Agano la Kale 2022
Aprili 25–Mei 1. Kutoka 24; 31–34: “Uso Wangu Utakwenda Pamoja Nawe”


“Aprili 25–Mei 1. Kutoka 24; 31–34: ‘Uso Wangu Utakwenda Pamoja Nawe,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Aprili 25–Mei 1. Kutoka 24; 31–34,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Famila: 2022

Picha
Yehova akimtokea Musa na Wazee wa Israel

Kielelezo cha Yehova akimtokea Musa na Wazee 70 wa Israeli, na Jerry Harston

Aprili 25–Mei 1

Kutoka 24; 31–34

“Uso Wangu Utakwenda Pamoja Nawe”

Si kila kanuni yenye maana katika maandiko inaweza kubainishwa katika mihutasari hii. Msikilize Roho kukusaidia kuzingatia kweli unazozihitaji.

Andika Misukumo Yako

Palikuwepo na sababu za kuwa na tumaini kwamba wana wa Israeli wangebaki kuwa wakweli kwa Mungu baada ya kufunua sheria Yake kwao (ona Kutoka 20–23). Hata kama walikuwa wamenung’unika na kuyumbayumba hapo nyuma, wakati Musa aliposoma sheria chini ya Mlima Sinai, walifanya agano hili: “Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii.” (Kutoka 24:7). Mungu baadae alimwita Musa mlimani, akimwambia kujenga hema ili “nipate kukaa kati yao”(Kutoka 25:8; ona sura ya 25–30).

Ila wakati Musa akiwa juu ya mlima akijifunza ni kwa namna gani Waisraeli wangeweza kuwa na uso wa Mungu kati yao, badala yake Waisraeli walikuwa chini ya mlima wakitengeneza sanamu ya dhahabu ili kuiabudu. Walikuwa wameahidi “kutokuwa na miungu wengine,” lakina bado “walipotoka upesi,” kutoka kwenye amri za Mungu (Kutoka 20:3; 32:8; ona pia Kutoka 24:3). Ilikuwa ni kugeuka kwa kushangaza, ila tunajua kutokana na uzoefu kwamba imani na ahadi vinaweza wakati mwingine kuzidiwa na kutokuwa na uvumilivu, woga, au wasiwasi. Kadiri tunavyotafuta uso wa Mungu katika maisha yetu, inatia moyo kujua kwamba Bwana hajawahi kukata tamaa kwa Israeli ya kale na hatakata tamaa kwetu sisi—kwani ni Yeye ni “mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kutoka 34:6).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Kutoka 24:1–11

Maagano yangu yanaonyesha utashi wangu kutii amri za Mungu.

Unaposoma katika Kutoka 24:3–8 kuhusu Waisraeli kuweka maagano ya kutii amri za Mungu mawazo yako yanaweza kugeuka katika maagano uliyofanya na Mungu. Maagano ya Israeli yalijumuisha mila ambazo ni tofauti na zile ambazo Mungu anazitaka leo, ila unaweza kuona aina fulani ya ufanano, hasa ukizingatia ukweli wa milele unaowakilishwa na mila hizi.

Kwa mfano, mstari wa 4, 5, na 8 inataja madhabahu, sadaka ya wanyama, na damu. Mambo haya yanaweza kuwakilisha nini, na yanahusiana vipi na maagano yako? Ni kwa namna gani maagano yako yanaweza kukusaidia kufanya “yale yote ambayo Bwana amesema”? (mstari wa 7).

Ona pia Musa 5:4–9; Becky Craven, “Makini dhidi ya Kawaida,” Liahona, Mei 2019, 9–11.

Kutoka 32–34

Dhambi ni kugeuka mbali na Mungu, ila Yeye hutoa njia ya kurudi.

Kwa kutafakari jinsi gani Waisraeli kwa haraka “walijiharibu nafsi zao” (Kutoka 32:7) kwa kuvunja maagano yao, tunaweza kuepuka makosa kama hayo. Unaposoma Kutoka 32:1–8, jaribu kujiweka katika nafasi ya Waisraeli—ukiwa nyikani, Musa alikuwa ameondoka kwa siku 40, hujui ikiwa atarudi au lini atarudi, na makabiliano na Wakanaani juu ya nchi ya ahadi yapo mbele yako (ona pia Kutoka 23:22–31). Unafikiri ni kwa nini Waisraeli walitaka sanamu ya dhahabu? Kwa nini dhambi ya Waisraeli ilikuwa kubwa sana? Mistari hii inaweza kukusukuma kutafakari njia ambazo unaweza kujaribiwa kuweka imani yako kwa mtu au kitu kingine zaidi ya Mwokozi. Je, kuna chochote unahisi kushawishika kufanya ili kwamba uweze kumweka Mungu mbele katika maisha yako? Ni nini kinakutia msukumo kuhusu ombi la Musa kwa Bwana katika Kutoka 33:11–17?

