2010–2019
Barabara na Safi: Kuwa Mwenye Kustahili Hekaluni—Kwa Nyakati Nzuri Na Nyakati Mbaya
Oktoba 2015


15:36

Barabara na Safi: Kuwa Mwenye Kustahili Hekaluni—Kwa Nyakati Nzuri Na Nyakati Mbaya

Kushikilia kanuni takatifu za injili kutatuwezesha kuwa wastahiki wa hekaluni, kupata furaha katika maisha haya na kutuongoza kurejea nyumbani mbinguni.

Nabii Lehi alitangaza, “Kama hakuna utakatifu hakuna furaha.”1

Adui amefanikiwa katika kupanda uwongo mkubwa akilini mwa watu wengi. Yeye na wawakilishi wake wanatangaza kwamba uchaguzi wa kweli tulionao ni kati ya furaha na starehe sasa katika maisha haya na furaha katika maisha yajayo (ambayo adui anayadai inawezekana yasiwepo). Uwongo huu ni uchaguzi usio kweli, lakini ni wakuvutia sana.2

Hatimaye sababu kuu adilifu ya mpango wa furaha wa Mungu ni kwa wafuasi wenye haki na familia za agano zitaunganishwa katika upendo, upatanifu, na amani katika maisha haya3 na kufikia utukufu wa selestia milele pamoja na Mungu Baba, Muumba wetu, na Mwanawe Mpendwa,Yesu Kristo, mwokozi wetu.4

Nilipokuwa mmisionari kijana niliyepangiwa misheni ya Uingereza, sehemu ya kwanza niliyohudumia ilikuwa kule kulikoitwa wakati ule Wilaya ya Bristol. Mmoja wa viongozi wenyeji alisistiza kwamba wamisionari wanaohudumia eneo lile walihitaji kuwa barabara na safi kama Bristol.

Meli Bandarini Bristol

Hapo mwanzo, sikuelewa wazo alilokuwa anamaanisha. Mara nilijifunza historia na maana ya kirai cha kibaharia “barabara na safi kama Bristol.” Wakati fulani Bristol ilikuwa bandari ya pili kwa shughuli nyingi katika Uingereza. Ilikuwa na maji mengi ya kujaa ya futi 43 (mita 13), ilikuwa ya pili ulimwenguni. Wakati wa maji kupwa wakati maji yamepungua, meli nzee zilifika chini ya bahari na kulala kiubavu, na kama meli hazikujengwa vizuri, zingeweza kuharibika. Pia, kila kitu ambacho hakikuhifadhiwa kwa uangalifu au kufungwa madhubuti kingetupwa kivurumai na kuharibika au kuangamia.5 Baada ya kuelewa nini kishazi kile kilimaanisha, ilikuwa ni wazi kwamba kiongozi huyu alikuwa anatuambia kwamba, kama wamisionari, lazima tuwe waadilifu, tufuate sheria, na tuwe tayari kwa hali ngumu.

Changamoto sawa na hii inatumika kwa kila mmoja wetu. Ningeeleza kuwa “kuwa barabara na safi kama Bristol” kama kuwa “wastahiki wa hekaluni—katika nyakati nzuri na katika nyakati mbaya.

Huku mabadiliko ya maji kujaa na kupwa katika Mlangobahari wa Bristol kwa kiasi fulani kunatabirika na kunaweza kujitayarishiwa, kwa matatizo na majaribu ya maisha haya mara kwa mara hayatabiriki. Lakini haya twayajua: yatakuja! Ili tushinde changamoto ambazo kila mmoja wetu atapambana nazo, itahitaji matayarisho ya kiadilifu na matumizi ya ulinzi uliotolewa wa kiungu Hatuna budi kuamua kuwa wastahiki wa hekaluni bila kujali majaribu na vishawishi tunayokumbana nayo. Kama mmejitayarisha hamtaogopa.6

Furaha katika maisha haya na furaha katika maisha yajayo imeunganishwa na uadilifu. Hata katika kipindi kati ya kifo na ufufuo, “roho za wale ambao ni wenye haki zinapokewa kwenye hali ya furaha, ambayo inaitwa paradizo, hali ya kupumzika, hali ya amani.”7

