Agano Jipya 2023
Julai 10–16. Matendo ya Mitume 6–9: “Ungetaka Nifanye Nini?”


“Julai 10–16. Matendo ya Mitume 6-9: ‘Ungetaka Nifanye Nini’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)

“Julai 10–16. Matendo ya Mitume 6–9,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Paulo akiwa ameanguka chini

Kuongoka Njiani kwenda Dameski, na Michelangelo Merisi da Caravaggio

Julai 10–16

Matendo ya Mitume 6–9

“Ungetaka Nifanye Nini?”

Anza kwa kusoma Matendo ya Mitume 6–9. Mapendekezo katika muhtasari huu yanaweza kukusaidia kutambua baadhi ya kanuni muhimu katika sura hizi, japokuwa unaweza kupata zingine katika kujifunza kwako mwenyewe.

Andika Misukumo Yako

Kama kuna mtu yeyote aliyeonekana kama mtu asiyewezekana kwa uongofu, yawezekana alikuwa Sauli—Mfarisayo ambaye alikuwa na sifa ya kuwatesa Wakristo. Hivyo Bwana alipomwambia mfuasi aliyeitwa Anania kumtafuta Sauli na kumpa baraka, Anania alikuwa na kusita kunakoeleweka. “Bwana,” alisema, “Nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako” (Matendo ya Mitume 9:13). Lakini Bwana aliujua moyo wa Sauli na uwezekano wake, na Alikuwa na wito akilini kwa ajili ya Sauli: “Huyu ni chombo kiteule kwangu, kulichukua Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo ya Mitume 9:15). Hivyo Anania alitii, na alipompata huyu mtesaji wa zamani, alimuita “Ndugu Sauli” (Matendo ya Mitume 9:17). Kama Sauli aliweza kubadilika kabisa na Anania kuweza kumkaribisha kwa uhuru, je, tunapaswa kumfikiria mtu yeyote kama asiyewezekana kubadilika—ikijumuisha sisi wenyewe?

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Matendo ya Mitume 6–8

Moyo wangu unahitaji kuwa “mnyofu mbele za Mungu.”

Kukua kwa kanisa kulimaanisha kukua kwa hitaji la wafuasi kuhudumu katika ufalme. Kulingana na Matendo ya Mitume 6:1–5, ni sifa zipi Mitume Kumi na Wawili waliangalia kwa wale ambao wangehudumu pamoja nao? Unaposoma Matendo ya Mitume 6–8, gundua jinsi sifa hizi, na zingine, zilivyodhihirishwa katika watu kama Stefano na Filipo. Nini kilipungua kwa Simoni, na nini tunaweza kujifunza kutoka kwake kuhusu kuwa radhi kubadilika?

Je, kuna chochote unahisi kushawishika kukibadilisha ili kuhakikisha kwamba moyo wako ni “mnyofu mbele za Mungu”? (Matendo ya Mitume 8:21–22). Ni kwa jinsi gani kufanya badiliko hili kutakubariki unapomtumikia Mungu?

Matendo ya Mitume 6–7

Kumpinga Roho Mtakatifu kunaweza kusababisha kumkataa Mwokozi na manabii Wake.

Viongozi wa Kiyahudi walikuwa na jukumu la kawaandaa watu kwa ajili ya kuja kwa Masiya. Na bado walishindwa kumtambua Masiya na wakamkataa Yeye. Ni kwa jinsi gani hili lilitokea? Sehemu ya jibu inaweza kupatikana katika maneno ya Stefano: “Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu” (Matendo ya Mitume 7:51). Unafikiri inamaanisha nini kumpinga Roho Mtakatifu? Kwa nini kumpinga Roho Mtakatifu husababisha kumkataa Mwokozi na watumishi Wake?

Unaposoma Matendo ya Mitume 6–7, tafuta jumbe zingine ambazo Stefano aliwafundisha Wayahudi. Alikuwa akionya dhidi ya mitazamo gani? Je, unagundua mitazamo yoyote kama hiyo ndani yako? Je, ni maneno gani ya Stefano hukufundisha kuhusu matokeo ya kumpinga Roho Mtakatifu? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwa mwepesi kuhisi na kuitikia ushawishi wa Roho Mtakatifu katika maisha yako?

Ona pia video ya “The Martyrdom of Stephen” ChurchofJesusChrist.org.

Matendo ya Mitume 8:26–39

Roho Mtakatifu atanisaidia kuwaongoza wengine kwa Yesu Kristo.

Je, unajifunza nini kuhusu kushiriki na wengine injili kutokana na tukio katika Matendo ya Mitume 8:26–39? Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alimsaidia Filipo? Ni kwa jinsi gani kushiriki injili kwa wengine ni kama kuwa kiongozi? (ona Matendo ya Mitume 8:31).

