“Kufundisha Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Kufundisha Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Kufundisha Watoto Wadogo
Kama una watoto wadogo katika familia yako, hizi ni baadhi ya shughuli zinazoweza kuwasaidia kujifunza:
-
Imba. Nyimbo za Kanisa na nyimbo kutoka Kitabu cha Nyimbo za Watoto zinafundisha mafundisho ya injili kwa nguvu zaidi. Tumia kielezo cha mada nyuma ya Kitabu cha Nyimbo za Watoto kutafuta nyimbo zinazohusiana na kanuni za injili unazofundisha. Wasaidie watoto wako kuhusisha jumbe za nyimbo na maisha yao. (Ona pia “Kujumuisha Muziki Mtakatifu katika Kujifunza Kwako Injili” katika nyenzo hii.)
-
Sikiliza au igiza hadithi. Watoto wadogo wanapenda hadithi—kutoka katika maandiko, kutoka katika maisha yako, kutoka katika historia ya Kanisa au ya familia yako, na kutoka kwenye magazeti ya Kanisa. Tafuta njia za kuwashirikisha kwenye usimuliaji wa hadithi. Wanaweza kushikilia picha au vitu, kuchora picha za kile wanachokisikia, kuigiza hadithi, au hata kusaidia kusimulia hadithi. Wasaidie watoto wako kutambua kweli za injili katika hadithi unazowasimulia.
-
Soma maandiko. Watoto wadogo wanaweza kushindwa kusoma vizuri, lakini bado unaweza kuwahusisha katika kujifunza kutoka kwenye maandiko. Unaweza kuhitaji kuzingatia kwenye mstari mmoja, kirai muhimu, au neno. Watoto wanaweza hata kukariri virai vifupi kutoka katika maandiko ikiwa watavirudia mara kadhaa. Wanaposikia neno la Mungu, wataguswa na Roho.
-
Tazama picha au angalia video. Unapowaonyesha watoto wako picha au video inayohusiana na kanuni ya injili au hadithi ya maandiko, waulize maswali yanayowasaidia kujifunza kutoka kwenye kitu wanachokiona. Kwa mfano, ungeweza kuuliza, “Je, ni nini kinatokea katika picha au video hii? Kinakufanya ujisikie vipi?” Programu ya Vyombo vya Habari vya Injili, GospelMedia.ChurchofJesusChrist.org, na children.ChurchofJesusChrist.org ni mahali pazuri pa kutafuta picha na video.
-
Buni. Watoto wanaweza kujenga, kuchora, au kupaka rangi kitu kinachohusiana na hadithi au kanuni wanayojifunza.
-
Shiriki katika masomo ya vitendo. Somo rahisi la vitendo linaweza kuwasaidia watoto wako waelewe kanuni ya injili ambayo ni ngumu kueleweka. Unapotumia masomo ya vitendo, tafuta njia za kuwafanya watoto wako kushiriki. Watajifunza zaidi kutokana na uzoefu wa kuchangamana kuliko kuangalia tu onyesho.
-
Igiza Nafasi. Watoto wanapoigiza nafasi ya aina fulani wanakayokutana nayo katika maisha halisi, wanaelewa vizuri zaidi jinsi kanuni ya injili inavyohusika kwenye maisha yao.
-
Rudia shughuli. Watoto wadogo wanaweza kuhitaji kusikia mawazo mara nyingi zaidi ili kuyaelewa. Usiogope kurudia hadithi au shughuli mara kwa mara. Kwa mfano, unaweza kusimulia hadithi ya maandiko mara nyingi katika njia tofauti—kwa kusoma kutoka kwenye maandiko, kufanya muhtasari kwa maneno yako mwenyewe, kuonyesha video, kuwaacha watoto wako wakusaidie kusimulia hadithi, kuwaalika waigize hadithi, na kadhalika.