Kuimarishwa na Upatanisho wa Yesu Kristo
Kwa sababu ya Upatanisho Wake, Mwokozi ana uwezo wa kusaidia---kutoa msaada---kwa kila machungu na maumivu.
Katika maisha ya duniani tuna uhakika wa kifo na mzigo wa dhambi. Upatanisho wa Yesu Kristo huondoa huu uhakika wa maisha ya duniani. Lakini licha ya kifo na dhambi, tuna changamoto zingine nyingi tunazopambana na maisha ya duniani. Kwa sababu ya Upatanisho huu huu, Mwokozi wetu anaweza kutupa nguvu tunazohitaji ili kushinda changamoto hizi za maisha ya duniani. Hii ndiyo mada yangu leo.
I.
Taarifa nyingi za kimaandiko kuhusu Upatanisho zinashughulika na Mwokozi akivunja kamba za kifo na kuteseka kwa ajili ya dhambi zetu. Katika mahubiri yake katika Kitabu cha Mormoni, Alma aliwafundisha misingi hii. Lakini pia alitoa hakikisho letu la kimaandiko wazi kwamba Mwokozi pia aliona maumivu na magonjwa na udhaifu wa watu Wake.
Alma alielezea sehemu hii ya Upatanisho wa Mwokozi: ”Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; na hii kwamba neno litimizwe ambalo linasema atabeba maumivu na magonjwa ya watu wake.” ((Alma 7:11; ona pia 2 Nefi 9:21).
Fikiria juu ya haya! Katika Upatanisho wa Mwokozi, Yeye aliteseka ”maumivu na mateso na majaribu ya kila aina.” Kama vile Rais Boyd K. Packer alivyoelezea: ”Yeye hakuwa na deni la kulipa. Hakutenda kosa lolote. ”Hata hivyo, jumla ya hatia zote, huzuni na hofu, maumivu na kufedheheshwa, mateso yote ya kiakili, mhemko, na kimwili yanayojulikana na mwanadamu—Yeye aliyapata yote.”1
Kwa nini Yeye apitie hizi changamoto za maisha ya duniani za ”kila aina”? Alma alielezea: ”Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake; na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:12).
Kwa mfano, Mtume Paulo alitangaza kwamba kwa sababu Mwokozi ”aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa”(Waebrania 2:18). Vivyo hivyo, Rais James E. Faust alifundisha ”Kwa vile Mwokozi aliteseka kila kitu chochote kwamba sisi tuweze kuhisi ama kupata uzoefu, Yeye anaweza kuwasaidia wanyonge kuwa thabiti.”2
Mwokozi wetu alipata na kuteseka changamoto zote za maisha ya duniani kwa wingi ”kulingana na mwili” ili Yeye aweze kujua ”kulingana na mwili” jinsi ya kuwasaidia [ambayo humaanisha kutoa msaada ama usaidizi kwa] watu Wake kulingana na udhaifu wao.” Yeye kwa hivyo anajua shida zetu, masumbuko yetu, majaribu yetu, na mateso yetu, kwani Yeye kwa hiari aliyapata yote kama sehemu muhimu ya Upatanisho Wake. Na sababu ya hivyo, Upatanisho Wake unampa uwezo wa kutusaidia—kutupa nguvu za kustahamili yote.
II.
Huku mafundisho ya Alma katika sura ya saba ni andiko moja wazi kabisa katika maandiko yote kuhusu hii nguvu ya Upatanisho, pia inafunzwa kote katika maandishi matakatifu.
Hapo mwanzoni wa huduma Yake, Yesu alieleza kwamba Yeye alitumwa ”kuwaponya wenye majonzi” (Luka 4:18). Biblia kila mara inatusimulia kuhusu uponyaji Wake wa watu ”magonjwa yao” (Luka 5:15; 7:21). Kitabu cha Mormoni kimerekodi uponyaji Wake kwa ”waliosumbuka kwa jinsi yoyote” (3 Nefi 17:9). Injili ya Mathayo inaeleza kwamba Yesu aliponya watu ”ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu” (Mathayo 8:17).
Isaya alifundisha kwamba Masiya ameyachukua ”masikitiko yetu” na ”huzuni zetu”Isaya 53:4). Isaya pia alifundisha kuhusu Yeye kutuimarisha sisi: ”Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; Nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia” (Isaya 41:10).
Ndiyo, tunaimba:
Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike,
Kwa maana mimi ni Mungu wako na bado nitakusaidia.
Nitakutia nguvu, nitakusaidia, na ninakuwezesha usimame,...
Umehiliwa na wema wangu, mkono wa Mwenyezi.3
Kuongea kuhusu baadhi ya changamoto zake mwenyewe za kibinadamu Mtume Paulo aliandika, ”Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”(Wafilifpi 4:13).
