Agano Jipya 2023
Juni 19–25. Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19: “Imekwisha”


“Juni 19–25. Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19: ‘Imekwisha’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya (2023)

“Juni 19–25. Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Kristo mbele ya Pilato

Ecce Homo, na Antonio Ciseri

Juni 19–25

Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19

“Imekwisha”

Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; na Yohana 19 zinajumuisha maelezo ya saa za mwisho za maisha ya Mwokozi duniani. Tafuta kuhisi upendo Wake kwako unapojifunza kuhusu dhabihu Yake na kifo Chake.

Andika Misukumo Yako

Katika kila neno na tendo, Yesu Kristo alionyesha mfano wa upendo safi—kile Mtume Paulo alichokiita hisani (ona 1 Wakorintho 13). Hakuna muda hili lilikuwa wazi zaidi kuliko wakati wa saa za mwisho za maisha ya Mwokozi duniani. Utulivu wake wa heshima mbele ya mashitaka ya uongo uliashiria kwamba Yeye “hauoni uchungu” (1 Wakorintho 13:5). Utayari Wake kuvumilia mijeledi, mzaha, na kusulubiwa—hali akizuia nguvu Zake kusitisha mateso Yake—ilionyesha kwamba Yeye “alivumilia yote” na “kustahimili yote” (1 Wakorintho 13:4, 7). Huruma Yake kwa mama Yake na rehema Zake kwa watesi Wake—hata katika maumivu Yake yasiyo na kifani—ilionyesha kwamba Yeye “hakutafuta mambo [Yake] mwenyewe” (1 Wakorintho 13:5). Katika nyakati Zake za mwisho duniani, Yesu alikuwa akifanya kile alichokifanya katika huduma Yake yote ya duniani—kutufundisha kwa kutuonyesha. Hakika, hisani ni “upendo msafi wa Kristo” (Moroni 7:47).

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19

Utayari wa Yesu Kristo kuteseka unaonyesha upendo Wake kwa Baba na kwetu sisi sote.

Japokuwa Mwokozi alikuwa na nguvu ya kushusha chini “majeshi ya malaika” (Mathayo 26:53), Yeye kwa hiari alichagua kuvumilia hukumu zisizo za haki, mzaha wa kikatili, na maumivu ya mwili yasiyofikirika. Je, kwa nini alifanya hivyo? “Kwa sababu ya upendo Wake mkarimu,” Nefi alishuhudia, “na uvumilivu wake kwa watoto wa watu” (1 Nefi 19:9).

Kristo akibeba msalaba

“Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka … Golgotha” (Yohana 19:17).

Unaweza kuanza kujifunza kwako juu ya saa za mwisho za Mwokozi kwa kusoma 1 Nefi 19:9. Je, ni wapi katika Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; na Yohana 19 unapata mifano ya kila jambo ambalo Nefi alisema kuwa Yesu angeteseka?

  • “[Wao] wanamhukumu kuwa kitu cha bure”

  • “Wanampiga mijeledi”

  • “Wanampiga”

  • “Wanamtemea mate”

Je, ni vifungu gani hukusaidia kuhisi “upendo mkarimu” wa Mwokozi kwako wewe? Je, ni fikra au mawazo gani mengine unakuwa nayo unaposoma hadithi hizi? Fikiria kuyaandika au kuyashiriki na mtu mwingine.

Ona pia video “Jesus Is Condemned before Pilate” na “Jesus Is Scourged and Crucified,” ChurchofJesusChrist.org.

Mathayo 27:27–49,54; Marko 15:16–32; Luka 23:11, 35–39; Yohana 19:1–5

Mzaha hauwezi kubadili ukweli.

Wakati Yesu alivumilia mzaha katika huduma Yake yote, ulikuwa mkali zaidi wakati wa kupigwa Kwake mijeledi na Kusulubiwa. Lakini mzaha huu haungeweza kubadilisha ukweli: Yesu ni Mwana wa Mungu. Unaposoma kuhusu udhalilishaji Yesu aliovumilia, fikiria kuhusu upinzani na mzaha uliopo kwenye kazi Yake leo. Je, ni utambuzi gani unaupata kuhusu kuvumilia upinzani? Je, ni kitu gani kinakuvutia kuhusu maneno ya akida katika Mathayo 27:54?

Mathayo 27:46; Marko 15:34

Yesu Kristo aliteseka peke yake ili mimi nisiteseke.

