“Novemba 14–20. Amos; Obadia: ‘Mtafuteni Bwana, Nanyi Mtaishi,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
“Novemba 14–20. Amos; Obadia,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Novemba 14–20
Amos; Obadia
“Mtafuteni Bwana, Nanyi Mtaishi”
Unapofokasi kwenye kufundisha mafundisho ya kweli kwa njia rahisi, unatoa fursa kwa Roho Mtakatifu kushuhudia kwa watoto. Tumia shughuli katika muhtasari huu—au buni ya kwako—ikusaidie kufundisha kanuni za injili katika njia rahisi.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waombe watoto kushiriki jambo walilojifunza hivi karibuni nyumbani au kanisani. Kwa mfano, waulize ikiwa wamepata maandiko yoyote mapya au kusikia ujumbe ambao wangeweza kuushiriki na darasa.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Manabii ni wajumbe wa Yesu Kristo.
Moja ya mambo ya muhimu watoto wanayoweza kujua kuhusu manabii ni kwamba wao ni wajumbe wa Yesu Kristo. Mawazo yafuatayo yanaweza kukusaidia kuwafundisha ukweli huu muhimu.
Shughuli Yamkini
-
Mnong’oneze mmoja wa watoto ujumbe kwa ajili ya wengine darasani (kama vile kuwaomba watoto wasimame kwa mguu mmoja au wageuke katika duara), na mwombe ashiriki ujumbe kwa watoto wengine. Rudia shughuli hii, ukiwapa nafasi watoto wengine kadhaa kuwa wajumbe. Wasaidie waelewe jinsi mjumbe katika shughuli hii alivyo sawa na nabii, anayeshiriki ujumbe wa Mungu pamoja nasi. Shiriki mifano kadhaa ya ujumbe wa hivi karibuni kutoka kwa nabii aliye hai ambao umekusaidia kuwa karibu na Yesu Kristo.
-
Mwalike mtoto asimame mbele ya chumba na kujifanya kuwa nabii Amosi. Unaposhiriki baadhi ya kweli kuhusu Amosi kutoka Amosi 7:14–15, mpe mtoto picha au mhimili ashikilie ambao unaenda sambamba na ukweli, kama vile picha ya kondoo, tunda, na Bwana. Eleza kwamba Amosi alikuwa mchunga kondoo ambaye Bwana alimwita kuwa mjumbe Wake. Kisha onesha picha za Bwana na nabii aliye hai na eleza kwamba Bwana anaendelea kuwaita wajumbe wake leo. Soma Amosi 3:7 kwa sauti, na waombe watoto waoneshe kwa kidole picha sahihi wakati wanaposikia maneno “Bwana” na “manabii.” Shiriki ushuhuda wako kwamba kama vile katika siku ya Amosi, Yesu Kristo huzungumza nasi kupitia manabii Wake.
-
Shiriki hadithi kutoka kwenye gazeti la Kanisa la hivi karibuni kuhusu nabii aliye hai au kuhusu uzoefu ambao waumini wa Kanisa wamekuwa nao wakati walipofuata ushauri wa nabii. (Ona pia “Meet Today’s Prophets and Apostles” kwenye ChurchofJesusChrist.org.)
-
Imba wimbo au piga wimbo uliorekodiwa kuhusu manabii, kama vile “Follow the Prophet” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 110–11), wakati watoto wakifanyia kazi ukurasa wa shughuli ya wiki hii. Waoneshe watoto virai katika wimbo ambavyo vinafundisha jinsi manabii wanavyoongoza njia iendayo kwa Yesu Kristo.
Nikitafuta mema, Bwana atakuwa pamoja nami.
Amosi aliwaalika Waisraeli “kutafuta mema, wala si mabaya” na aliwaahidi kwamba ikiwa wangefanya hivyo, “Bwana … atakuwa pamoja nanyi.” Ni jinsi gani utawasaidia watoto kuitikia mwaliko huu na kupokea ahadi hii?
Shughuli Yamkini
-
Onesha picha kadhaa za watoto wakifanya mambo mema, kama vile kuwasaidia wengine au kupokea sakramenti. Mruhusu kila mtoto afanye zamu kuelezea moja ya picha wakati watoto wengine wakibashiri ni picha ipi anaielezea. Soma Amosi 5:14, na wasaidie watoto wafikirie njia ambazo “watatafuta” mema kila siku.
