Oktoba 31–Novemba6. Danieli 1–6: ‘Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
Oktoba 31–Novemba6. Danieli 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Oktoba 31–Novemba6
Danieli 1–6
“Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa”
Unaposoma Danieli 1–6, rekodi ukweli unaohisi kuupata ili kuwasaidia watoto kuwa wagunduzi.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Onesha picha za matukio katika Danieli 1–6 (ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia au Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 23, 24, 25, 26). Waombe watoto kushiriki kitu wanachojua kuhusu matukio kwenye picha. Waalike kushiriki wakati ambapo walichagua kumfuata Mwokozi, kama Danieli na rafiki zake walivyofanya.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Baba wa Mbinguni anataka niutunze mwili wangu.
Danieli na rafiki zake walikataa nyama na divai waliyopewa na mfalme kwa sababu walitaka kufuata amri za Mungu na kuepuka kuidhuru miili yao. Leo Neno la Hekima linatusaidia kuepuka vitu ambavyo vinaweza kuidhuru miili yetu.
Shughuli Yamkini
-
Shiriki pamoja na watoto “Danieli na Rafiki Zake” (katika Hadithi za Agano la Kale), au fanyia ufupisho Danieli 1:1–17. Waalike watoto waigize hadithi. Wasaidie waelewe jinsi Bwana alivyowabariki Danieli na rafiki zake kwa kuchagua kumtii Yeye (ona mstari wa17). Ni baraka zipi tunapokea kutoka kwa Mungu wakati tunapochagua mema?
-
Waoneshe watoto picha ya vitu ambavyo Neno la Hekima linatufundisha tule au tutumie na vitu ambavyo linatuambia tusile au tusivitumie (ona Mafundisho na Maagano 89). Waalike watoto wajifanye kula vitu vizuri na kusema hapana kwenye vitu vibaya. Shuhudia kwamba Bwana anatubariki tunapoitunza miili yetu. Imbeni wimbo kwa pamoja kuhusu kuitunza miili yetu, kama vile “The Lord Gave Me a Temple” au “The Word of Wisdom” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 153, 154–55). Je, wimbo huu unatufundisha nini?
Mungu atanibariki ninapochagua kumfuata Yesu Kristo.
Kitabu cha Danieli kina hadithi za watu waliochagua kufuata amri za Mungu hata wakati ilipokuwa vigumu kufanya hivyo. Ni jinsi gani utawasaidia watoto kujifunza kutoka kwenye mifano hii?
Shughuli Yamkini
-
Pata picha za hadithi hizi katika Danieli1, 3, na6 (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii, muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, au Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 23, 25, 26). Weka picha uso ukiwa chini ubaoni au sakafuni. Mwalike mtoto ageuze moja ya picha, na msaidie asimulie hadithi inayowakilishwa na picha hiyo. (Kwa msaada, ona “Danieli na Rafiki Zake,” “Shadraka, Meshaki, na Abednego,” na “Danieli na Tundu la Simba” katika Hadithi za Agano la Kale.) Baada ya kila hadithi, jadilini maswali kama haya: Je, Watu walifanya nini ili kumfuata Bwana? Ni kwa namna gani Bwana aliwabariki? Shiriki jinsi ulivyobarikiwa kwa kuchagua kumfuata Yesu Kristo. Waombe watoto kushiriki uzoefu wao.
-
Waalike watoto waigize hali ambazo wanaweza kuonesha imani yao kwa Mungu kwa kutii amri Zake. Hizi zinaweza kujumuisha kuwa mkarimu kwa ndugu, kumwambia mtu kuhusu Mwokozi au kusali kila usiku. Onesha picha ya Shadraka, Meshaki na Abednego katika tanuru la moto (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili na.25), na waombe watoto wahesabu watu walioko katika tanuru. Someni Danieli 3:24–25 ili kugundua mtu mwingine aliyekuwa katika tanuru. Shiriki ushuhuda wako kwamba Bwana yu pamoja nasi wakati tunapomfuata Yeye.
Baba wa Mbinguni ananitaka nisali kila wakati.
Danieli alikuwa radhi kuhatarisha maisha yake ili aweze kusali kwa Baba wa Mbinguni kila siku. Ni jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kujenga hamu sawa na hiyo ya kusali?
