2010–2019
Kamwe Si Mapema Sana na Kamwe Hatujachelewa Sana
Oktoba 2015


10:19

Kamwe Si Mapema Sana na Kamwe Hatujachelewa Sana

Kamwe si mapema sana na kamwe hatujachelewa sana kuongoza, kuelekeza, na kutembea kando ya watoto wetu kwa sababu familia ni za milele.

Kina ndugu na dada, tunakumbana vita na ulimwengu. Zamani, ulimwengu ulishindania nguvu na wakati wa watoto wetu. Leo unapigania utambulisho wao na akili. Sauti nyingi kubwa na maarufu zinajaribu kufafanua watoto wetu ni nani, na kile wanapaswa kuamini. Hatuwezi kuruhusu jamii kugeuza familia zetu kuwa katika sura ya ulimwengu. Ni lazima tushinde vita hivi. Kila kitu kinaitegemea .

Watoto wa Kanisa huimba wimbo unaowafundisha kuhusu utambulisho wao halisi: “Mie mwana wa Mungu. ... Kanileta hapa, kanipa wazazi wema, na makao mema.” Kisha, ombi la watoto kwetu: “Niongoze, nielekeze, tembea kando yangu. ... Nisaidie nielewe haraka manenoYake kabla haijachelewa.”1

Rais Russell  M. Nelson alitufundisha katika mkutano wetu mkuu uliopita kwamba, kuanzia hapa kwenda mbele, ni lazima tujihusishe katika “malezi ya dhamira.”2 Hizi ni nyakati za hatari. Lakini habari njema ni kwamba Mungu alijua hali itakuwa hivi, na Ametoa shauri katika maandiko kwetu ili tujue jinsi ya kusaidia watoto wetu na wajukuu wetu.

Mwokozi na watoto wa Kitabu cha Mormoni

Katika Kitabu cha Mormoni, Mwokozi alijitokeza kwa Wanefi. Alikusanya watoto wao wadogo kando Yake. Aliwabariki, akawaombea, na kulia juu yao.3 Kisha akawaambia wazazi, “Tazameni wachanga wenu.”4

Neno tazama linamaanisha kuangalia na kuona. Yesu alitaka wazazi waone nini katika watoto wao wachanga? Je, aliwataka waelewe uwezo wa kiungu wa watoto wao?

Tunapoangalia watoto wetu na wajukuu wetu leo, Mwokozi anataka tuone nini kwao? Je, tunatambua kwamba watoto wetu ndio kundi kubwa zaidi ya wachunguzi wa Kanisa? Tutafanya nini ili tuwezeshe uongofu wao wa kudumu?

Katika kitabu cha Mathayo, Mwokozi atufundisha kuhusu uongofu wa kudumu. Kundi kubwa la watu lilikuwa limekusanyika karibu na Bahari ya Galilaya ili kumsikia Akifundisha.

Katika tukio hili, Yesu aliwaambia hadithi kuhusu kupanda mbegu—fumbo la mpanzi.5 Katika kueleza haya kwa wanafunzi Wake, na hatimaye kwetu, Alisema, “Ila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake.”6 Ujumbe kwa wazazi ni wazi: kuna tofauti kati ya kusikia na kulewa. Kama watoto wetu watasikia tu bali hawaelewi injili, basi mlango unaachwa wazi kwa Shetani kuondoa ukweli huo kutoka nyoyo zao.

Hata hivyo, kama tunaweza kuwasaidia kukuza mizizi ya uongofu kwa kina, basi katika joto la mchana, wakati maisha haya yanakuwa magumu— na itakuwepo—injili ya Yesu Kristo kuwapa kitu ndani yao ambacho hakiwezi kuathirika kutoka nje. Tunawezaje kuhakikisha kwamba kweli hizi za nguvu hazipitii tu katika sikio moja na kutoka nje na nyingine? Kusikia maneno tu pengine haitoshi.

Sote tunajua kwamba maneno hubadilika. Wakati mwingine tunasema maneno yetu, nao husikia maneno yao. Unaweza kusema kwa watoto wako wachanga, “Unasikika kama santuri iliyovunjika.” Pengine wao watajibu, “Baba, santuri ni nini?”

