“Julai 17–23. Matendo ya Mitume 10–15: ‘Neno la Mungu Likazidi na Kuenea’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Julai 17–23. Matendo ya Mitume 10–15,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Julai 17–23
Matendo ya Mitume 10–15.
“Neno la Mungu Likazidi na Kuenea”
Soma Matendo ya Mitume 10–15 kwa makini, ukitoa muda kwa Roho kukushawishi kwa mawazo na hisia. Je, kuna nini kwako cha kujifunza katika sura hizi?
Andika Misukumo Yako
Wakati wa huduma Yake katika mwili wenye kufa, Yesu Kristo kila mara alipingana na tamaduni na imani za watu walizokuwa wameshikilia kwa muda mrefu. Hii haikwisha baada ya kupaa Kwake mbinguni, Yeye aliendelea kuliongoza Kanisa Lake kwa ufunuo. Kwa mfano, wakati wa uhai wa Yesu Kristo wanafunzi Wake waliihubiri injili kwa Wayahudi wenzao tu. Lakini punde baada ya Mwokozi kufa na Petro kuwa kiongozi wa Kanisa, Yesu Kristo alimfunulia Petro kwamba muda ulikuwa umefika kwa injili kuhubiriwa kwa wasio Wayahudi. Wazo la kushiriki injili na Wayunani halionekani la kushangaza leo, hivyo, ni somo gani sisi tunajifunza katika tukio hili? Pengine somo moja ni kwamba katika Kanisa la kale na la sasa, Mwokozi mwenye upendo huwaongoza viongozi Wake wateule (ona Amosi 3:7; Mafundisho na Maagano 1:38). Ufunuo endelevu ni ishara muhimu ya Kanisa la kweli na lililo hai la Yesu Kristo. Kama Petro, ni lazima tuwe tayari kukubali ufunuo endelevu na kuishi “kwa kila neno la Mungu” (Luka 4:4), ikijumuisha “yale yote ambayo [Yeye] ameyafunua, na ambayo sasa anayafunua” na “mambo mengi makuu na muhimu” Yeye atakayoyafunua “yahusuyo ufalme wa Mungu” (Makala ya Imani 1:9).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
“Mungu hana upendeleo.”
Kwa vizazi kadhaa, Wayahudi walikuwa wameamini kwamba kuwa wa “viuno vya Ibrahimu,” au uzao halisi wa nasaba ya Ibrahimu, ilimaanisha kwamba mtu alikuwa amekubaliwa na kuteuliwa na Mungu (ona Luka 3:8). Mtu mwingine yeyote alichukuliwa kama Myunani “mchafu” ambaye hakukubaliwa na Mungu. Katika Matendo ya Mitume 10, Bwana alimfundisha nini Petro kuhusu nani “anakubaliwa na Yeye”? (Matendo ya Mitume 10:35). Ni ushahidi gani unapata katika sura hii kwamba maisha ya Kornelio yalikubalika kwa Bwana? Tafakari ilimaanisha nini kwa maelezo ya “Mungu hana upendeleo” (mstari wa 34; ona pia 1 Nefi 17:13). Kwa nini ni muhimu kwako kujua ukweli huu?
Kama Wayahudi walivyowadharau wale ambao hawakuwa wa ukoo wa Ibrahimu, je, umewahi kujikuta ukiwaza mawazo yasiyo mema au yasiyo ya kweli kuhusu mtu ambaye yuko tofauti na wewe? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kushinda mazoea haya? Inaweza kuwa ya kuvutia kujaribu shughuli rahisi kwa siku chache zijazo: Wakati wowote unapojumuika na mtu, jaribu kufikiria mwenyewe, “Mtu huyu ni mtoto wa Mungu.” Unapofanya hivi, ni mabadiliko yapi unayagundua katika jinsi ya kuwafikiria na kujumuika na wengine?
Ona pia 1 Samweli 16:7; 2 Nefi 26:13, 33; Russell M. Nelson, “Acha Mungu Ashinde,” Liahona, Nov. 2020, 92–95; “Peter’s Revelation to Take the Gospel to the Gentiles” (video), ChurchofJesusChrist.org.
Matendo ya Mitume 10; 11:1–18; 15
Baba wa Mbinguni hunifundisha mstari juu ya mstari kwa njia ya ufunuo.
