“Oktoba 31–Novemba 6. Danieli 1–6: ‘‘Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)
“Oktoba 31–Novemba 6. Danieli 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Famila: 2022
Oktoba 31–Novemba 6
Danieli 1–6
“Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa”
Mzee Richard G. Scott alielezea kwamba kuandika uvuvio “unamuonyesha Mungu kwamba mawasiliano Yake ni matakatifu kwetu. Kuandika pia kutaongeza uwezo wetu wa kukumbuka ufunuo” (“Namna ya Kupata Ufunuo na Msukumo Kwa Ajili ya Maisha Yako Binafsi,” Ensign au Liahona, Mei 2012, 46).
Andika Misukumo Yako
Uwezekano mkubwa hakuna mtu atakayetishia kukutupa kwenye tanuru la moto au tundu la simba kwa sababu ya imani yako katika Yesu Kristo. Lakini hakuna hata mmoja wetu anayepitia maisha haya bila jaribio la imani. Sote tunaweza kufaidika na mfano wa watu kama Danieli, Shadraka, Meshaki, na Abednego, ambao walichukuliwa mateka wakiwa vijana na Dola kuu la Babeli (ona 2 Wafalme 24:10–15). Vijana hawa walikuwa wamezungukwa na tamaduni isiyojulikana na maadili tofauti, na walikabiliwa na vishawishi vikubwa vya kuacha imani zao na mila za haki. Walakini walibaki wakweli kwenye maagano yao. Kama Yusufu huko Misri na Esta huko Uajemi, Danieli na marafiki zake huko Babeli waliweka imani yao kwa Mungu, na Mungu alifanya miujiza ambayo bado inawahimiza waumini hadi leo.
Je! Walipataje nguvu ya kubaki waaminifu hivyo? Walifanya vitu vidogo na rahisi ambavyo Mungu ametutaka sisi sote tufanye—kuomba, kufunga, kuchagua marafiki wazuri, kumtumaini Mungu, na kuwa nuru kwa wengine. Tunapoimarishwa kwa kufanya vitu vile vile vidogo na rahisi, tunaweza kukabiliana na simba na tanuu za moto katika maisha yetu wenyewe na imani.
Kwa ajili ya muhtasari wa kitabu cha Danieli, ona “Danieli, kitabu cha” katika Kamusi ya Biblia.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Ninaweza kumtumaini Bwana wakati imani yangu inapojaribiwa.
Kwa maana fulani, sisi sote tunaishi Babeli. Ulimwengu unaotuzunguka umejaa na vishawishi vingi vya kuvunja viwango vyetu na kuhoji imani yetu kwa Yesu Kristo. Unaposoma Danieli 1, 3, na 6, angalia njia ambazo Danieli, Shadraka, Meshaki, na Abednego walishinikizwa kufanya mambo ambayo walijua ni makosa. Je, umewahi kuhisi kushinikizwa kubatilisha imani yako? Unajifunza nini kutoka kwa wanaume hawa ambacho kitakusaidia kumtumaini Bwana wakati unakabiliwa na upinzani?
Kitabu cha Danieli na maandiko mengine mengi hurekodi uzoefu ambao imani kubwa ilisababisha miujiza mikubwa. Lakini vipi ikiwa imani yetu haiongozi kwa miujiza tunayotafuta? (ona, kwa mfano, Alma 14:8–13). Kulingana na yale uliyosoma katika Danieli 3:13–18, unafikiri Shadraka, Meshaki, na Abednego wangejibu swali hili vipi? Je! Mfano wao unawezaje kuathiri jinsi unavyokabili majaribio yako ya imani? Kwa habari zaidi juu ya mstari hii, angalia ujumbe wa Mzee Dennis E. Simmons “Lakini Ikiwa Siyo…,” ((Ensign au Liahona, Mei 2004, 73–75 ).
Kitabu cha Danieli pia kinaonyesha jinsi chaguzi za haki za mtu binafsi zinaweza kusababisha wengine kuwa na imani kubwa katika Bwana. Je! Unapata mifano gani ya hii katika sura ya 1, 3, na 6? Tafakari athari ambazo chaguzi zako zinaweza kuwa kwa wengine (ona Mathayo 5:16).
