Agano la Kale 2022
Mawazo ya Kuweka Akilini: Tabenako na Sadaka ya Kuteketezwa


“Mawazo ya Kuweka Akilini: Tabenako na Sadaka ya Kuteketezwa,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Mawazo ya Kuweka Akilini: Tabenako na Sadaka ya Kuteketezwa,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022

Picha
ikoni ya mawazo

Mawazo ya Kuweka Akilini

Tabenako na Sadaka ya Kuteketezwa

Tunaposoma Agano la Kale, wakati mwingine tunakumbana na vifungu virefu kuhusu mambo ambayo yalikuwa muhimu hasa kwa Bwana ila yaweza kuwa hayana umuhimu wa moja kwa moja kwetu leo. Kutoka 25–30; 35–40; Mambo ya Walawi 1–9; 16–17 ni mifano. Sura hizi zinaelezea kwa undani tabenako la Israeli katika nyika na sadaka ya wanyama iliyopaswa kufanyika humo.1 Tabenako lilikuwa hekalu dogo, makazi ya Bwana kukaa kati ya watu Wake.

Mahekalu yetu ya kisasa yana mifanano na tabenako la Waisraeli, ila kiuhalisia hayafanani na maelezo katika Kutoka. Na hatuui wanyama katika mahekalu yetu—Upatanisho wa Bwana ulisitisha sadaka za wanyama zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Licha ya hizi tofauti, kuna thamani kubwa leo katika kusoma kuhusu mitindo ya kuabudu ya Waisraeli wa zamani, hasa ikiwa tutaiona jinsi watu wa Mungu katika Kitabu cha Mormoni walivyoiona—kama njia “ya kuimarisha imani zao katika Kristo” (Alma 25:16; ona pia Yakobo 4:5; Yaromu 1:11). Tunapoelewa ishara ya tabenako na sadaka ya wanyama, tunaweza kupata umaizi wa kiroho ambao utaimarisha pia imani yetu katika Kristo.

Picha
watu wakileta mwanakondoo kwa makuhani katika tabenako

Kielelezo cha Waisraeli wakileta mwanakondoo kwenye tabenako, na Robert T. Barrett

Tabenako huimarisha imani katika Yesu Kristo.

Wakati Mungu alipomwamuru Musa kujenga tabenako katika kambi ya Waisraeli, Yeye alitangaza kusudi lake: “ili nipate kukaa kati yao” (Kutoka 25:8). Ndani ya tabenako, uwepo wa Mungu uliwakilishwa na sanduku la agano—kisanduku cha mbao, kilichofunikwa kwa dhahabu, kikiwa na kumbukumbu ya maandishi ya maagano ya Mungu na watu Wake (ona Kutoka 25:10–22). Sanduku lilikuwa linatunzwa katika mahali patakatifu sana , chumba cha ndani kabisa, kilichotengwa na vingine vya tabenako kwa pazia. Pazia hili ni ishara ya kutengwa kwetu kutoka uwepo wa Mungu kwa sababu ya Anguko.

Isipokuwa Musa, tunamjua mtu mwingine mmoja tu ambaye angeweza kuingia “mahali patakatifu sana” (Kutoka 26:34)—kuhani mkuu. Kama makuhani wengine, kwanza alipaswa kuoshwa na kupakwa mafuta (ona Kutoka 40:12–13) na kuvikwa mavazi matakatifu kama ishara ya ofisi yake (ona Kutoka 28). Mara moja kwa mwaka, katika siku iliyoitwa Siku ya Upatanisho, kuhani mkuu angetoa sadaka kwa niaba ya watu kabla ya kuingia peke yake kwenye tabenako. Katika pazia, angechoma ubani (ona Mambo ya Walawi 16:12). Harufu ya moshi iliyopaa mbinguni iliwakilisha sala za watu zikipaa kwa Mungu (ona Zaburi 141:2). Kisha kuhani mkuu, akibeba damu kutoka kwenye sadaka ya mnyama, angepita kwenye pazia na kukaribia kiti cha Mungu, kilichoashiriwa na sanduku la agano (ona Mambo ya Walawi 16:14–15).

Ukijua kile unachojua kumhusu Yesu Kristo na wajibu Wake katika mpango wa Baba wa Mbinguni, je, unaweza kuona jinsi tabenako inavyotuelekeza sisi kwa Mwokozi? Kama vile tabenako, na sanduku ndani yake, ilivyowakilisha uwepo wa Mungu kati ya Watu wake, Yesu Kristo alikuwa uwepo wa Mungu kati ya watu Wake (ona Yohana 1:14). Kama vile kuhani mkuu, Yesu Kristo ni mpatanishi kati yetu sisi na Mungu Baba. Alipita kwenye pazia kufanya maombezi kwa ajili yetu kwa fadhili ya sadaka ya damu Yake mwenyewe (ona Waebrania 8–10).

Baadhi ya vipengele vya tabenako la Israeli vinaweza kuwa vya kawaida kwako, hasa kama umewahi kuwa hekaluni kupokea ibada zako mwenyewe. Kama mahali patakatifu sana pa tabenako, chumba cha selestia katika hekalu huwakilisha uwepo wa Mungu. Ili kuingia, lazima kwanza tuoshwe na kupakwa mafuta. Tunavaa mavazi matakatifu. Tunasali katika madhabahu ambapo kutoka hapo sala hupanda kwa Mungu. Na mwishowe tunapita kwenye pazia na kwenda katika uwepo wa Mungu.

