Agano la Kale 2022
Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Mashairi katika Agano la Kale


“Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Mashairi katika Agano la Kale,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Mawazo ya Kuweka Akilini: Usomaji wa Mashairi katika Agano la Kale,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022

Picha
ikoni ya mawazo

Mawazo ya Kuweka Akilini

Usomaji wa Mashairi katika Agano la Kale

Katika vitabu vya Agano la Kale vinavyotangulia kitabu cha Ayubu, tunapata hadithi nyingi—maelezo simulizi yanayoelezea matukio ya kihistoria kutokana na mtazamo wa kiroho. Nuhu alijenga safina, Musa aliikomboa Israeli, Hana alisali kupata mtoto wa kiume, na mengineyo. Tukianzia na Ayubu, tunakutana na mfumo tofauti wa uandishi, wakati waandishi wa Agano la Kale walipogeukia katika lugha ya ushairi ili kuelezea hisia za ndani kabisa au kumbukumbu za unabii katika njia ya kukumbukwa.

Tumekwisha kuona mifano michache ya ushairi iliyotawanywa kote katika vitabu vya kihistoria vya Agano la Kale. Na kutoka katika kitabu cha Ayubu na kuendelea, tutaona mengi ya hayo. Vitabu vya Ayubu, Zaburi na Mithali, karibu vyote ni ushairi, kama zilivyo sehemu ya maandishi ya manabii kama Isaya, Yeremia, na Amosi. Kwa sababu usomaji wa mashairi ni tofauti na usomaji wa hadithi, kuelewa wakati mwingine kunahitaji mtazamo tofauti. Hapa kuna baadhi ya mawazo ambayo yatafanya usomaji wako wa mashairi ya Agano la Kale kuwa wa maana zaidi.

Kupata Kujua Mashairi ya Kiebrania

Kwanza, itakusaidia kuweka akilini kuwa mashairi ya Kiebrania katika Agano la Kale hayana msingi wa vina, kama aina nyingine za mashairi. Na ingawa mdundo, maneno, na kurudiarudia kwa sauti ni vipengele vya kawaida vya mashairi ya kale ya Kiebrania, vitu hivyo vimepotea kabisa katika tafsiri. Kipengele kimoja utakachogundua, hata hivyo, ni kujirudiarudia kwa fikra au mawazo, wakati mwingine ikiitwa “usambamba.” Mstari huu kutoka katika Isaya unajumuisha mfano rahisi:

  • Jivike nguvu zako, Ee Sayuni;

  • Jivike mavazi yako mazuri, Ee Yerusalemu (Isaya 52:1).

Zaburi 29 ina mistari mingi sambamba—hapa ni mfano mmoja:

  • Sauti ya Bwana ina nguvu;

  • Sauti ya Bwana ina adhama (Zaburi 29:4).

Na hapa kuna mfano ambao ukijua kuwa mstari unaofuata ni sambamba na wa kwanza kimsingi inafanya kifungu kueleweka kwa urahisi:

  • Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote,

  • na kutindikiwa na mkate mahali penu pote (Amosi 4:6).

Katika mifano hii, wazo linarudiwa kwa mabadiliko kidogo. Mbinu hii inaweza kusisitiza wazo linalorudiwa wakati ikitumiwa tofauti kwa ukamilifu kulielezea au kulikuza.

Katika hali nyingine, vifungu sambamba viwili hutumia lugha sawa kuwasilisha mawazo yanayopingana, kama katika mfano huu:

  • Jawabu la upole hugeuza hasira;

  • bali neno liumizalo huchochea ghadhabu (Mithali 15:1).

Usambamba huu haukutokea kwa bahati mbaya. Waandishi waliufanya kwa makusudi. Uliwaruhusu kuelezea hisia za kiroho au kweli za kiroho katika njia iliyoonekana kwao yenye nguvu na nzuri. Kwa hiyo unapoona usambamba katika maandishi ya Agano la Kale, jiulize mwenyewe unakusaidiaje kuelewa ujumbe wa mwandishi. Kwa mfano, ni kitu gani Isaya amekuwa akijaribu kusema kwa kuhusisha “nguvu” na “mavazi mazuri” na “Sayuni” na “Yerusalemu”? (Isaya 52:1). Tunaweza kufahamu nini kuhusu kirai “jawabu la upole” ikiwa tunajua kwamba “neno liumizalo” ni kinyume chake? (Mithali15:1).

