2010–2019
Ziweke Amri
Oktoba 2015


14:24

Ziweke Amri

Yule ambaye aliyetuumba sisi na ambaye anatupenda kikamilifu anajua jinsi tunahitaji kuishi maisha yetu ili tupate furaha kuu iwezekanavyo.

Ndugu zangu wapendwa, ni furaha iliyoje kuwa nanyi tena. Tumepata maongozi jioni hii kutokana na maneno ambayo tumesia. Naomba pia nami niongozwe kwa yale nitakayosema.

Ujumbe wangu kwenu usiku wa leo ni bayana. Nao ni huu: tii amri.

Amri za Mungu hazijatolewa ili kutufisha moyo au kuwa vizuizi kwa furaha yetu. Ila tu kinyume ni kweli. Yeye ambaye alituumba na anayetupenda kikamilifu anafahamu jinsi tunavyohitaji kuishi maisha yetu ili tuweze kupata furaha kuu kabisa iwezekanavyo. Ametupa mwongozo ambao, tukiufuata, utatuelekeza salama katika safari hii ya maisha ya dunia ambayo mara nyingi ni hatari. Tunakumbuka maneno ya wimbo wa injili unaofahamika sana: ”Tii Amri! Katika hii kuna amani; katika hii kuna amani.”1

Baba yetu wa Mbinguni anatupenda kiasi cha kusema: Usidanganye; usiibe; usizini; mpende jirani yako kama nafsi yako; na kadhalika.2 Tunafahamu amri. Anaelewa kuwa tunapotii amri, maisha yetu yatakuwa na furaha tele, yaliyo makamilifu, na sio ya kutatanisha sana. Changamoto na shida zetu zitakuwa rahisi kuvumilia, na tutapokea baraka zake alizoahidi. Lakini anapotupatia sheria na amri, anaturuhusu pia kuchagua ikiwa tutakubali au kuzikataa. Uamuzi wetu katika suala hili utaamua hatima yetu.

Nina imani kuwa kila mmoja wetu ana lengo lake la mwisho maisha ya milele katika uwepo Baba wa Mbinguni na Mwana wake, Yesu Kristo walipo. Ni muhimu, kwa hivyo, kwetu sisi kufanya uchaguzi kwa maisha yetu yote ambao utatuelekeza kwa lengo hili. Tunafahamu, hata hivyo, kuwa adui ana nia yetu sisi kushindwa. Yeye na majeshi yake hawachoki katika jitihadi zao za kuangamiza matamanio yetu ya haki. Wanawakilisha tisho hatari na la daima kwa wokovu wetu wa milele ila nasi pia tusichoke katika azimio na jitihadi zetu za kutimiza lengo letu. Mtume Petro anatutahadharisha, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”3

Ingawa hakuna wakati katika maisha yetu ambapo tumeruhusiwa kutojaribiwa, nyinyi wavulana mko kwenye umri ambao hasa mnaweza kudhuriwa. Miaka ya ujana mara nyingi ni miaka ya wahaka, ya kuhisi kama kwamba hauhitimu, ya kujaribu kutafuta nafasi yako katika rika lako, na kujaribu kupatana na rika yako. Unaweza kujaribiwa kushusha viwango vyako na kufuata umati ili ukubaliwe na wale unaotamani wawe marafiki. Tafadhali kuwa imara, na tahadhari kwa chochote kinachoweza kukupokonya baraka za milele. Uchanguzi unaofanya hapa na sasa ni wa muhimu milele.

Tunasoma katika 1 Wakorintho:“Yamkini ziko … sauti za namna nyingi duniani.”4 Tumezingirwa na sauti za kuvutia, sauti za kulaghai, sauti za kudhalilisha, sauti staarabu na sauti za kuchanganya. Naweza kusema pia kwamba sauti hizi nikubwa. Nawaonya enyi mpunguze sauti na mshawishike badala yake na ile sauti ndogo tulivu, ambayo itawaongoza kwenye usalama. Kumbuka kuwa mtu fulani aliye na mamlaka aliweka mikono yake kwa kichwa chako baada ya kubatizwa; kukudhibitisha kama mshiriki wa Kanisa na kusema, ”Pokea Roho Mtakatifu.”5Fungueni mioyo yenu, hata nafsi zenu hasa, kwa ile sauti maalum ya yule anayeshuhudia ukweli. Vile nabii Isaya alivyoahidi, “Na masikio yako yatasikia neno … , likisema, Njia ni hii, ifuateni.”6 Na tuwe daima tayari kumsikiliza, ili tuweze kusikia hii sauti ya kuongoza, ya faraja ambayo itatukinga sisi.

Kutotii amri kumefungua njia kwa kile ninachofikiria kuwa ni mabaa makubwa sana katika siku zetu. Yanajumuisha baa la uhuru mwingi wa kuona na kutenda, baa la ponografia, baa la madawa ya kulevya, baa la uovu, baa la kuavya mimba, kutaja tu chache. Maandiko yanatuambia kwamba adui “ni [msingi] cha vitu hivi vyote.”7 Tunajua kwamba yeye ni “baba wa uwongo wote, ili kudanganya, na kuwapofusha watu.”8

Ninawasihi muepukane na chochote ambacho kitawapokonya furaha yenu hapa katika maisha ya dunia na maisha ya milele katika ulimwengu ujao. Kwa udanganyifu wake na uwongo, adui atakuelekeza chini kwenye mteremko ulioteleza hadi kuangamia kwako ukimruhusu kufanya hivyo. Kuna uwezekano kwamba utakuwa kwenye mteremko huo ulioteleza hata kabla hujagundua kwamba hakuna njia ya kusimama. Umesikia ujumbe wa adui. Anaita kwa ujanja: Hii mara moja tu haitajalisha; kila mtu anafanya hivyo; usifuate mitindo ya zamani; nyakati zimebadilika; haitamuumiza yeyote; maisha yako ni yako kuishi. Adui anatufahamu, na anajui majaribu ambayo yatakuwa magumu kwetu kupuuza. Ni muhimu kiasi gani kwetu kuwa daima waangalifu ili tuepukane na uwongo na majaribu kama haya.