Shughuli Yamkini
-
Simulia hadithi katika Danieli 6 (ona “Danieli na Tundu la Simba” katika Hadithi za Agano la Kale), na waalike watoto wachore picha ya hadithi. Waombe watumie picha zao kusimuliana hadithi. Kwa nini Baba wa Mbinguni anatutaka tuombe kwake Yeye? Shiriki kwa nini maombi ni muhimu kwako.
-
Zungumza na watoto kuhusu nyakati wanazoweza kusali, kama vile wakati wanapoogopa, wakati wanapofanya makosa au wakati wanapohitaji msaada shuleni. Kwa nini ni vizuri kusali katika hali hizi? Wafundishe watoto kwamba popote pale walipo, wanaweza mara zote kusali ndani ya mioyo yao.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu sala, kama vile “We Bow Our Heads” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,25). Zungumza na watoto kuhusu mambo tunayoweza kuyaombea.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninaweza kufanya kilicho chema hata wakati inapokuwa vigumu.
Hadithi katika Danieli1, 3, na6 inaweza kuwapa watoto unaowafundisha ujasiri na imani ya kufanya chaguzi nzuri, hata wakati wanapohisi kuwa wapweke.
Shughuli Yamkini
-
Chora ubaoni mishale kadhaa yote ikielekeza uelekeo mmoja na kisha mshale mmoja ukielekeza uelekeo tofauti. Ni kwa jinsi gani Danieli na rafiki zake ni sawa na huo mshale mmoja? Waalike watoto watoe mifano kutoka kwenye hadithi katika Danieli1, 3, na6 (ona “Danieli na Rafiki Zake,” “Shadraka, Meshaki, na Abednego,” na “Danieli na Tundu la Simba” katika Hadithi za Agano la Kale). Waulize watoto kwa nini wanadhani ilikuwa vigumu kwa Danieli na rafiki zake kufanya chaguzi nzuri. Ni jinsi gani Bwana aliwabariki wao kwa kuchagua mema?
-
Wasaidie watoto wafikirie hali ambazo wanaweza kupata msukumo wa kufanya uchaguzi mbaya. Waalike kushiriki uzoefu wakati walipobarikiwa kwa kuchagua mema hata wakati ilipokuwa vigumu. Imbeni pamoja wimbo unaohusiana na mada hii, kama vile “Choose the Right” (Nyimbo za Kanisa, na. 239).
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani.
Wakati Danieli alipotoa tafsiri yake yenye mwongozo wa kiungu ya ndoto ya Nebukadreza, aliona jiwe “lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono” (Danieli 2:45). Jiwe hili linawakilisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ambalo limekusudiwa kuijaza dunia.
Shughuli Yamkini
-
Soma Danieli 2:31–35, 44–45 pamoja na watoto, na waalike wachore picha ya kile Nebukadreza alichoona katika ndoto yake. Waulize watoto kile wanachojifunza kutokana na mistari hii kuhusu lile jiwe katika ndoto. Eleza kwamba jiwe hili linawakilisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Waombe watoto wataje baadhi ya mambo aliyofanya Baba wa Mbinguni ili kuanzisha Kanisa Lake katika siku hizi za mwisho. Ili kuwapa mawazo, onesha picha za matukio katika Urejesho wa Kanisa (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 90–95).
-
Mpe kila mtoto kipande cha karatasi kilichokunjwakunjwa kuwakilisha jiwe katika ndoto ya Nebukadreza. Muombe kila mtoto ashiriki jinsi anavyojua kwamba Kanisa lilirejeshwa na Mungu. Wakati watoto wanaposhiriki, waalike wakupe “mawe” yao. Funga mawe hayo pamoja kwa kutumia utepe au kamba ili kutengeneza jiwe kubwa. Shuhudia kwamba tunapoimarisha shuhuda zetu na kushiriki injili na wengine, tunaunganisha imani yetu ili kusaidia ufalme wa Mungu “[kuijaza] dunia yote” (Danieli 2:35).
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto wafanye jambo fulani wiki hii ambalo linaonesha imani katika Yesu Kristo.