Mkutano Mkuu
Basi, Kesheni Ninyi Kila Wakati, Mkiomba
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


15:1

Basi, Kesheni Ninyi Kila Wakati, Mkiomba

Leo, napanua wito wangu wa maombi kwa watu wote kutoka kila nchi ulimwenguni.

Kaka na dada zangu wapendwa, katika juma la mwisho la huduma Yake hapa duniani, Yesu aliwafundisha wanafunzi Wake “Kesheni Ninyi Kila Wakati, Mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.”1

Miongoni mwa “mambo yatakayotokea” kabla ya Kuja Kwake Mara ya Pili ni “vita na uvumi wa vita[,] … njaa, na magonjwa, na matetemeko ya ardhi, katika sehemu mbali mbali.”2

Kwenye Mafundisho na Maagano Mwokozi alisema, “Na vitu vyote vitakuwa katika vurugu; … kwa kuwa hofu itakuja juu ya watu wote.”3

Hakika, tunaishi katika wakati ambapo vitu vipo katika vurugu. Watu wengi wanaogopa siku za usoni, na mioyo mingi imeacha imani yao kwa Mungu na Mwanawe, Yesu Kristo.

Ripoti za habari zimejazwa taarifa za vurugu. Mmomonyoko wa maadili unachapishwa mtandaoni. Makaburi, makanisa, misikiti, masinagogi, na sehemu za kuabudu za kidini zimenajisiwa.

Maradhi yaliyoenea ulimwengu kote yamefika karibu kila kona ya dunia: mamilioni ya watu wameambukizwa, zaidi ya milioni wamekufa. Mahafali ya shule, ibada za kanisa, ndoa, huduma ya umisionari, na hafla zingine muhimu za maisha zimevurugwa. Kwa kuongezea, watu wasio na idadi wameachwa peke yao na kutengwa.

Machafuko ya kiuchumi yamesababisha changamoto kwa wengi, hasa kwa wanyonge zaidi wa watoto wa Baba yetu wa Mbinguni.

Tumeona watu wakitumia kwa hamu haki yao ya maandamano ya amani, na tumeona watu wenye hasira wakifanya ghasia.

Wakati huo huo, tunaendelea kuona mizozo kote ulimwenguni.

Nawafikiria mara nyingi wale kati yenu ambao wanateseka, wana wasiwasi, wanaogopa, au wanahisi upweke. Ninawahakikishia kila mmoja wenu kwamba Bwana anakujua, kwamba Anajua wasiwasi wako na uchungu, na kwamba Anakupenda—kwa karibu na kibinafsi, kwa undani na milele.

Kila usiku ninapoomba, ninamwomba Bwana awabariki wote ambao wanalemewa na huzuni, maumivu, upweke, na kusikitishwa. Ninajua kwamba viongozi wengine wa Kanisa wanarudia sala hiyo hiyo. Mioyo yetu, mmoja mmoja na kwa pamoja, inawafikia na maombi yetu yanakwenda kwa Mungu kwa niaba yako.

Nilikaa siku kadhaa mwaka jana katika sehemu ya kaskazini mashariki mwa Marekani kutembelea maeneo ya kihistoria ya Amerika na Kanisa, kuhudhuria mikutano na wamisionari wetu na waumini wetu, na kuwatembelea viongozi wa serikali na wafanyabiashara.

Siku ya Jumapili, Oktoba 20, nilizungumza na mkutano mkubwa karibu na Boston, Massachusetts. Wakati nilipokuwa ninaongea, nilihamasishwa kusema, “ninawasihi ninyi … kuiombea nchi hii, kwa ajili ya viongozi wetu, kwa watu wetu, na kwa familia zinazoishi katika taifa hili kubwa lililoanzishwa na Mungu.”4

Nilisema pia kwamba Marekani na mataifa mengi ya dunia, kama zamani, wako katika njia panda ya hatari na wanahitaji maombi yetu.5

Ombi langu halikuwa katika hotuba yangu iliyoandaliwa. Maneno hayo yalinijia nilipohisi Roho akinishawishi kuwaalika waliohudhuria kuiombea nchi yao na viongozi wao.

