“Januari 13–19. 1 Nefi 8–10: ‘Njoo na Ule Tunda,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Januari 13–19. 1 Nefi 8–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Januari 13–19
1 Nefi 8–10
“Njoo na Ule Tunda”
Kwa kuongezea kwenye kujiona mwenyewe kwenye ono la Lehi, jaribu kuwaona watoto unaowafundisha. Ni kwa jinsi gani ono hili hutumika kwao?
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Wasiliana na watoto kadhaa kabla ya na waombe kufikiria juu ya uzoefu au maandiko wanayoweza kushiriki ambayo yamewasaidia kuhisi upendo wa Mungu.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Neno la Mungu huniongoza kwa Mungu na kunisaidia kuhisi upendo wake.
Katika ono la Lehi, tunaalikwa kupokea upendo wa Mungu, uliowakilishwa na mti na matunda yake. Unawezaje kuwasaidia watoto kukubali mwaliko huu?
Shughuli za Yakini
-
Waalike watoto wakusaidie kusimulia hadithi ya ono la Lehi kutoka 1 Nefi 8:10–34. Kuwasaidia kupata taswira ya hadithi, ungeweza kuonyesha picha ya ono la Lehi (ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia) au picha kwenye “Sura ya 6: Ndoto ya Lehi” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 18–20, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Hakikisha kwamba watoto wanajua kwamba fimbo ya chuma huwakilisha neno la Mungu, ambalo tunalisoma kwenye maandiko na kulisikia kutoka kwa manabii wanaoishi. Wasaidie kuelewa kwamba mti huwakilisha upendo wa Mungu kwetu.
-
Leta kamba kuwakilisha fimbo ya chuma katika ono la Lehi. Waombe watoto kuishikilia wakati ukiwaongoza kuzunguka chumba kuelekea picha ya mti. Wasaidie kuelewa kwamba neno la Mungu hutuleta karibu na Yeye, kama vile kamba inayowakilisha fimbo ya chuma ilivyotuongoza kwenye mti. Kuonyesha kwamba mti huwakilisha upendo wa Mungu, unaweza kuonyesha picha ya vitu ambavyo Mungu ametupatia ambavyo vinaonyesha upendo wake kwetu, kama vile Mwokozi, familia zetu, na ulimwengu wa kupendeza.
-
Leta matunda kadhaa na moyo ukiwa umeshikizwa kwayo. Wape watoto kipande cha tunda ili waonje na waulize kuhusu matunda wanayoyapenda sana. Elezea kwamba tunda katika ono la Lehi lilikuwa tunda tamu sana kuliko yote aliyowahi kuonja, na lilijaza nafsi yake na shangwe. Kama vile tunda tamu linavyotupatia furaha, tutahisi furaha tunapomfuata Yesu na kuishi na Baba wa Mbinguni tena.
-
Soma 1 Nefi 8:12, na uwaalike watoto kusikiliza kwa makini kile Lehi alichotaka kufanya baada ya kuonja tunda. Acha watoto wafanye zamu kujichukulia wao ni Lehi wakiwaalika wengine kuja na kula tunda. Je, tunaweza kufanya nini kuwaalika wengine kuja na kufurahia baraka za injili pamoja nasi?
Mungu atafunua ukweli kwangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Baada ya kusikia kuhusu ono la baba yake, Nefi alikuwa na hamu ambayo sote tunapaswa kuwa nayo—hamu ya kujua ukweli mwenyewe.
Shughuli za Yakini
-
Soma 1 Nefi 10:19, na waalike watoto kunyanyua mikono yao pale wanaposikia maneno “funuliwa” na “Roho Mtakatifu.” Wasaidie watoto kuelewa andiko hili, ambalo linafundisha kwamba Roho Mtakatifu atatusaidia kujua majibu ya maswali yetu. Kuwasaidia watoto kupata taswira ya kile inachomaanisha kwa ukweli “kufunuliwa,” leta blanketi lililokunjwa likiwa na picha ya Mwokozi ndani, na waombe watoto walifunue.
-
Imba na watoto wimbo kuhusu kutafuta ukweli, kama vile “Search, Ponder, and Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109). Onyesha picha ambazo huelezea kwa mifano maneno katika wimbo kuwasaidia watoto kukumbuka jinsi Roho Mtakatifu anavyotufundisha.
