Agano Jipya 2023
Mei 29–Juni 4. Mathayo 26; Marko 14; Yohana 13: “Kwa Ukumbusho”


“Mei 29–Juni 4. Mathayo 26; Marko 14; Yohana 13: ‘Kwa Ukumbusho’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya (2023)

“Mei 29–Juni 4. Mathayo 26 ; Marko 14; Yohana 13,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023

Karamu ya Mwisho

Kwa Ukumbusho Wangu, na Walter Rane

Mei 29–Juni 4.

Mathayo 26; Marko 14; Yohana13

“Kwa Ukumbusho”

Unaposoma matukio yaliyoelezewa katika Mathayo 26; Marko 14; Yohana 13; tilia maanani misukumo yoyote unayopokea, hasa misukumo ambayo inaongeza imani yako katika Yesu Kristo na msimamo wako Kwake.

Andika Misukumo Yako

Siku moja kabla ya Yeye kufariki, Yesu aliwapa wanafunzi wake kitu cha kumkumbukia Yeye. Yeye “alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, na akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki kwa maana hii ndiyo damu yangu” (Mathayo 26:26–28).

Hili lilitokea karibia miaka 2,000 iliyopita, katika mahali ambapo sisi kamwe hatutapaona, katika lugha wachache wetu wanaweza kuelewa. Lakini sasa, kila Jumapili katika sehemu zetu wenyewe za mikutano, wenye ukuhani, walioidhinishwa kutenda katika jina la Yesu Kristo, hufanya kile Yeye alichofanya wakati fulani. Wanachukua mkate na maji, wanavibariki, na kumpatia kila mmoja wetu, wafuasi Wake. Ni tendo rahisi—je, kunaweza kuwa na chochote kilicho rahisi zaidi, cha msingi zaidi, kuliko kula mkate na kunywa maji? Lakini mkate na maji hayo ni vitakatifu kwetu kwa sababu hutusaidia kumkumbuka Yeye. Ndiyo njia yetu ya kusema, “Kamwe sitamsahau Yeye”—sio tu, “Kamwe sitasahau kile nilichosoma kuhusu mafundisho Yake na maisha Yake.” Bali, tunasema, “Kamwe sitasahau kile Yeye alichonifanyia mimi.” “Kamwe sitasahau jinsi Yeye alivyoniokoa wakati nilipolia ili nisaidiwe.” “Na kamwe sitasahau msimamo Wake kwangu na msimamo wangu Kwake— agano tulilofanya.”

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mathayo 26:6–13; Marko 14:3–9

“Ametangulia … kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.”

Kwa tendo la unyenyekevu la kuabudu, mwanamke aliyeelezewa katika mistari hii alionyesha kwamba alijua Yesu alikuwa nani na kile Yesu alichokuwa karibu kukifanya (ona Mathayo 26:12). Kwa nini unadhani matendo yake yalikuwa na maana sana kwa Mwokozi? (ona mstari wa 13). Ni nini kinachokuvutia kuhusu mwanamke huyu na imani yake? Tafakari jinsi unavyoweza kufuata mfano wake.

Ona pia Yohana 12:1–8.

Mathayo 26:20–22; Marko 14:17–19

Bwana, ni mimi?”

Unajifunza nini kuhusu wanafunzi kutokana na swali hili kwa Bwana katika mistari hii? Unafikiri ni kwa nini waliuliza hivi? Fikiria jinsi ambavyo ungeweza kumuuliza Bwana, “Ni mimi?

Ona pia Dieter F. Uchtdorf, “Bwana, Ni Mimi?,” Liahona, Nov. 2014, 56–59.

Mathayo 26:26–29; Marko 14:22–25

Sakramenti ni fursa ya kumkumbuka Mwokozi.

Wakati Mwokozi alipoanzisha sakramenti kwa wanafunzi Wake, ni mawazo gani na hisia gani unafikiri wanafunzi walikuwa nazo? Fikiria kuhusu hili unaposoma kuhusu uzoefu wao katika Mathayo 26:26–29 na Marko 14:22–25. Kwa nini unafikiri Yesu alichagua njia hii kwa ajili yetu ili kumkumbuka Yeye? Ungeweza pia kutafakari uzoefu ulioupata wakati wa sakramenti. Kuna chochote ambacho ungeweza kufanya ili kuufanya uzoefu wako kuwa mtakatifu zaidi na wa maana zaidi?

Baada ya kusoma na kutafakari mistari hii, ungeweza kuandika baadhi ya mambo unayohisi kuongozwa kukumbuka kuhusu Mwokozi. Ungeweza kurejelea mambo hayo wakati mwingine utakapokuwa unapokea sakramenti. Ungeweza pia kupitia tena wakati mwingine, kama njia ya “daima kumkumbuka” (Moroni 4:3).

