Agano la Kale 2022
Novemba 28–Desemba 4. Nahumu; Habakuki; Sefania: “Njia Zake Ni Za Milele”


“Novemba 28–Desemba 4. Nahumu; Habakuki; Sefania: ‘Njia Zake Ni Za Milele,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Novemba 28–Desemba 4. Nahumu; Habakuki; Sefania,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022

Picha
Yesu akitazama nyota juu

“Njia zake ni za milele” (Habakuki 3:6). Hapo Mwanzo Kulikuwako Neno, na Eva Timothy

Novemba 28–Desemba 4

Nahumu; Habakuki; Sefania

“Njia Zake Ni Za Milele”

Unaweza kusoma maandiko katika maisha yote na bado upate umaizi mpya. Usihisi kuwa lazima uelewe kila kitu sasa hivi. Omba msaada wa kutambua ujumbe unaohitaji leo.

Andika Misukumo Yako

Kusoma Agano la Kale mara nyingi kunamaanisha kusoma unabii juu ya uharibifu. Bwana mara kwa mara aliwaita manabii kuwaonya waovu kwamba hukumu Zake ziko juu yao. Huduma za Nahumu, Habakuki, na Sefania ni mifano mizuri. Kwa maelezo ya kutisha, manabii hawa walitabiri kuanguka kwa miji ambayo, wakati huo, ilionekana kuwa na nguvu na uwezo—Ninawi, Babeli, na hata Yerusalemu. Lakini hiyo ilikuwa maelfu ya miaka iliyopita. Kwa nini ni muhimu kusoma unabii huu leo?

Ingawa miji hiyo yenye kiburi, na waovu iliharibiwa, kiburi na uovu vinaendelea. Katika ulimwengu wa leo, wakati mwingine tunaweza kuhisi kuzungukwa na maovu ambayo yalilaaniwa na manabii wa kale. Tunaweza hata kugundua athari zake mioyoni mwetu. Unabii huu wa Agano la Kale unaonyesha jinsi Bwana anavyohisi juu ya kiburi na uovu, na unafundisha kwamba tunaweza kuachana na maovu haya. Labda hiyo ni sababu moja bado tunasoma unabii huu wa kale leo. Nahumu, Habakuki, Sefania, na wale wengine hawakuwa manabii wa maangamizi tu—walikuwa manabii wa ukombozi. Maelezo ya uharibifu yametiwa moyo na mialiko ya kuja kwa Kristo na kupokea rehema Yake: “Mtafuteni Bwana …; tafuta haki, tafuta upole” (Sefania 2:3). Hii ilikuwa njia ya Bwana zamani, na ni njia yake leo. “Njia zake ni za milele” (Habakuki 3:6).

Kwa muhtasari wa vitabu hivi, ona “Nahumu,” “Habakuki,” na “Sefania” katika Kamusi ya Biblia.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Nahumu 1

Bwana ni mwenye nguvu na mwenye huruma.

Ujumbe wa Nahumu ulikuwa kutabiri uharibifu wa Ninawi—mji mkuu wa milki yenye jeuri ya Ashuru, ambayo ilitawanya Israeli na kuitesa Yuda. Nahumu alianza kwa kuelezea ghadhabu ya Mungu na nguvu isiyo na kifani, lakini pia alisema juu ya huruma na wema wa Mungu. Unaweza kufikiria kutambua mistari katika sura ya 1 inayokusaidia kuelewa kila moja ya sifa hizi—na sifa zingine za Mungu unazoziona. Kwa nini unahisi ni muhimu kujua kila mojawapo ya mambo haya kumhusu Bwana?

Wengine wanaweza kupata shida kupatanisha mafundisho ya maandiko kwamba “Bwana ni mwema” (Nahumu 1:7) na mafundisho kwamba Yeye “atalipiza kisasi kwa wapinzani wake” (Nahumu 1:2). Katika Kitabu cha Mormoni, Koriantoni mtoto wa Alma alikuwa na maswali kama hayo “kuhusu haki ya Mungu katika adhabu ya mwenye dhambi” (Alma 42:1). Ili kujifunza zaidi juu ya rehema ya Mungu na jinsi inavyohusiana na haki Yake, soma jibu la Alma kwa Koriantoni katika Alma 42.

Picha
ngome ya mawe

Bwana ni mwema, ni ngome katika siku ya taabu” (Nahumu 1:7).

Habakuki

Ninaweza kuamini mapenzi ya Bwana na wakati wake.

Hata manabii wakati mwingine wana maswali juu ya njia za Bwana. Habakuki, ambaye aliishi wakati wa uovu ulioenea katika Yuda, alianza rekodi yake na maswali kwa Bwana (ona Habakuki 1:1–4). Ni kwa jinsi gani ungeweza kufupisha wasiwasi wa Habakuki? Je, umewahi kuwa na hisia sawa na hizo?

