2010–2019
Ukweli ulio Wazi na Wenye Thamani
Oktoba 2015


7:10

Ukweli ulio Wazi na Wenye Thamani

Fidia ya ukarimu wa Baba wa Mbinguni kwa kuishi katika nyakati za hatari ni kwamba pia tunaishi katika utimilifu wa nyakati.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, imekuwa miongo mingi tangu mkutano mkuu uitishwe ambapo Rais Boyd K. Packer na Wazee L. Tom Perry na Richard G. Scott hawakuwa wameketi nyuma tu ya mimbari na kuzungumza katika mojawapo ya vikao hivi. Kumbukumbu zetu juu yao ni zenye kutia uchungu, na ninaongeza shukrani zangu katika kuwaheshimu, kila mmoja akiwa wa kipekee kwa namna yake lakini wakiwa wameunganishwa kabisa katika ushahidi na ushuhuda wao juu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

Zaidi ya hayo, mimi, kama ninyi, ninapata nguvu katika kukubali na kumtii Rais Thomas S. Monson kama nabii, muonaji, na mfunuzi, na ninastaajabia uaminifu na kuwajibika kwake katika huduma yake ya kitume inayodumu zaidi ya miaka 50 ya ajabu.

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa Jumanne asubuhi wiki hii, baada tu ya 3:00 asubuhi wakati Uaskofu ulipokuwa ukianza mkutano na Urais wa Eneo la Asia, ambao wako hapa kwa ajili ya mkutano huu, kwamba niliitwa kukutana na Rais Monson, pamoja na washauri wake. Muda kidogo baadaye, nilipokuwa nikielekea katika chumba cha mikutano kilicho kando ya ofisi yake, ni lazima nilikuwa ninaonekana mwenye wasiwasi nikiwa nimeketi upande mmoja wa meza, huku akizungumza kwa ukarimu kutuliza wasiwasi wangu. Akitoa maoni, huku akiangalia umri wangu, kwamba nilionekana kijana na hata nilionekana kijana kuliko umri wangu halisi.

Kisha, katika muda mfupi huo, Rais Monson alieleza kwamba alikuwa akitekeleza mapenzi ya Bwana, alikuwa analeta wito wa Akidi ya Kumi na Wawili kwangu. Aliniuliza ikiwa ningekubali wito huu, ambapo, kufuatia kile nilicho na uhakika nacho kwamba nilikuwa nikitweta kwa sauti iliyosikika vyema, kwa mshangao mkubwa, nilijibu ndio. Na kisha, kabla sijaweza kusema tsunami ya mhemko ambao ni ngumu kuelezea, nyingi ya hisia hizi zilikuwa hisia za upungufu, Rais Monson kwa ukarimu alininyooshea mkono, akielezea jinsi yeye alivyopewa wito miaka mingi iliyopita wa kuwa Mtume na Rais David O. McKay, wakati ambapo pia na yeye alijiona mpungufu. Kwa upole akanifundisha, ”Askofu Stevenson, Bwana atawapasisha wale ambao Yeye huwaita.” Maneno haya ya kutuliza ya nabii yamekuwa chanzo cha amani, utulivu katika tufani ya uchungu wa kujichunguza binafsi na hisia dhaifu katika masaa ya masumbuko yaliyofuata ambayo yamepita mchana na usiku tangu wakati huo.

Nilikariri yale ambayo nimetoka tu kuwaeleza kwa mwenza wangu kipenzi, Lesa, baadaye siku hiyo, tukiwa tumeketi kwenye kona tulivu pale Temple Square, na maandhari tulivu ya hekalu na Tabenakulo ya kihistoria mbele yetu. Tulipokuwa tukijaribu kuelewa na kutafakari matukio ya siku, tuligundua kuwa nanga yetu ni katika imani yetu katika Yesu Kristo na ufahamu wetu juu ya mpango mkuu wa furaha. Hii inaniongoza katika kuelezea juu ya upendo wangu wa dhati kwa Lesa. Yeye ni nuru ndani yangu na ya maisha yangu na ni binti wa ajabu wa Mungu. Yake ni maisha yaliyoingiliwa na huduma isiyo na uchoyo na upendo usio na masharti kwa wote. Nitajitahidi kuomba ili niwe mwenye kustahili baraka ya muungano wetu wa milele.

