“Juni 12–18. Luka 22; Yohana 18: ‘Walakini si Mapenzi Yangu, bali Yako Yatendeke.’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Juni 12–18. Luka 22; Yohana 18,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023
Juni 12–18
Luka 22; Yohana 18
“Walakini si Mapenzi Yangu, bali Yako Yatendeke”
Chukua muda wako kusoma Luka 22 na Yohana 18 wiki hii. Tafakari na uombe kuhusu kile ulichosoma. Kufanya hivi kunaweza kumpatia Roho fursa ya kushuhudia katika moyo wako kwamba maandiko ni ya kweli.
Andika Misukumo Yako
Kulikuwa na mashahidi watatu tu wa mateso ya Kristo katika Bustani ya Gethsemane—na walilala kwa kipindi kirefu cha mateso hayo. Katika bustani ile na baadaye msalabani, Yesu alijichukulia juu Yake dhambi, maumivu, na mateso ya kila mtu aliyewahi kuishi, ingawa karibu wote waliokuwa hai kwa wakati huo hakuna hata mmoja aliyejua kilichokuwa kinatokea. Matukio muhimu zaidi na ya milele mara nyingi yanapita bila kutiliwa maanani na ulimwengu. Lakini Mungu Baba alijua. Yeye alisikia ombi la Mwanawe mwaminifu: “Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki: walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu” (Luka 22:42–43). Wakati hatukuwepo hapo kushuhudia tendo hili lisilo na ubinafsi na la unyenyekevu, sisi ni mashahidi wa Upatanisho wa Yesu Kristo. Kila tunapotubu na kupokea msamaha wa dhambi zetu na kila tunapohisi nguvu ya uimarisho ya Mwokozi, tunaweza kushuhudia juu ya kile kilichotokea katika Bustani ya Gethsemane.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Luka 22:31–34, 54–62; Yohana 18:17–27
Uongofu ni mchakato unaoendelea.
Fikiria kuhusu uzoefu ambao Petro alikuwa nao kwa Mwokozi—miujiza aliyoshuhudia na mafundisho aliyojifunza. Je, ni kwa nini sasa Mwokozi alimwambia Petro, “Nawe utakapoongoka, waimarishe ndugu zako”?(Luka 22:32; italiki zimeongezwa). Unapotafakari hili, ingekuwa yenye msaada kufikiria kile Mzee David A. Bednar alichofundisha kuhusu tofauti kati ya kuwa na ushuhuda na kuongoka kweli kweli (ona pia “Kuongoka kwa Bwana,” Liahona, Nov. 2012, 106–9).
Unaposoma kuhusu uzoefu wa Petro katika Luka 22:31–34, 54–62 (ona pia Yohana 18:17–27), fikiria kuhusu uongofu wako wewe mwenyewe. Je, umewahi kuhisi kuwa na msimamo ambao, kama Petro, ulikuwa “tayari kwenda pamoja na [Mwokozi], kote gerezani, na hata kifo”? (Luka 22:33). Kwa nini hisia hizo wakati mwingine hufifia? Kuna fursa za kila siku za aidha kumkana au kumshuhudia Mwokozi; je, utafanya nini ili kuwa shahidi Wake wa kila siku? Ni masomo gani mengine unayojifunza kutoka katika tukio hili la Petro?
Unapoendelea kusoma Agano Jipya, tazama ushahidi wa uongofu endelevu wa Petro. Pia tilia maanani vile yeye alivyopokea agizo la Bwana la “waimarishe ndugu zako” (Luka 22:32; ona Matendo ya Mitume 3–4).
(ona pia Marko 14:27–31).
Mwokozi aliteseka kwa ajili yangu katika Gethsemane.
Rais Russell M. Nelson alitualika “kuwekeza muda katika kujifunza kuhusu Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi” (“Kuleta Nguvu ya Yesu Kristo katika Maisha yetu,” Liahona, Mei 2017, 40).
Fikiria wewe utafanya nini ili kukubali mwaliko wa Rais Nelson. Ungeweza kuanza kwa kutafakari kwa maombi mateso ya Mwokozi katika Gethsemane, kama yalivyoelezewa katika mistari hii, na kuandika mawazo na maswali yanayokujia akilini.