Labda ufanano wa muhimu sana kati ya mahekalu ya kisasa na tabenako la kale ni kwamba yote, kama itaeleweka vizuri, huimarisha imani yetu katika Yesu Kristo na kutujaza na shukrani kwa ajili ya dhabihu Yake ya upatanisho. Mungu anataka watoto Wake wote kuingia katika uwepo Wake; Yeye anataka “ufalme wa makuhani” na watawa (Kutoka 19:6). Lakini dhambi zetu hutuzuia sisi kupata baraka hiyo, kwani “hakuna kitu kichafu chaweza kuishi na Mungu” (1 Nefi 10:21). Kwa hiyo Mungu Baba alimtuma Yesu Kristo, “kuhani wetu mkuu wa mambo mazuri yajayo” (Waebrania 9:11). Yeye hufunua pazia kwa ajili yetu na kuwapa uwezo watoto wote wa Mungu “kuja kwa ujasiri katika kiti cha neema, ili tuweze kupata huruma” (Waebrania 4:16).

Leo, madhumuni ya mahekalu ni zaidi ya kupata kuinuliwa kwetu. Baada ya kupokea ibada zetu, tunaweza kusimama katika nafasi ya mababu zetu, kama wawakilishi ili kupokea ibada kwa niaba yao. Katika maana, tunaweza kuwa kama kuhani wa kale—na Kuhani Mkuu Sana—tukifungua njia ya uwepo wa Mungu kwa ajili ya wengine.

Dhabihu huimarisha Imani katika Yesu Kristo.

Kanuni za upatanisho na kupatanishwa zinafundishwa kwa nguvu katika matendo ya kale ya sadaka za wanyama, ambazo zilikuwapo kabla ya sheria ya Musa. Kwa sababu ya injili ya urejesho, tunajua kwamba Adamu na Hawa walitoa sadaka, walifahamu ishara ya kiwakilishi chake kwa Dhabihu ya Mwokozi, na walifundisha hili kwa watoto wao (ona Musa 5:4–12; ona pia Mwanzo 4:4).

Ishara ya sadaka ya wanyama inaweza kuonekana hasa yenye ukali katika Siku za Upatanisho wa Waisraeli wa kale (“Yom Kippur” kwa Kiebrania). Uhitaji wa sherehe hii ya mwaka ulielezewa katika Mambo ya Walawi 16:30: “Katika siku hiyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yenu, kuwatakasa, ili muweze kusafishwa kutoka kwenye dhambi zenu zote mbele ya Bwana.” Ili uwepo wa Mungu ukae kati ya watu. Upatanisho huu ulikamilishwa kupita sherehe mbalimbali. Katika mojawapo ya hizi, mbuzi aliuwawa kama matoleo kwa ajili ya dhambi za watu, na kuhani mkuu alichukua damu ya mbuzi na kupeleka katika mahali patakatifu sana. Baadae, kuhani mkuu aliweka mikono yake juu ya mbuzi aliye hai na kuungama dhambi za wana wa Israeli—kuashiria kuhamisha dhambi hizo kwa mbuzi. Baadae mbuzi alifukuzwa nje ya kambi ya Israeli.

Katika utoaji huu wa kafara, mbuzi waliashiria Yesu Kristo, akichukua nafasi ya watu wenye dhambi. Dhambi haipaswi kuruhusiwa katika uwepo wa Mungu. Lakini badala ya kuwateketeza au kuwafukuza nje wenye dhambi, Mungu alitoa njia mbadala—badala yake mbuzi angeuwawa au kufukuzwa nje. “Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote,” (Mambo ya Walawi 16:22).

Ishara ya kafara hizi ilionyesha njia ambayo Mungu ametoa ili kutuleta sisi tena kwenye uwepo Wake—Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Mwokozi “ameyachukua masikitiko yetu, na amejitwika huzuni zetu,” hata “maovu yetu sisi sote”(Isaya 53:4, 6). Alisimama katika nafasi yetu, alitoa maisha Yake kulipia adhabu ya dhambi, na baadae kukishinda kifo kupitia Ufufuko Wake (ona Mosia 15:8–9). Dhabihu ya Yesu Kristo ilikuwa “dhabihu kuu na ya mwisho; ndio, sio dhabihu ya mtu, wala ya mnyama” badala yake “dhabihu isiyo ya mwisho na ya milele” (Alma 34:10). Alikuwa ni ukamilisho wa kila kitu sadaka ya kale ilichoelekeza.

Kwa sababu hii, baada ya dhabihu Yake kukamilika, Alisema, “Na hamtatoa kwangu tena kumwagwa kwa damu; ndio, dhabihu na sadaka zenu … zitakomeshwa. … Na mtatoa kwangu dhabihu ya moyo uliopondeka na roho iliyovunjika” (3 Nefi 9:19–20).

Kwa hiyo unapopata vifungu katika Agano la Kale kuhusu dhabibu na tabenako (au baadae, hekalu)—na utavikuta vingi—kumbuka kwamba sababu ya msingi ya yote haya ni kuimarisha imani yako katika Masiya, Yesu Kristo. Acha moyo wako na akili zako zimgeukie Yeye. Tafakari aliyoyafanya kukurudisha katika uwepo wa Mungu—na nini utafanya kumfuata Yeye.

Muhtasari

  1. Kutoka 33:7–11 inataja “tabenako la kusanyiko,” ambapo Musa aliwasiliana na Bwana, ila huu haukuwa mpangilio wa sadaka ulioelezwa katika Kutoka na Mambo ya Walawi. Sadaka hizo zilifanywa katika tabenako lililoelezwa katika Kutoka 25–30, ambalo Mungu alimuamuru Musa kujenga na ambalo wana wa Israeli walijenga (ona Kutoka 35–40). Tabenako hili, ambapo Haruni na wanawe walitoa dhabibu za wanyama, mara nyingi lilirejelewa kama “tabenako la kusanyiko”(ona, kwa mfano, Kutoka 28:43; 38:30; Mambo ya Walawi 1:3).

Chapisha