Katika mwanzo wa huduma ya dunianiya Mwokozi katika Israeli na baadaye miongoni mwa Wanefi, Mwokozi alizungumzia kuhusu suala la furaha kote katika maisha haya na ya milele. Yeye alisisitiza ibada, lakini pia Aliweka mkazo mkubwa kwenye uadilifu wa tabia. Kwa mfano, wafuasi watabarikiwa kama watakuwa na njaa na kuwa na kiu kwa ajili ya haki, kuwa wenye huruma, kuwa wenye moyo safi, kuwa wapatanishi, na kufuata kanuni zingine za msingi. Kwa hakika kama ujumbe wa kimsingi wa kimafundisho, Bwana wetu Yesu Kristo alisisitiza vyote mtazamo wa haki na tabia katika maisha ya kila siku. Mafundisho yake hayakurudisha tu na kuzidi vipengele vya sheria ya Musa8 lakini pia kulikuwa na kukataliwa kwa falsafa za uwongo za binadamu.

Kwa karne nyingi, injili ya Yesu kristo imevutia imani nyingi na imeanzisha viwango vya tabia kuhusiana na kile chema, kinachotamanika, na uadilifu na matokeo katika furaha, baraka, na shangwe. Hata hivyo, kanuni na uadilifu wa msingi ambazo Mwokozi alifundisha ziko chini ya shambulizi la hatari katika ulimwengu wa sasa. Ukristo unashambuliwa. Wengi wanaamini kwamba kile kilicho adilifu kimsingi kimebadilika.9

Tunaishi nyakati za shida. Kuna ongezeko la mwelekeo wa “kuita uovu ni wema na wema ni uovu.”10 Ulimwengu unaosisitiza kujitwaza binafsi, na malimwengu kunatia hofu sana. Mwandishi mmoja mashuhuri, ambaye siye muumini wa dini yetu, amesema hivi: Kwa bahati mbaya naona ushahidi mdogo kwamba watu kwa hakika hufurahi mno katika kipindi cha muda tunaoingia, ama kwamba watoto wao wako katika hali mzuri, ama kwamba kusudi la haki ya jamii alijashughulikiwa vyema, ama kwamba kushuka kwa kiasi cha ndoa na kupungua kwa uzazi … kunaahidi chochote zaidi isipokuwa upweke mkubwa kwa walio wengi, na kwa ujumla kukwama kwa maendeleo.11

Kama wafuasi wa Mwokozi, tunategemewa kupanga na kutayarisha. Katika mpango mkuu wa furaha, uadilifu wa kuchagua ni kitovu cha kupanga kanuni na uchaguzi wetu una maana.12 Mwokozi alisisitiza hili kupitia huduma Yake, pamoja na mafumbo yake mabikira wajinga na talanta.13 Katika kila moja wapo ya hali hizi, Bwana alitukuza matayarisho na matendo na alishutumu uahirishaji na uvivu.

Natambua kwamba, licha ya kujawa na furaha ambayo inakuja kutoka kwa mpango mtakatifu wa Mungu, wakati mwingine inaweza kuhisika mbali sana na imetenganishwa kutoka hali ya wakati wetu wa sasa. Inaweza kuhisika mbali na mfiko wetu kama wafuasi wa wanaojitahidi. Kutoka kwa mtazamo wetu finyu, majaribu ya sasa na vishawishi vinaweza kuonekana kuvutia. Zawadi kwa kushinda majaribu haya, kinyume, inaweza kuhisiwa mbali na isiyofikika. Lakini uelewa wa kweli wa mpango wa Baba unaonyesha kwamba zawadi za wema zinapatikana sasa hivi. Uovu, kama vile tabia utovu wa maadili, kamwe si sehemu ya jibu. Alma alisema waziwazi kwa mwanawe Koriantoni: Tazama, nakwambia, uovu haujapata kuwa furaha14.

Mafundisho yetu yameelezwa kwa wazi wazi na Amuleki katika Alma 34:32: ”Kwani tazama, maisha haya ndiyo wakati wa watu kujitayarisha kukutana na Mungu; ndio, tazama, wakati wa maisha haya ndiyo siku ya watu kufanya kazi yao wanayohitaji.”

Vipi, basi tunajitayarisha katika wakati mgumu kama huu? Pamoja na nyongeza kuwa wastahiki wa hekaluni, kuna kanuni nyingi ambazo zinachangia kwenye wema. Nitasisitiza tatu.