Mzee Ulisses Soares alisema kwamba tukio hili “ni ukumbusho wa agizo la kiungu tulilonalo sote la kutafuta kujifunza na kufundishana sisi kwa sisi injili ya Yesu Kristo. Wakati mwingine sisi ni kama yule mtu wa Kushi—tunahitaji usaidizi wa mwalimu mwaminifu na mwenye mwongozo wa kiungu; na wakati mwingine sisi ni kama Filipo—tunahitaji kufundisha na kuimarisha wengine katika uongofu wao” (“Nawezaje Kuelewa?,” Liahona, Mei 2019, 6). Fikiria kusoma ujumbe wote wa Mzee Soares na kutafakari jinsi Roho Mtakatifu anavyoweza kukusaidia kuwa mwanafunzi bora na mwalimu bora wa injili.

Matendo ya Mitume 9

Ninapojiweka chini ya mapenzi ya Bwana, ninaweza kuwa chombo katika mikono Yake.

Uongofu wa Sauli unaonekana wa ghafla sana; alikwenda haraka sana kutoka kwenye kuwafunga Wakristo mpaka kwenye kumhubiri Kristo katika masinagogi. Unaposoma hadithi yake, tafakari ni kwa nini alikuwa radhi mno kubadilika. (Kusoma maelezo ya Sauli mwenyewe juu ya uongofu wake, ona Matendo ya Mitume 22:1–16 na 26:9–18. Zingatia kwamba katika matukio haya, Sauli alijulikana kwa jina la Paulo [ona Matendo ya Mitume 13:9].)

Wakati ni kweli kwamba tukio la Sauli siyo la kawaida—kwa watu wengi, uongofu ni mchakato mrefu zaidi—je, kuna chochote unachoweza kujifunza kutoka kwa Sauli kuhusu uongofu? Je, unajifunza nini kutokana na jinsi Anania na wafuasi wengine walivyopokea uongofu wa Sauli? Je, utafanya nini ili kutumia mafundisho haya maishani mwako? Unaweza kuanza kwa kuuliza katika maombi, kama Sauli alivyofanya, “Unataka Nifanye Nini?”

Unaposoma Matendo ya Mitume 9:36–42, fikiria jinsi Tabitha alivyokuwa chombo katika mikono ya Mungu. Je, ni kitu gani kinakuvutia wewe kuhusu mfano wake?

Ona pia DieterF. Uchtdorf, “Kusubiri katika Barabara ya Dameski,” Liahona, Mei 2011, 70–77; (video) “The Road to Damascus”, ChurchofJesusChrist.org.

ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Matendo ya Mitume 6:2–8, 7; 7:51–60Linganisha matukio ya Stefano katika Matendo ya Mitume 6:8 na Matendo ya Mitume 7:51–60 na matukio ya Mwokozi katika Luka 23:1–46. Ni kwa jinsi gani Stefano alifuata mfano wa Mwokozi?

Matendo ya Mitume 7:51–60.Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alimbariki Stefano alipokuwa akiteswa? Ni lini tumepokea nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu wakati wa nyakati ngumu?

Matendo ya Mitume 9:5. Mchomo ilikuwa ni mkuki wenye ncha kali uliotumika kuwafukuza wanyama. Kwa kawaida wanyama wangepiga teke kwa nyuma wakati wakichomwa, tendo ambalo lingefanya mkuki kuzama zaidi kwenye mwili wa mnyama. Ni kwa jinsi gani isitiari hii inatuhusu sisi? Tunaweza kufanya nini ili kujiandaa kupokea masahihisho kutoka kwa Bwana?

Petro akimfufua Tabitha kutoka kwa wafu

Tabitha Inuka, na Sandy Freckleton Gagon

Matendo ya Mitume 9:32–43.Fikiria kuwaalika wanafamilia wako kuchora picha za hadithi katika Matendo ya Mitume 9:32–43. Tunajifunza nini kuhusu ufuasi wa kweli kutoka katika hadithi hizi? Ni kwa jinsi gani mtu aliyekuwa “amejaa matendo mema,” kama vile ilivyokuwa kwa Tabitha , huwasaidia wengine kuamini katika Bwana? (ona Matendo ya Mitume 9:36; “Sura ya 60: Petro Anamfufua Tabitha” (katika Hadithi za Agano Jipya, 156–57, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org).

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “I’ll Go Where You Want Me to Go,” Nyimbo za Kanisa, na. 270.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Linganisha maandiko na maisha Yako. Unaposoma, fikiria ni kwa jinsi gani hadithi na mafundisho katika maandiko haya vinatumika katika maisha yako. Kwa mfano, ni fursa zipi unapata za kuwatumikia wengine, kama Tabitha alivyofanya katika Matendo ya Mitume 9:36–39?

Stefano akipigwa mawe hadi kufa

“Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba kwa Mungu, alisema, Bwana Yesu, ipokee roho yangu” (Tafsiri ya Joseph Smith, Matendo ya Mitume 7:59 [katika Matendo ya Mitume 7:59, tanbihi c]).