. Kikawa beji yangu ya utiifu kwa nabii wa Mungu.” 7
Ikiwa bado hujapokea kibali au ikiwa kibali chako kimeisha muda wa matumizi, panga mstari kwenye mlango wa askofu kama vile Watakatifu wa mwanzo walivyopanga mstari kwenye mlango wa Hekalu la Nauvoo mnamo 1845 na 1846. 8 Mababu zangu walikuwa kati ya waaminifu hao. Walikuwa wakiacha mji wao mzuri na kuelekea magharibi, lakini walijua kwamba kulikuwa na uzoefu mtakatifu ukiwasubiri ndani ya hekalu. Aliandika Sarah Rich kutoka kwenye njia zenye mawemawe huko lowa, “Kama isingekuwa imani na maarifa ambayo tulipata katika hekalu lile …, safari yetu ingekuwa kama … kuruka gizani.” 9 Hicho ndicho tunachokosa ikiwa tunasafiri katika maisha haya peke yetu bila uvuvio na amani iliyoahidiwa hekaluni.
Anza mchakato sasa wa “kujikabidhi kwa Bwana” kwamba Roho Wake awe nawe kwa wingi na viwango vyake vitakuletea “amani ya dhamira.” 10
Viongozi wako wa vijana, rais wako wa akidi, rais wako wa Muungano wa Usaidizi, na kaka zako na dada zako wahudumiaji watakusaidia kujiandaa, na askofu au rais wako wa tawi kwa upendo watakuongoza.
Tumepitia wakati ambapo mahekalu yamefungwa au kuwekewa ukomo katika matumizi. Kwa Rais Nelson na wale kati yetu wanaotumikia pamoja naye, uamuzi wenye uvuvio wa kufunga mahekalu ulikuwa wa “kuumiza” na “uliojaa wasiwasi.” Rais Nelson alijikuta akiuliza, “Ningesema nini kwa Nabii Joseph Smith? Ningesema nini kwa Brigham Young, Wilford Woodruff, na marais wengine mpaka kwa Rais Thomas S. Monson?” 11
Sasa, taratibu na kwa shukrani tunafungua tena mahekalu kwa ajili ya kuunganishwa na endaumenti kwa kiwango chenye ukomo.
Kuwa wenye kustahili kuhudhuria hekaluni, hata hivyo, hakujasimamishwa. Acha nisisitize, iwe unaweza kufika hekaluni au la, unahitaji kibali cha sasa cha hekaluni ili kubaki imara kwenye njia ya agano.
Mwishoni mwa mwaka uliopita mimi na Dada Rasband tulikuwa kwenye jukumu huko New Zealand tukizungumza na kundi kubwa la vijana wakubwa waseja. Hawakuweza kufikia hekalu kirahisi; lile lililokuwa Hamilton lilikuwa likifanyiwa ukarabati, na walikuwa bado wakingojea uvunjaji wa ardhi kwa ajili ya hekalu huko Auckland. Hata hivyo, nilihisi msukumo wa kuwahimiza kufanya upya au kupokea vibali vya hekaluni.
Japokuwa hawangeweza kuvionyesha hekaluni, wangeweza kujionyesha wao wenyewe mbele za Bwana wakiwa safi na waliojiandaa kumtumikia Yeye. Kuwa mwenye kustahili kuwa na kibali cha hekaluni ni ulinzi kutokana na adui, kwa sababu umeweka msimamo imara kwa Bwana kuhusu maisha yako, na ahadi kwamba Roho atakuwa pamoja nawe.
Tunafanya kazi ya hekalu wakati tunapowatafuta mababu zetu na kuwasilisha majina yao kwa ajili ya ibada. Wakati mahekalu yetu yamefungwa, bado tumeweza kutafiti familia zetu. Tukiwa na Roho wa Mungu katika mioyo yetu, sisi, kwa uwakilishi, tunasimama kwa niaba yao “tunajikabidhi kwa Bwana.”
Nilipokuwa nikitumikia kama Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Hekalu, mara kwa mara nilimsikia Rais Gordon B. Hinckley akirejelea andiko hili lililozungumzwa na Bwana kuhusu Hekalu la Nauvoo: “Acha kazi ya hekalu langu, na kazi zote ambazo nimewapangia, ziendelezwe na zisisimame; na jitihada zenu, na uvumilivu wenu, na ustahimilivu, na kazi zenu zizidishwe mara mbili, nanyi kwa vyovyote vile hamtakosa ujira wenu, asema Bwana wa Majeshi.” 12
Kazi yetu ndani ya hekalu imefungwa kwenye ujira wa milele. Hivi karibuni tumewekwa kwenye jaribu. Bwana ametuita kufanya kazi katika mahekalu kwa “jitihada … uvumilivu na ustahimilivu.” 13 “Kujikabidhi kwa Bwana” kunahitaji sifa hizo. Lazima tuwe na jitihada katika kuishi amri, uvumilivu katika umakini wetu kwenye maagano yetu ya hekaluni, na kuwa wenye shukrani kwa kile Bwana anachoendelea kufundisha kuhusu maagano hayo, na kuwa wastahimilivu wakati tunapongojea mahekalu yafunguliwe kwa ukamilifu.
Wakati Bwana anapotuhitaji “tuzidishe mara mbili” jitihada zetu, Anatuomba kwamba tuongezeke katika uadilifu. Kwa mfano, tunaweza kuongeza usomaji wetu wa maandiko, utafiti wetu wa historia ya familia, na sala zetu za imani kwamba tuweze kushiriki upendo wetu kwa ajili ya nyumba ya Bwana pamoja na wale wanaojiandaa kupokea kibali cha hekaluni, familia zetu hasa.
Ninakuahidi kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo kwamba unapozidisha mara mbili jitihada zako za haki, utahisi kufanywa upya katika kujizatiti kwako kwa Mungu Baba na Yesu Kristo, utamhisi Roho Mtakatifu kwa kiasi kikubwa akikuongoza, utakuwa mwenye shukrani kwa maagano yako matakatifu, na utahisi amani ukijua kuwa wewe “umejikabidhi kwa Bwana.” Katika Jina la Yesu Kristo, amina.