Mkutano Mkuu
Kupata Shangwe katika Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


9:56

Kupata Shangwe katika Kristo

Njia ya uhakika ya kupata shangwe katika maisha haya ni kuungana na Kristo katika kuwasaidia wengine.

Bwana hawaombi vijana wetu wa Ukuhani wa Haruni kufanya kila kitu, lakini kile Anachoomba ni chenye msukumo wa kupendeza.

Miaka michache iliyopita, familia yetu ilipitia kile ambacho familia nyingi zinapitia katika ulimwengu huu ulioanguka. Mwana wetu mdogo, Tanner Christian Lund, aliugua saratani. Alikuwa ni roho ya kushangaza, kama watoto wa miaka tisa mara nyingi walivyo. Alikuwa mtundu sana na, wakati huo huo, mwenye kujitambua kiroho. Mtundu na malaika, mkorofi na mwema. Wakati alipokuwa mdogo na kila siku alipokuwa akitushangaza kwa ubunifu na ukorofi wake, tulijiuliza ikiwa angekua nabii au mnyang’anyi wa benki. Vyovyote vile, ilionekana kwamba ataacha alama ya ukumbusho ulimwenguni.

Na kisha alikuwa mgonjwa sana. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyofuatia, dawa za kisasa ziliongoza kwenye hatua za kishujaa, zikijumuisha upandikizaji mara mbili wa mafuta kwenye mfupa, ambapo alipata nimonia, iliyomlazimu kutumia wiki 10 bila fahamu kwenye mashine ya kupumulia. Kimuujiza, alirejea kuwa sawa kwa muda mfupi, lakini kisha kansa yake ikarudi tena.

Muda mfupi kabla ya kufariki, ugonjwa wa Tanner ulikuwa umevamia mifupa yake, na hata pamoja na dawa zenye nguvu za maumivu, bado aliumia. Alitoka kitandani kwa shida sana. Asubuhi moja ya Jumapili, mama yake, Kalleen, aliingia chumbani mwake kumwangalia kabla ya familia kuondoka kwenda kanisani. Mama alishangaa kuona kwamba alikuwa amevaa nguo na alikuwa ameketi pembeni mwa kitanda chake, akihangaika kwa maumivu kufunga kifungo cha shati. Kalleen aliketi karibu naye. “Tanner,” alisema, “una uhakika una nafuu ya kutosha kwenda kanisani? Pengine leo unapaswa kubaki nyumbani na upumzike.”

Alitazama sakafuni. Alikuwa ni shemasi. Alikuwa na akidi. Na alikuwa na jukumu.

“Ninapaswa kupitisha sakramenti leo.”

“Vyema, nina hakika kuna mtu atafanya hilo kwa niaba yako.”

“Ndiyo,” Tanner alisema, “lakini … ninaona jinsi watu wanavyonitazama ninapopitisha sakramenti. Nadhani inawasaidia.”

Kwa hivyo Kalleen alimsaidia kufunga vifungo vya shati lake na kufunga tai yake, na wakaelekea kanisani. Kwa dhahiri, jambo muhimu lilikuwa likitendeka.

Niliingia kanisani baada ya mkutano wa mapema asubuhi na hivyo nilishangaa kumwona Tanner ameketi kwenye safu ya mashemasi. Kalleen kwa utulivu aliniambia kwa nini Tanner alikuwapo pale na kile alichokuwa amesema: “Inasaidia watu.”

Na hivyo nilitazama wakati mashemasi walipopiga hatua kwenye meza ya sakramenti. Alimwegemea taratibu shemasi mwingine wakati makuhani walipowapitishia trei. Na kisha Tanner aliyumba na kwenda mahali alipopangiwa na kushika mwisho wa benchi la kanisani ili kujiimarisha wakati akitoa sakramenti.

Ilionekana kuwa kila jicho ndani ya kanisa lilikuwa kwake, wakihisi maumivu yake wakati akifanya sehemu yake rahisi. Kwa kiasi fulani Tanner alielezea mahubiri ya kimya kimya wakati kwa dhati, kwa kusita akisogea kutoka mstari hadi mstari—kichwa chake kisicho na nywele kikiwa na unyevu wa jasho—akimwakilisha Mwokozi kwa njia ambayo mashemasi hufanya. Mwili wake wa kishemasi uliowahi kuwa imara ulikuwa kidogo umejeruhiwa, umevunjika, na umepasuka, kwa hiari akiteseka ili kutumikia kwa kubeba nembo za Upatanisho wa Mwokozi maishani mwetu.