Wakati Petro alipoona ono lililoelezwa katika Matendo ya Mitume 10, mwanzo alihangaika kulielewa na “aliona shaka ndani ya nafsi yake juu ya [ono] lilipasa kumaanisha nini” (mstari wa 17). Lakini bado Bwana alimpa Petro uelewa mkubwa pale Petro alipoutafuta. Unaposoma Matendo ya Mitume 10, 11, na 15, gundua ni kwa jinsi gani uelewa wa Petro juu ya ono lake uliongezeka baada ya muda. Ni kwa jinsi gani umetafuta na kupata uelewa mkubwa kutoka kwa Mungu ulipokuwa na maswali?
Matendo ya Mitume 10, 11, na 15 husimulia nyakati ambazo Bwana aliwaongoza watumishi Wake kupitia ufunuo. Inaweza kusaidia kuandika kile unachojifunza kuhusu ufunuo unaposoma sura hizi. Ni kwa njia zipi Roho husema nasi?
Ona pia Mada za Injili, “Ufunuo,” topics.ChurchofJesusChrist.org; Quentin L. Cook, “Baraka za Ufunuo Unaoendelea kwa Manabii na Ufunuo Binafsi ili Kuongoza Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2020, 96–100; “The Jerusalem Conference” (video), ChurchofJesusChrist.org.
Mimi ni Mkristo kwa sababu ninamwamini na kumfuata Yesu Kristo.
Ni nini cha kipekee kuhusu mtu kuitwa Mkristo? (ona Matendo ya Mitume 11:26). Inamaanisha nini kwako kujulikana kama Mkristo? Fikiria upekee wa majina. Kwa mfano, jina la familia yako linamaanisha nini kwako? Kwa nini jina la Kanisa ni muhimu kwako? (ona Mafundisho na Maagano 115:4). Inamaanisha nini kwako kujichukulia juu yako mwenyewe jina la Yesu Kristo kwa agano? (ona Mafundisho na Maagano 20:77).
Ona pia Mosia 5:7–15; Alma 46:13–15; 3 Nefi 27:3–8; Russell M. Nelson, “Jina Sahihi la Kanisa,” Liahona, Nov. 2018, 87–90.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Matendo ya Mitume 10:17, 20.Je, tumewahi kupata uzoefu wa kiroho na baadaye kutilia shaka kile tulichohisi au kujifunza? Ni ushauri gani tunaweza kutoa ambao unaweza kutusaidia kuyashinda shaka yetu? Ona Neil L. Andersen, “Kumbukumbu za Kuelekeza Kiroho,” Liahona, Mei 2020, 18–22.
-
Matendo ya Mitume 10:34–35.Ni kwa jinsi gani unaweza kuifundisha familia yako kwamba “Mungu hana upendeleo”? (Matendo ya Mitume 10:34). Pengine ungeweza kuonyesha picha za watu kutoka asili na tamaduli tofauti wakati familia yako ikisoma mistari hii. Ni kwa jinsi gani kweli katika mistari hii zinapaswa kushawishi matendo yako? (Ona, kwa mfano, “I’ll Walk with You” [Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 140–41]).
-
Matendo ya Mitume 12:1–17.Familia yako ingeweza kuigiza tukio la Petro akitupwa gerezani na waumini wa Kanisa wakikusanyika pamoja na kusali kwa ajili yake. Je, ni lini tumewahi kubarikiwa kwa sababu ya sala? Je, kuna mtu yeyote tunahisi kushawishika kumuombea, kama vile kiongozi wa Kanisa au mpendwa wenu? Inamaanisha nini kuomba “bila kukoma”? (Matendo ya Mitume 12:5; ona pia Alma 34:27).
-
Matendo ya Mitume 14.Mnaposoma sura hii pamoja, baadhi ya wanafamilia wanaweza kuandika baraka ambazo zilikuja kwa wafuasi na kwa Kanisa. Wanafamilia wengine wanaweza kuandika upinzani au majaribu waliyopata wafuasi. Kwa nini Mungu huruhusu mambo magumu kuwapata wenye haki?
-
Matendo ya Mitume 15:1–21.Mistari hii huelezea kutokuelewana ndani ya Kanisa kuhusiana na ikiwa waongofu walihitaji kushika sheria ya Musa, ikijumuisha kutahiriwa. Mitume walifanya nini kuhusu kutoelewana huku? Tunaweza kujifunza nini kutokana na mfano huu kuhusu jinsi viongozi wa Kanisa wanavyoelekeza kazi ya Kanisa?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “I’ll Walk with You,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 140–41.