Majira Ya Joto na Shangazi Mkubwa Rose
Unapotembea njiani mwako katika mapito angavu ya uanafunzi, naomba kwamba imani itaimarisha kila hatua katika njia yako.
Dada zangu na marafiki wapendwa, nina furaha kubwa kuwa pamoja nanyi leo, na ninafurahia kuwa katika uwepo wa nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson. Rais, tunakupenda. Tumehuzunishwa kwa kuwapoteza marafiki zetu wa dhati watatu na Mitume wa Mungu. Tutawakosa Rais Packer, Mzee Perry, na Mzee Scott; tunawapenda wao. Tunaombea familia na marafiki zao.
Siku zote mimi hungojea kwa hamu kikao hiki cha mkutano—muziki mzuri na ushauri kutoka kwa dada zetu walio na maongozi humleta Roho kwa wingi sana. Mimi ni mtu bora baada ya kuwa pamoja nanyi.
Nilipokuwa nikitafakari yale ambayo ningekuja kusema nanyi leo, mawazo yangu yalielekea katika jinsi ambavyo Mwokozi alifundisha. Inavutia jinsi Alivyokuwa na uwezo wa kufundisha ukweli mtukufu zaidi kupitia hadithi rahisi. Hadithi Zake za mafumbo zilikuwa zikiwaalika wanafunzi Wake kupokea ukweli sio tu kwa akili zao lakini pia kwa mioyo yao, na kuunganisha kanuni za milele na maisha yao ya kila siku.1 Rais wetu mpendwa Monson naye pia ni stadi kwa kufundisha kutumia tajriba ya kibinafsi.2
Leo, nami pia ninayo hadithi ya kushiriki. Ninawaalika msikilize kwa Roho. Roho Mtakatifu atawasaidia kupata ujumbe wenu binafsi katika hadithi hii.
Shangazi Mkubwa Rose.
Hadithi hii inamhusu msichana kwa jina la Eva. Kuna mambo mawili muhimu unastahili kufahamu kuhusu Eva. Moja ni kuwa alikuwa na miaka 11 katika hadithi hii. Na lingine ni kuwa kabisa, hakika hakutaka kwenda kuishi na Shangaziye mkubwa Rose. Kabisa. Hakuna namna.
Lakini mamake Eva alikuwa anaenda kufanyiwa upasuaji ambao ulihitaji muda mrefu ili kupona. Kwa hivyo wazazi wake Eva walikuwa wanamtuma Eva kwenda kukaa na Shangazi Mkubwa Rose.
Mawazoni mwake Eva, kulikuwepo na sababu elfu moja za kueleza kwa nini hili lilikuwa wazo baya. Moja ni kuwa, ingemaanisha yeye kuwa mbali na mamake. Ingemaanisha pia aiache familia yake na marafiki zake. Na licha ya hayo, hata yeye hakumfahamu Shangazi Mkubwa Rose. Alikuwa amejisikia vizuri kabisa, na kupendezwa na pale alipokuwa.
Lakini hakuna kiasi chochote cha kubishana au kugeuzageuza macho kungeweza kubadili uamuzi ule. Kwa hivyo Eva alifungashaa sanduku lake na kuanza safari hiyo ndefu na babake kuelekea nyumbani kwa Shangazi Mkubwa Rose.
Kuanzia wakati ambapo Eva alikanyaga ndani ya nyumba ile, aliichukia.
Kila kitu kilikuwa kikuukuu sana! Kila mahali palikuwa pamejazwa na vitabu vikuukuu, chupa zenye rangi ya ajabu, mapipa ya plastiki yaliyokuwa yamefurika na shanga, fundo za tepe, na vifungo.
Shangazi Mkubwa Rose aliishi kule pekee yake; hakuwa amewahi kuolewa. Mkazi mwingine mmoja aliyeishi pale alikuwa paka mwenye rangi ya kijivu aliyependa kutafuta mahali palipo juu zaidi katika chumba chochote na kuketi pale, akikodolea macho kila kitu kilichoko chini yake kama chui mwenye njaa.
Hata nyumba yenyewe ilionekana ya upweke. Ilikuwa kule mashambani, ambako nyumba ziko mbali mbali. Hakuna yeyote wa rika yake Eva aliyeishi chini ya nusu maili kutoka pale. Hilo lilimfanya Eva ahisi upweke pia.
