Agano Jipya 2023
Mei 15–21. Mathayo 21–23; Marko 11; Luka 19–20; Yohana 12: “Tazama, Mfalme Wako Anakuja”


“Mei 15–21. Mathayo 21–23; Marko 11; Luka 19–20; Yohana 12: ‘Tazama, Mfalme Wako Anakuja’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)

“Mei 15–21. Mathayo 21–23; Marko 11; Luka 19–20; Yohana 12: ‘Tazama, Mfalme Wako Anakuja’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Picha
mtu akiwa juu ya mti wakati Yesu akikaribia

Zakayo juu ya Mti wa Mkuyu, na James Tissot

Mei 15–21

Mathayo 21–23; Marko 11; Luka 19–20; Yohana 12

“Tazama, Mfalme Wako Anakuja”

Kabla ya kusoma mawazo katika muhtasari huu, soma Mathayo 21–23; Marko 11; Luka 19–20; na Yohana 12. Andika misukumo ambayo unaweza kushiriki na familia yako au katika madarasa yako kanisani.

Andika Misukumo Yako

Mwokozi alikuwa na njaa baada ya kusafiri kutoka Bethania kwenda Yerusalemu, na mti wa mtini kwa mbali ulionekana kama chanzo cha chakula. Lakini Yesu alipoukaribia mti, Yeye aliona kwamba haukuwa na matunda (ona Mathayo 21:17–20; Marko 11:12–14,20). Kwa namna fulani, mti wa mtini ulifanana na viongozi wa dini wanafiki katika Yerusalemu: mafundisho yao matupu na kuonyesha utakatifu kwa nje havikutoa lishe ya kiroho. Mafarisayo na waandishi walionekana kutii amri nyingi lakini bado walikosa amri kuu mbili: kumpenda Mungu na kumpenda jirani yako kama nafsi yako (ona Mathayo 22:34–40; 23:23).

Kwa upande mwingine, watu wengi walikuwa wameanza kutambua matunda mazuri katika mafundisho ya Yesu. Alipofika Yerusalemu, walimkaribisha kwa matawi yaliyokatwa kutoka kwenye miti kumuandalia njia Yake, wakishangilia kwamba hatimaye, kama unabii wa kale ulivyosema, “Mfalme wako anakuja” (Zakaria 9:9). Unaposoma wiki hii, fikiria kuhusu matunda ya mafundisho ya Mwokozi na dhabihu ya kulipia dhambi katika maisha yako na kwa jinsi gani unaweza kutoa “mazao mengi” (Yohana 12:24).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Luka 19:1–10

Bwana hahukumu kwa muonekano wa nje bali kwa matamanio ya moyo.

Katika siku za Yesu, watu wengi walidhania kwamba watoza ushuru, au wakusanya kodi, hawakuwa waaminifu na waliwaibia watu. Hivyo kwa sababu Zakayo, mtoza ushuru mkuu, alikuwa tajiri, aliweza hata kutiliwa shaka zaidi. Lakini Yesu aliangalia moyo wa Zakayo. Je, Luka 19:1–10 hufunua nini kuhusu moyo wa Zakayo? Unaweza kuandika maneno katika mistari hii ambayo huelezea ni kitu gani Zakayo alifanya ili kuonyesha kujitoa kwake kwa Mwokozi. Je, ni yapi matamanio ya moyo wako? Je, unafanya nini ili kumtafuta Mwokozi, kama Zakayo alivyofanya?

Ona pia Mafundisho na Maagano 137:9.

Mathayo 23; Luka 20:45–47

Yesu analaani unafiki.

Mwingiliano wa Mwokozi na waandishi na Mafarisayo unatengeneza utofauti wa kuvutia kwenye mwingiliano Wake na Zakayo. Kama Rais Dieter F. Uchtdorf alivyoelezea, “[Yesu] alipandwa na hasira ya haki dhidi ya wanafiki kama waandishi, Mafarisayo na Masadukayo—wale ambao walijaribu kuonekana wenye haki ili kupokea sifa, ushawishi na utajiri wa ulimwengu, na wakati huo huo wakiwakandamiza watu ambao wangepaswa kuwabariki” (“Katika Kuwa Wakweli,” Liahona, Mei 2015, 81).

Katika Mathayo 23, Mwokozi alitumia sitiari kadhaa kuelezea unafiki. Fikiria kuwekea alama au kuorodhesha sitiari hizi na kuandika zinafundisha nini kuhusu unafiki. Kuna tofauti gani kati ya unafiki na udhaifu wa kibinadamu ambao wote tunaupata tunapojaribu kuishi injili? Je, wewe unashawishika kufanya nini tofauti kwa sababu ya mafundisho ya Mwokozi?

Ona pia Kamusi ya Biblia, “Mnafiki.”

