“Kujumuisha Muziki Mtakatifu katika Kujifunza Kwako Injili,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2023 (2022)
“Kujumuisha Muziki Mtakatifu katika Kujifunza Kwako Injili,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Kujumuisha Muziki Mtakatifu katika Kujifunza Kwako Injili
Kuimba Nyimbo za Msingi na nyimbo za Kanisa kunaweza kukubariki wewe na familia yako kwa njia nyingi. Mawazo haya yanaweza kukusaidia kutumia muziki mtakatifu unapojitahidi kujifunza na kuishi injili.
-
Jifunze kanuni za kimafundisho. Tafuta ukweli unaofundishwa katika nyimbo unazoimba au kusikiliza. Hii inaweza kukuongoza kwenye majadiliano ya injili juu ya kweli hizi siku nzima. Imba au sikiliza nyimbo za Msingi au nyimbo za kanisa zinazofundisha juu ya Yesu Kristo na injili Yake. Sikiliza kwa makini njia ambazo Roho Mtakatifu anashuhudia juu ya Mwokozi na mafundisho Yake.
-
Tambua nguvu ya muziki. Kuimba au kusikiliza nyimbo za Msingi na nyimbo za Kanisa kunaweza kuwa baraka katika nyakati za shida. Kwa mfano, kuimba wimbo kunaweza kumtuliza mtoto wakati wa kulala, kuleta furaha wakati familia yako inafanya kazi pamoja, kumwinua jirani ambaye ni mgonjwa, au kumfariji mtu anayehisi wasiwasi.
-
Shiriki uzoefu. Shiriki uzoefu binafsi na wa familia ambao unahusiana na ujumbe wa nyimbo. Unaweza pia kushiriki hadithi zinazohusiana za maandiko.
-
Shirikisha familia yako. Familia yako itajifunza zaidi kutokana na nyimbo ikiwa wanashiriki kikamilifu. Ili kuwashirikisha wanafamilia, unaweza kumwalika mtoto mkubwa kusaidia kufundisha wimbo kwa wadogo au kuwaalika watoto kufundisha familia wimbo ambao walijifunza katika Msingi. Unaweza pia kuruhusu wanafamilia kupeana zamu ya kuongoza wimbo.
-
Kuwa mbunifu. Tumia njia anuwai za kujifunza muziki mtakatifu kama familia. Kwa mfano, unaweza kufanya vitendo vinavyoendana na maneno na virai katika wimbo. Au mnaweza kufanya zamu kuigiza sehemu za wimbo wakati wanafamilia wakijaribu kubahatisha ni wimbo gani. Familia yako inaweza kufurahia kuimba nyimbo kwa kasi tofauti au toni tofauti za sauti. Programu ya Maktaba ya Injili na programu ya Injili kwa ajili ya Watoto zina rekodi na video ambazo zinaweza kuwasaidia kujifunza nyimbo. Unaweza pia kutengeneza orodha ya muziki mtakatifu wa kusikiliza.
Kwa mawazo zaidi, ona sehemu “Kutumia Muziki Kufundisha Mafundisho” na “Kuwasaidia Watoto Kujifunza na Kukumbuka Nyimbo za Msingi na Nyimbo za Kanisa,” inayopatikana katika “Maelekezo ya Wakati wa Kuimba na Uwasilishaji wa Watoto katika Mkutano wa Sakramenti” katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili Ya Msingi.