Agano la Kale 2022
Desemba 19–25. Krismasi: “Ndiye Tuliyemngoja, Naye Atatuokoa”


“Desemba 19–25. Krismasi: ’Ndiye Tuliyemngoja, Naye Atatuokoa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)

“Desemba 19-25. Krismasi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022

Mtoto Yesu amevikwa nguo nyeupe na amelazwa kwenye majani

Kwa ajili Yetu Mtoto Amezaliwa, na Simon Dewey

Desemba 19–25

Krismasi

“Ndiye Tuliyemngoja, Naye Atatuokoa”

Wakati wa msimu huu wa Krismasi, fikiria jinsi Agano la Kale limeimarisha ushuhuda wako wa Yesu Kristo kwa mwaka mzima.

Andika Misukumo Yako

Agano la Kale hubeba roho ya matarajio ya hamu. Kwa njia hiyo, ni kidogo kama msimu wa Krismasi. Kuanzia na Adamu na Hawa, wahenga wa Agano la Kale, manabii, washairi, na watu walitazamia siku nzuri, zilizojazwa na tumaini la kufanywa upya na ukombozi wa Masiya. Na Waisraeli mara kwa mara walihitaji tumaini hilo—iwe walikuwa utumwani Misri au Babeli au wafungwa kwa dhambi au uasi wao wenyewe. Katika hayo yote, manabii waliwakumbusha kwamba Masiya, Mkombozi, atakuja “kutangaza uhuru kwa wafungwa” (Isaya 61:1).

Tumaini hilo lilianza kutimizwa wakati Yesu Kristo alipozaliwa huko Bethlehemu. Mkombozi hodari wa Israeli alizaliwa katika zizi na kulazwa katika hori la ng’ombe (ona Luka 2:7). Lakini Yeye hakuwa Mkombozi tu wa Waisraeli wa kale. Alikuja kukukomboa—kuchukua masikitiko yako, kujitwika huzuni zako, kuchubuliwa kwa maovu yako, ili kwamba kwa kupigwa Kwake upate kuponywa (ona Isaya 53:4–5). Hii ndio sababu Krismasi imejaa matarajio ya furaha hata leo. Masiya alikuja zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, na Anaendelea kuja maishani mwetu kila tunapomtafuta.

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Ninafurahi kwa Mkombozi wangu.

Krismasi inajulikana kama majira ya shangwe kwa sababu shangwe ambayo Yesu Kristo anaileta ulimwenguni. Hata watu wasiomwabudu Yesu kama Mwana wa Mungu mara nyingi wanaweza kuhisi furaha ya Krismasi. Tafakari furaha unayohisi kwa sababu Baba wa Mbinguni alimtuma Mwanawe.

Karne kabla ya Mwokozi kuzaliwa, manabii wa Agano la Kale pia walihisi furaha walipokuwa wakisema juu ya Masiya anayekuja. Soma baadhi ya vifungu vifuatavyo, na ufikirie kwa nini vingekuwa vya thamani kwa wale ambao walitarajia misheni ya Mwokozi: Zaburi 35:9; Isaya 25:8–9; 44:21–24; 51:11; Sefania 3:14–20; Musa 5:5–11. Kwa nini vifungu hivi ni muhimu kwako?

Ona pia Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 81–84.

Ishara zinaweza kunisaidia kumkumbuka Yesu Kristo.

Mila nyingi zinazohusiana na Krismasi zinaweza kuwa na maana ya ishara ambayo inatuelekeza kwa Kristo. Mapambo yenye umbo la nyota yanawakilisha nyota angavu iliyong’aa usiku wa kuzaliwa kwa Yesu (ona Mathayo 2:2). Waimbaji wanaweza kutukumbusha juu ya malaika ambao walionekana kwa wachungaji (ona Luka 2:13–14). Unapojifunza Agano la Kale mwaka huu, unaweza kuwa umeona ishara nyingi za Mwokozi. Chache zimeorodheshwa chini: Fikiria kujifunza hizi na kuandika kile zinachokufundisha kumhusu Yeye.

Je! Ni ishara gani zingine, vifungu, na maelezo umeyapata katika maandiko ambayo yanayoshuhudia juu ya Yesu Kristo?

