“Juni 26–Julai 2. Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; Yohana 20–21: ‘Amefufuka’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Juni 26–Julai 2. Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; Yohana 20–21,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Juni 26–Julai 2
Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; Yohana 20–21
“Amefufuka”
Kwa maombi soma Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; na Yohana 20–21, ukikumbuka furaha uliyonayo kwa sababu ya Ufufuko wa Kristo. Ni nani anaweza kubarikiwa kwa kusikia ushuhuda wako juu ya tukio hili?
Andika Misukumo Yako
Kwa waangalizi wengi, kifo cha Yesu wa Nazareti kingeliweza kuonekana kama mwisho wa mzaha kwa maisha ya kusifika. Je, huyu siye mtu aliyemfufua Lazaro kutoka kwa wafu? Je, sisi Yeye alistahamili vitisho vya mauaji kutoka kwa Mafarisayo kila mara? Alionyesha nguvu ya kuponya upofu, ukoma, na kupooza. Hata pepo na bahari vilimtii Yeye. Na sasa yuko hapa, akining’inia msalabani, akitangaza, “Imekwisha” (Yohana 19:30). Yaweza kuwa kulikuweko na mshangao wa dhati katika maneno ya kejeli “Aliokoa wengine; hawezi kujiokoa mwenyewe” (Mathayo 27:42). Lakini tunajua kwamba kifo cha Yesu haikuwa mwisho wa yote. Tunajua kwamba ukimya wa kaburi ulikuwa wa muda na kwamba kazi ya Kristo ya kuokoa ilikuwa ndiyo kwanza imeanza. Leo anapatikana si “miongoni mwa wafu” bali miongoni mwa walio hai (Luka 24:5). Mafundisho Yake hayakuweza kunyamazishwa, kwani wanafunzi Wake waaminifu wangeihubiri injili kwa “mataifa yote,” wakiamini ahadi Yake kwamba atakuwa “pamoja [nao] daima, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:19–20).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; Yohana 20
Yesu Kristo alifufuka.
Katika vifungu hivi, utasoma kuhusu moja ya matukio muhimu sana katika historia ya mwanadamu: Ufufuko wa Yesu Kristo. Unaposoma, jiweke katika nafasi ya watu walioshuhudia matukio yaliyozunguka Ufufuko. Je, unajifunza nini kutokana na uzoefu wao?
Je, wewe unajisikiaje unaposoma kuhusu Ufufuko wa Mwokozi? Fikiria jinsi gani ulivyokugusa—mtazamo wako juu ya maisha, uhusiano wako, imani yako katika Kristo, na imani yako katika kweli zingine za injili.
Ona pia Kamusi ya Biblia, “Ufufuko”; Mada za Injili, “Ufufuko,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
Naweza kumwalika Mwokozi “kukaa pamoja [nami].”
Unaposoma tukio la wale wafuasi wawili waliokuwa wakisafiri ambao walikutana na Mwokozi aliyefufuka, tafuta kulingalisha na matukio yako wewe kama mfuasi wa Kristo. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kutembea Naye leo na kumualika “kukaa” kwa muda zaidi na wewe? (Luka 24:29). Je, ni kwa jinsi gani unatambua uwepo Wake katika maisha yako? Ni kwa njia zipi Roho Mtakatifu ameshuhudia juu ya uungu wa Yesu Kristo kwako?
Ona pia “Abide with Me; ’Tis Eventide,” “Abide with Me!,” Nyimbo za Kanisa, na. 165–66.
Ufufuko ni kuunganika tena kwa hali ya kudumu kwa roho na mwili.
Hadithi juu ya Ufufuko wa Yesu Kristo inaweza kukusaidia kuelewa kile inachomaanisha kufufuka. Kwa mfano, ni kweli zipi unazozipata katika Luka 24:36–43 na Yohana 20 kuhusu miili iliyofufuka? Ungeweza pia kuchambua maandiko mengine kuhusu ufufuko, kama vile 1 Wakorintho 15:35–44; Wafilipi 3:20–21; 3 Nefi 11:13–15; Mafundisho na Maagano 88:27–31; 110:2–3; 130:1, 22.
“Wa heri wale wasioona, wakasadiki.”
