Mkutano Mkuu
Tutawajaribu Kwa Njia Hii
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


15:19

Tutawajaribu Kwa Njia Hii

(Ibrahimu 3:25)

Sasa ni wakati wa kujitayarisha na kujithibitisha wenyewe kwamba tuko tayari na tunaweza kufanya mambo yote Bwana Mungu wetu atakayotuamuru.

Ninaomba msaada wa Roho Mtakatifu kwa ajili yetu sote wakati ninaposhiriki nanyi mawazo na hisia ambazo zimenijia akilini na moyoni mwangu katika maandalizi ya mkutano huu mkuu.

Umuhimu wa Majaribio

Kwa zaidi ya miongo miwili kabla ya wito wangu wa huduma ya kudumu katika Kanisa, nilifanya kazi kama mwalimu na mtawala katika Chuo Kikuu. Wajibu wangu wa msingi kama mwalimu ulikuwa kuwasaidia wanafunzi kujifunza jinsi ya kujifunza wao wenyewe. Na elementi muhimu ya kazi yangu ilikuwa kutengeneza, kupanga madaraja, na kutoa mrejesho kuhusu ufanisi wa wanafunzi katika majaribio. Kama ambavyo tayari mnaweza kuwa mnajua kutokana na uzoefu binafsi, majaribio kwa asili siyo sehemu ya mchakato wa kujifunza ambao wanafunzi wanaupenda sana!

Lakini majaribio ya mara kwa mara bila shaka ni muhimu katika kujifunza. Jaribio la kufaa linatusaidia sisi kulinganisha kile tunachohitaji kujua na kile tunachojua kuhusu somo husika; pia linatoa kipimo ambacho kupitia hicho tunaweza kutathmini kujifunza kwetu na maendeleo yetu.

Vile vile, majaribio katika shule ya maisha ya duniani ni elementi ya muhimu sana ya maendeleo yetu ya milele. La kushangaza, hata hivyo, neno jaribio halipatikani hata mara moja katika maandiko ya Vitabu Vitakatifu vya Kanisa vya Kiingereza. Badala yake, maneno kama vile thibitisha, pima, na jaribu yanatumika kuelezea mipangilio mbalimbali ya kuonyesha kwa usahihi maarifa yetu ya kiroho kuhusu, uelewa wa, na kujitoa kwetu katika mpango wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni na uwezo wetu wa kutafuta baraka za Upatanisho wa Mwokozi.

Yeye aliyeanzisha mpango wa wokovu alielezea lengo hasa la maisha yetu ya hapa duniani kwa kutumia maneno thibitisha, pima, na jaribu katika maandiko ya kale na ya sasa. “Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru.” 1

Zingatia kusihi huku kwa Daudi Mtunga zaburi:

Unipime mimi, Ee Bwana, na unijaribu mimi; unisafishe mtima wangu na moyo wangu.

“Maana fadhili zako zi mbele ya macho yangu: nami nimekwenda katika kweli yako.” 2

Na Bwana akatamka mnamo 1833, “Kwa hiyo, msiwaogope maadui zenu, kwani nimeazimia moyoni mwangu, asema Bwana, kwamba nitawajaribu ninyi katika mambo yote, ikiwa mtakaa katika agano langu, hata mpaka kifo, ili muweze kuwa wenye kustahili.” 3

Kuthibitisha na Kujaribiwa kwa Hivi Leo

Mwaka 2020 umewekwa alama, kwa sehemu, na janga la ulimwengu ambalo limetujaribu, na kutupima katika njia nyingi. Ninaomba kwamba sisi kama watu binafsi na kama familia tunajifunza masomo ya thamani ambayo yanaweza kufundishwa na nyakati zenye changamoto pekee. Pia ninatumaini kwamba sisi sote tutatambua kwa ukamilifu zaidi “ukuu wa Mungu” na ukweli kwamba “Yeye atayatakasa mateso [yetu] kwa faida [yetu].” 4

Kanuni mbili za msingi zinaweza kutuongoza na kutuimarisha sisi tunapokabiliwa na hali za kuthibitisha na kujaribu katika maisha yetu, vyovyote zinavyoweza kuwa: (1) kanuni ya matayarisho na (2) kanuni ya kusonga mbele kwa uthabiti katika Kristo.