Ona pia 2 Nefi 11:4; Mosia 3:14–15; Musa 6:63; “Aina za Ishara za Kristo,” katika Mwongozo wa Maandiko, “Yesu Kristo,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.

“Jina Lake litaitwa Ajabu.”

Yesu Kristo anatajwa kwa majina na vyeo vingi tofauti. Ni vyeo gani unavipata katika mistari ifuatayo? Zaburi 23:1; 83:18; Isaya 7:14; 9:6; 12:2; 63:16; Amosi 4:13; Zekaria 14:16; Musa 7:53. Je! Ni vyeo gani vingine unavyoweza kuvifikiria? Unaweza kufurahia kuorodhesha vyeo vya Yesu Kristo ambavyo umevipata katika nyimbo za Krismasi. Je! Kila jina linaathirije jinsi unavyofikiria juu Yake?

ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Mila ya Krismasi inaweza kumwonyesha Yesu Kristo.Familia za Waisraeli zilikuwa na mila, kama Pasaka na karamu zingine, ambazo zilikusudiwa kuelekeza mioyo na akili zao kwa Bwana (ona Kutoka 12). Je! Familia yako ina mila gani wakati wa Krismasi ambayo inakusaidia kuzingatia Yesu Kristo? Je! Ni mila gani unayoijua kutoka kwa historia ya familia yako? Unaweza kufikiria kujadili kama familia mila kadhaa unazotaka kuanza. Mawazo mengine yanaweza kujumuisha kumtumikia mtu anayehitaji (kwa mawazo, ona ComeuntoChrist.org/light-the-world), kumwalika rafiki kutazama Ibada ya Krismasi ya Urais wa Kwanza pamoja nawe (broadcasts.ChurchofJesusChrist.org), kuandika wimbo wako wa Krismasi, au kutafuta njia ya ubunifu ya kushiriki ujumbe wa kuzaliwa kwa Kristo.

“Mtoto Kristo: Hadithi ya Kuzaliwa kwa Yesu.”Unawezaje kuwasaidia wanafamilia kuhisi heshima na furaha ya kuzaliwa kwa Kristo? Unaweza kutazama video ya “The Christ Child: A Nativity Story”” (ChurchofJesusChrist.org) au soma pamoja Mathayo 1:18–25; 2:1–12; Luka 1:26–38; 2:1–20. Kila mwanafamilia anaweza kuchagua mtu kutoka kwenye video au maandiko na kushiriki jinsi mtu huyo alivyohisi kuhusu Mwokozi. Wanafamilia pia wangeweza kushiriki hisia zao kumhusu Yeye.

Kumtafuta Mwokozi katika Agano la Kale.Unapojiandaa kusoma maisha ya Yesu Kristo katika Agano Jipya mwaka ujao, fikiria kupitia pamoja na familia yako yale waliyojifunza kumhusu Yeye mwaka huu katika Agano la Kale. Unaweza kukagua muhtasari wa nyenzo hii na maelezo yoyote ya kibinafsi ya kukusaidia kukumbuka kile ulichojifunza. Watoto wadogo wanaweza kufaidika kwa kutazama Hadithi za Agano la Kale au picha kwenye nyenzo hii. Je! Ni unabii gani au hadithi gani zimejitokeza bayana kwetu? Je, tunajifunza nini kuhusu Mwokozi?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “O Little Town of Bethlehem,” Nyimbo za Kanisa, na. 6.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Wasikilize wanafamilia wako. Kusikiliza ni kitendo cha upendo. Inahitaji ya kwamba tujali zaidi kuhusu kile kilicho ndani ya moyo wa mtu mwingine kuliko kile kinachofuatia katika agenda yetu au ratiba. Unapozingatia kwa makini jumbe za [wanafamilia] za kusema na zisizo za kusema, utakuja kuelewa vyema mahitaji yao, wasiwasi wao, na matamanio yao. Roho atakusaidia kujua jinsi ya kuwafundisha” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 34).

Maria na mtoto Yesu katika zizi pamoja na Wachungaji

Kuzaliwa kwa Yesu Kristo na N.C. Wyeth