Mathayo 21:1–11; Marko 11:1–11; Luka 19:29–44; Yohana 12: 1– 8, 12–16

Yesu Kristo ni Mfalme wangu

Wakati Yesu alipowasili Yerusalemu siku chache tu kabla Yeye hajakamilisha Upatanisho Wake, wale waliomtambua kama Mfalme wao walionyesha kujitoa kwao kwa kumpaka mafuta, kutandaza nguo na matawi ya mitende katika njia Yake ya kuingia Yerusalemu, na wakipiga kelele za sifa. Fikiria jinsi gani taarifa hizi zinavyoweza kuongeza uelewa wako wa matukio haya, ambayo yalianza wiki ya mwisho ya maisha ya Mwokozi.

  • Mfano wa kale wa kumpaka mafuta mfalme: 2 Wafalme 9:1–6, 13

  • Unabii wa kale wa kuingia kwa shangwe: Zakaria 9:9

  • Maana ya neno hosana: “Hosana” katika Mwongozo wa Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org)

  • Unabii kuhusu jinsi Mwokozi atakavyokuja tena: Ufunuo 7:9–12

Je, ni kwa jinsi gani unaweza kumheshimu na kumpokea Mwokozi kama Bwana na Mfalme wako?

Ona pia Gerrit W. Gong, “Hosana na Haleluya—Yesu Kristo Aliye Hai: Kiini cha Urejesho na Pasaka,” Liahona, Mei 2020, 52–55; “The Lord’s Triumphal Entry into Jerusalem” (video), ChurchofJesusChrist.org.

Mathayo 22:34–40

Amri mbili kuu ni kumpenda Mungu na kuwapenda wengine kama nafsi yangu.

Kama umewahi kuhisi kushindwa unapojitahidi kumfuata Yesu Kristo, maneno ya Mwokozi kwa mwanasheria katika Mathayo 22 yanaweza kukusaidia kurahisisha na kufokasi ufuasi wako. Hii ni njia mojawapo ya kufanya hili: Tengeneza orodha ya amri kadhaa za Bwana. Je, ni kwa jinsi gani kila amri katika orodha yako huunganika kwenye amri kuu mbili? Je, ni kwa jinsi gani kufokasi kwenye amri hizi kuu mbili hukusaidia kushika hizo zingine?

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Mathayo 21:12–14.Ni kwa jinsi gani maneno na vitendo vya Yesu katika Mathayo 21:12–14 huonyesha jinsi Yeye anavyohisi kuhusu hekalu? Ni kwa jinsi gani tunaonyesha jinsi tunavyohisi kuhusu hekalu? Tunaweza “kufukuza” nini (mstari wa 12) kutoka katika maisha yetu ili kufanya nyumba yetu kuwa zaidi kama hekalu? Fikirieni kuimba pamoja wimbo kuhusu hekalu, kama vile “I Love to See the Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95).

Mathayo 21:28–32.Je, ni masomo gani kutoka kwenye fumbo la mtu mwenye wana wawili yanaweza kuisaidia familia yako? Kwa mfano, unaweza kutumia hadithi kujadili umuhimu wa utiifu wa dhati na toba. Pengine familia yako inaweza kuandika fumbo hili kama muswada wa mchezo wa kuigiza na kupeana zamu kuigiza majukumu tofauti.

Mathayo 22:15–22; Luka 20:21–26..Watoto wanaweza kufurahia kutengeneza mifano ya sarafu ikiwa na “sura na anwani” juu yake. Wangeweza kuandika nyuma ya sarafu baadhi ya “vitu ambavyo ni vya Mungu” (Mathayo 22:21) ambavyo tunapaswa kumpa. Ungeweza pia kuzungumza kuhusu kile inachomaanisha kuwa na “sura na anwani” ya Mwokozi juu yetu (Mathayo 22:20; ona pia Mosia 5:8; Alma 5:14).

Yohana 12:1–8.Je, ni kwa jinsi gani Mariamu alionyesha upendo wake kwa Mwokozi? Je, ni kwa jinsi gani sisi tunaonyesha upendo wetu Kwake?

Picha
mwanamke akipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake

Kuosha Miguu ya Yesu, na Brian Call

Yohana 12:42–43.Je, ni matokeo gani ya kijamii wakati mwingine hutuvunja moyo kuelezea au kutetea imani yetu katika Kristo? Kwa ajili ya mifano ya watu ambao hawakukubali kushindwa na shinikizo la kijamii, ona Danieli 1:3–20; 3; 6; Yohana 7:45–53; 9:1–38; na Mosia 17:1–4. Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha heshima kwa wengine pale wanapoelezea au kutetea imani zao za kidini?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa “Rejoice, the Lord Is KingNyimbo za Dini, na. 66.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia sanaa kuwashirikisha wanafamilia.Kitabu cha Sanaa za Injili na Gospel Media Library kwenye ChurchofJesusChrist.org vina picha nyingi na video ambazo zinaweza kuisaidia [familia yako] kujenga taswira za dhana au matukio haya” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi22).

Picha
Kuingia kwa shangwe kwa Kristo

Kuingia kwa Shangwe, na Walter Rane

Chapisha