Ona pia Dieter F. Uchtdorf, “Usiogope, Amini Tu,” Ensign au Liahona, Nov. 2015, 76–79; David R. Stone, “Sayuni Katikati ya Babeli,” Ensign au Liahona, Mei 2006, 90–93.
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani.
Kupitia ufunuo, Danieli aliona kwamba ndoto ya Nebukadreza ilitabiri falme za ulimwengu zijazo, pamoja na ufalme wa Mungu wa siku za usoni, ambao “hautaangamizwa kamwe” (Daniel 2:44). Kanisa ni ufalme ule ambao ulitabiriwa katika siku za mwisho,” Mzee D.Todd Christofferson alifundisha, “usioumbwa na binadamu, bali uliowekwa na Mungu wa Mbinguni na unasonga mbele kama jiwe lililochongwa kutoka mlimani bila mikono kujaza dunia” (“Kwa Nini Kanisa,” Ensign au Liahona, Nov. 2015,111). Fikiria juu ya ufalme wa Mungu wa siku za mwisho unaposoma maelezo ya jiwe katika Danieli 2:34–35, 44–45. Ni mifanano gani unayoiona kati ya jiwe na ufalme? Je! Unaonaje ufalme wa Mungu ukijaza dunia leo?
Ona pia Gordon B. Hinckley, “Jiwe Lilichongwa Toka Mlimani,” Ensign au Liahona, Mei 2007, 83-86; L.Whitney Clayton, “Wakati Utafika,” Ensign au Liahona, Nov. 2011, 11–13.
Bwana atanisaidia katika majaribu yangu.
Ni umaizi gani unaokujia unaposoma juu ya sura ya nne inayoonekana katika tanuru la moto na Shadraka, Meshaki, na Abednego? Jinsi gani maelezo haya yanaweza kukusaidia katika majaribu unayokabiliana nayo? Unaweza kupata umaizi wa ziada katika Mosia 3:5–7; Alma 7:11–13; na Mafundisho na Maagano 61:36–37; 121:5–8.
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Danieli 1–2.Mnaposoma Danieli 1 na 2 pamoja, unaweza kuangalia baraka ambazo Danieli na rafiki zake walipokea kwa kukataa kula nyama na kunywa mvinyo wa mfalme? (Ona video “God Gave Them Knowledge,” ChurchofJesusChrist.org.) Unaweza kulinganisha hizo baraka na ahadi ya Bwana kwetu tunapozishika amri Zake, kama vile Neno la Hekima (ona Mafundisho na Maagano 89:18–21)). Je, Bwana amekubariki vipi kwa kutii Neno la Hekima?
-
Danieli 3.Ni kwa jinsi gani unaweza kuisaidia familia yako kujifunza kuhusu hadithi katika Danieli 3? “ Shadraka, Meshaki, na Abednego” katika Hadithi za Agano la Kale ingeweza kusaidia. Ni nini kinachotupendeza kuhusu Shadraka, Meshaki, na Abednego? Je! Ni hali zipi tunakabiliwa nazo ambazo zinatoa changamoto kwa imani yetu na zinahitaji tuonyeshe kwamba tunamtumaini Mungu?
-
Danieli 6:1–23.Familia yako inaweza kufurahia kuigiza sehemu za hadithi katika Danieli 6:1–23 (kwa mfano, mstari wa 10–12 au 16–23). Tunajifunza nini kutoka kwenye mfano Danieli? Tunatakiwa kufanya nini ili tuweze kuwa kama yeye?
-
Danieli 6:25–27.Kulingana na mistari hii, Mfalme Dario aliathirikaje wakati Bwana alipomwokoa Danieli kutoka kwa simba? Unaweza pia kusoma katika Danieli 2:47; 3:28–29 kuhusu jinsi Mfalme Nebukadreza alivyoathirika kwa njia hiyo hiyo. Je! Ni fursa gani tunazo za kuwashawishi wengine? Jadili mifano ambayo umeiona ya jinsi imani ya watu wengine, pamoja na wanafamilia, imewagusa wengine kwa mema.
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “I Want to Live the Gospel,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 148.