-
Waalike watoto wajichore wao wenyewe wakifanya jambo jema. Soma Amosi 5:14, na sisitiza ahadi ya Bwana kwamba Yeye atakuwa pamoja nasi wakati tunapotafuta mema. Waalike watoto waongeze kwenye michoro yao picha ya Yesu akiwa amesimama pamoja nao.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Manabii ni wajumbe wa Yesu Kristo.
Amosi 3:7 ni kifungu cha maandiko kuwasaidia watoto watambue kwamba tunapomsikiliza nabii, tunamsikiliza mjumbe wa Yesu Kristo.
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto wakariri mstari wote au sehemu ya Amosi 3:7. Kwa mfano, wape dakika chache za kusoma mstari mara kadhaa wakati ukiandika kila neno linalofuata la mstari ubaoni. Waalike watoto wafunike maandiko yao na wauseme mstari pamoja kwa sauti, wakitumia vidokezo ubaoni. Kisha futa maneno machache moja baada ya jingine mpaka watoto waweze kurudia mstari wote bila vidokezo vyovyote. Mstari huu unatufundisha nini kuhusu manabii? Ni jinsi gani nabii wetu aliye hai ametusaidia kujua kile Mwokozi anachotutaka tufanye?
-
Andika maswali kadhaa kuhusu manabii kwenye vipande vya karatasi, kama yafuatayo: Kwa nini tunao manabii? Je, manabii wana kazi gani? Je, ni kwa nini unamfuata nabii? Je, manabii wanatufundisha kuhusu nini? Waombe watoto wakae katika jozi na mtake mtoto mmoja kutoka kila jozi achague swali na amwombe mwenzake alijibu. Kama watoto wanahitaji msaada kujibu swali, wanaweza kutazama katika “Nabii” kwenye Mwongozo wa Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Baada ya mwenza kujibu swali, watoto wanaweza kubadilishana jukumu na kuchagua swali lingine.
-
Shiriki na watoto ukweli fulani kuhusu nabii wa Agano la Kale ambaye wamejifunza juu yake mwaka huu (kama vile Nuhu, Musa au Isaya). Waombe wabashiri ni nabii gani unayemwelezea. Rudia hili kwa manabii wengine.
Nikitafuta mema, Bwana atakuwa pamoja nami.
Watoto wana fursa nyingi za kuchagua mema na mabaya. Fikiria jinsi unavyoweza kuwashawishi watafute “mema na si mabaya” (mstari wa 14).
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto wachunguze Amosi 5:4–15, wakitafuta neno “tafuta.” Ni nini Bwana anataka tutafute na ahadi ipi Yeye anatoa kwa wale wanaofanya hivyo? Je, tunamtafutaje Bwana?
-
Wasaidie watoto wakariri sentensi ya mwisho ya makala ya imani ya kumi na tatu. Ni jinsi gani sisi “tunayatafuta mambo haya”?
Urejesho wa Injili ulihitimisha njaa ya ukengeufu.
Kuelewa kuhusu kitu ambacho Amosi alifundisha kuhusu ukengeufu kunaweza kuwasaidia watoto wajisikie kuwa na shukrani kwa ajili ya Urejesho wa injili.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto wasome Amosi 8:11–12, na zungumza kuhusu kile kinachotokea wakati watu hawana neno la Bwana. Wasaidie watoto watoe maana ya maneno ukengeufu na njaa, wakitumia Mwongozo wa Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org) au kamusi. Ni jinsi gani ukengeufu ni kama njaa?
-
Ili kuwasaidia watoto waelewe Ukengeufu Mkuu, rejelea pamoja nao “Baada ya Agano Jipya” (katika Hadithi za Agano Jipya, 167–70). Kisha jadilini maswali kama haya: Kwa nini kulikuwa na Ukengeufu? Ni nini kilitokea kama matokeo ya Ukengeufu? Kwa nini Bwana alirejesha injili Yake? (ona pia “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo kwa Ulimwengu la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili,” ChurchofJesusChrist.org). Wahimize watoto kuandika maswali haya na majibu yake na kushiriki na wengine wawapo na familia zao nyumbani.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Wape watoto dakika chache za kufikiri juu ya jambo walilojifunza leo ambalo wangependa kulishiriki na mwanafamilia. Wahimize kuamua ni nani watashiriki naye na jinsi gani watalishiriki.