“Novemba 21–27. Yona; Mika: ‘Yeye Hufurahia Rehema,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)
“Novemba 21–27. Yona; Mika,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022
Novemba 21–27
Yona; Mika
“Yeye Hufurahia Rehema”
Unapoandika misukumo yako, fikiria jinsi kanuni katika Yona na Mika zinavyoshabihiana na vitu vingine ulivyojifunza katika maandiko.
Andika Misukumo Yako
Yona alikuwa kwenye meli iliyokuwa ikielekea Tarshishi. Hakuna chochote kibaya kwa kusafiri kwenda Tarshishi, isipokuwa kwamba ni mbali sana na Ninawi, ambapo Yona alipaswa kwenda kutoa ujumbe wa Mungu. Kwa hivyo meli ilipokutana na dhoruba kubwa, Yona alijua ni kwa sababu ya kutotii kwake. Kwa msisitizo kwa Yona, mabaharia wenzake walimtupa ndani ya kina cha bahari ili kuzuia dhoruba. Ilionekana kama mwisho wa Yona na huduma yake. Lakini Bwana hakuwa amemwacha Yona—kama vile hakuwa amewaacha watu wa Ninawi na kama vile hakati tamaa kwa yeyote kati yetu. Kama vile Mika alivyofundisha, Bwana hafurahii kutulaani, lakini “hufurahia rehema.” Tunapomgeukia Yeye, “Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; [Yeye] atazitupa dhambi [zetu] zote katika vilindi vya bahari.” (Mika 7:18–19).
Kwa ajili ya muhtasari wa vitabu vya Yona na Mika, ona “Yona” na “Mika” katika Kamusi ya Biblia.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Bwana ni mwenye rehema kwa wale wote wanaomgeukia.
Kitabu cha Yona kinaonyesha, kati ya mambo mengine, jinsi Bwana alivyo mwenye rehema tunapotubu. Unaposoma Yona, tafuta mifano ya rehema Yake. Tafakari jinsi ulivyoona rehema hiyo maishani mwako. Unajifunza nini ambacho kinaweza kukusaidia kuwa na rehema zaidi kwa wengine?
Kushuhudia rehema ya Bwana mara nyingi huchochea hisia za upendo na shukrani. Walakini, Yona “hakuridhishwa” na “alikasirika sana” (Yona 4:1) wakati Bwana alipowarehemu watu wa Ninawi, ambao walikuwa maadui wa Israeli. Kwa nini huenda Yona alihisi hivyo? Je, umewahi kuwa na hisia sawa na hizo? Je! Unahisi Bwana alikuwa anajaribu kumsaidia Yona kuelewa nini katika sura ya 4?
Tafakari mafundisho katika Mika 7:18–19. Je! Kweli hizi zingewezaje kumsaidia Yona kubadilisha mtazamo wake juu ya Bwana na watu wa Ninawi?
Ona pia Luka 15:11–32; Jeffrey R. Holland, “Haki na Huruma ya Mungu,” Ensign au Liahona, Mei 2013, 16–21.
Watoto wote wa Mungu wanahitaji kusikia injili.
Ninawi ilikuwa sehemu ya milki ya Ashuru, adui wa Israeli iliyojulikana kwa vurugu na ukatili. Kwa Yona, labda ilionekana kutowezekana kwamba watu wa Ninawi walikuwa tayari kukubali neno la Mungu na kutubu. Walakini, kama Rais Dallin H. Oaks alivyofundisha: “Tusijiweke wenyewe kuwa waamuzi juu ya nani yu tayari na nani hayuko tayari. Bwana anajua mioyo ya watoto Wake wote, na kama tutaomba kwa ajili ya maongozi, Yeye atatusaidia kumpata mtu ambaye Yeye anamjua yuko “katika maandalizi ya kulisikia hilo neno’ (Alma 32:6)” (“Kushiriki Injili ya Urejesho,” Ensign au Liahona, Nov. 2016, 58–59). Je! Unajifunza nini kutoka kwa Yona 3 ambacho kinakuhimiza kushiriki injili hata na wale ambao hawaonekani kuwa tayari kubadilika?