Kwanza: Maadili ya Kujithibiti Nafsi na Mwenendo

Ninaamini kwamba wakati mwingine Baba yetu aliye Mbinguni mwenye upendo lazima atutazama sisi kwa furaha tunayohisi wakati tunawatazama watoto wetu wadogo wanapojifunza na kukua. Sote tunajikwaa na kuanguka tunapopata uzoefu.

Jaribio la Marshmallow

Nilipendezwa na hotuba katika mkutano mkuu ambao Rais Dieter F. Uchtdorf aliitoa mwaka 201015 kuhusu jaribio maarufu ya marshmallow lililofanywa katika Chuo Kikuu cha Stanford miaka ya 1960. Mtakumbuka kwamba watoto wa miaka mine walipewa marshmallow moja. Kama wangeweza kungoja kwa muda wa dakika 15 ama 20 bila kuila, wangepata marshmallow ya pili. Video zilitolewa zikionesha upindaji viungo watoto wengi walifanya ili kujizuia kula marshmallow. Wengine hawakufaulu.16

Mwaka jana profesa aliyeongoza jaribio la asili,Dr. Walter Mischel, aliandika kitabu ambacho alisema utafiti ule ulitokana kwa kiasi fulani kutoka mfadhaiko kuhusu kujithibiti nafsi na mazoea yake ya uvutaji sigara. Alikuwa amefadhaika hasa baada ya ripoti ya Daktari Mkuu wa Upasuaji wa Marekani ya mwaka 1964 kuamua kwamba kuvuta sigara kulisababisha saratani ya mapafu.17 Kutokana na utafiti wa miaka mingi, mmojawapo wa washiriki wake aliripoti kwamba “kujithibiti nafsi ni kama msuli: unavyoutumia zaidi, ndivyo unavyopata nguvu. Kujizuia kitu fulani cha kukujaribu mara moja kutakusaidia kujenga uwezo wa kushinda majaribu mengine katika siku za usoni.”18

Kanuni ya maendeleo ya milele ni kutumia kujithibiti nafsi na kuishi kwa uadilifu kunaimarisha uwezo wetu wa kushinda majaribu. Hii ni kweli kote katika ulimwengu wa kiroho na katika mambo ya kimwili.

Wamisionari wetu ni mfano mzuri sana. Wanajenga sifa kama za Kristo na kusisitiza utii na mambo ya Kiroho. Wanatarajiwa kufuata ratiba inayowahitaji kutumia siku zao katika huduma za wengine. Wana mwonekano wa adabu, wa kushika kanuni badala ya mavazi ya kawaida au ukosefu wa maadili katika mavazi ambao umezidi siku hizi. Mwenendo wao na mwonekano unaonyesha ujumbe wa uadilifu na makini.19

Tuna takribani vijana 230,000 ambao wakati huu wanahudumu kama wamisionari au ambao wamerudi kutoka huduma ya umisionari katika miaka mitano iliyopita. Wamejenga nguvu za kiroho za ajabu na kijiongoza ambazo zinahitaji kufanyiwa mazoezi kila mara, au tabia hizi zitafifia kama ile misuli ambayo haitumiki. Sisi sote tunahitaji kukuza na kuonyesha tabia na mwonekano ambao unatangaza sisi ni wafuasi wa kweli wa Kristo. Wale ambao wanaacha aidha tabia ya uadilifu au mwonekano wote wa staha wanajifunua wenyewe kwa aina ya maisha ambayo hayaleti shangwe wala furaha.

Injili ya urejesho inatupa utaratibu wa mpango wa furaha na motisha kuelewa na kujithibiti nafsi na kujizuia majaribu. Pia inatufundisha jinsi ya kutubu wakati ukiukaji umetokea.

