Agano la Kale 2022
Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Agano la Kale


“Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Agano la Kale,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Agano la Kale,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022

ikoni ya mawazo

Mawazo ya Kuweka Akilini

Usomaji wa Agano la Kale

Tafuta Maana Binafsi

Unapotafakari juu ya fursa yako ya kujifunza Agano la Kale mwaka huu, je, unajisikiaje? Mwenye shauku? Usiye na uhakika? Mwenye kuogopa? Hisia hizi zote zinaeleweka. Agano la Kale ni moja ya mikusanyo ya zamani sana ya maandishi ulimwenguni, na hicho kinaweza kufanya vyote kusisimua na kutisha. Maandishi haya yanatokana na utamaduni wa kale ambao unaweza kuonekana wa kigeni na nyakati zingine ya ajabu au hata kuwa ya wasiwasi sana. Na bado katika maandishi haya tunaona watu wakiwa na uzoefu ambao unaonekana kuwa wa kawaida, na tunatambua maudhui ya injili ambayo yanatoa ushahidi wa uungu wa Yesu Kristo na injili Yake.

Ndiyo, watu kama Ibrahimu, Sara, Hana, na Danieli waliishi maisha ambayo, katika njia fulani, yalikuwa tofauti sana na ya kwetu. Lakini wao pia walipatwa na shangwe ya kifamilia na kutoelewana kifamilia, nyakati za imani na nyakati za mashaka, na mafanikio na kushindwa—kama sisi sote tufanyavyo. Muhimu zaidi, wao walitumia imani, walitubu, walifanya maagano, na kupata uzoefu wa kiroho, na kamwe hawakukata tamaa katika jitihada zao za kumtii Mungu.

Kama unajiuliza kama wewe na familia yako mnaweza kupata maana binafsi katika Agano la Kale mwaka huu, weka akilini mwako kwamba familia ya Lehi na Saria walipata. Nefi alielezea hadithi kuhusu Musa na mafundisho kutoka kwa Isaya wakati kaka zake walipohitaji kutiwa moyo au kusahihishwa au matumaini. Nefi aliposema, “Moyo wangu unafurahia maandiko” (2 Nefi 4:15), alikuwa akiongelea kuhusu maandiko ambayo sasa ni sehemu ya Agano la Kale.

Mtafute Mwokozi

Kama unajiuliza kama wewe na familia yako mnaweza kujongea zaidi kwa Yesu Kristo kupitia kujifunza Agano la Kale, weka akilini kwamba Mwokozi Mwenyewe anatualika kufanya hivyo. Wakati Yeye alipowaambia viongozi wa Wayahudi “Maandiko… yananishuhudia” (Yohana 5:39), Yeye alikuwa akiongelea kuhusu maandishi tunayoyaita Agano la Kale. Ili kumpata Mwokozi katika kitu unachokisoma, utahitajika kutafakari kwa uvumilivu na tafuta mwongozo wa kiroho. Nyakati zingine marejeleo Kwake Yeye huonekana moja kwa moja, kama vile katika tamko la Isaya “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume: … naye ataitwa jina lake … Mfalme wa Amani” (Isaya 9:6). Katika mahali pengine, Mwokozi amewakilishwa kwa ustadi zaidi, kupitia alama na mifanano—kwa mfano, kupitia maelezo ya dhabihu za wanyama (ona Lawi 1:3–4) au hadithi ya Yusufu anawasamehe kaka zake na kuwaokoa kutokana na njaa.

Kama unatafuta kuwa na imani kubwa zaidi katika Mwokozi unaposoma Agano la Kale, utaipata. Pengine hili linaweza kuwa kusudi la kujifunza kwako mwaka huu. Omba kwamba Roho akuongoze ili kupata na kufokasi juu ya vifungu vya maneno, hadithi, na unabii ambao utakuleta karibu zaidi na Yesu Kristo.

nabii wa kale anaandika

Nabii wa Agano la Kale, Judith A. Mehr

Yalihifadhiwa Kiungu

Usitegemee Agano la Kale kuwasilisha historia safi na sahihi ya mwanadamu. Hicho sio kitu ambacho waandishi na wakusanya taarifa wa mwanzo walikuwa wakijaribu kukitengeneza. Hamu yao kubwa zaidi ilikuwa ni kufundisha kitu fulani kuhusu Mungu—kuhusu mpango Wake kwa ajili ya watoto Wake, kuhusu inamaanisha nini kuwa watu Wake wa agano, na kuhusu jinsi ya kupata ukombozi wakati tunapokuwa hatuishi kulingana na maagano yetu. Wakati mwingine walifanya hivyo kwa kuhusisha matukio ya kihistoria kadiri wao walivyoelewa—ikijumuisha hadithi kutoka katika maisha ya manabii wakubwa. Kitabu cha Mwanzo ni mfano wa hili, vile vile vitabu vya Yoshua, Waamuzi, na 1 na 2 Wafalme. Lakini waandishi wengine wa Agano la Kale hawakukusudia kuwa cha kihistoria kabisa. Badala yake, walifundisha kwa njia ya matendo ya kisanii kama vile mashairi na fasihi andishi. Zaburi na Methali zinaingia katika kundi hili. Na kuna maneno ya thamani ya manabii, kutoka Isaya hadi Malaki, ambao walinena maneno ya Mungu wa kale wa Israeli—na, kupitia muujiza wa Biblia, bado ananena kwetu leo.

