“Juni 19–25. Mathayo 27; Marko 15: Luka 23; Yohana 19: ‘Imekwisha’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2022)
“Juni 19–25. Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023
Juni 19–25
Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; Yohana 19
“Imekwisha”
Anza maandalizi yako kwa kusoma Mathayo 27; Marko 15; Luka 23; na Yohana 19. Kwa maombi tafuta kuelewa mahitaji ya watoto.
Alika Kushiriki
Mwache kila mtoto achukue zamu kushikilia picha kutoka muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia. Wakati wakishikilia picha, kila mtoto anaweza kushiriki kitu anachokiona katika picha.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Mathayo 27:11–66; Luka 23; Yohana 19
Kwa sababu Yesu alikufa kwa ajili yangu, naweza kufufuka.
Watoto wadogo wanaweza kufadhaishwa na hadithi hii ya kusulubiwa kwa Yesu. “Sura ya 52: Majaribu ya Yesu” na “Sura ya 53: Yesu Anasulubiwa” (katika Hadithi za Agano Jipya, 133–38, au video zinazoambatana katika ChurchofJesusChrist.org) zinatoa mfano mzuri kwa ajili ya jinsi ungeweza kushiriki kiusahihi hadithi hii pamoja nao.
Shughuli Yamkini
-
Onyesha picha katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia unaposimulia kuhusu shitaka la Yesu, Kusulubiwa, na mazishi (ona pia Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 57–58). Waalike watoto kushiriki kile wanachojua kuhusiana na matukio haya. Sisitiza kwamba katika siku ya tatu, Yesu alifufuka. Kwa maneno mengine, Yeye akarudi kuwa uhai tena.
-
Waombe watoto kutaja baadhi ya vitu wazazi wao huwafanyia ambavyo hawawezi kujifanyia wao wenyewe. Onyesha picha ya Mwokozi. Eleza kwamba kwa sababu ya Yesu, tunaweza kufufuka—kitu ambacho hatuwezi kujifanyia sisi wenyewe.
-
Onyesha picha ya mtu fulani unayemjua ambaye amefariki. Shiriki ushuhuda wako kwamba kwa sababu ya Yesu huyo mtu siku moja ataishi tena.
Ninaweza kuwasamehe wengine kama Yesu alivyofanya.
Unawezaje kuwasaidia watoto kuelewa jinsi ya kuwasamehe wale wasio wakarimu, kama Yesu Alivyofanya?
Shughuli Yamkini
-
Elezea jinsi askari hawakuwa na huruma kwa Yesu (ona Mathayo 27:26–37), na kisha soma Luka 23:34. Elezea kwamba tunapowasamehe wengine, hatuwakasirikii tena na tunaonyesha upendo kwao.
-
Shiriki mifano ambayo mtu anasema au anafanya kitu kibaya. Waalike watoto kuzungumza kuhusu jinsi ambavyo wao wangeweza kuonyesha msamaha katika hali hizi.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu msamaha, kama vile “Help Me, Dear Father” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 99). Uliza maswali ambayo yanajibiwa na wimbo, kama “Nani tunapaswa kumsamehe?” au “Nani anayeweza kutusaidia wakati kusamehe inakuwa vigumu?”
-
Pekua toleo la hivi karibuni la Rafiki ili kuona hadithi kuhusu mtoto aliyemsamehe mtu. Shiriki hadithi hii na watoto.
Kwa sababu Yesu aliteseka na alikufa kwa ajili yangu, ninaweza kutubu na kusamehewa.
Ingawa watoto chini ya umri wa miaka minane bado hawawajibiki, ni muhimu kwao kuanza kujifunza jinsi ya kutubu dhidi ya chaguzi zisizofaa wanazofanya.
Shughuli Yamkini
-
Fanya muhtasari wa Luka 23:32–33, 39–43, na wasaidie watoto kuwapata wale wezi wawili katika picha ya 57 katika Kitabu cha Sanaa za Injili. Eleza kwamba wakati mwizi wa kwanza akimkejeli Yesu, mwizi wa pili alikiri kwamba amefanya kitu kibaya—alikuwa anaanza kutubu.
-
Wasomee watoto Mafundisho na Maagano 19:16. Kwa nini Yesu aliteseka kwa ajili yetu?
-
Onyesha video “The Shiny Bicycle” (ChurchofJesusChrist.org). Elezea kwamba tunaweza kusali kwa Baba wa Mbinguni Naye anaweza kutusaidia kurekebisha dhambi na makosa yetu na kupokea msamaha.