Katika moja ya nyakati Zake ngumu msalabani, Yesu, ambaye alikuwa daima amemtegemea Baba Yake wa Mbinguni, ghafla alihisi kutelekezwa. Kusoma kuhusu hili kungeweza kukuongoza kuhusu nyakati ambapo ulihisi kuwa mbali na Mungu. Ungeweza kufikiria jinsi ambavyo dhabihu ya Mwokozi msalabani hufanya iwezekane kwako kushinda umbali huo. Kama Mzee Jeffrey R. Holland alivyoshuhudia, “Kwa sababu Yesu alitembea njia hiyo ndefu ya upweke kabisa peke yake, sisi hatuhitaji kufanya hivyo. … Ukitangazwa kutoka kilele cha Kalvari ni ukweli kwamba kamwe hatutaachwa peke yetu wala bila msaada, hata kama wakati mwingine tunaweza kuhisi kuwa tumeachwa” (“Hakuna Aliyekuwa pamoja Naye,” Liahona, Mei 2009, 88). Fikiria jinsi Mwokozi anavyoweza kukusaidia kushinda upweke unaposoma ujumbe wote wa Mzee Holland.

Luka 23:34

Mwokozi ndiye mfano wetu wa msamaha.

Je, unajisikiaje unaposoma maneno ya Mwokozi katika Luka 23:34? (Ona umaizi uliotolewa kwa Tafsiri ya Joseph Smith katika tanbihi c). Akirejelea maneno ya Mwokozi, Rais Henry B. Eyring alifundisha: “Tunalazimika kusamehe na kutoweka kinyongo dhidi ya wale wanaotukwaza. Mwokozi alionyesha mfano kutoka msalabani. … Sisi hatujui mioyo ya wale wanaotukwaza” (“That We May Be One,” Ensign, Mei 1998, 68). Je, ni kwa jinsi gani mstari huu hukusaidia kama ukiwa na tatizo la kumsamehe mtu?

ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19Ili kuisaidia familia yako kujifunza kuhusu matukio yaliyoelezewa katika sura hizi, ungeweza kushiriki nao “Sura ya 52: Majaribu ya Yesu” na (Sura ya 53: Yesu Amesulubiwa” (katika Hadithi za Agano Jipya, 133–38, au video zinazohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Au mngeweza kutazama pamoja video zinazoonyesha matukio haya: “Jesus Is Condemned before Pilate” na “Jesus Is Scourged and Crucified” (ChurchofJesusChrist.org). Ungeweza kuwaalika watoto kusimulia hadithi hizi kwa maneno yao wenyewe. Wanafamilia wangeweza kushiriki jinsi wanavyohisi kuhusu Mwokozi kwa sababu ya kile Yeye alichoteseka kwa ajili yetu.

Mathayo 27:11–26; Marko 15:1–15; Luka 23:12–25; Yohana 19:1–16Je, ni kwa nini Pilato alimtoa Yesu asulubiwe, japokuwa alijua kuwa Yesu hakuwa na hatia? Je, ni masomo gani tunayojifunza kutokana na uzoefu wa Pilato kuhusu kusimamia kile tunachojua ni sahihi? Ingeweza kuwa yenye msaada kwa familia yako kuigiza-matukio ambayo huwapa nafasi ya kujaribu kusimamia kile ambacho ni sahihi.

Mathayo 27:46; Luka 23:34, 43, 46; Yohana 19:26–28, 30Pengine unaweza kumpangia kila mwanafamilia kusoma moja au zaidi ya kauli za Mwokozi alizozisema msalabani, zinazopatikana katika mistari hii. Waombe washiriki kile walichojifunza kutokana na maelezo haya kuhusu Mwokozi na misheni Yake.

Marko 15:39.Je, ni kwa jinsi gani kusoma kuhusu Kusulubiwa kumeimarisha ushuhuda wako kwamba Yesu ni “Mwana wa Mungu”?

Yohana 19:25–27.Je, tunajifunza nini kutoka katika mistari hii kuhusu jinsi tunavyoweza kuwapenda na kuwasaidia wanafamilia?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa “Upon the Cross of Calvary,” Nyimbo za Kanisa, na. 184.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Iga Maisha ya Mwokozi. “Inasaidia kujifunza njia ambazo Mwokozi alifundisha—mbinu alizotumia na mambo ambayo Yeye aliyasema. Kwani nguvu za Mwokozi za kufundisha na kuwainua wengine zilikuja kutokana na jinsi alivyoishi na aina ya mtu Aliyekuwa. Kadiri unavyojitahidi kwa bidii kuishi kama Yesu Kristo, ndivyo utakavyoweza zaidi kufundisha kama Yeye” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi13).

Kristo msalabani

Kristo Msalabani, na Carl Heinrich Bloch