Ninaelezea mapenzi yangu ya dhati kwa wana wetu wanne na familia zao, watatu kati yao wako hapa na wake zao warembo, kina mama wa wajukuu wetu sita; wa nne ni mmisionari, ana ruhusa ya kuwa macho baada ya muda uliowekwa na amri ya umisionari na anatazama yanayoendelea hapa moja kwa moja na rais wake wa misheni na mke wa rais wa misheni kutoka nyumba ya misheni yao kule Taiwan. Ninampenda kila mmoja wao na ninapenda jinsi wanavyompenda Mwokozi na jinsi wanavyoipenda injili.

Ninaelezea upendo wangu kwa kila mwana familia yangu: kwa mama yangu mpendwa na kwa baba yangu, ambaye aliaga dunia mwaka uliopita, ambaye alimimina ndani yangu ushuhuda ambao ulionekana kukaa ndani yangu kutoka kumbukumbu zangu za utotoni. Ninatoa pia shukrani kwa kaka yangu, dada zangu, na wenza wao waaminifu, na pia familia ya Lesa, wengi wao kwa kweli wako hapa leo hii. Ninatupa jarife hili la shukrani kwa ndugu na jamaa wengi, marafiki, wamisionari, viongozi, na walimu njiani.

Nimebarikiwa kuwa na uhusiano wa karibu na washiriki wa Urais wa Kwanza, Kumi na Wawili, Sabini, na urais mkuu wa makundi saidizi. Ninaelezea upendo wangu na heshima kwa kila mmoja wenu kina dada na akina kaka na nitajitahidi kuwa mstahiki wa ushirikiano wenu. Uaskofu Simamizi unafurahia karibu ule umoja wa mbinguni. Nitaukosa uhusiano wangu kila siku na Askofu Gérald Caussé, Askofu Dean M. Davies, na wafanyakazi wote.

Ninasimama mbele yenu kama ushahidi wa maneno ya Bwana yaliyoandikwa katika sehemu ya kwanza ya Mafundisho na Maagano: “Kwamba utimilifu [wa] injili yangu uweze kutangazwa na watu walio dhaifu na kawaida hata mwisho wa dunia, na mbele ya wafalme na watawala.”1 Maneno haya yanatanguliwa na tamko la Bwana ambalo linaonyesha upendo wa Bwana kwa watoto wake: “Hivyo basi, mimi Bwana, nikijua majanga yajayo juu ya wakazi wa dunia, nimemwita mtumishi wangu Joseph Smith, mdogo, na kusema naye kutoka mbinguni, na nikampa yeye amri.”2

Baba yetu wa Mbinguni mpendwa na Mwanawe, Yehova, na ufahamu wa mwisho kutoka mwanzo,3 walifungua mbingu na kipindi kipya cha Mungu kukabiliana na majanga ambayo Wao walijua yangekuja. Mtume Paulo alieleza majanga yanayokuja kama ”nyakati za hatari.”4 Kwangu mimi, hili linapendekeza kwamba fidia karimu ya Baba wa Mbinguni kwa kuishi katika nyakati za hatari ni kwamba pia tunaishi katika nyakati za utimilifu.

Nilipokuwa nikisumbuka wiki hii kuhusu upungufu wangu, nilipokea wazo tofauti ambalo lilinirekebisha na kunifariji: sio kutilia maanani kwa kile ambacho siwezi kufanya ila kwa kile ninachoweza kufanya. Ninaweza kushuhudia ukweli wa injili ulio wazi na wenye thamani.

Haya ni maneno ambayo nimeyaeleza mara nyingi sana kwa wote wale walio waumini wa Kanisa na wengi ambao sio waumini: ”Mungu ni Baba yetu [mpendwa] wa Mbinguni. Sisi ni watoto Wake … Analia nasi tunapoteseka na kufurahia pamoja nasi tunapotenda kile kilicho cha haki. Anataka kuwasiliana nasi, na tunaweza kuwasiliana naye kupitia maombi ya dhati …

”Baba wa Mbinguni ametutayarishia sisi, watoto Wake, njia ya … kurudi kuishi katika uwepo Wake … Jambo la muhimu sana katika mpango wa Baba [wa Mbinguni] ni Upatanisho wa Yesu Kristo.”5

Baba wa Mbinguni alimtuma Mwanawe duniani aje kulipia dhambi za kila mwanadamu. Juu ya ukweli huu ulio wazi na wa thamani ninatoa ushuhuda wangu, na ninafanya hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.