Na kwa hivyo tunaona kwamba kwa sababu ya Upatanisho Wake, Mwokozi ana nguvu za kusaidia—kutoa msaada—kwa kila maumivu na mateso ya binadamu. Wakati mwingine nguvu Zake huponya udhaifu, lakini maandiko na uzoefu wetu unafunza kwamba wakati mwingine Yeye hutusaidia ama hututia nguvu kwa kutupa nguvu ama subira ya kuvumilia udhaifu wetu.4
III.
Ni maumivu na mateso na udhaifu gani wa duniani ambao Mwokozi wetu alipata na kuteseka.
Sisi sote tuna maumivu na mateso na udhaifu wakati mmoja ama mwingine. Kando na kile kinachotupata kwa sababu ya dhambi zetu, maisha ya duniani yamejawa na masumbuko, machungu, na mateso ya kila mara.
Sisi na wale tuwapendao huwa tunaugua maradhi. Wakati fulani kila mmoja wetu pia hupata maumivu kutokana na majeraha makali ama kutoka na shida zingine za kimwili ama kiakili. Sisi sote tunateseka na kuhuzunika kwa ajili ya kifo cha mpendwa wetu. Sisi tunapatwa na ushinde katika majukumu yetu ya kinafsi, mahusiano ya kifamilia, ama ajira zetu.
Wakati mwenzi ama mtoto anapokataa kile tunachojua ni kweli na kuchepuka kutoka kwenye mapito ya haki, tunapatwa hasa na maumivu makali, kama vile baba ya mwana mpotevu katika fumbo la Yesu linalojulikana sana (ona Luka 15:11–32).
Kama Mtungaji wa zaburi alivyotamka.”Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote” (Zaburi 34:19).
Basi, nyimbo zetu zina hili hakikisho la kweli. ”Ulimwengu hauna huzuni ambayo mbingu haziwezi kuponya.”5 Kile kinachotuponya ni Mwokozi wetu na Upatanisho Wake.
Hasa kinachowavunja moyo matineja ni hisia za kukataliwa, wakati wenzi wao wanaonekana kuingia katika mahusiano ya furaha na kwa makusudi kuwaacha kando. Ubaguzi wa ukoo na makabila huleta kukataliwa kwingine ambao una machungu, kwa vijana na watu wazima. Maisha yana changamoto zingine nyingi, kama vile kukosa ajira ama kuvunjika kwa mipango yetu.
Mimi naongea kuhusu udhaifu wa kimwili usiosababishwa na dhambi zetu. Wengine wanazaliwa na ulemavu wa kimwili ama kiakili ambao husababisha mateso ya kibinafsi kwao na masumbuko kwa wale wanaowapenda na kuwatunza. Kwa wengi, udhaifu wa msononeko una machungu ama unalemaza kabisa. Mateso mengine yenye maumivu ni hali ya upweke. Wale wanaoteseka kutokana na hali hii wanapaswa kukumbuka kwamba Mwokozi wetu alipatwa pia na aina hii maumivu na kwamba, kupitia Upatanisho Wake, Yeye anatoa nguvu za kuyavumilia.
Ulemavu mchache unalemaza sana maisha yetu kimwili ama kiroho kushinda uteja. Baadhi yazo, kama vile uteja wa ponografia ama madawa, kuna uwezekano mkubwa husababishwa na tabia za dhambi. Hata wakati tabia hiyo imetubiwa, uteja unaweza kubakia. Huu mnaso wa kulemaza pia unaweza kutulizwa na nguvu za dhati zinazopatikana kutoka kwa Mwokozi. Vivyo hivyo kwa changamoto kali zinazowapata wale wanaotiwa gerezani kwa ajili ya jinai. Barua ya hivi majuzi inashuhudia nguvu ambayo inaweza kuja kwa mtu katika hali hiyo. ”Mimi najua Mwokozi wangu anatembea katika shoroba hizi, na mimi kila mara nimehisi upendo Wake ndani ya hizi kuta za gereza.”6
Mimi naupenda ushuhuda wa mtunzi wa mashairi na rafiki yetu Emma Lou Thayne. Katika maneno ambayo sisi huimba kama wimbo, yeye aliandika:
Ninaweza kugeukia wapi nipate amani?
Faraja yangu iko wapi
Wakati zile nyenzo zinakoma kunitibu?
Wakati kwa moyo wenye donda, ghadhabu, ama hila,
Mimi hujitenga mbali,
Nikipekua nafsi yangu?