Kuthibitisha na Matayarisho

Kama wafuasi wa Mwokozi, tumeamriwa “kutayarisha kila kitu kinachohitajika; na kuijenga nyumba, hata nyumba ya sala, nyumba ya kufunga, nyumba ya imani, nyumba ya kujifunza, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu.” 5

Pia tumeahidiwa kwamba “kama mmejitayarisha hamtaogopa.”

“Na hivyo muweze kuiepuka nguvu ya adui, na kukusanyika kwangu watu wenye haki, pasipo mawaa na aibu.” 6

Maandiko haya yanatoa mpangilio mkamilifu kwa ajili ya kupangilia na kutayarisha maisha yetu na nyumba zetu kimwili na kiroho. Juhudi zetu za kujitayarisha kwa ajili ya uzoefu wa kuthibitisha wa maisha zinapaswa kufuata mfano wa Mwokozi, ambaye kwa kiasi kikubwa “aliongezeka katika hekima na kimo, na kumpendeza Mungu na wanadamu” 7 —usawa uliowekwa pamoja wa utayari wa kiakili, kimwili, kiroho na kijamii.

Mnamo majira ya mchana miezi michahce iliyopita, mimi na Susan tuliweka kumbukumbu ya akiba yetu ya chakula na vifaa vya dharura. Wakati huo, COVID-19 ilikuwa ikisambaa kwa kasi, na mfululizo wa matetemeko ulikuwa umetikisa nyumba yetu huko Utah. Tumefanya kazi tangu siku za mwanzo za ndoa yetu kufuata ushauri wa kinabii kuhusu kujitayarisha kwa ajili ya changamoto zisizoonekana, hivyo “kutathmini” hali yetu ya utayari katikati ya kirusi na matetemeko ilionekana kama jambo zuri na muafaka kufanya. Tulitaka kupata viwango vyetu kwenye majaribio haya yaliyokuja bila taarifa.

Tulijifunza kwa kiasi kikubwa. Katika maeneo mengi, kazi yetu ya kujitayarisha ilikuwa sahihi. Katika baadhi ya maeneo, hata hivyo, maboresho yalikuwa lazima kwa sababu hatukutambua na kushughulikia mahitaji fulani kwa wakati unaofaa.

Pia tulicheka sana. Tuligundua, kwa mfano, vitu katika sehemu ya nyuma ya chumba ambavyo vimekuwa kwenye akiba yetu ya chakula kwa miongo mingi. Kusema kweli, tuliogopa kufungua na kukagua baadhi ya makopo kwa hofu ya kufungua janga lingine la ulimwengu! Lakini unapaswa kuwa na furaha kujua kwamba kwa usahihi tulitupa vitu hatari na kwamba hatari ya kiafya kwa ulimwengu iliondolewa.

Baadhi ya waumini wa Kanisa wanapendekeza kwamba mipango na vifaa vya dharura, akiba ya chakula na visanduku vya saa 72 havina ulazima tena kwa sababu akina Kaka hawajazungumza hivi karibuni na sana kuhusu mada hizi na zinazohusiana katika mkutano mkuu. Lakini maonyo yanayorudiwa ya kujitayarisha yamekuwa yakitangazwa na viongozi wa Kanisa kwa miongo mingi. Uendelevu wa ushauri wa kinabii baada ya muda hutengeneza burudani yenye nguvu ya usahihi na sauti ya onyo iliyo juu kuliko maonyesho ya mtu mmoja mmjoa yanavyoweza kutoa.

