Agano la Kale 2022
Novemba 7–13. Hosea 1–6; 10–14; Yoeli: “Nitawapenda Bure”


“Novemba 7–13. Hosea 1–6; 10–14; Yoeli: ‘Nitawapenda Bure,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)

“Novemba 7–13. Hosea 1–6; 10–14; Yoeli,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022

bibi na bwana harusi kwenye viwanja vya hekalu

Novemba 7–13

Hosea 1–6; 10–14; Yoeli

“Nitawapenda Bure”

Unaposoma maandiko na kujiandaa kufundisha, tafuta mwongozo wa kiungu kutoka kwa Roho Mtakatifu. Je, unahisi kushawishiwa kufokasi juu ya kitu gani wakati wa darasa wiki hii?

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Onesha picha ya Mwokozi na waalike watoto kushiriki jambo wanalofahamu au walilojifunza kuhusu Yeye wiki hii. Waruhusu wafanye zamu kushikilia picha wakati wanaposhiriki.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Hosea 10:12

Ninaweza kumtafuta Bwana.

Hosea 10:12 hutumia picha za kupanda mbegu, kuvuna, majira na mvua ili kutualika sisi kumtafuta Bwana. Unaposoma mstari huu, ni mawazo gani ya ubunifu huja akilini ambayo yanaweza kuwapa ushawishi watoto wamtafute Yeye?

Shughuli Yamkini

  • Wasomee watoto Hosea 10:12 na waalike wafanye matendo rahisi ili yawasaidie kuelewa mstari, kama vile kujifanya kupanda mbegu, kuchuma mboga kutoka kwenye mmea au kusimama kwenye mvua. Au onesha picha za mbegu, mimea na mvua. Wasaidie watoto walinganishe kupanda mbegu na kuvuna chakula kizuri na kuishi kwa uadilifu na kupokea baraka za Bwana. Shuhudia juu ya baraka ambazo Bwana amezimimina juu yako wakati ulipojaribu kumtafuta Yeye.

  • Chora saa ubaoni, na waombe watoto kushiriki njia tunazoweza kumtafuta Bwana kwenye nyakati tofauti za siku. Waalike watoto warudie pamoja nawe kirai “Wakati umewadia wa kumtafuta Bwana” (Hosea 10:12). Wasaidie waelewe kwamba wakati wote ni muda wa kumtafuta Bwana. Shiriki kile unachofanya kumkumbuka Yeye nyakati zote.

Yesu akiwa ameketi na watoto

Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu.

Hosea 13:4,14

Yesu Kristo ni Mwokozi wangu.

Unapofundisha kuhusu Mwokozi na Upatanisho Wake, toa ushuhuda wa upendo Wake kwa kila mmoja wa watoto.

Shughuli Yamkini

  • Onesha picha za watu kadhaa, ikiwa ni pamoja na Yesu na waombe watoto watafute nani kati ya hawa ni Mwokozi wetu. Soma Hosea 13:4, na sisitiza kwamba hakuna Mwokozi isipokuwa Yesu Kristo. Shuhudia kwamba kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kurudi kuishi na Baba wa Mbinguni tena.

  • Waruhusu watoto wafanye zamu kushikilia picha ya Yesu akiwa msalabani au kaburini na picha ya Yesu akiwa nje ya kaburi tupu. Waalike watoto wazungumze kuhusu ni kitu gani picha hiyo inakionyesha. Soma kutoka Hosea 13:14 kifungu cha maneno “Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti.” Shuhudia kwamba Yesu Kristo alituokoa na mauti na kwamba tunaweza kufufuka. Imbeni pamoja wimbo kuhusu Ufufuko, kama vile “Did Jesus Really Live Again?” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,64). Wasaidie watoto kumtambua Roho wakati wakiimba.

Yoeli 2:28

Roho Mtakatifu anaweza kuniongoza.

Unapofundisha kuhusu unabii wa Yoeli katika Yoeli 2:28, zingatia jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto kujiandaa kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu baada ya kuwa wamebatizwa.

Shughuli Yamkini

  • Wasomee watoto Yoeli 2:28 na elezea kwamba maneno “wote wenye mwili” yana maana kila mtu, inajumuisha “wana” na “mabinti” kama wao. Waalike watoto wachore picha za watu waliorejelewa katika mstari huu (wana na mabinti, wazee na vijana), ikiwa ni pamoja na wao. Eleza kwamba njia moja ambayo Baba wa Mbinguni anamimina Roho Wake ni kwa kutupatia kipawa cha Roho Mtakatifu wakati tunapobatizwa.