Wapi, wakati machungu yanapozidi,
Wapi, wakati ninaangamia,
Wapi, katika haja yangu ya kujua, wapi nitatorokea?
U wapi mkono wa amani utulize fedheha yangu?
Nani, nani awezaye kuelewa?
Yeye, Pekee tu.7
IV.
Ni nani anayeweza kusaidiwa na kuimarishwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo? Alma aliwafundisha kwamba Mwokozi angejichukulia juu Yake ”maumivu na magonjwa ya watu Wake” (Alma 7:11–12;” na ”kuwasaidia watu Wake” (Alma 7:11, 12; mkazo umeongezewa). ”Watu Wake” ni kina nani katika ahadi hii? Ni binadamu wote—wote ambao wanafurahia uhalisi wa ufufuko kupitia Upatanisho? Ama ni tu wale watumishi waliochaguliwa wanahitimu kupitia ibada na maagano.
Neno watu lina maana nyingi katika maandiko. Maana inayofaa sana kwa mafundisho kwamba Mwokozi atawasaidia ”watu wake” ni maana ambayo Amoni alitumia wakati alipofundisha kwamba ”Mungu ni mwangalifu kwa kila watu, nchi yoyote ambayo wangekuwa ndani”(Alma 26:37). Hiyo ndiyo pia kile malaika walimaanisha wakati walitangaza kuzaliwa kwa mtoto Kristo: ”Habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote” (Luka 2:10).
Kwa sababu ya tukio la upatanisho Wake katika maisha ya duniani, Mwokozi wetu aliweza kufariji, kuponya, na kuimarisha wanaume na wanawake wote kila mahali, lakini mimi naamini Yeye atafanya hivyo tu kwa wale ambao walimtafuta Yeye na kuomba msaada Wake. Mtume Yakobo alifundisha: ”Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza” (Yakobo 4:10). Tunahitimu kwa baraka hiyo tunapoamini katika Yeye na kuomba msaada Wake.
Kuna mamilioni ya watu wanaomcha Mungu ambao wanamwomba Mungu awakuze kutoka kwa mateso yao. Mwokozi wetu amefunua kwamba Yeye ”alishuka chini ya vitu vyote” (M&M 88:6). Kama Mzee Neal A. Maxwell alifunza, ”Kwa yeye ’kushuka chini ya vitu vyote,’ Yeye anafahamu, vyema na kibinafsi, upana wote wa mateso ya mwanadamu.”8 Hata tunaweza pia kusema kwamba kwa kujishusha chini ya vitu vyote, Yeye alijiweka vyema kutuinua na kutupa nguvu tunazohitaji kuvumilia mateso yetu. Tunahitaji tu kuomba.
Mara nyingi katika ufunuo wa kisasa, Bwana hutangaza, ”Kwa hivyo, kama wewe utaniomba Mimi utapata, kama utabisha utafunguliwa” (kwa mfano, M&M 6:5; 11:5; ona pia Mathayo 7:7). Hakika, kwa sababu ya upendo Wao unaokumbatia, Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, wanasikia na kujibu vilivyo maombi ya wote wanaotafuta kwa imani. Kama Mtume Paulo alivyoandika, ”Tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio” (1 Timotheo 4:10).
Ninajua vitu hivi ni kweli. Upatanisho wa Mwokozi wetu unafanya zaidi ya kutuhakikishia kutokufa kwa kupitia ufufuko wote na kutoa nafasi kwetu kutakaswa kutoka kwa dhambi kwa toba na ubatizo. Upatanisho Wake pia hutupatia nafasi ya kumwita Yeye ambaye ameshapitia udhaifu wote wa wanadamu ili kutuponya na kutupa nguvu za kubeba mizigo ya maisha ya binadamu. Yeye anajua mfadhaiko wetu, na Yeye yupo hapa kwa ajili yetu. Kama Msamaria mwema, wakati Yeye alitupata njiani tumejeruhiwa, Yeye alitufunga vidonda vyetu na kututunza (ona Luka 10:34). Nguvu za kuponya na kuimarisha za Upatanisho wa Yesu Kristo ni kwa sisi sote ambao tutuomba. Mimi nashuhudia juu ya hayo pia ninaposhuhudia juu ya Mwokozi wetu, ambaye hufanya yote yawezekane.
Siku moja hii mizigo yote ya binadamu itapita na hakutakuwa na maumivu zaidi (ona Ufunuo 21:4). Mimi naomba kwamba sisi sote tutaelewa tumaini na nguvu za Upatanisho wa Mwokozi: hakikisho la maisha ya milele, nafasi ya uzima wa milele, na nguvu za kuhimili tunazoweza kupokea kama tutaomba tu, katika jina la Yesu Kristo, amina.