Baba yetu wa Mbinguni anataka tufanikiwe kwa sababu hakika, walikuwa watoto Wake kabla wawe wetu. Kama wazazi katika Sayuni, mmepokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Mnapoomba kwa ajili ya uongozi, “atawaonyesha vitu vyote ambavyo mnastahili kutenda”7 katika kuwafundisha watoto wenu. Unapokuza michakato ya kujifunza, “Roho Mtakatifu huyapeleka katika mioyo ya watoto.”8

Siwezi kufikiria mfano mzuri wa kusaidia mtu kupata uelewa kuliko hadithi ya Helen Keller. Alikuwa kipofu na kiziwi, na aliishi katika dunia iliyokuwa giza na tulivu. Mwalimu aitwaye Anne Sullivan alikuja kumsaidia. Unawezaje kumfundisha mtoto ambaye hawezi hata kuona au kukusikia?

Helen Keller na Anne Sullivan

Kwa muda mrefu, Anne alijitahidi kuwasiliana na Helen. Siku moja mwendo wa mchana, alimpeleka nje kwa pampu ya maji. Aliweka mkono mmoja wa Helen chini ya mfereji wa maji na kuanza kusukuma maji. Anne kisha akakariri neno M - A - J - I kwenye mkono mwingine wa Helen. Hakuna kilichotokea. Hivyo akajaribu tena. M - A - J - I. Helen akafinya mkono wa Anne kwa sababu alianza kuelewa. Kufikia jioni, alikuwa amejifunza maneno 30. Kwa miezi kadha, alikuwa amejifunza maneno 600 na alikuwa na uwezo wa kusoma Braille. Helen Keller aliendelea na kupata shahada ya chuo na kusaidia kuleta mabadiliko ulimwenguni kwa watu ambao hawakuweza kuona au kusikia.9 Ilikuwa ni miujiza, na mwalimu wake alikuwa ndiye mtenda miujiza, wazazi, kama vile ninyi mtavyokuwa.

Niliona matokeo ya mwalimu mwingine wa ajabu nilipokuwa nikihudumu kama rais wa kigingi cha waseja wazima huko BYU-Idaho. Tukio hilo lilibadilisha maisha yangu. Siku moja Jumanne jioni, nilimhoji kijana mmoja aliyeitwa Pablo, kutoka Jiji la Mexico, aliyetaka kuhudumu katika misheni. Nilimwuliza kuhusu ushuhuda wake na nia yake ya kuhudumu. Majibu yake kwa maswali yangu yalikuwa kamilifu. Kisha mimi nikamwuliza kuhusu ustahiki wake. Majibu yake yalikuwa halisi. Kwa kweli, yalikuwa mazuri sana, hata nilijiuliza, “Labda haelewi kile ninachomwuliza.” Kwa hiyo nikauliza maswali kwa njia nyingine na kujua ya kwamba alijua vilivyo kile nilichomaanisha na kuwa alikuwa mwaminifu kabisa.

Nilivutiwa sana na kijana huyu kiasi kwamba nilimuuliza, “Pablo, ni nani ambaye alikusaidia kufika mahali hapa pa maisha yako ukisimama wima mbele ya Mungu?”

Alisema, “Baba yangu.”

Nilisema, “Pablo, niambie hadithi yako.”

Pablo akaendelea: “Nilipokuwa na umri wa miaka tisa, baba yangu alinipeleka pembeni na akaniambia, ‘Pablo, hata mimi pia siku moja nilikuwa na miaka tisa. Haya ndio baadhi ya mambo unayoweza kupitia. Utaona watu wakidanganya shuleni. Unaweza kuwa karibu na watu wanaoapa. Pengine kutakuwa na siku ambapo hutaki kwenda kanisani. Sasa, utakapoona mambo kama haya yakitokea—au kitu chochote kinachokusumbua—Nataka wewe huje kwangu na uniambie, nami nitakusaidia kuyashinda. Na kisha nitakuambia kitakachofuata.”’

“Kwa hivyo, Pablo, alikwambia nini ulipokuwa umri wa miaka 10?”

“Naam, alinionya kuhusu picha za ngono na utani mchafu.”

“Je, na ulipokuwa umri wa miaka 11?” Niliuliza.

“Alinionya kuhusu mambo ambayo yanaweza kuleta anasa na kunikumbusha kuhusu kutumia wakala wangu.”

Hapa palikuwa na baba, mwaka baada ya mwaka, “mstari juu ya mstari, huku kidogo na huku kidogo,”10 aliyemsaidia mwanawe si tu kusikia lakini kuelewa. Babake Pablo alijua watoto hujifunza wanapokuwa tayari kujifunza, na si tu wakati tuko tayari kuwafundisha. Nilijivunia kuwa na Pablo tulipokuwa tukiwasilisha maombi yake ya umisionari usiku huo, lakini nilijivunia hata zaidi juu ya babake Pablo.