Leo napanua wito wangu wa maombi kwa watu wote kutoka kila nchi ulimwenguni. Haijalishi unaombaje au unaomba kwa nani, tafadhali tumia imani yako—bila kujali imani yako ikoje—na uombee nchi yako na viongozi wako wa kitaifa. Kama nilivyosema Oktoba iliyopita huko Massachusetts, tunasimama leo katika njia panda katika historia, na mataifa ya dunia yanahitaji sana msukumo na mwongozo wa kiungu. Hii haihusu siasa au sera. Hii ni juu ya amani na uponyaji ambavyo vinaweza kuja kwa roho ya mtu binafsi na pia kwa roho ya nchi—majiji yao, miji, na vijiji—kupitia Mfalme wa Amani na chanzo cha uponyaji wote, Bwana Yesu Kristo.

Katika miezi michache iliyopita nimekuwa na msukumo ukinijia kuwa njia bora ya kusaidia hali ya ulimwengu ya sasa ni kwa watu wote kumtegemea Mungu kikamilifu na kugeuza mioyo yao kwake kupitia maombi ya dhati. Kujinyenyekeza na kutafuta msukumo wa mbinguni kuvumilia au kushinda kile kilicho mbele yetu itakuwa njia yetu salama na ya uhakika zaidi ya kusonga mbele kwa ujasiri kupitia nyakati hizi zenye shida.

Maandiko yanaangazia maombi yaliyotolewa na Yesu pamoja na mafundisho Yake juu ya maombi wakati wa huduma Yake ya kufa. Utakumbuka Sala ya Bwana:

“Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.

“Ufalme wako uje. Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.

“Utupe leo mkate wetu wa kila siku.

“Na utusamehe deni zetu, kama tunavyowasamehe wadeni wetu.

“Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu: kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.”6

Sala hii nzuri iliyoelekezwa, inayorudiwa mara kwa mara kote katika Ukristo, inaweka wazi kuwa inafaa kuomba moja kwa moja “Baba yetu uliye mbinguni” kwa ajili ya majibu ya kile kinachotusumbua. Kwa hivyo, acheni tuombe kwa ajili ya mwongozo wa kimungu.

Ninakualika uombe kila wakati.7 Ombea familia yako. Waombee viongozi wa mataifa. Ombea watu wenye ujasiri walio katika mstari wa mbele katika vita vya sasa dhidi ya magonjwa ya kijamii, mazingira, kisiasa, na kibaolojia ambayo yanaathiri watu wote ulimwenguni kote: matajiri na maskini, vijana na wazee.

Mwokozi alitufundisha kutoweka ukomo wa wale tunaowaombea. Alisema, “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, watendeeni mema wanaowachukia, na waombeeni wanaowatumia kwa hila, na kuwatesa.”8

Kwenye msalaba wa Kalvari, ambapo Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, Alifanya kile alichofundisha wakati Akiomba, “Baba, wasamehe; maana hawajui watendalo.”9

Kuwaombea kwa dhati wale wanaoweza kuchukuliwa kuwa maadui zetu kunaonyesha imani yetu kwamba Mungu anaweza kubadilisha mioyo yetu na mioyo ya wengine. Maombi kama haya yanapaswa kuimarisha azimio letu la kufanya mabadiliko yoyote ambayo ni muhimu katika maisha yetu, familia, na jamii.

Bila kujali unaishi wapi, unazungumza lugha gani, au changamoto unazokabiliana nazo, Mungu husikia na kukujibu kwa njia yake mwenyewe na kwa wakati wake. Kwa sababu sisi ni watoto Wake, tunaweza kumkaribia kutafuta msaada, faraja, na hamu mpya ya kufanya mabadiliko mazuri ulimwenguni.

Kuombea haki, amani, masikini, na wagonjwa mara nyingi haitoshi. Baada ya kupiga magoti katika maombi, tunahitaji kuinuka kutoka kwenye magoti yetu na kufanya kile tunachoweza kusaidia—kujisaidia sisi wenyewe na wengine.10

Maandiko yamejaa mifano ya watu wa imani ambao waliunganisha sala na hatua ili kuleta mabadiliko katika maisha yao wenyewe na katika maisha ya wengine. Kwa mfano katika Kitabu cha Mormoni, tunasoma juu ya Enoshi. Imeonekana kuwa “karibu theluthi mbili ya kitabu chake kifupi kinaelezea sala, au safu ya sala, na usawa huelezea kile alichofanya kama matokeo ya majibu aliyopokea.”11