Kama vile nyakati za changamoto zinavyofunua upungufu wa matayarisho kimwili, ndivyo pia maradhi ya ukawaida wa kiroho na kiburi vinavyolazimisha matokeo yake yenye madhara wakati wa majaribu magumu. Tunajifunza, kwa mfano, katika mfano wa wanawali kumi kwamba kuahirisha matayarisho huongoza kwenye kuthibitisha kusiko na mafanikio. Kumbuka jinsi wanawali watano wapumbavu walivyoshindwa kujitayarisha ipasavyo kwa ajili ya mtihani uliotolewa kwao kwenye siku ya ujio wa bwana harusi.

“Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao:

“Bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. …

“Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

“Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

“Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

“Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

“Na hao walikuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.

“Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.” 8

“Akajibu akasema, Amin, nawaambia, hamkunijua ninyi.” 9

Angalau kwenye mtihani huu, wanawali watano wapumbavu walithibitisha kuwa wasikiaji tu na si watendaji wa neno. 10

Ninaye rafiki ambaye alikuwa mwanafunzi makini katika shule ya sheria. Wakati wa kipindi cha muhula, Sam aliwekeza muda kila siku kufanya marejeo, kufupisha na kujifunza kutoka kwenye maandishi yake kwa kila kozi ambayo alikuwa amejiandikisha. Alifuata mpangilio unaofanana kwa madarasa yake yote kila mwisho wa wiki na mwisho wa mwezi. Mbinu yake ilimwezesha kujifunza sheria na si tu kukariri maelezo. Na wakati mtihani wa mwisho ulipokaribia, Sam alikuwa amejitayarisha. Kwa kweli, kipindi cha mtihani wa mwisho kilikuwa sehemu ambayo haikumpa mawazo mengi wakati wa mafunzo yake ya sheria. Matayarisho yanayofaa na yanayofanywa kwa muda muafaka hupita uthibitisho wenye mafanikio.

Mbinu ya Sam kwenye elimu yake ya sheria inaonyesha moja ya mipangilio muhimu ya Bwana kwa ajili ya ukuaji na maendeleo. “Kwani tazama, hivi asema Bwana Mungu: Nitawapatia watoto wa watu mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo; na heri wale wanaosikiliza kanuni zangu, na kutii mashauri yangu, kwani watasoma hekima, kwani kwa yule atakayepokea nitampatia zaidi.” 11

Ninamualika kila mmoja wetu “kuzitafakari njia [zetu]” 12 na “tujijaribu [wenyewe[, kwamba [sisi] tumekuwa katika imani; [na] tujithibitishe [sisi] wenyewe.” 13 Ni kipi tumejifunza kipindi cha miezi hii ya karibuni ya marekebisho ya maisha na vizuizi? Ni nini tunahitaji kuboresha katika maisha yetu kiroho, kimwili, kijamii, kihisia na kiakili? Sasa ni wakati wa kujitayarisha na kujithibitisha wenyewe kwamba tuko tayari na tunaweza kufanya mambo yote Bwana Mungu wetu atakayotuamuru.

Kuthibitisha na Kusonga Mbele

Niliwahi kuhudhuria mazishi ya mmsisionari kijana aliyeuawa katika ajali. Baba wa mmisionari alizungumza kwenye shughuli ya mazishi na kuelezea maumivu ya moyo ya utengano usiotarajiwa kutoka kwa mtoto mpendwa. Alitangaza waziwazi kwamba yeye binafsi hakuelewa sababu au muda wa tukio kama hilo. Lakini daima nitakumbuka mwanamume huyu mwema pia akitangaza kwamba alijua kuwa Mungu alijua sababu na muda wa kufa mtoto wake—na hilo lilitosha kabisa kwake. Aliwaambia mkusanyiko kwamba yeye na familia yake, japo wana huzuni, watakuwa sawa; shuhuda zao zilibaki imara na thabiti. Alihitimisha maneno yake kwa tangazo hili: “ninataka mjue kwamba kadiri injili ya Yesu Kristo inavyohusika, familia yetu yote imo ndani. Sote “tumo ndani.”