Nikiendesha gari kwenda nyumbani usiku huo, nilijiuliza, “Pablo atakuwa baba wa aina gani?” Na jibu lilikuwa wazi kabisa: atakuwa kama baba yake. Yesu alisema, “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda.”11 Hiki ni kielelezo cha jinsi Baba wa Mbinguni huwabariki watoto Wake kutoka kizazi hadi kizazi.

Nilipoendelea kufikiria kuhusu uzoefu wangu na Pablo, nilihuzunika kwa sababu mabinti wangu wanne walikuwa wamekua na wajukuu tisa niliokuwa nao wakati huo hawakuishi karibu. Kisha nikafikiria “Nitawezaje kuwasaidia jinsi babake Pablo alivyomsaidia? Wakati mwingi ulikuwa umepita?” Nilipotoa maombi moyoni mwangu, Roho alinong’onezea ukweli huu: “Si mapema sana na kamwe sijachelewa sana kuanza mchakato huu muhimu.” Nilijua mara moja maana yake ilikuwa nini. Singesubiri kurudi nyumbani. Niliuliza mke wangu, Sharol, kuwaita watoto wetu wote na kuwaambia kwamba tulitaka kuwatembelea; nilikuwa na kitu muhimu cha kuwaambia.  Haraka yangu iliwashangaza kidogo.

Tulianza  na binti yetu mkubwa na mume wake Nikasema: “Mama yako nami tungetaka mjue kwamba tulikuwa wa umri wenu siku moja. Tulikuwa umri wa miaka 31, na familia ndogo. Tunaelewa kile mnaweza kupitia. Inaweza kuwa changamoto ya kifedha au ya kiafya. Inaweza kuwa ni mgogoro wa imani. Mnaweza kuzidiwa na maisha. Wakati mambo haya yatakapotokea, nataka mzungumze na sisi. Tutawasaidia kuyashinda. Sasa, hatutaki kujiingiza katika maisha yenu wakati wote, lakini tunataka mjue kwamba tutawasaidia kila wakati. Tukiwa pamoja, nataka niwaambie kuhusu mahojiano niliokuwa nao na kijana mmoja jina lake Pablo.”

Baada ya masimulizi, nilisema, “Hatutaki mkose kusaidia watoto wenu na wajukuu wetu kuelewa ukweli huu muhimu.”

Ndugu na dada zangu, sasa natambua kwa njia ya maana zaidi kile Bwana anatarajia kutoka kwangu kama baba na babu katika kuanzisha mchakato wa kusaidia familia yangu si tu kusikia lakini kuelewa.

Ninapoendelea kuzee, najipata nikitafakari maneno haya:

Ee wakati, Ee wakati, rudi nyuma kwa upesi,

Na waache wawe watoto wangu wadogo kwa usiku moja tu zaidi!12

Najua siwezi kurudisha muda nyuma, lakini hii sasa ninajua—kwamba kamwe si mapema sana na kamwe sijachelewa sana kuongoza, kuelekeza, na kutembea kando ya watoto wetu kwa sababu familia ni za milele.

Ni ushuhuda wangu kwamba Baba yetu wa Mbinguni anatupenda sana, kiasi kwamba Alimtuma mwanawe wa pekee kuishi maisha ya duniani ili Yesu aweze kutuambia, “Nimekuwa mahali ulipo, najua kile kinachofuata, na nitakusaidia kukishinda.” Najua Yeye atafanya hivyo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “I Am a Child of God,” Hymns, no. 301.

  2. Ona Russell M. Nelson, “The Sabbath Is a Delight,” Liahona, May 2015, 131.

  3. Ona 3 Nefi 17:21.

  4. 3 Nefi 17:23 PM.

  5. Ona Mathayo 13:1–13.

  6. Mathayo13:19; mkazo umeongezewa.

  7. 2 Nefi 32:5.

  8. 2 Nefi 33:1.

  9. Ona “Anne Sullivan,” biography.com/people/anne-sullivan-9498826; “Helen Keller,” biography.com/people/helen-keller-9361967.

  10. Isaya 28:10.

  11. Yohana 5:19.

  12. Imetoholewa kutoka kwenye shairi la Elizabeth Akers Allen “Rock Me to Sleep,” katika William Cullen Bryant, ed., The Family Library of Poetry andSong (1870), 222–23.