Bwana alijibu maswali ya Habakuki kwa kusema kwamba Atawatuma Wakaldayo (Wababeli) kuiadhibu Yuda (ona Habakuki 1:5–11). Lakini Habakuki bado alikuwa na wasiwasi, kwani ilionekana kuwa sio haki kwa Bwana kusimama karibu “wakati yule mwovu [Babeli] atamla mtu aliye mwadilifu zaidi [Yuda]” (ona mstari wa 12–17). Unapata nini katika Habakuki 2:1–4 ambayo yanakuhimiza kumtumaini Bwana wakati una maswali yasiyo na majibu?

Sura ya 3 ya Habakuki ni sala ya sifa kwa Mungu na usemi wa imani Kwake. Nini kinakuvutia kuhusu maneno ya Habakuki katika mistari wa 17–19? Ni jinsi gani sauti ya mistari hii ni tofauti na Habakkuk 1:1–4? Tafakari jinsi unaweza kukuza imani kubwa katika Mungu, hata wakati maisha yanaonekana kutokuwa sawa.

Ona pia Waebrania 10:32–39; 11; Mafundisho na Maagano 121:1–6; Robert D. Hales, “Kumsubiria Bwana: Mapenzi Yako Yatimie,” Liahona, Nov. 2011, 71–74.

Sefania

“Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia.”

Sefania alitoa unabii kwamba watu wa Yuda wataangamizwa kabisa na Wababeli kwa sababu ya uovu wao. “Nitakomesha kabisa vitu vyote visionekane juu ya uso wa dunia, asema Bwana” (Sefania 1:2). Na bado Sefania pia alisema kuwa “mabaki” yatahifadhiwa (Sefania 3:13). Unaposoma unabii huu, angalia aina ya mitazamo na tabia ambazo zilisababisha Yuda na vikundi vingine kuangamizwa Sefania 1:4–6, 12; 2:8, 10, 15; 3:1–4. Kisha tafuta sifa za watu ambao Mungu angewahifadhi—ona Sefania 2:1–3; 3:12–13, 18–19. Je, ni ujumbe gani unahisi Bwana alionao kwako katika mistari hii?

Sefania 3:14–20 inaelezea furaha ya wenye haki baada ya Bwana “kumtupa nje adui yako” (mstari wa 15). Ni baraka gani zilizoahidiwa katika mistari hii zinajitokeza kwako? Kwa nini ni muhimu kwako kujua kuhusu baraka hizi? Unaweza kulinganisha mstari hii na uzoefu ulioelezewa katika 3 Nefi 17 na utafakari jinsi Yesu Kristo anahisi juu ya watu Wake—pamoja na wewe.

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Nahumu 1:7Ni kwa jinsi gani Bwana ni kama “ngome imara”? Labda familia yako inaweza kujenga boma rahisi au ngome katika nyumba yako na kujadili Nahumu 1:7 ukiwa ndani yake. Ni nini kinachofanya siku yetu iwe “siku ya taabu”? Je! Yesu Kristo na injili Yake hutuimarishaje? Je! Ni jinsi gani tunaonesha kwamba “tunamwamini”?

Habakuki 2:14.Je! Tunawezaje kusaidia kutimiza unabii katika mstari huu?

Habakuki 3:17–19.Je, tunajifunza nini kutoka kwenye mfano wa Habakuki katika mistari hii?

Sefania 2:3.Ungeweza kucheza mchezo ambao wanafamilia wanapaswa kupata maneno “haki” na “upole” kwenye ukurasa pamoja na maneno mengine mengi. Wangeweza kuzungumza juu ya mifano ya haki na upole ambao wameona kati yao. Inamaanisha nini kutafuta haki na upole?

Sefania 3:14–20.Je! Tunapata nini katika Sefania 3:14–20 kinachotufanya tutake “kuimba, … kufurahia na kushangilia kwa moyo wote”? Labda familia yako inaweza kuimba nyimbo za Kanisa au nyimbo ambazo zinakuja akilini wakati wanasoma mistari hii.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa “Seek the Lord Early,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 108.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Kuwa mvumilivu. Wakati mwingine tunataka majibu ya maswali yetu mara moja, lakini umaizi wa kiroho huchukua muda na hauwezi kulazimishwa. Kama Bwana alivyomwambia Habakuki, “Ingojee; kwa kuwa haina budi kuja” (Habakuki 2:3).

Picha
Yesu akishuka na amevaa joho jekundu

“Bwana Mungu wako katikati yako ni mwenye nguvu” (Sefania 3:17). Anakuja Tena Kuamuru na Kutawala, na Mary R. Sauer

Chapisha