Ona pia Luka 22:7–39; 3 Nefi 18:1–13; Mafundisho na Maagano 20:76–79; Mada za Injili, “Sakramenti,” topics.ChurchofJesusChrist.org; “Always Remember Him” (video), ChurchofJesusChrist.org.

Yohana 13:1–17

Mwokozi ni mfano wetu wa kuhudumia wengine kwa unyenyekevu.

Katika wakati wa Yesu, kuosha miguu ya mtu mwingine ilikuwa wajibu wa watumishi, wala si viongozi. Lakini Yesu alitaka wanafunzi Wake wafikiri katika njia tofauti kuhusu kile ilichomaanisha kuongoza na kutumikia. Ni jumbe gani unazipata katika maneno na matendo ya Mwokozi katika Yohana 13:1–17? Katika utamaduni wako, kuosha miguu ya wengine inaweza kuwa si desturi ya kutumikia. Lakini fikiria kile unachoweza kufanya ili kufuata mfano wa Mwokozi wa huduma ya unyenyekevu.

Ingeweza pia kuwa ya kuvutia kutambua mambo ambayo Yesu aliyajua na kuyahisi wakati wa sakramenti hii pamoja na Mitume Wake. (ona mstari 1 na 3). Je, umaizi huu unakusaida kuelewa nini kuhusu Mwokozi?

Ona pia Luka 22:24–27.

Yohana 13:34–35

Upendo wangu kwa wengine ni ishara kwamba mimi ni mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.

Mwanzo, Yesu alitoa amri ya “Mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 22:39). Sasa Yeye ametupatia “amri mpya.” Unafikiri inamaanisha nini kuwapenda wengine kama Yesu anavyokupenda wewe? (ona Yohana 13:34).

Ungeweza pia kutafakari jinsi watu wengine wanavyojua kwamba wewe ni mfuasi wa Yesu Kristo. Ni kwa jinsi gani unaweza kuhakikisha kwamba upendo ndiyo sifa yako inayokutambulisha kama Mkristo.

ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Mathayo 26:26–29; Marko 14:22–25.Je, ni upi uzoefu wa familia yako wakati wa sakramenti kila wiki? Kusoma kuhusu sakramenti ya kwanza kunaweza kuleta mwongozo wa majadiliano kuhusu umuhimu wa sakramenti na njia za kuboresha uzoefu wako. Fikiria kuonyesha picha Kupitisha Sakramenti (Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 108) na kushiriki mawazo kuhusu kile mnachoweza kufanya kabla, wakati wa, na baada ya sakramenti.

mwanamke akipokea sakramenti

Sakramenti inatusaidia kumkumbuka Yesu Kristo.

Mathayo 26:30.Fikiria kuimba wimbo, kama Yesu na Mitume Wake walivyofanya—pengine nyimbo za sakramenti. Ni kwa jinsi gani kuimba wimbo wa kanisa kungeweza kuwa baraka kwa Yesu na Mitume Wake wakati huo? Ni kwa jinsi gani nyimbo za kanisa ni baraka kwetu sisi?

Yohana 13:1–17.Unaweza kutaka kuionyesha familia yako picha iliyo mwisho wa muhtasari huu wakati unaposoma mistari hii. Ni kweli gani Mwokozi alifundisha kwa matendo Yake? Ni maelezo gani ya kina katika picha hii hutusaidia kuelewa kweli hizi? Pengine wanafamilia wangeweza kushiriki jinsi ambavyo kuishi kweli hizi kumewaletea furaha (ona Yohana 13:17).

Yohana 13:34–35.Baada ya kusoma mistari hii, wangeweza kuzungumza pamoja kuhusu jinsi watu wengine wanavyojua kwamba ninyi ni wafuasi wa Yesu Kristo. Ni kwa jinsi gani Mwokozi anataka wafuasi Wake wajulikane? Unaweza kuwaomba wanafamilia kuzungumza kuhusu watu ambao upendo wao kwa wengine huonyesha kwamba wao ni wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Mngeweza pia kujadili njia ambazo kwazo mngeweza kuonyesha upendo zaidi kama familia.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Love One Another,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,136.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Tafakari. Maandiko yana maana za kiroho ambazo tunaweza kuzikosa kama tunasoma bila kuwa makini, kama tunavyosoma taarifa nyinginezo. Usiwe na haraka ya kumaliza sura. Chukua muda kufikiria kwa kina kuhusu kile unachosoma.

Yesu akiosha miguu ya wanafunzi

Mkuu katika Ufalme, na J. Kirk Richards