Baadhi ya watu wanahisi kuwa kama Tomaso, ambaye alisema, “Mimi nisipoziona … Mimi sisadiki hata kidogo” (Yohana 20:25). Kwa maoni yako, kwa nini kusadiki bila kuona kunaweza kuwa baraka? (Ona Yohana 20:29). Tafakari jinsi ambavyo umebarikiwa kwa kuamini katika mambo ya kiroho ambayo hujayaona. Je, ni kitu gani kinachokusaidia wewe kuwa na imani katika Mwokozi hata wakati humuoni? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuendelea kuimarisha imani yako katika “vitu visivyoonekana, ambavyo ni vya kweli”? (ona Alma 32:16–21; Etheri 12:6). Fikiria kuandika katika shajara mambo ambayo yamekusaidia wewe kuamini katika Yesu Kristo, au ushiriki na mtu unayemjua.
Mwokozi hunialika kuwalisha kondoo Wake.
Inaweza kuwa ya kuvutia kulinganisha mchangamano wa Mwokozi na Mitume Wake katika Yohana 21 na mara ya kwanza Alipowaamuru kuacha nyavu zao, ilivyoandikwa katika Luka 5:1–11. Je, ni mifanano na tofauti zipi unazipata? Je, ni umaizi gani unaupata kuhusu ufuasi?
Fikiria jinsi gani maneno ya Mwokozi kwa Petro katika Yohana 21:15–17 yanaweza kutumika kwako. Je, kuna kitu kinachokurudisha nyuma kwenye kuwatumikia kondoo wa Bwana? Je, jibu lako lingekuwaje kama Bwana angekuuliza “Je, wanipenda?” Tafakari jinsi unavyoweza kuonyesha upendo wako kwa Bwana.
Ona pia 1 Petro 5:2–4, 8; Jeffrey R. Holland, “Amri Kuu ya Kwanza,” Liahona, Nov. 2012, 83–85.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Luka 24:5–6.Rais Thomas S. Monson alisema juu ya Luka 24:5–6, “Hakuna maneno katika Ukristo yanayotoa uelewa zaidi kwangu kama hayo” (“Amefufuka!,” Liahona, Mei 2010, 89). Je, maneno haya yana maana gani kwako na kwa familia yako?
-
Mathayo 28; Marko 16; Luka 24; Yohana 20–21.Familia yako inaposoma sura hizi, watambueni watu waliojihusisha na Yesu katika kila hadithi. Kwa mfano, ni nini kinakuvutia kuhusu watu waliomtembelea Mwokozi kaburini? Ni nini unajifunza kutokana na maneno au matendo ya Mitume au wale wafuasi katika barabara ya kwenda Emau?
Fikirieni kuimba pamoja “Did Jesus Really Live Again?”(Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 64). Zungumzeni kuhusu mtu ambaye familia yako inamjua kwamba ameshafariki, na mjadili jinsi kweli katika wimbo huu unavyoleta faraja.
-
Mathayo 28:16–20; Marko 16:14–20; Luka 24:44–53.Katika mistari hii, Yesu alikuwa akiwaomba Mitume Wake wafanye nini? Je, ni kwa jinsi gani sisi tunaweza kusaidia kutimiza kazi hii? Wanafamilia wangeweza kuelezea uzoefu ambapo wao walihisi “Bwana akifanya kazi pamoja nao” ili kutimiza madhumuni Yake (Marko 16:20).
-
Yohana 21:15–17.Fikirieni kusoma mistari hii wakati mkila pamoja. Hii inaweza kuongeza maana kwenye maneno ya Mwokozi “lisha kondoo wangu.” Kulingana na kile ambacho Yesu alifundisha kuhusu kondoo katika Agano Jipya (ona, kwa mfano, Mathayo 9:35–36; 10:5–6; 25:31–46; Luka 15:4–7; Yohana 10:1–16), kwa nini kulisha kondoo ni njia nzuri ya kuelezea kuwahudumia watoto wa Mungu? Je, sitiari hii hufundisha nini kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni na Yesu wanavyohisi kutuhusu sisi?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa. “Did Jesus Really Live Again?,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 64.