Inaweza kusaidia kulinganisha mtazamo wa Yona (ona Yona 1; 3–4) na hisia za Alma na wana wa Mosia (ona Mosia 28:1–5; Alma 17:23–25).
Ona pia 3 Nefi 18:32.
Yesu Kristo alinukuu maandishi ya Mika.
Inajulikana vizuri kuwa Mwokozi alinukuu Isaya na Zaburi. Je! Unajua kwamba Yeye pia alimnukuu Mika mara kadhaa? Fikiria mifano ifuatayo, na utafakari kwa nini vifungu hivi vinaweza kuwa muhimu kwa Mwokozi. Kwa nini vina umuhimu kwako?
Mathayo 4:11–13 (ona 3 Nefi 20:18–20). Bwana alilinganisha mkusanyiko wa siku za mwisho na mavuno ya ngano (ona Alma 26:5–7; Mafundisho na Maagano 11:3–4). Ni nini mlingano huu unapendekeza kwako kuhusu kukusanyika kwa Israeli?
Mika 5:8–15 (ona 3 Nefi 21:12–21). Mistari hii inapendekeza nini kwako kuhusu watu wa Mungu (“uzao wa Yakobo”) katika siku za mwisho?
Mika 7:5–7 (ona Mathayo 10:35–36). Kulingana na mistari hii, kwa nini ni muhimu “kumtazamia Bwana” kwanza? Kwa nini ushauri huu ni muhimu leo?
“Je! Bwana anataka nini kutoka kwako?”
Mika anatualika tufikirie itakuwaje “kuja mbele za Bwana, na kuinama … mbele za Mungu aliye juu” (Mika 6:6). Je mistari wa 6–8 inakupa maoni gani juu ya kile ambacho ni muhimu kwa Bwana anapotathmini maisha yako?
Ona pia Mathayo 7:21–23; 25:31–40; Dale G. Renlund, “Fanya Uadilifu, Penda Huruma, na Tembea kwa Unyenyekevu na Mungu,” Ensign au Liahona, Nov. 2020, 109–12.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Yona 1–4.Watoto wako wanaweza kufurahia kufanya vitendo ambavyo vinaelezea hadithi ya Yona, kama kujifanya kukimbia, kutoa sauti kama bahari yenye dhoruba, au kujifanya kumezwa na samaki mkubwa (ona “Yona Nabii” katika Hadithi za Agano la Kale). Waulize wanafamilia wanajifunza nini kutoka kwenye uzoefu wa Yona. Kwa mfano mmojawapo wa somo kutoka kwa Yona, ona mstari wa 7 wa “Follow the Prophet” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 110–11).
-
Yona 3.Je! Yona alijifunza nini kuhusu kushiriki injili? Je! Ni nani tunamjua ambaye angebarikiwa kwa kusikiliza ujumbe wa injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo?
-
Mika 4:1–5.Kulingana na mistari hii, ni nini kitakacholeta amani na mafanikio kwa watu wa Bwana? Je, tunaweza kufanya nini ili kusaidia kutimiza unabii huu nyumbani kwetu?
-
Mika 5:2.Unaweza kuonyesha picha ya Yesu akiwa mtoto na mama yake (ona Kitabu cha Sanaa cha Injili, na. 33) upande mmoja wa chumba na picha ya Mamajusi upande mwingine. Someni pamoja Mika 5:2 na Mathayo 2:1–6. Je! Unabii wa Mika uliwasaidiaje Mamajusi kumpata Yesu? Wanafamilia wangeweza kusogeza picha ya Mamajusi karibu na picha ya Yesu. Familia yako pia inaweza kufurahia kutazama video “The Christ Child: A Nativity Story” (ChurchofJesusChrist.org).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “I’ll Go Where You Want Me to Go,” Nyimbo za Kanisa, na. 270.