Kwa ajili ya kujifunza kwa kina zaidi juu ya Mwokozi na Upatanisho Wake, jaribu kutafuta maandiko mengine kwa ajili ya majibu ya maswali kama haya:
-
Kwa nini Upatanisho wa Mwokozi ulikuwa muhimu? (Ona 2 Nefi 2:5–10, 17–26; 9:5–26; Alma 34:8–16; 42:9–26.)
-
Je, Mwokozi alipitia nini wakati Alipokuwa akiteseka? (Ona Isaya 53:3–5; Mosia 3:7; Alma 7:11–13; Mafundisho na Maagano 19:16–19.)
-
Je, ni kwa jinsi gani mateso ya Mwokozi yanagusa maisha yangu? (Ona Yohana 10:10–11; Waebrania 4:14–16; 1 Yohana 1:7; Alma 34:31; Moroni 10:32–33; Dallin H. Oaks, “Kuimarishwa na Upatanisho wa Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2015, 61–64.)
-
Maswali mengine niliyonayo:
Unapojifunza kuhusu kile kilichotokea Gethsemane, inaweza kuwa ya kuvutia kujua kwamba Gethsemane ilikuwa bustani ya miti ya mzeituni na ilijumuisha mtambo wa kusindika mizeituni, uliotumika kusaga mizeituni na kutoa mafuta yaliyotumika kwa ajili ya kuwashia moto na kwa chakula vile vile kwa kuponya (ona Luka 10:34). Ni kwa jinsi gani mchakato wa usindikaji wa mafuta ya mzeituni unaashiria kile Mwokozi alichofanya kwa ajili yetu katika Gethsemane? Kwa ajili ya mawazo, ona ujumbe wa D. Todd Christofferson, “Kaeni katika Pendo Langu,” (Liahona, Nov. 2016, 50–51).
Ona Pia Mathayo 26:36–46; Luka 14:32–42.
Ufalme wa Mwokozi: “sio wa ulimwengu huu.”
Kama kiongozi wa kisiasa, Pontio Pilato alikuwa na uelewa wa nguvu na falme za ulimwengu huu. Lakini Yesu alizungumzia aina tofauti sana ya ufalme. Ukirejea nyuma kuhusu kile ulichosoma kuhusu maisha ya Mwokozi, ni ushahidi gani unaouona kwamba “ufalme Wake si wa ulimwengu huu”? (Yohana 18:36). Kwa nini ni muhimu kwako kujua hili? Je, ni kitu kipi kingine kilicho wazi kwako kuhusu maneno ya Yesu kwa Pilato?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Luka 22:31–32.Ni kwa jinsi gani Petro angehisi kujua kwamba Yesu alikuwa amesali kwa ajili yake yeye na imani yake? Je, tunaweza kusali kwa ajili ya nani, “kwamba imani [yao] isitindike”? (mstari wa 32).
-
Luka 22:39–46.Kujifunza kuhusu kuteseka kwa Mwokozi katika Gethsemane kunaweza kuwa tukio takatifu kwa familia yako. Fikiria kile unachoweza kufanya ili kuwa na staha na roho wa kuabudu unapojifunza Luka 22:39–46. Mngeweza kucheza au kuimba pamoja baadhi ya nyimbo pendwa za familia yako za kanisa au nyimbo za watoto kuhusu Mwokozi. Mngeweza kuangalia sanaa inayohusiana au kutazama video kama “The Savior Suffers in Gethsemane” (ChurchofJesusChrist.org). Mnaposoma mistari hiyo, wanafamilia wangeweza kushiriki vifungu ambavyo hasa vina maana kwao—labda kifungu ambacho husaidia kuhisi upendo wa Mwokozi (ona pia Mathayo 26:36–46; Marko 14:32–42). Ungeweza pia kuwaalika wao kushiriki shuhuda zao juu ya Yesu Kristo na Upatanisho Yake.
-
Luka 22:42.Wanafamilia wangeweza kushiriki uzoefu wakati walipojifunza kusema “Si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.”
-
Luka 22:50–51; Yohana 18:10–11.Tunajifunza nini kuhusu Yesu kutoka kwenye mistari hii?
-
Yohana 18:37–38.Tungewezaje kujibu swali la Pilato “Kweli ni nini? (mstari wa 38). Kwa ajili ya mawazo, ona Yohana 8:32; Mafundisho na Maagano 84:45; 93:23–28; na “Oh Say, What Is Truth?,” Nyimbo za Kanisa, na. 272.
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “I Stand All Amazed,” Nyimbo za Kanisa,, na.193.