Macho ya Kuona na Masikio ya Kusikia
Kama tukimtegemea Kristo na tufungue macho yetu na masikio yetu, Roho Mtakatifu atatubariki kumwona Bwana Yesu Kristo akifanya kazi katika maisha yetu.
Katika huduma yake ya duniani, Yesu alifanya miujiza ya ajabu ya kuponya na kufundisha kwa mamlaka na nguvu kwamba maandiko yanasema, “Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu ... na makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia.”1
Wengine waliomwona Akiponya na kumsikia akifundisha walimkataa. Wengine walimfuata kwa muda, lakini hawakuendelea tena kutembea naye.2 Bwana Yesu Kristo alikuwa mbele yao, lakini hawakumjua Yeye ni nani. Walikuwa vipofu, na walichagua kutomfuata. Kwao, Yesu alisema:
”Nilikuja kwangu na walio wangu hawakunipokea.”3
“Masiko yao ni mazito kusikia, na macho yao wameyafumba.”4
Hata hivyo, kulikuwa na wanaume na wanawake wengi, wakiwemo Mitume Wake, ambao waliyaweka maisha yao Kwake. Ijapokuwa walitaabika kwa mhangaisho wa kidunia, na kuchanganyikiwa kuhusu kile Alichokifundisha, na hata kwa woga, walimwamini, walimpenda, na walimfuata.
Kuwahusu wao, Yesu alisema:“ Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona: na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”5
Kabla ya mateso yake kule Gethsemane na Kalvari, Yesu aliwapa wanafunzi Wake ahadi hii ya ajabu: Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa kuliko hizo atafanya; kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.”6
Yesu alitimiza ahadi hiyo: kuanzia siku ya Pentekosti, wafuasi walibarikiwa kwa ubatizo wa moto na wa Roho Mtakatifu.7 Kupitia kwa imani katika Kristo, toba, na utiifu, Roho Mtakatifu akawa mwenza wao, alibadilisha mioyo yao, aliwabariki kwa ushahidi unaodumu wa ukweli.
Vipawa na baraka hizi ziliwaimarisha wafuasi wa Bwana. Ijapokuwa wakati mwingine waliisha katika hatari na mkanganyiko, walipokea kipawa cha kiroho cha macho kuona na masikio kusikia. Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, walianza kuona ukweli wa mambo kama yalivyokuwa kihalisi, hususani Bwana Yesu Kristo na kazi Yake miongoni mwao.8 Roho Mtakatifu aliongeza kuelewa kwao, na walisikia sauti ya Bwana kwa uwazi kabisa. Injili ya Yesu Kristo ilizama ndani ya mioyo yao.9 Walikuwa na imani na wenye kutii.10 Walihubiri injili kwa ushujaa na nguvu na waliujenga ufalme wa Mungu.11 Walikuwa na furaha katika Yesu Kristo.
Tuna mambo mengi yanayofanana na wale wanaume na wanawake wenye imani wakati wa meridiani. Nasi pia tunaishi katika wakati ambao Bwana Yesu Kristo alifanya miujiza miongoni mwetu—ikiwemo kuponya wagonjwa, kutusafisha dhambi, kubadilisha mioyo yetu, na kufungua wokovu kwa watoto wa Mungu katika sehemu zote mbili za pazia. Katika wakati wetu pia tuna manabii walio hai na mitume, nguvu za ukuhani, vipawa vya roho, na baraka takatifu za ibada ya wokovu.
Wakati wetu ni wakati hatari—wakati wa maovu na majaribu makubwa, wakati za mkanganyiko na vurugu. Katika nyakati hizi za hatari, nabii wa Bwana hapa duniani, Rais Thomas S. Monson, ametuita sisi kuziokoa roho zilizojeruhuliwa,12 kusimama kwa ajili ya ukweli na ujasiri,13 na kuujenga ufalme wa Mungu.14 Ngazi yoyote ya wema au imani au utii tulionao sasa, haitatosha kwa kazi iliyo mbele yetu. Tunahitaji nuru na nguvu kubwa ya kiroho. Tunahitaji macho ili kuona vizuri zaidi Mwokozi akitenda kazi katika maisha yetu na masikio kusikia sauti Yake ikiingia zaidi katika mioyo yetu.
Baraka hizi nzuri zinakuja wakati tunapofungua mioyo yetu na kumpokea,15 kumpokea kikweli, Bwana Yesu Kristo, mafundisho Yake, na Kanisa Lake katika maisha yetu. Hatuhitaji kuwa wakamilifu, lakini tunahitaji kuwa wazuri na kuwa wazuri zaidi. Tunahitaji kuishi maisha mepesi na kweli rahisi za injili. Kama tunajichukulia juu yetu jina la Kristo, kutenda kwa imani katika Yeye kutubu dhambi zetu, kutii amri Zake, na daima kumkumbuka Yeye, tutapokea wenzi wa Roho Mtakatifu kupitia huruma na neema ya Yesu Kristo.
