“Aprili 17–23. Mathayo 18; Luka 10: ‘Nifanye Nini ili Kurithi Uzima wa Milele?’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Aprili 17–23. Mathayo 18; Luka 10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023
Aprili 17–23
Mathayo 18; Luka 10
“Nifanye Nini ili Kurithi Uzima wa Milele?”
Kwa maombi unaposoma na kutafakari Mathayo 18 na Luka 10, kuwa mwangalifu na ushawishi wa kimya kimya wa Roho Mtakatifu. Atakuambia jinsi gani mafundisho na hadithi hizi zinatumika kwako. Andika misukumo unayopokea.
Andika Misukumo Yako
Unapomuuliza Bwana swali, unaweza kupokea jibu ambalo hukutegemea. Jirani yangu ni nani? Yeyote anayehitaji msaada na upendo wako. Je, ni nani aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Mtoto. Je, inatosha kumsamehe mkosaji mara saba? Hapana, unapaswa kusamehe saba mara sabini. (Ona Luka 10:29–37; Mathayo 18:4, 21–22.) Majibu yasiyotarajiwa kutoka kwa Bwana yanaweza kukualika ubadili namna unavyofikiri, unavyohisi, na kutenda. Kama unatafuta mapenzi ya Bwana kwa sababu kweli unataka kujifunza kutoka Kwake, Bwana atakufundisha jinsi ya kuishi katika njia inayokuongoza kwenye uzima wa milele pamoja na Yeye.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Ni lazima niwasamehe wengine ili nipokee msamaha wa Bwana.
Pendekezo la Petro kwamba angeweza kumsamehe mtu mara saba lingeweza kuonekana la ukarimu sana, lakini Yesu alifundisha sheria ya juu zaidi. Jibu Lake, “Sikuambii, Hata mara saba: bali, Hata saba mara sabini” (mstari wa 22), hakukufundisha kuhusu idadi bali hasa kuhusu mtazamo kama wa Kristo juu ya msamaha. Unaposoma fumbo la mtumwa asiye na huruma, tafakari nyakati ambapo wewe ulihisi rehema na huruma ya Mungu. Je, kuna yeyote anayehitaji kuhisi rehema na huruma kutoka kwako?
Mzee David E. Sorensen alitoa tahadhari hii muhimu: “Ingawaje ni lazima tumsamehe jirani yetu anayetuumiza, tunapaswa bado kufanya kazi chanya ya kuzuia madhara hayo ili kuzuia madhara yasijirudie. … Msamaha hautuhitaji sisi kukubali au kuvumilia uovu. … Lakini tunapopigana dhidi ya dhambi, ni sharti tusiruhusu chuki au hasira kumiliki mawazo au matendo yetu” (“Msamaha Utabadilisha Machungu kuwa Upendo,” Liahona, Mei 2003, 12).
Sabini ni nani?
Akifuata mpangilio ulioanzishwa nyakati za Agano la Kale (ona Kutoka 24:1; Hesabu 11:16), Yesu Kristo “alichagua wengine sabini,” kuongezea kwa Mitume Wake Kumi na Wawili, ili kumshuhudia Yeye, kuhubiri injili Yake, na kumsaidia katika kazi Yake. Mpangilio huu unaendelea katika Kanisa lililorejeshwa. Sabini huitwa ili kuwasaidia Mitume katika huduma yao kama mashahidi maalumu wa Yesu Kristo kwa ulimwengu wote.
Ili kupata uzima wa milele, ninalazimika kumpenda Mungu na kumpenda jirani yangu kama ninavyojipenda mimi mwenyewe.
Inasaidia kukumbuka kwamba fumbo la Msamaria mwema lilikuwa ni njia ya Yesu kujibu maswali mawili: Nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?” na “Jirani yangu ni nani?” (Luka 10:25, 29). Unaposoma fumbo hili, yaweke maswali haya akilini. Je, unapata majibu gani?