Tunayo mifano mingi ya jinsi sala ilivyofanya mabadiliko katika historia yetu ya Kanisa, tukianza na sala ya kwanza ya sauti ya Joseph Smith katika eneo lenye miti karibu na nyumba ya magogo ya wazazi wake katika majira ya chemchemi ya mwaka 1820. Kutafuta msamaha na mwelekeo wa kiroho, sala ya Joseph ilifungua mbingu. Leo, sisi ndio wanufaikaji wa Joseph Nabii na wanaume na wanawake wengine waaminifu wa Siku za Mwisho ambao waliomba na kutenda kusaidia kuanzisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Mara nyingi mimi hufikiria juu ya maombi ya wanawake waaminifu kama Mary Fielding Smith ambaye, kwa msaada wa Mungu, kwa ujasiri aliongoza familia yake kutoka kwenye mateso huko Illinois hadi kufika salama katika bonde hili ambapo familia yake ilifanikiwa kiroho na kimwili. Baada ya kuomba kwa bidii akiwa amepiga magoti, basi alifanya kazi kwa bidii kushinda changamoto zake na kubariki familia yake.

Maombi yatatuinua na kutuvuta pamoja kama watu binafsi, kama familia, kama Kanisa, na kama ulimwengu. Maombi yatashawishi wanasayansi na kuwasaidia kuelekea uvumbuzi wa chanjo na dawa ambazo zitamaliza janga hili. Maombi yatawafariji wale waliofiwa na mpendwa wao. Yatatuongoza katika kujua nini cha kufanya kwa ulinzi wetu binafsi.

Akina kaka na akina dada, nawasihi mzidishe kujitolea kwenu katika maombi. Ninakuhimizeni kusali mahala penu pa sirini, katika matembezi yenu ya kila siku, nyumbani mwenu, katika kata zenu, na kila wakati mioyoni mwenu.12

Kwa niaba ya viongozi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ninawashukuru kwa maombi yenu kwa ajili yetu. Ninakuhimizeni muendelee kuomba ili tupate msukumo na ufunuo kuliongoza Kanisa katika nyakati hizi ngumu.

Maombi yanaweza kubadilisha maisha yetu wenyewe. Tukichochewa na maombi ya dhati, tunaweza kuboresha na kusaidia wengine wafanye vivyo hivyo.

Najua nguvu ya maombi kwa uzoefu wangu mwenyewe. Hivi majuzi nilikuwa peke yangu ofisini kwangu. Nilikuwa nimepitia utaratibu wa matibabu katika mkono wangu. ulikuwa mweusi na wa bluu, umevimba, na ulikuwa na maumivu. Nilipokuwa nimeketi kwenye meza yangu, sikuweza kuzingatia mambo muhimu na ya dharura kwa sababu nilikuwa nikisumbuliwa na maumivu haya.

Nilimwomba Bwana anisaidie kuzingatia ili niweze kukamilisha kazi yangu. Nilisimama na kurudi kwenye lundo la karatasi kwenye meza yangu. Karibu mara moja, uwazi na umakini vilikuja akilini mwangu, na niliweza kumaliza mambo ya muhimu mbele yangu.

Hali ya sasa ya machafuko ya ulimwengu inaweza kuonekana kuwa ya kutisha tunapofikiria wingi wa maswala na changamoto. Lakini ni ushuhuda wangu wa dhati kwamba ikiwa tutaomba na kumuuliza Baba wa Mbinguni baraka na mwongozo unaohitajika, tutakuja kujua jinsi tunavyoweza kubariki familia zetu, majirani, jamii, na hata nchi tunamoishi.

Mwokozi aliomba na kisha “akazunguka na kufanya mema”13 kwa kulisha maskini, kutoa ujasiri na msaada kwa wale wanaohitaji, na kufikia kwa upendo, msamaha, amani, na kupumzika kwa wale wote ambao wangekuja kwake. Anaendelea kutufikia.

Ninawaalika waumini wote wa Kanisa, pamoja na majirani zetu na marafiki wa vikundi vingine vya imani ulimwenguni, kufanya kama Mwokozi alivyowashauri wanafunzi Wake: “Basi, Kesheni Ninyi Kila Wakati, Mkiomba,”14 kwa ajili ya amani, faraja, usalama, na fursa za kuhudumiana.

Jinsi gani nguvu kubwa ya maombi na sala zetu za imani katika Mungu na Mwana Wake Mpendwa zinahitajika ulimwenguni leo! Acha tukumbuke na kuthamini nguvu ya maombi. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.