-
Waache watoto waweke alama za chaki katika ubao kuwakilisha chaguzi mbaya. Kisha waombe wafute ubao kuwakilisha toba. Onyesha picha ya Mwokozi, na shuhudia kwamba tunaweza kutubu kwa sababu Yake.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Mathayo 27:11–66; Luka 23; Yohana 19
Yesu alikufa kwa ajili yangu kwa sababu Yeye ananipenda.
Kwa nini unashukuru kwamba Yesu Kristo alikufa kwa ajili yako? Fikiria jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto kuelewa umuhimu wa dhabihu ya Mwokozi kwao.
Shughuli Yamkini
-
Orodhesha matukio muhimu kutoka Mathayo 27:11–66 kwenye vipande tofauti vya karatasi (kwa msaada katika kufanya hili, ona “Sura ya 52: Majaribu ya Yesu” na “Sura ya 53: Yesu Asulubiwa,” katika Hadithi za Agano Jipya, 133–38, au video inayoambatana nayo katika ChurchofJesusChrist.org). Waalike watoto kusoma mistari hii na kuweka matukio katika utaratibu sahihi.
-
Muombe mtoto asome Mathayo 27:54, na waalike watoto kushiriki vitu kuhusu Yesu vinavyowasaidia kufahamu kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu.
-
Waulize watoto kile wanachojifunza juu ya Kusulibiwa kutoka “Behold the Great Redeemer Die” (Nyimbo, na.191), au wimbo mwingine wa sakramenti. Je, ni kwa nini Yesu aliteseka kwa ajili yetu sisi? (ona Mafundisho na Maagano 18:10–11; 19:16).
Ninaweza kuwasamehe wengine kama Yesu alivyofanya.
Inaweza kuwa vigumu kuwasamehe wengine. Watoto unaowafundisha watabarikiwa kama wanafuata mfano wa Mwokozi na kujifunza kusamehe.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kuchukua zamu kusoma kuhusu askari wakiwa hawana huruma kwa Yesu katika Mathayo 27:26–37 na Yesu akiwasamehe katika Luka 23:34. (Ona umaizi unaotolewa na Tafsiri ya Joseph Smith katika Luka 23:34, tanbihi c.) Tunajifunza nini kutoka katika mfano wa Yesu?
-
Andika katika ubao Je, unaweza kufanya nini kumsamehe mtu asiye na huruma kwako? Waache watoto wachukue zamu kuandika mawazo katika ubao, kama vile Sali ili upate kuwa na hisia zenye upendo kwa mtu huyo au Fikiria kitu fulani kizuri kuhusiana na mtu huyo.
Kwa sababu Yesu aliteseka na alikufa kwa ajili yangu, Ninaweza kutubu na kusamehewa.
Somo hili ni wakati mzuri wa kushuhudia kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, tunaweza kutubu dhambi zetu na kusamehewa.
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mtoto asome kwa sauti Luka 23:32–33, 39–43. Elezea kwamba watu wawili waliosulubiwa na Yesu walikuwa wezi. Mmoja wa wezi hao alionyesha kwamba alikuwa anaanza kutubu? Je, tunaweza kufanya nini ili kumwonesha kwamba tunatubu? (Ona Mwongozo wa Maandiko, “Tubu, Toba,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.)
-
Andika sentensi ifuatayo ubaoni, ukiacha mapengo kwa ajili ya maneno ya kiitaliki: “Ninaweza samehewa wakati ninatubu kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo.” Wapatie watoto vidokezo ili viwasaidie kujaza mapengo hayo.
-
Mwalike mtoto kushikilia mfuko, na kuujaza kwa mawe madogo wakati watoto wengine wanataja chaguzi zisizofaa ambazo mtu anaweza kufanya. Wasaidie watoto kulinganisha mfuko na mzigo wa kiroho tunaobeba pale tutendapo dhambi. Ni kwa jinsi gani toba ni kama kuyatoa mawe nje ya mfuko? Unaweza kuwakumbusha watoto kwamba toba siyo tukio la wakati mmoja bali ni mchakato wa kila siku.
-
Angalia kwenye toleo la hivi karibuni la Rafiki kwa ajili ya hadithi au ujumbe kuhusu toba, na shiriki pamoja na watoto.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Wahimize watoto kufikiria mtu wanayehitaji kumsamehe na kuamua juu ya jambo moja watakalofanya ili kumuonyesha mtu huyo kwamba wamemsamehe.