Mara ya kwanza hakumjali sana Shangazi Mkubwa Rose. Alifikiria sana juu ya mamake. Mara nyingine, angekaa macho bila usingizi usiku, akiomba kwa moyo wake wote kwamba mama yake apone. Na ingawa hilo halikutendeka mara moja, Eva alianza kuhisi kuwa Mungu alikuwa akimlinda mama yake.
Hatimaye ujumbe ukaja kwamba upasuaji ulifanyika salama, na kile kilichokuwa kimebaki ni Eva kuvumilia hadi mwisho wa majira ya joto. Lakini loo, jinsi alivyochukia kuvumilia hadi mwisho!
Mawazo yake yote juu ya mamake yakiwa yametulia, Eva alianza kumjua Shangazi Mkubwa Rose vizuri kidogo. Alikuwa mwanamke mkubwa—kila kitu juu yake kilikuwa kikubwa: sauti yake, tabasamu lake, utu wake. Haikuwa rahisi kwake kujishughulisha, lakini siku zote aliimba na kucheka huku akifanya kazi, na sauti ya kicheko chake ilienea nyumbani kote. Kila usiku aliketi chini kwenye sofa yake iliyoshindiliwa kupita kiasi, na kutoa maandiko yake, na kuyasoma kwa sauti kubwa. Na alipokuwa akisoma, mara nyingine alitoa maoni kama ”Loo, asingelifanya hivyo!” au ”Ni kipi singalitoa kuwepo mahali pale!” au ”Je, hiki si kitu kizuri zaidi ambacho umewahi kusikia!” Na kila jioni wakati wote wawili wakipiga magoti pembeni mwa kitanda chake Eva kuomba, Shangazi Mkubwa Rose angaliomba maombi mazuri zaidi, akimshukuru Baba wa Mbinguni kwa ndege wa bluu na miti ya prusia, machweo ya jua na nyota, na ”maajabu ya kuwa hai.” Ilionekana kwake Eva kana kwamba Rose alimfahamu Mungu kama rafiki.
Baada ya muda, Eva aligundua jambo la kushangaza: Kulikuwa na uwezekano kuwa Shangazi Mkubwa Rose alikuwa mtu mwe furaha kubwa sana ambaye alikuwa amewahi kumfahamu.
Lakini hilo linawezekanaje?
Alikuwa na nini cha kumfurahisha?
Hakuwa amewahi kuolewa, hakuwa na watoto, hakuwa na mtu wa kukaa pamoja naye ila tu yule paka mwenye msisimiko, na alikuwa na wakati mgumu kufanya kazi rahisi kama kufunga viatu vyake na kupanda juu ghorofani.
Alipokuwa akienda mjini, alivaa kofia kubwa za kuaibisha, na zenye kung’ara. Lakini watu hawakumcheka. Badala yake, walimzingira, wakitaka kusema naye. Rose aliwahi kuwa mwalimu na ilikuwa kawaida kwa wanafunzi wake wa zamani—sasa ni watu wazima wenye watoto wao—kusimama na kusema naye. Walimshukuru kwa kuwa na ushawishi mzuri kwa maisha yao. Mara nyingi wao walicheka. Wakati mwingine wao walilia.
Vile majira ya joto yalipokuwa yakiendelea, Eva alitumia muda zaidi na zaidi wa kukaa na Rose. Walienda kwa matembezi ya muda mrefu na Eva akajifunza tofauti baina ya shomoro na shorewanda. Alikusanya matunda ya mwituni na kutengeneza jamu kutokana na matunda ya mpungate. Alijifunza kuhusu bibi wa bibi wa mama yake ambaye alitoka nchi yake ya asili aliyoipenda, akafunga safari ya baharini, na kuvuka nyanda tambarare ili awe pamoja na watakatifu.
Muda mfupi baadaye, Eva aligundua jambo jingine la kushangaza: sio tu kwamba Shangazi Mkubwa Rose alikuwa mmojawapo wa watu wenye furaha nyingi aliowafahamu, lakini Eva naye alikuwa mwenye furaha sana wakati wote alipokuwa karibu naye.