Pili: Kuheshimu Sabato Kutaongeza Uadilifu na Kuwa Ulinzi kwa Familia

Kanisa la Kikristo la kale lilibadili maadhimisho ya Sabato kutoka Jumamosi kuwa Jumapili kuadhimisha ufufuo wa Bwana. Sababu zingine takatifu za msingi za Sabato zilibaki hazikubadilishwa. Kwa Wayahudi na Wakristo, Sabato inaashiria kazi kubwa za Mungu.20

Mke wangu nami na wenzangu wangu wawili na wake zao, hivi majuzi tulishiriki katika Shabbat (Sabato) ya Kiyahudi kwa mwaliko wa rafiki mpendwa, Robert Abrams na mke wake, Diane nyumbani kwao New York.21 Ilianza mwanzoni mwa Sabato ya Kiyahudi Ijumaa jioni. Kiini kilikuwa kumheshimu Mungu kama Muumbaji. Ilianza kwa kubariki familia na wimbo wa Sabato.22 Tulijiunga katika ibada ya kunawa mikono, kubariki mkate, sala, mlo wa kosher, utongoaji wa maandiko, na kuimba nyimbo za Sabato katika hali ya kusherekea. Tulisikiliza maneno ya Kiebrania, yakifuatiwa na tafsiri ya Kiingereza. Maandiko yenye mguso sana iliyosomwa kutoka Agano la Kale,ambayo pia ni yenye wakifu kwetu, yalikuwa kutoka kwa Isaya, yakitangaza Sabato ya furaha,23 na kutoka Ezekieli, kwamba Sabato ”itakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”24

Fikra iliyotujaa kutoka jioni hii ya ajabu ilikuwa upendo wa familia, moyo wa ibada, na uwajibikaji kwa Mungu. Wakati nilipofikiria kuhusu tukio hili, mateso makali ambayo Wayaudi wameyapitia katika karne zilizopita. Ni wazi, kuiheshimu Sabato kumekuwa “agano la kudumu,” kuhifadhi na kubariki watu wa Kiyahudi katika utimilifu wa maandiko.25 Pia inechangia kwa maisha kifamila ya ajabu na furaha ambayo ni wazi katika maisha ya watu wengi wa Kiyahudi.26

Kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kuiheshimu Sabato ni aina ya wema ambao utabariki na kuimarisha familia, kutuunganisha sisi na Muumba, na kuongeza furaha. Sabato inaweza kututenganisha kutoka kile ambacho ni cha upuuzi, kisichofaa, ama kisicho adilifu. Inaturuhusu kuwa ulimwenguni, lakini si wa ulimwengu.

Katika miezi sita iliyopita, mabadiliko ya ajabu sana yametokea katika Kanisa. Hii imekuwa katika kujibu msisitizo uliorudiwa upya kwa waumini juu ya Sabato na Urais wa Kwanza na Akidi ya Wale Kumi na wawili na kwa changamoto ya Rais Russell M. Nelson kufanya Sabato kuwa furaha.27 Waumini wengi wanaelewa kwamba kuitukuza kikweli siku ya Sabato takatifu ni kimbilio kutoka dhoruba za maisha haya. Pia ni ishara ya moyo wetu wa ibada kwa Baba yetu wa Mbinguni na ongezeko la uelewa wa utukufu wa mkutano wa sakramenti. Bado, tuna mengi ya kuboresha, lakini tuna mwanzo wa ajabu. Natoa changamoto kwetu wote kuendelea kukubali kabisa ushauri huu na kuboresha ibada yetu ya Sabato.

Tatu: Ulinzi Mtakatifu Hutolewa Wakati Tunapokuwa Waadilifu

Kama sehemu ya mpango mtakatifu wa Mungu, tumebarikiwa na karama za Roho Mtakatifu. Karama hii “ni haki ya kuwa,wakati wowote mtu anapostahili, wenza wa Roho Mtakatifu.”28 Huyu mshiriki wa Uungu anahudumu kama mnadhifishaji kama injili ni kipaumbele katika maisha yetu. Pia ni sauti ya onyo dhidi ya uovu na sauti ya ulinzi dhidi ya hatari. Tunaposafiri katika bahari ya maisha, kufuata maono ya Roho Mtakatifu ni muhimu. Roho atatusaidia kujizuia majaribu na hatari, na kutufariji na kutuongoza hadi mwisho wa changamoto. ”Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, upole, utu wema, imani.”29

Kushikilia kanuni takatifu za injili kutatuwezesha kuwa wastahiki wa hekaluni, kupata furaha katika maisha haya na kutuongoza kurejea nyumbani mbinguni.