Utiifu rahisi huleta Roho katika mioyo yetu. Katika nyumba zetu tunaomba kwa imani, tunajifunza maandiko, na kuitakasa siku ya Sabato. Katika makanisa yetu tunapokea sakramenti na kufanya ahadi takatifu kwa Baba yetu wa Mbinguni katika jina la Kristo. Katika mahekalu matakatifu tunashiriki katika ibada takatifu kwa niaba ya kaka na dada zetu walio upande ule mwingine wa pazia. Katika familia zetu na katika majukumu yetu toka kwa Bwana, tunawafikia wengine, tukiinua mizigo yao na kuwaalika kuja kwa Kristo.
Ndugu na akina dada, ninajua kwamba kama tutafanya mambo haya, Roho Mtakatifu atakuja! Tutakua kiroho na kupata uzoefu pamoja na Roho Mtakatifu, na Yeye atakuwa mwenza wetu. Kama tutamtegemea Kristo na kufungua macho na masikio yetu, Roho Mtakatifu atatubariki kuona Bwana Yesu Kristo akifanya kazi katika maisha yetu, kuimarisha imani Kwake kwa uhakika na ushahidi. Tutazidi kuwaona kaka na dada zetu kadiri Mungu awaonavyo, kwa upendo na huruma. Tutaisikia sauti ya Mwokozi katika maandiko, katika minong’ono ya Roho, na katika maneno ya manabii waliohai.16 Tutaona nguvu ya Mungu ikija kwa nabii Wake na viongozi wote wa Kanisa Lake la kweli na lililo hai, na tutajua kwa ukweli kwamba hii ni kazi takatifu ya Mungu.17 Tutaona na kuelewa wenyewe na ulimwengu unaotuzunguka jinsi Mwokozi afanyavyo kazi. Tutapata kile Mtume Paulo alichokiita “nia ya Kristo.”18 Tutakuwa na macho ya kuona na masikio ya kusikia, na tutaujenga ufalme wa Mungu.
Maisha yaweza kuwa magumu, yenye utata, uchungu, na kukatisha tamaa. Ninatoa ushahidi wangu kwamba kupitia huruma ya Roho Mtakatifu, nuru ya injili ya Yesu Kristo itaondoa utata, uchungu, na giza. Iwe inakuja mara moja au kwa kusuburia au katika mtiririko mpole, kwamba nguvu ya utukufu wa kiroho italeta upendo wa uponyaji na ufariji kwa anayetubu, nafsi iliyojeruhiwa, giza kuondolewa na nuru ya kweli, na kuondoa kukatishwa tamaa kupitia tumaini katika Kristo. Tutaona baraka zikija, na tutajua kwa ushahidi wa Roho kwamba ni Bwana Yesu Kristo anafanyakazi katika maisha yetu. Mizigo yetu hakika “itamezwa kwenye shangwe ya [Mkombozi wetu].”19
Uzoefu ambao mama na baba yangu walikuwanao miaka mingi iliyopita unaelezea umuhimu na nguvu ya macho kuona na masikio kusikia. Mwaka 1982 wazazi wangu waliitwa kutumikia Misheni ya Davao Ufilipino. Wakati mama yangu alipofungua barua na kuona sehemu waliyoitwa, alipaza sauti kwa baba yangu, “La hasha! Ni lazima uwapigie simu na kuwaambia hatuwezi kwenda Ufilipino. Wanajua una ugonjwa wa pumu.” Baba yangu alikuwa anaugua ugonjwa wa pumu kwa miaka mingi, na mama yangu alikuwa na wasiwasi mwingi juu yake.
Siku kadhaa baadaye mama yangu aliamwamsha baba yangu karibu saa 8:30 usiku. Alisema, “Merlin, umeisikia hiyo sauti?”
Hapana, sikusikia sauti yoyote.”
“Haya, nimeisikia sauti hiyo hiyo mara tatu usiku huu, ikisema, “Kwa nini una wasiwasi? Hujui kwamba ninajua ana ugonjwa wa pumu? Mimi nitamtunza, na nitakutunza wewe pia. Jiandaeni kuhudumu huko Ufilipino.”’
Mama na baba yangu walitumikia Huko Ufilipino na walipata uzoefu wa ajabu. Roho Mtakatifu alikuwa mwenza wao, na walibarikiwa na walilindwa. Baba yangu kamwe hakuwa na tatizo lolote la pumu. Alihudumu kama mshauri wa kwanza katika urais wa misheni, na yeye na mama yangu waliwafundisha mamia ya wamisioanri na maelfu wa Watakatifu wa Siku za Mwisho katika maandalizi ya kata na vigingi katika visiwa vya Mindanao. Walibarikiwa na macho ya kuona na masikio ya kusikia.
Ndugu na dada, ninatoa ushahidi wa Yesu Kristo. Ninajua Yeye yu hai. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Ninajua kwamba kama tutampokea Yeye katika maisha yetu na kuishi na kweli rahisi za injili Yake, tutafurahia uenzi wa Roho Mtakatifu. Tutakuwa na zawadi ya thamani ya macho kuona na masikio kusikia. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.