Kuona jinsi alivyokuja kufikiria kuhusu kuwa shemasi kulitufanya sisi pia kufikiria kitofauti—kuhusu sakramenti, kuhusu Mwokozi, na kuhusu mashemasi, na walimu na makuhani.

Ninastaajabu kwa muujiza usioelezeka ambao ulimsukuma kuitikia kwa ujasiri wito ule mtulivu, mdogo wa kutumikia, na kuhusu nguvu na uwezo wa vijana wetu wote wanaoinukia pale wanapokazana kuitikia mwito wa nabii wa kujiandikisha katika vikosi vya Mungu na kujiunga katika kazi ya wokovu na kuinuliwa.

Kila wakati shemasi anaposhika trei ya sakramenti, tunakumbushwa juu ya hadithi takatifu ya Karamu ya Mwisho, juu ya Gethsemane, juu ya Kalvari, na juu ya kaburi la bustani. Wakati Mwokozi alipowaambia Mitume Wake, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 1 Alikuwa pia akizungumza kwa vizazi vyote kwa kila mmoja wetu. Alikuwa akizungumza juu ya muujiza ambao angetoa wakati mashemasi wa baadaye, waalimu, na makuhani watakapowasilisha nembo Zake na kuwaalika watoto Wake kukubali zawadi ya upatanisho Wake.

Ishara zote za ibada ya sakramenti zinatuelekeza kwenye zawadi hiyo. Tunatafakari mkate ambao aliwahi kuumega—na mkate ambao makuhani walio mbele yetu, nao, sasa wanaumega. Tunafikiria maana ya kimiminika kilichowekwa wakfu, wakati ule na sasa, wakati sala za dhati za sakramenti zinapotoka kwenye vinywa vya makuhani wadogo kwenda kwenye mioyo yetu na kwenda mbinguni, zikifanya upya maagano ambayo yanatuunganisha hasa na nguvu za wokovu wa Kristo. Tunaweza kufikiria juu ya kile inachomaanisha wakati shemasi anapobeba nembo takatifu kwetu, akiwa amesimama jinsi anavyosimama mahali ambapo Yesu angesimama kama angekuwepo, akijitoa kuinua mizigo yetu na kuponya maumivu yetu.

Kwa bahati nzuri, vijana wa kiume na wa kike hawapaswi kuugua ili kugundua shangwe na kusudi katika kumtumikia Mwokozi.

Mzee David A. Bednar amefundisha kwamba ili kuwa kama wamisionari walivyo, tunapaswa kufanya kile wamisionari wanachofanya, na kisha, “mstari juu ya mstari na amri juu ya amri, … [tunaweza] polepole kuwa wamisionari … ambao Mwokozi anatarajia.” 2

Vilevile, ikiwa tunatamani “kuwa kama Yesu,” 3 tunapaswa kufanya kile Yesu anachofanya, na katika sentensi moja ya kustaajabisha, Bwana anaeleza kile ambacho Yeye hufanya: Alisema, “Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.” 4

Dhamira ya Mwokozi daima imekuwa na milele itakuwa kumtumikia Baba Yake kwa kuokoa watoto Wake.

Na njia ya uhakika ya kupata furaha katika maisha haya ni kuungana na Kristo katika kuwasaidia wengine.

Huu ni ukweli rahisi ambao ulichochea programu ya Watoto na Vijana.

Shughuli zote za Watoto na Vijana na mafundisho yote ya Watoto na Vijana ni juu ya kuwasaidia vijana kuwa zaidi kama Yesu kwa kuungana Naye katika kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa.