Siku za majira ya joto zilikuwa zinapita kwa haraka mno sasa. Kabla ya yeye kujua, Shangazi Mkubwa Rose alisema kuwa wakati ulikuwa unakaribia kwa Eva kurudi nyumbani. Ingawaje Eva alikuwa akingojea kwa hamu siku hiyo tangu siku aliyowasili, hakuwa na hakika kabisa kwamba sasa atajisikiaje. Yeye alijua hakika angelikosa hii nyumba kuukuu ya ajabu na paka mnyemeleaji na Shangaziye Mkubwa mpendwa Rose.
Siku moja kabla ya babake kufika kumchukua, Eva aliuliza swali lililokuwa likimtatanisha kwa wiki nyingi: ”Shangazi Rose, kwa nini una furaha tele?”
Shangazi Rose alimtazama kwa makini na kumuelekeza kwenye picha ambayo ilikuwa imening’inia ukutani. Ilikuwa zawadi kutoka kwa rafiki mpendwa mwenye kipaji.
”Ni kipi unachoona pale?” aliuliza.
Eva alikuwa ameshaitambua ile picha zamani, lakini hakuwa ameitazama kwa karibu. Msichana aliyekuwa ameva gauni la watangulizi alicheza kwa kuruka kamba katika njia ya rangi ya bluu angavu. Nyasi na miti ilikuwa rangi ya kijani kibichi cha kusisimua. Eva akasema, ”Ni mchoro wa picha ya msichana. Inaonekana ni kama anaruka kamba.”
”Ndio, ni msichana mtangulizi akiruka kamba kwa furaha,” Shangazi Rose alisema. ”Ninafikiri kulikuwepo na siku nyingi zenye giza na kuchosha kwa watangulizi. Maisha yao yalikuwa magumu mno—hatuwezi hata kufikiria. Lakini katika mchoro huu, kila kitu kinang’aa na ni chenye kutia matumaini. Msichana huyu ananesanesa kwa kutembea kwake, na anasonga mbele na juu.”
Eva alikuwa kimya, kwa hiyo Shangazi Mkubwa Rose aliendelea: “Yako mengi ya kutosha ambayo hayaendi sawa maishani, kwa hivyo mtu yeyote anaweza kujikuta katika kidimbwi cha kukosa rajua na shida yenye huzuni. Lakini nimewahi kuwajua watu ambao hata wakati mambo hayakuenda jinsi walivyotarajia, waliamua kulenga katika maajabu na miujiza ya maisha. Watu hawa ni watu wenye furaha zaidi ya watu ninaowajua.”
”Lakini, hauwezi tu kuwasha swichi kutoka kuwa mwenye huzuni na kuwa mwenye furaha,” Eva akasema.
“La, pengine haiwezekani,” Shangazi Rose alitabasamu kwa upole, “lakini Mungu hakutuumba tuwe na huzuni. Alituumba sisi tuwe na furaha!3 Kwa hivyo tukiwa na imani ndani Yake, Ataweza kutusaidia kutambua vile vilivyo bora na vya matumaini katika maisha. Na kwa hakika kabisa, dunia itakuwa angavu. La, hilo halifanyiki kwa mara moja, lakini kwa kweli, ni mangapi mazuri hutendeka? Inaonekana kwangu kuwa vitu vizuri zaidi, kama mkate wa kutengenezwa nyumbani au jemu ya machungwa, huhitaji subira na kazi.”
Eva alifikiri kuhusu hayo kwa muda kiasi na akasema, ”Pengine sio rahisi kwa wale watu ambao mambo yote si shwari maishani mwao.”
”Mpendwa Eva, je unafikiri kuwa kabisa maisha yangu ni kamili?” Aliketi naye Eva kwenye sofa iliyoshindiliwa kupita kiasi. ”Hata kuna wakati ambapo nilikuwa nimekufa moyo, na sikuona maana yoyote ya kuendelea.”
”Wewe?” Eva akauliza.
Shangazi Rose akaashiria kwa kichwa. ”Kuna vitu vingi nilivyovitaka maishani mwangu.” Vile alizungumza, sauti yake ilikuwa na huzuni ambayo Eva hakuwa amewahi kuisikia mwanzoni. ”Mengi kati ya hayo hayajatendeka. Ilikuwa ni kuvunjika moyo kumoja baada ya kwingine. Siku moja nilikuja kugundua kuwa maisha yangu hayangekuwa jinsi ambavyo nilitarajia. Hiyo ilikuwa siku ya kusononesha. Nilikuwa tayari kukata tamaa na kujidhalilisha.