Je, wote hawa manabii, watunga mashairi, na wakusanya habari walijua kwamba maneno yao yangekuja kusomwa na watu ulimwenguni kote maelfu ya miaka baadae? Sisi hatujui. Lakini tunastaajabia kwamba hili ndilo haswaa lililotokea. Mataifa yaliibuka na kuanguka, miji ilitwaliwa kwa nguvu wakati wa vita, wafalme waliishi na kufa, lakini Agano la Kale limedumu kuliko vyote, kutoka kizazi hadi kizazi, kutoka mwandishi hadi mwandishi, kutoka tafsiri hadi tafsiri. Ndiyo baadhi ya vitu vilipotea au kubadilishwa, lakini bado kwa kiasi fulani mengi sana kimiujiza yamehifadhiwa.1

Haya ni baadhi ya mambo machache tunayoyaweka akilini tunaposoma Agano la Kale mwaka huu. Pengine Mungu amehifadhi maandishi haya ya kale kwa sababu Yeye anakujua wewe na yale unayopitia. Pengine ameandaa ujumbe wa kiroho kwa ajili yako katika maneno haya, kitu kitakacho kuvuta wewe uje karibu zaidi na Yeye na ujenge imani yako katika mpango Wake na Mwanawe Mpendwa. Pengine atakuongoza kwenye kifungu cha maneno au utambuzi ambao utambariki mtu fulani unayemjua—ujumbe unaoweza kushirikiana na rafiki, mwana familia, au Mtakatifu mwenzako. Kuna uwezekano mwingi sana. Je, hii haisisimui kufikiria hivyo?

Vitabu katika Agano la Kale

Katika matoleo mengi ya Kikristo ya Agano la Kale, vitabu vimepangiliwa tofauti kutokana na jinsi vilivyokuwa vimepangiliwa wakati mwanzoni vilipokuwa vimekusanywa katika mkusanyiko mmoja. Hivyo basi wakati Biblia ya Kiebrania imeweka vitabu hivyo katika makundi ya aina tatu—sheria, manabii, na maandishi—Bibilia nyingi za Kikristo zinapanga vitabu hivyo katika makundi ya aina nne: sheria (Mwanzo–KumbuKumbu la Torati), historia (Joshua–Esta), vitabu vya mashairi (Ayubu–Mhubiri), na manabii (Isaya–Malaki).

Kwa nini hizi aina za makundi ni muhimu? Kwa sababu kujua aina ya kitabu unachosoma inaweza kukusaidia wewe kuelewa jinsi ya kujifunza kitabu hicho.

Hapa kuna kitu cha kukiweka akilini unapoanza kusoma “sheria,” au vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale. Vitabu hivi, ambavyo vinadhaniwa kuwa ni vya Musa, yawezekana vimepita kupitia mikono ya waandishi na wakusanya habari wengi kwa muda mrefu. Bado, vitabu hivi vya Musa ni neno la Mungu lenye mwongozo wa kiungu, ingawa ni—kama kazi nyingine yoyote iliyopitishwa kupitia kwa mwanadamu—unategemea mapungufu ya mwanadamu (ona Musa 1:41; Makala ya Imani 1:8). Maneno ya Moroni, akiashiria Kitabu Kitakatifu cha Mormoni kumbukumbu ambayo alisaidia kuikusanya, ni zenye msaada hapa: “Kama kuna makosa ni hitilafu ya wanadamu; kwa hivyo, usilaumu vitu vya Mungu” (ukurasa wa jina la Kitabu cha Mormoni). Katika maneno mengine, kitabu cha maandiko hakihitaji kuwa bila makosa ya kibinadamu ili kuwa neno la Mungu.

Muhtasari

  1. Rais M. Russell Ballard alisema: “Siyo kwa bahati au jambo lililotokea kulingana na jingine kwamba tunayo Biblia leo. Watu wenye haki walisukumwa na Roho kuandika vyote mambo matakatifu waliyoyaona na maneno yenye mwongozo wa kiungu waliyoyasikia na kunena. Watu wengine waaminifu walishawishika kulinda na kuhifadhi kumbukumbu hizi” (“The Miracle of the Holy Bible,” Liahona, Mei 2007, 80).