  • Waalike watoto kushiriki kile wanachojua kuhusu Roho Mtakatifu. Wasaidie waelewe kwamba Roho Mtakatifu anaweza kutufundisha kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na anaweza kutusaidia kujua kitu kilicho cha kweli (ona Yohana 14:26; Mafundisho na Maagano 42:17). Shiriki uzoefu ili kuwasaidia watoto waelewe jinsi Roho anavyoweza kutusaidia.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Hosea 2:19–20

Ninaweza kushika maagano yangu kwa uaminifu.

Katika kitabu cha Hosea, Bwana alilinganisha maagano Yake kwa Waisraeli na ndoa. Licha ya Waisraeli kukosa uaminifu, Yeye bado aliwapenda na aliwataka warudi. Mlingano huu unaweza kukusaidia kuwafundisha watoto kuhusu umuhimu wa kutunza maagano yetu na Bwana.

Shughuli Yamkini

  • Waambie watoto kwamba katika kitabu cha Hosea, Bwana alilinganisha maagano Yake kwa Waisraeli na ndoa. Waoneshe watoto picha ya bibi harusi na bwana harusi. Ni jinsi gani Baba wa Mbinguni anataka mume na mke watendeane? Ni jinsi gani tunaweza kumwonesha Bwana kwamba tunampenda na tutakuwa waaminifu Kwake?

  • Wasaidie watoto waelewe kwamba maagano tunayofanya na Bwana yamekusudiwa kudumu milele. Waalike watoto wasome Hosea 2:19–20, wakitafuta maneno yanayofafanua jinsi Bwana anavyohisi kuhusu maagano Yake na sisi. Je, tunaagana kufanya nini wakati tunapobatizwa? Je, tunawezaje kushika agano hili tulilolifanya na Bwana?

Hosea 13:4,14

Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wangu.

Ni jinsi gani unaweza kutumia maneno ya Hosea kuimarisha shuhuda za watoto juu ya Mwokozi na Mkombozi wao? Unapofundisha, wasaidie watoto wahisi shangwe na upendo wa Upatanisho wa Yesu Kristo.

Shughuli Yamkini

  • Waalike watoto wasome Hosea 13:4,14, wakitafuta maneno au virai vinavyomwelezea Yesu Kristo. Je, mistari hii inatufundisha nini kuhusu Yeye? Waalike watoto watumie Mwongozo wa Mada au Mwongozo wa Maandiko ili kutafuta na kushiriki maandiko mengine yanayofundisha kuhusu Yesu Kristo kama Mwokozi na Mkombozi. Shiriki ushuhuda wako juu ya Mwokozi na wape watoto fursa ya kufanya vivyo hivyo.

  • Ili kuwasaidia watoto waelewe jinsi Mwokozi anavyotoa fidia au kutukomboa kutokana na mauti, onesha video “Handel’s Messiah: Debtor’s Prison” (ChurchofJesusChrist.org). Tunajifunza nini kutokana na video hii ambacho hutusaidia kuelewa kitu ambacho Mwokozi alikifanya kwa ajili yetu?

Yoeli 2:28–29

Roho Mtakatifu anaweza kuniongoza.

Wengi wa watoto unaowafundisha yawezekana wamebatizwa na wamepokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Ni jinsi gani unaweza kutumia maandiko haya kuwasaidia waelewe nguvu na baraka ambazo huja kutokana na kusikia sauti ya Roho?

Shughuli Yamkini

  • Waalike watoto wasome pamoja Yoeli 2:28–29, wakiweka jina la kila mmoja mahali penye kirai “wanaume” na “wanawake.” Andika ubaoni sentensi kama Roho Mtakatifu anaweza… na waalike watoto wafanye zamu kumalizia sentensi. Wahimize wajumuishe mambo wanayojifunza kutoka Yohana 14:16; Moroni 10:5; Mafundisho na Maagano 42:17, na maandiko mengine.

  • Weka kitu ndani ya bakuli na waruhusu watoto wafanye zamu kumimina maji juu yake. Eleza kwamba kile kitu kinatuwakilisha sisi na maji yanamwakilisha Roho Mtakatifu. Wakati tunapobatizwa, tunapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, ambacho ni njia mojawapo ya Bwana kutimiza ahadi Yake ya “kuimimina roho [Yake].” Je ni lazima tufanye nini ili kumpokea Roho Mtakatifu? Waalike watoto kushiriki nyakati ambapo wamehisi ushawishi wa Roho Mtakatifu.

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Wasaidie watoto wabainishe jambo walilojifunza kuhusu Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo au Roho Mtakatifu leo katika darasa. Wahimize kushiriki hili pamoja na familia zao.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tafuta ufunuo kila siku. Unapojiandaa kufundisha, sali na yatafakari maandiko kwa wiki yote. Mawazo na misukumo kuhusu jinsi ya kufundisha vinaweza kukujia muda wowote na mahali popote. (Ona Kufundisha Katika Njia ya Mwokozi, 12.)