Ndugu na dada zangu wapendwa, maisha si rahisi, wala hayakutakiwa yawe hivyo. Ni muda wa kupimwa na kujaribiwa. Kama meli za kale katika Bandari ya Bristol, kutakuwa na muda wakati wa maji kupwa na inaonekana kama kwamba kila kitu katika ulimwengu huu kinachofanya tuelee kimepotea. Tunaweza kufika chini ya bahari na hata kuinama upande. Wakati wa majaribu haya, ninawaahidi kwamba kuishi na kudumisha maisha ustahiki wa hekalu kutatushikamanisha na yale yote yenye maana. Baraka tamu za amani, furaha, na shangwe, pamoja na baraka za maisha ya milele na utukufu wa selestia pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe,Yesu Kristo zitapatikana. Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. 2 Nefi 2:13 . Maandiko haya ni sehemu ya usambamba katika Kitabu cha Mormoni. Inashangaza kwamba wengi wa manabii ambao maandishi na mahubiri yamejumuishwa katika Kitabu cha Mormoni walitumia mfumo huu wa fasihi kusisitiza umuhimu wa dhana za kimafundisho. Ona, kwa mfano, 2 Nefi 9:25 (Yakobo) na 2 Nefi 11:7 (Nefi).

  2. Ona 2 Nefi 28.

  3. Ona 4  Nefi 1:15–17.

  4. Ona Mafundisho na Maagano 59:23.

  5. Ona Wiktionary, “shipshape and Bristol fashion.”

  6. Ona Mafundisho na Maagano 38:30.

  7. Alma 40:12; mkazo umeongezewa.

  8. Ona Mathayo 5, muhtasari wa sura.

  9. Ona Carl Cederstrom, “The Dangers of Happiness,” New York Times, July 19, 2015, Sunday Review section, 8.

  10. 2 Nefi 15:20 PM.

  11. Ross Douthat, “Gay Conservatism and Straight Liberation,” New York Times, June 28, 2015, Sunday Review section, 11.

  12. Ona 2 Nefi 2.

  13. Ona Mathayo 25:1–30.

  14. Alma 41:10.

  15. Ona Dieter F. Uchtdorf, “Continue in Patience,” Liahona, May 2010, 56.

  16. Ona Walter Mischel, The Marshmallow Test: Mastering Self-Control (2014); see also Jacoba Urist, “What the Marshmallow Test Really Teaches about Self-Control,” Atlantic, Sept. 24, 2014, theatlantic.com.

  17. Ona Mischel, The Marshmallow Test, 136–38.

  18. Maria Konnikova, “The Struggles of a Psychologist Studying Self-Control,” New Yorker, Oct. 9, 2014, newyorker.com, Alimnukuu Roy Baumeiter, profesa wa saikologia katika Chuo Kikuu cha Jimbo cha Florida ambaye hufanya utafiti wa kujiamini na kujithibiti nafsi.

  19. Ona Malia Wollan, “How to Proselytize,” New York Times Magazine, July 19, 2015, 21. Yeye anamnukuu Mario Dias Kituo cha Mafunzo ya Missionari Brazili.

  20. Ona Bible Dictionary, “Sabbath.”

  21. Elder Von G. Keetch na mkewe, Bernice, na John Taylor na mkewe, Jan, waliungana na mke wangu nami katika Shabbat ya furaha pamoja na Robert Abrams na mkewe, Diane, mnamo Mei 8, 2015. Mr. Abrams alikuwa amehudumu kama wakili mkuu wa jimbo la New York na rafiki ya Kanisa kwa miaka mingi. Mr. Abrams pia aliwaalika wenzake wawili wa Kiyaudi pamoja wake wao.

  22. The Sabbath table hymn Shalom Aleichem (“Peace upon You”) was sung.

  23. Ona Isaya 58:13–14.

  24. Ezekieli 20:20.

  25. Ona Kutoka 31:16–17.

  26. Ona Joe Lieberman, The Gift of Rest: Rest:Rediscovering the Beauty of the Sabbath (2011). Kitabu cha kufurahisha cha Senata Lieberman kinaeelzea Shabbat na kutoa umaizi wenye maongozi.

  27. Ona Isaya 58:13–14; ona pia Russell M. Nelson, “The Sabbath Is a Delight,” Liahona, May 2015, 129–32.

  28. Bible Dictionary, “Holy Ghost.”

  29. Wagalatia 5:22.