Watoto na Vijana ni nyenzo ya kumsaidia kila mtoto wa Msingi na kijana kukua katika ufuasi na kupata maono yaliyojaa imani ya jinsi njia ya furaha ilivyo. Wanaweza kutarajia na kutamani vituo vya njiani na mabango ya alama kwenye njia ya agano, ambapo watabatizwa na kuthibitishwa kwa kipawa cha Roho Mtakatifu na kisha kuwa sehemu ya akidi na madarasa ya Wasichana, ambapo watahisi shangwe ya kuwasaidia wengine kupitia urithi wa matendo ya huduma kama ya Kristo. Wataweka malengo, makubwa na madogo, ambayo yataleta usawa kwenye maisha yao pale wanapokua zaidi kama Mwokozi. Mikutano ya Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana na majarida, Rafiki, na programu ya Kuishi Injili vitasaidia kuwakita kwenye kupata shangwe katika Kristo. Watafurahia baraka za kuwa na vibali vya hekalu vyenye ukomo wa matumizi, na watahisi roho ya Eliya kupitia ushawishi wa Roho Mtakatifu pale wanapotafuta baraka za hekalu na historia ya familia. Wataongozwa na baraka za patriaki. Hatimaye, watajiona wakiingia kwenye mahekalu kujaliwa nguvu na kupata shangwe pale wanapounganishwa milele, bila kizuizi chochote, wao na familia zao.

Kinyume na pepo za maradhi yaliyoenea kote na majanga, uletaji wa ahadi timilifu ya programu mpya ya Watoto na Vijana bado ni kazi inayoendelea—ila kuna uharaka. Vijana wetu hawawezi kusubiri ulimwengu ukae sawa kabla hawajamjua Mwokozi. Baadhi wanafanya maamuzi hata sasa ambayo hawangeyafanya ikiwa wangeelewa utambulisho wao wa kweli—na wa Mwokozi.

Na hivyo mwito wa dharura kutoka kwenye vikosi vya Mungu kwa ajili ya mafunzo ya kudra ni “mikono yote kwenye sitaha!”

Akina mama na akina baba, wana wenu wanahitaji muwaunge mkono sasa kwa shauku kama vile mlivyofanya siku za nyuma walipokuwa kwenye mambo madogo kama beji na pini. Akina mama na akina baba, viongozi wa ukuhani na Wasichana, ikiwa vijana wenu wanakabiliwa na changamoto, Watoto na Vijana itawasaidia kuwaleta kwa Mwokozi, na Mwokozi atawapa amani. 5

Urais wa akidi na darasa, simameni na chukueni nafasi zenu sahihi katika kazi ya Bwana.

Maaskofu, unganisheni funguo zenu na zile za marais wa akidi, na akidi zenu—na kata zenu—zitabadilika milele.

Na kwenu ninyi kizazi kinachoinukia, ninashuhudia, kama mtu anayejua, kwamba ninyi ni wana na mabinti wapendwa wa Mungu na ana kazi ya kufanya kwa ajili yenu.

Mnapoinuka kwenye ukuu wa miito yenu, kwa mioyo yenu yote, nguvu, akili, na uwezo, mtakuja kumpenda Mungu na kutunza maagano yenu na kuamini katika ukuhani Wake wakati mnapofanya kazi ya kuwabariki wengine, mkianzia katika nyumba zenu wenyewe.

Ninaomba kwamba mtajitahidi, kwa nguvu maradufu inayostahili wakati huu, kutumikia, kuonyesha imani, kutubu, na kuwa bora kila siku, ili kustahili kupokea baraka za hekaluni na furaha ya kudumu ambayo huja tu kupitia injili ya Yesu Kristo. Ninaomba kwamba mtajitayarisha kuwa mmishonari yule mwenye bidii, mume au mke mwaminifu, baba au mama mwenye upendo, ambaye umeahidiwa kwamba unaweza hatimaye kuwa kwa kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.

Naomba msaidie kuuandaa ulimwengu kwa kurudi kwa Mwokozi kwa kuwaalika wote kuja kwa Kristo na kupokea baraka za Upatanisho Wake. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Luka 22:19.

  2. David A. Bednar, “Becoming a Missionary,” Liahona, Nov. 2005, 46.

  3. “Ninajaribu kuwa kama Yesu; Ninafuata katika njia zake. Ninajaribu kupenda kama alivyopenda, katika yote ninayofanya na kusema” (“Ninajaribu Kuwa Kama Yesu,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78–79).

  4. Musa 1:39.

  5. Binafsi ninaelezea shukrani kwa wazazi na viongozi waliojitoa kote katika historia yetu ambao kwa ushujaa wamesaidia vijana kupata uzoefu wa ukuaji. Ninatambua kwamba juhudi mpya ya Watoto na Vijana ina deni kubwa kwa kila programu ya shughuli na mafanikio ambayo imeitangulia.