”Kwa hivyo ulifanya nini?”
”Si kufanya kitu kwa muda. Nilikuwa na hasira tu. Sikuwa mtu mzuri kuwa karibu naye.” Halafu akacheka kidogo, lakini hakikuwa kicheko chake cha kawaida cha sauti juu, kilichoenea chumbani. ”’Sio haki’ ndio wimbo nilioimba kila mara kichwani mwangu. Lakini nilikuja kugundua kitu kimoja ambacho kilibadili maisha yangu yote.”
”Ilikuwa ni nini?
”Imani,” Shangazi Rose alitabasamu. ”Mimi niligundua imani. Na imani ikaleta tumaini. Na imani na tumaini vilinifanya kuamini kuwa siku moja ningepata kuelewa kila kitu, kwa sababu ya Mwokozi, makosa yote yatakuja kurekebishwa. Baada ya hapo, niliona kuwa njia iliyokuwa mbele yangu haikuwa ya kuchosha na vumbi vile nilivyokuwa nimedhania. Nilianza kuona anga ya bluu, rangi iliyong’aa ya kijani kibichi, na iliyo nyekundu kabisa, na nikaamua kuwa nilikuwa na chaguo la kufanya—ningeweza kuinamisha kichwa changu na kukokota miguu yangu kwenye barabara hiyo yenye vumbi ya kujihurumia, ama ningekuwa na imani kidogo, nivae nguo yenye kung’aa, nivae viatu vyangu vya kukatika, na nirukeruke chini ya barabara ya maisha, huku nikiimba.” Sasa sauti yake ilikuwa ikiruka kama yule msichana kwenye picha.
Shangazi Rose alifikia ukingoni mwa meza na kuchukua maandiko yake yaliyokuwa yametumika sana na kuyaweka magotini. ”Sidhani kuwa nilikuwa na huzuni kiasi cha kuhitaji tiba—sina uhakika kama unaweza kujitibu ukiwa umeugua kiasi hicho. Lakini hakika nilikuwa nimejiingiza mwenyewe katika shida hii! Ndio, nilikuwa na kiza kwa siku kadhaa, lakini kununa na wasiwasi hakungebadili chochote—kulikuwa kunasababisha tu shida zaidi. Imani katika Mwokozi ilinifundisha kwamba bila kujali kile kilitokea awali, hadithi yangu ingeweza kuwa ya furaha”
”Unajuaje hayo?” Eva akauliza.
Shangazi Rose alifunua ukurasa katika Biblia yake na kusema, ”Inasema hivyo hapa:
”Mungu ... naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao, na awe Mungu wao.
”Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”4
Shangazi Mkubwa Rose alimtazama Eva. Tabasamu lake lilikuwa pana huku akiongea kwa sauti ya chini, na kulikuwa na mtetemo kidogo katika sauti yake, ”Hilo sio jambo zuri kabisa ambalo umewahi kusikia?”
Ni kweli lilionekana kama jambo zuri, Eva alifikiria.
Shangazi Rose alifungua kurasa zingine chache kisha akazielekeza aya zile kwa Eva asome: ”Jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.”5
”Na siku kama hizi tukufu zijazo,” Shangazi Rose alisema, ”kwa nini tupotelee katika yaliyopita ama mambo ya sasa hivi ambayo huwa hayaendi kulingana na vile yalivyopangwa?”
Eva alikunja sura. ”Lakini subiri kidogo,” alisema. ”Je, unasema kwamba, kuwa mwenye furaha inamaanisha tu kutazamia furaha kwa siku za usoni? Je, furaha yetu yote inapatikana katika maisha ya milele? Je, hatuwezi kuwa na kiasi hapa?”
”Ah, bila shaka inawezekana!” Shangazi Rose akasema. ”Mtoto mpendwa, sasa ni sehemu ya maisha ya milele. Hayaanzi wakati tunapofariki! Inahusu kufungua macho yetu ili kuona furaha iliyo mbele yetu sasa hivi.