-
Fikiria kushiriki uzoefu ambapo Roho Mtakatifu alikusaidia wewe kujua jambo fulani lilikuwa la kweli. Waambie watoto jinsi Roho Mtakatifu alivyozungumza nawe.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Neno la Mungu huniongoza kwa Mungu na kunisaidia kuhisi upendo wake.
Wakati watoto katika darasa lako wakijifunza kuhusu ono la Lehi, wahimize kujifunza neno la Mungu na kushiriki upendo wa Mungu pamoja na wengine.
Shughuli za Yakini
-
Wakati watoto wakisoma mistari iliyochaguliwa kutoka 1 Nefi 8, waalike kutafuta maelezo kutoka kwenye mistari hii kwenye picha ya ono la Lehi (kama vile ile iliyoko kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia). Au waalike kuchora picha ubaoni za maelezo wanayosoma. Kisha wasaidie watoto kugundua kile ambacho alama katika ndoto huwakilisha (ona 1 Nefi 11:21–22; 12:16–18; 15:23–33, 36).
-
Kama inawezekana, leta kipande cha chuma au metali nyingine darasani na waalike watoto waelezee baadhi ya sehemu zake na vitu inavyoweza kutumika kufanya. Ni kwa jinsi gani neno la Mungu ni kama fimbo ya chuma? Wapi tunapata neno la Mungu? Kwa nini fimbo ya chuma ni muhimu sana katika ono la Lehi?
-
Waalike watoto kuandika kwenye karatasi uzoefu ambapo neno la Mungu liliwasaidia kujua kile wanachopaswa kufanya au kuwasaidia kuhisi kuwa karibu na Baba wa Mbinguni. Wanaposhiriki kile walichoandika, waalike kuviringisha karatasi zao kutengeneza umbo la fimbo. Ungeweza hata kuunganisha “fimbo” za watoto pamoja kama kiwakilishi cha fimbo ya chuma katika ndoto ya Lehi.
-
Alika baadhi ya watoto kusoma 1 Nefi 8:10–12 na waelezee kile Lehi alichoona. Waombe wengine wasome 1 Nefi 11:20–23 na waelezee kile Nefi alichoona. Kwa nini malaika alimwonyesha Nefi mtoto Yesu kumfundisha kuhusu upendo wa Mungu? Kusaidia kujibu swali hili, someni kwa pamoja Yohana 3:16 au imbeni kwa pamoja wimbo kuhusu Mwokozi, kama vile “He Sent His Son” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–35). Waambie watoto jinsi ambavyo umehisi upendo wa Baba wa Mbinguni na Mwana Wake Yesu Kristo katika maisha yako.
-
Andika ubaoni: Tunajifunza nini kutoka kwenye mfano wa Lehi? Waalike watoto kufikiria juu ya ono la Lehi na kuandika majibu mengi kadiri wawezavyo. Waombe kushiriki na darasa majibu yao. Kisha waombe watoto kumfikiria mtu wanayeweza kushiriki naye furaha ya injili.
Mungu atafunua ukweli kwangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Kama tutamuomba Baba wa Mbinguni kwa imani, ukweli “utafunuliwa [kwetu] kwa nguvu ya Roho Mtakatifu” (1 Nefi 10:19). Unawezaje kuwasaidia watoto unaowafundisha kuelewa ukweli huu?
Shughuli za Yakini
-
Waalike watoto kuzungumza kuhusu jinsi wanavyoweza kupata majibu ya swali. Wahimize watoto kusoma 1 Nefi 10:17–19 na 11:1. Ni nini Nefi angesema kama mtu angemuuliza jinsi ya kupata majibu kwa swali kuhusu injili? Ni kwa jinsi gani Mungu hutufundisha kupitia Roho Mtakatifu?. (ona M&M 8:2).
-
Waombe watoto kuzungumzia wakati ambapo Roho Mtakatifu aliwasaidia kujua kwamba jambo fulani lilikuwa la kweli. Waombe kuvuta taswira kwamba wana rafiki anayefikiria kwamba hawezi kupokea majibu kupitia Roho Mtakatifu. Nini wangeweza kushiriki kutoka 1 Nefi 10:17–19 na 11:1 kumsaidia rafiki huyo?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Wahimize watoto kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kushiriki na familia zao kile walichojifunza kuhusu ono la Lehi la mti wa uzima.