Ujasiri mkubwa utahitajika tunapoendelea kuwa waaminifu na wakweli katikati mwa shinikizo zinazozidi kuongezeka na athari zinazosambaa bila ya kujulikana ambazo zimetuzingira na ambazo zinapotosha ukweli, kuharibu mazuri na yanayoheshimika, na kujaribu mbadala kuwa na falsafa za dunia za binadamu. Ikiwa amri zingekuwa zimeandikwa na binadamu, basi kuzibadili kwa kupendelea au sheria au kwa njia nyingine yeyote ingekuwa uamuzi wa mwanadamu. Amri, hata hivyo, zilitolewa na Mungu. Tukitumia wakala wetu, tunaweza kuzitupilia mbali. Hatuwezi, hata hivyo, kubadili kama, vile tu hatuwezi kubadili matokeo ambayo huja kwa kutotii na kuzivunja.

Na tutambue kuwa furaha yetu kuu katika maisha haya itapatikana kutokana na kufuata na kutii amri zake! Ninapenda maneno yanayopatikana katika Isaya Mlango wa 32, aya ya17:”Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima.” ” Amani hii, matumaini haya yanaweza tu kuja kupitia haki.

Hatuwezi kukubali sisi wenyewe kuwa na njia hata kidogo ya kupuuza dhambi. Hatuwezi kukubali sisi wenyewe kuamini kuwa tunaweza kushiriki ”kidogo tu” katika kutotii amri za Mungu, kwa vile dhambi inaweza kutunyakua na mkono wa chuma ambapo kujinasua ni vigumu na uchungu mno. Uraibu ambao unaweza kuja kwa ajili ya dawa za kulevya, pombe, ponografia, na uovu ni wa kweli na karibu kutowezekana kuuacha bila mapambano makubwa na usaidizi mwingi.

Ikiwa mmoja wenu amejikwaa safarini mwake, nampa matumaini kwamba kuna njia ya kurekebisha. Njia inaitwa toba. Ingawa njia ni ngumu, wokovu wako wa milele unategemea kwayo. Ni kipi kinachoweza kuwa cha kustahili zaidi jitihadi zako? Ninawasihi mfanye uamuzi papa hapa na mchukue hatua zinazohitajika kutubu kikamilifu. Mapema unavyofanya hivyo, ndivyo haraka itakavyowezekana kwako kuhisi amani na utulivu na matumaini yaliyozungumziwa na Isaya.

Muda mfupi uliopita nilisikiza ushuhuda wa mwanamke ambaye, pamoja na mumewe, walipotea kutoka njia ya usalama, kuvunja amri na, katika hali hiyo, karibu wavunje familia yao. Wakati ambapo kila mmoja wao angeweza hatimaye kuona ndani ya ukungu mnene wa utawaliwa na kutambua jinsi walivyokosa furaha katika maisha yao, na pia jinsi walivokuwa wakiwaumiza wapendwa wao, walianza kubadilika. Njia ya toba ilionekana kuwa pole na kuwa, mara nyingine, chungu, lakini kwa usaidizi wa viongozi wa ukuhani, pamoja na usaidizi kutoka familia na kutoka kwa marafiki waaminifu, walipata njia ya kurudi.

Ninashiriki nanyi sehemu ya ushuhuda wa dada huyu kuhusu nguvu za uponyaji wa toba: ”Mtu anatokaje kutoka kuwa mojawapo ya kondoo waliopotea na kushikwa na [dhambi], hadi amani na furaha tunayoihisi sasa? Hilo linafanyikaje? Jibu ... ni kwa sababu ya injili kamilifu, Mwana mkamilifu na dhabihu Yake kwa ajili yangu. ... Palipokuwa na giza, sasa kuna mwangaza. Palipokuwa na kukata tamaa na maumivu, kuna furaha na matumaini. Tumebarikiwa bila kipimo na mabadiliko ambayo yanaweza tu kuja kupitia toba inayowezeshwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Mwokozi wetu alikufa kutupa wewe na mimi ile zawadi ya heri. Licha ya ukweli kwamba njia ni ngumu, ahadi ni ya kweli. Alisema Bwana kwa wale wanaotubu:

“Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji.”9

“Sitakumbuka [wao] tena.”10

Katika maisha yetu yote tutahitaji kukuza shuhuda dhabiti kwa kusoma maandiko na kuomba na kutafakari ukweli wa injili ya Yesu Kristo. Zinapokuwa imara, shuhuda zetu za injili, ya Mwokozi, na Baba yetu wa Mbinguni zitashawishi yote ambayo tutafanya.

Nashuhudia kuwa sisi sote ni wana wapendwa wa Baba yetu wa Mbinguni, tuliotumwa duniani siku hii na wakati huu kwa lengo, na tumepewa ukuhani wa Mungu ili tuweze kuwatumukia wengine na kufanya kazi ya Mungu duniani. Tumeamriwa kuishi maisha yetu ili tuendelee kuwa wenye kustahili kuwa na ukuhani.

Ndugu zangu, na tutii amri! Vitu vya ajabu na tukufu viko kwenye akiba ikiwa tutatenda hivyo. Na hii iwe baraka yetu, ninaomba katika jina la Yesu Kristo, Mwokozi wetu na Mkombozi, amina.