”Ninafahamu shairi ambalo linasema, ”Milele ni jumla ya sasa hivi nyingi.’6 Sikutaka milele yangu kuwa jumla ya huzuni na uoga wa ”hivi sasa.’ Na sikutaka kuishi katika ghala la huzuni, nikisaga meno, kufunga macho yangu, na kuvumilia hadi mwisho kwa shingo upande. Imani ilinipa tumaini nililohitaji kuishi kwa furaha sasa!”
”Kwa hivyo ni kipi ulichofanya?” Eva akauliza.
”Niliweka imani ndani ya ahadi za Mungu kwa kushiriki katika kutenda mambo ya maana maishani mwangu. Nilienda shuleni. Nikapata elimu. Hiyo ikaniongoza kupata kazi niliyoipenda.”
Eva alifikiri kwa muda na akasema, ”Lakini kusema kweli kuwa na shughuli nyingi sio kilichokufanya kuwa na furaha. Kuna watu wengi wenye shughuli nyingi ambao hawana furaha.”
”Unawezaje kuwa na busara hivi kwa mtu mwenye umri mdogo?” Shangazi Rose aliuliza. ”Umesema kweli kabisa. Na wengi wa hao watu walio na shughuli nyingi mno, wamesahau kitu kimoja cha muhimu sana katika dunia nzima—kitu ambacho Yesu alisema ni moyo wa injili Yake.
”Na ni nini hicho?” Eva akauliza.
Ni upendo—upendo halisi wa Kristo,” Rose alisema. “Unaona, kila kitu kingine katika injili—kila tenda hivi na lazima na utafanya hivi —zinaongoza kwenye upendo. Tunapompenda Mungu, tunataka kumtumikia. Tunataka kuwa kama Yeye. Tunapowapenda majirani zetu, sisi huacha kufikiria sana juu ya shida zetu na kuwasaidia zao.7
Na hilo ndilo linalotufanya tuwe wenye furaha?” Eva akauliza.
Shangazi Mkubwa Rose aliashiria kwa kichwa na kutabasamu, huku machozi yakimlenga machoni. ”Ndio, mpendwa. Hilo ndilo linatufanya kuwa na furaha.”
Daima akiwa amebadilika
Siku iliyofuata Eva alimkumbatia Shangazi Mkubwa Rose na kumshukuru kwa yote aliyokuwa amefanya. Alirudi nyumbani kwa familia yake na marafiki zake, na nyumba yao, na mtaa wao.
Lakini hakuwa tena kama vile alivyokuwa awali.
Vile Eva aliendelea kuwa mtu mzima, mara nyingi alifikiri kuhusu maneno ya Shanga Mkubwa Rose. Hatimaye Eva aliolewa, na kulea watoto, na kuishi maisha mazuri marefu.
Na siku moja, alipokuwa amesimama ndani ya nyumba yake, akivutiwa na mchoro wa msichana aliyekuwa amevalia gauni la watangulizi akiruka njia ya bluu angavu, aligundua kuwa alikuwa amefikia umri sawa na ule wa Shangazi Mkubwa Rose wakati wa yale majira ya ajabu ya joto.
Alipogundua hili, alihisi maombi maalum ndani ya roho yake. Na Eva akahisi shukrani kwa maisha yake, kwa familia yake, kwa injili ya Yesu Kristo iliyorejeshwa, na kwa majira ya joto kitambo sana wakati Shangazi Mkubwa Rose8 alipoimfunza kuhusu imani, tumaini na upendo.9
Baraka
Dada zangu wapendwa katika Kristo, natumaini na kuomba kuwa kitu fulani katika hadithi hii kiguse mioyo wenu na kuwapa msukumo wa nafsi. Mimi najua kwamba Mungu yu hai na kwamba Yeye anawapenda.
Mnapotembea katika njia yenu angavu ya uanafunzi, mimi naomba kwamba imani itaimarisha kila hatua katika njia yenu; kwamba tumaini litafungua macho yenu kwa utukufu wa Baba wa Mbinguni aliowahifadhia ninyi; na kwamba upendo wa Mungu na watoto Wake wote utajaza mioyo yenu. Kama Mtume wa Bwana, naacha haya, kama ushuhuda na baraka zangu, katika jina la Yesu Kristo, amina.