Ingawa dhambi ya Waisraeli ilikuwa kubwa mno, hadithi hii inajumuisha pia ujumbe wa huruma ya Mungu na msamaha. Ni nini Kutoka 34:1–10 inakufundisha juu ya Mwokozi? Ni kwa namna gani matendo ya Musa kwa niaba ya wana wa Waisraeli yanakukumbusha kile ambacho Yesu Kristo alifanya kwa watu? (ona Kutoka 32:30–32; Mosia 14:4–8; 15:9; Mafundisho na Maagano 45:3–5).

Tafsiri ya Joseph Smith, Mwanzo 34:1–2 (katika kiambatanisho cha Biblia)

Ni nini ilikuwa tofauti kati ya seti mbili za mbao za mawe alizotengeneza Musa?

Musa aliposhuka chini kutoka mlimani, alileta sheria iliyoandikwa kwenye mbao za mawe. Baada ya kugundua kwamba Waisraeli walikuwa wamevunja agano lao, Musa alivunja mbao (ona Kutoka 31:18; 32:19). Baadae, Mungu alimwamuru Musa kutengeneza seti nyingine za mbao za mawe na kuzipeleka tena mlimani (ona Kutoka 34:1–4). Tafisiri ya Joseph Smith, Kutoka 34:1–2 (katika kiambatanisho cha Biblia) inadhibitisha kwamba seti ya kwanza ya mbao za mawe ilijumuisha ibada za Mungu za “mpangilio mtakatifu,” au Ukuhani wa Melkizedeki. Seti ya pili ilijumuisha “amri ya sheria ya kimwili.” Hii ilikuwa sheria ya chini iliyohudumiwa na “ukuhani mdogo” (ona Mafundisho na Maagano 84:17–27), iliyokuwa imenuiwa kuwaandaa Waisraeli kwa sheria ya juu na ukuhani mkubwa ili waweze kuingia kikamilifu katika uwepo wa Mungu.

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Kutoka 31:12–13, 16–17.Baada ya kusoma mistari hii, labda familia yako ingeweza kujadili swali la Rais Russell M. Nelson kuhusiana na tabia yetu juu ya Sabato: “Ni ishara gani utampa Bwana kuonyesha upendo wako Kwake?” (“Sabato ni Furaha,” Liahona, Mei 2015, 130). Familia yako ingeweza kutengeneza baadhi ya ishara na kuziweka nyumbani kuwakumbusha kwa namna gani mtaonyesha upendo wenu kwa Bwana siku ya Sabato. (Ona pia mkusanyiko wa video “Sabbath Day—At Home” [ChurchofJesusChrist.org].)

Picha
watu wakiembea mbele ya kanisa

Kwa kuiheshimu Sabato, tunaonyesha upendo wetu kwa Bwana.

Kutoka 32:1–8.Ili kuisaidia familia yako kujadili ni kwa jinsi gani Waisraeli walienda kinyume na Mungu, fikiria kutengeneza njia kwenye sakafu (au tafuta moja jirani na nyumbani). Mkiwa mnatembea kwenye njia, wanafamilia wanaweza kuzungumza juu ya majaribu tunayokumbana nayo ili kuchepuka “nje ya njia ambayo [Bwana] ameamuru.” Ni kwa jinsi gani tunaweza kubaki katika njia? Ikiwa tutachepuka, ni kwa namna gani tunaweza kurudi? Ni kwa jinsi gani Mwokozi anatusaidia sisi?

Kutoka 32:26.Baada ya Waisraeli kukutwa wanaabudu sanamu, Musa aliuliza, “Nani yupo upande wa Bwana?” Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha tupo upande wa Bwana?

Kutoka 33:14–15.Wanafamilia wanaweza kushiriki uzoefu ambapo wamehisi kile Mungu alichomuahidi Musa: “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Mngeweza kuimba wimbo juu ya utegemezi wetu kwa Mungu, kama vile “Abide with Me!” (Nyimbo za Kanisa, na. 166).

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo iliopendekezwa: “Who’s on the Lord’s Side?Nyimbo za Kanisa, na. 260.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Mwalike Roho. Zingatia jinsi muziki mtakatifu, sanaa, na maonyesho ya upendo yanavyoshawishi hali ya kiroho katika nyumba yako pale unapofundisha familia yako (ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 15).

Picha
Musa akivunja mbao za mawe

Kuabudu Ndama, na W. C. Simmonds

Chapisha