Japo kumpoteza mpendwa wao ilikuwa ya kuvunja moyo na ngumu, wana familia wa familia hii jasiri walikuwa wamejitayarisha kiroho kuthibitisha kwamba wangeweza kujifunza masomo yenye umuhimu wa milele kupitia mambo waliyoteseka. 14

Uaminifu si upumbavu au ushabiki. Bali, ni kuamini na kuweka ujasiri wetu katika Yesu Kristo kama Mwokozi wetu, kwenye jina Lake na katika ahadi Zake. Wakati “tunaposonga mbele tukiwa na imani imara katika Kristo, tukiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote,” 15 tunabarikiwa kwa mtazamo na ono la milele ambalo linaenda mbali zaidi ya uwezo wetu wenye ukomo wa maisha haya. Tutawezeshwa “kukusanyika pamoja, na kusimama mahali patakatifu” 16 na “wala tusiondoshwe, hadi siku ya Bwana itapofika.” 17

Wakati nilipokuwa nikihudumu kama rais wa Chuo Kikuu cha Brigham Young—Idaho, Mzee Jeffrey R. Holland alikuja chuoni mnamo Desemba 1998 ili kuzungumza kwenye mikutano yetu ya ibada ya kila wiki. Mimi na Susan tulialika kundi la wanafunzi kukutana na kuzungumza na Mzee Holland kabla hajatoa ujumbe wake. Wakati muda wetu pamoja ulipokuwa ukielekea ukingoni, nilimuuliza Mzee Holland, “ikiwa ungepaswa kuwafundisha wanafunzi hawa jambo moja tu, jambo hilo lingekuwa nini?”

Alijibu:

“Tunashuhudia ongezeko kubwa zaidi kuelekea upinzani. Mapendeleo ya kuwa katikati yataondolewa kwetu kama Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kuwa katikati ya njia kutaondolewa.

“Ikiwa umekanyaga maji kwenye mkondo wa mto, utaenda mahala fulani. Kwa urahisi utaenda tu popote mkondo unapokupeleka. Kwenda na mtiririko, kufuata mawimbi, kuteleza kwenye mkondo havitasaidia chochote.

“Chaguzi hazina budi kufanywa. Kutokufanya uchaguzi ni uchaguzi. Jifunze kuchagua sasa.”

Kauli ya Mzee Holland kuhusu ongezeko la upinzani imethibitishwa kinabii kwa mitindo ya kijamii na matukio ya miaka 22 tangu alipojibu swali langu. Akitabiri ongezeko la utofauti kati ya njia za Bwana na za ulimwengu, Mzee Holland alionya kwamba siku za kujisikia vizuri kuwa na mguu mmoja kwenye Kanisa lililorejeshwa na mguu mwingine ulimwenguni zilikuwa zikitoweka kwa haraka. Mtumishi huyu wa Bwana alikuwa akiwahimiza vijana kuchagua, kujitayarisha na kuwa wafuasi wenye msimamo wa Mwokozi. Alikuwa akiwasaidia kujitayarisha na kusonga mbele kwenye, na kupitia uzoefu wa kuthibitisha, kutathmini na wa kujaribu wa maisha yao.

Ahadi na Ushuhuda

Mchakato wa kujithibitisha ni sehemu muhimu ya mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni. Ninaahidi kwamba kadiri sote tunavyojitayarisha na kusonga mbele tukiwa na imani kwa Mwokozi, sote tunaweza kupokea kiwango kinachofanana kwenye mtihani wa mwisho wa maisha ya duniani: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu: ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako.” 18

Ninatoa ushahidi kwamba Mungu Baba wa Milele ni Baba yetu. Yesu Kristo ndiye Mwanawe Mzaliwa wa Pekee, Mwokozi na Mkombozi wetu. Juu ya kweli hizi ninashuhudia kwa furaha katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.