Katika siku ya Yesu, chuki kati ya Wayahudi na Wasamaria ilikuwa imedumu kwa karne nyingi. Wasamaria walikuwa ni uzao wa Wayahudi walioishi katika Samaria ambao walikuwa wameoana na Wayunani. Wayahudi waliona kwamba Wasamaria walikuwa wameharibika kwa muingiliano wao na Wayunani na walikuwa wamekengeuka. Wayahudi wangesafiri maili nyingi nje ya njia yao kuepuka kupita katika Samaria. (Ona pia Luka 9:52–54; 17:11–18; Yohana 4:9; 8:48.)
Je, ni kwa nini unafikiri Mwokozi alimchagua Msamaria, mtu ambaye alichukiwa na Wayahudi, kama mfano wa huruma na kumpenda jirani yako? Je, fumbo hili linakufanya ushawishike kufanya nini?
Ona pia Mosia 2:17.; “Parable of the Good Samaritan” na “Good Samaritan” (video, ChurchofJesusChrist.org).
Tunachagua “fungu lililo jema” kwa kufanya chaguzi kila siku ambazo zinatuongoza kwenye uzima wa milele.
Katika Luka 10:38–42, Yesu kwa upole alimwalika Martha kufikiri katika njia tofauti kuhusu jinsi alivyokuwa akitumia muda wake. Baada ya kunukuu mistari hii, Dada Carol F. McConkie alifundisha: “Kama tunataka tuwe watakatifu, ni lazima tujifunze kuketi miguuni pake Mtakatifu wa Israeli na tutenge muda kwa ajili ya utakatifu. Je, tunaiweka simu kando, orodha ya majukumu yasiyo na kikomo, na shida za dunia? Sala, kujifunza, na kushika neno la Mungu vinaalika upendo Wake utakasao na kuponya katika nafsi zetu. Acha tutenga muda wa kuwa watakatifu, ili tuweze kujazwa na roho Wake mtakatifu na Roho wa kutakasa” (“Uzuri wa Utakatifu,” Liahona, Mei 2017, 11). Unaweza kutaka kujichunguza jinsi unavyotumia muda wako—hata kama ni kwa mambo mazuri. Je, kuna jambo “linalohitajika” (mstari wa 42) ambalo linahitaji zaidi usikivu wako?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Mathayo 18:1–11.Je, ni kwa nini Yesu alitaka sisi tuwe kama mtoto mdogo? Ni sifa gani watoto wanazo ambazo tunaweza kukuza ili kuwa zaidi kama Kristo? (Ona Mosia 3:19).
-
Mathayo 18:15.Ni kwa jinsi gani tunaweza kutumia ushauri katika Mathayo 18:15 katika miingiliano ya familia yetu? Ni kwa jinsi gani kufanya hivi kutabariki familia yetu?
-
Mathayo 18:21–35.Fumbo hili linatufundisha nini kumhusu Yesu Kristo? Je, linatufundisha nini kuhusu jinsi ya kuwatendea wengine?
-
Luka 10:25–37.Wanafamilia wanaweza kufurahia kuvaa mavazi na kuigiza fumbo hili. Ni kwa jinsi gani sisi wakati mwingine ni kama watu katika fumbo hili? Ni kwa jinsi gani Mwokozi ni kama Msamaria mwema? Ni kwa jinsi gani sisi tunaweza kuwa kama Msamaria mwema?
Unaweza kufikiria kuimba wimbo wa kanisa au wimbo wa watoto ambao unaunga mkono kweli katika fumbo hili. Mfano mmoja ni “Lord, I Would Follow Thee” (Nyimbo za Kanisa, na. 220), lakini kuna nyingine nyingi. Wanafamilia wanaweza kufurahia kutafuta wimbo na kuelezea jinsi unavyohusiana na fumbo hili.
-
Luka 10:38–42.Je, ni vigumu kuingiza mambo ya kiroho katika ratiba ya familia yako? Hadithi ya Mariamu na Martha inaweza kushawishi baraza la familia au jioni ya familia nyumbani kuhusu jinsi ya kufanya hili vizuri zaidi. Kama familia, mnaweza kutengeneza orodha ya njia za kuchagua “fungu lililo jema” (Luka 10:42).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa. “Jesus Said Love Everyone,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 61.