Picha
mtu akiandika kwenye karatasi ya kukunja

Anarejesha Moyo Wangu, na Walter Rane

Mashairi ya Kiebrania kama Rafiki Mpya

Yaweza kuwa msaada kwako kulinganisha usomaji wa mashairi na kukutana na mtu mpya. Kwa mfano, unaweza kulinganisha usomaji wa mashairi ya Agano la Kale na kukutana na mtu kutoka nchi ya mbali na utamaduni mgeni ambaye hazungumzi lugha moja kama sisi—na ambaye anaweza kuwa na umri wa zaidi ya miaka elfu mbili. Mtu huyu huenda atazugumuza vitu ambavyo mwanzoni hatuvielewi, lakini hiyo haina maana kwamba hana kitu cha thamani cha kutuambia. Tukiwa na subira kiasi na ukarimu kiasi, rafiki yetu mpya anaweza baadae kuwa rafiki wa dhati. Tunahitaji tu kutumia muda kiasi kuwa pamoja, tukijaribu kuona vitu kutokana na mtazamo wake. Tunaweza kukuta kwamba katika mioyo yetu tunaelewana vizuri sana.

Kwa hiyo mara ya kwanza unaposoma kifungu kutoka katika Isaya, kwa mfano, kifikirie kama utambulisho wako wa kwanza kwa mtu mpya. Jiulize mwenyewe, “Ni nini msukumo wangu kwa ujumla?” Ni kwa jinsi gani kifungu hiki kinakufanya ujihisi—hata kama huelewi kila neno? Kisha kisome tena, mara nyingi kama inawezekana. Watu wengine hupata maana ya nyongeza kwa kusoma kifungu kwa sauti. Gundua maneno maalum Isaya aliyochagua, hususan maneno yanayoleta picha katika akili yako. Je, picha hizi zinakufanya uhisi vipi? Taswira inapendekeza nini kuhusu Isaya alivyohisi? Kadri unavyosoma maneno ya washairi hawa wa Agano la Kale, ndivyo zaidi utagundua kuwa kwa makusudi walichagua maneno yao na mbinu kuelezea ujumbe wa kina wa kiroho.

Mashairi yanaweza kuwa marafiki wa kupendeza kwa sababu yanatusaidia kuelewa hisia zetu na uzoefu wetu. Mashairi ya Agano la Kale yana thamani hasa, kwa sababu yanatusaidia kuelewa hisia zetu muhimu na uzoefu wetu—ule ambao unaendana na uhusiano wetu na Mungu.

Unapojifunza ushairi katika Agano la Kale, kumbuka kwamba kujifunza maandiko kuna thamani kubwa wakati yanapotuongoza kwa Yesu Kristo. Tafuta ishara, taswira, na kweli zinazojenga imani yako katika Yeye. Sikiliza minong’ono ya Roho Mtakatifu wakati unapojifunza.

Fasihi ya Hekima

Kipengele kimoja cha mashairi ya Agano la Kale ni kile ambacho wasomi hukiita “fasihi ya hekima.” Ayubu, Mithali, na Mhubiri huangukia katika kundi hili. Wakati zaburi huelezea hisia za sifa, maombolezo, na kuabudu, fasihi ya hekima inafokasi zaidi kwenye ushauri usiopitwa na wakati au maswali ya kina ya kifalsafa. Kitabu cha Ayubu, kwa mfano, kinaangazia haki ya Mungu na sababu za mateso ya mwanadamu. Mithali hutoa ushauri juu ya jinsi ya kuishi vyema, ikiwa ni pamoja na misemo yenye hekima iliyokusanywa na kurithishwa kutoka vizazi vya zamani. Na Mhubiri inaongoza kwenye kujiuliza kuhusu lengo la maisha—wakati kila kitu kinapoonekana kusambaa na bila mpangilio, wapi tunapata maana ya kweli? Unaweza kufikiria fasihi ya hekima kama mazungumzo ya kujali na washauri wenye mwongozo ambao wanataka kushiriki baadhi ya mitazamo kuhusu Mungu na dunia ambayo Yeye aliiumba—na pengine kukusaidia kuelewa mambo haya vizuri zaidi kuliko ulivyoelewa hapo awali.

Chapisha