“Juni 15–21. Alma 13–16: ‘Ingia katika Pumziko la Bwana,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Juni 15–21. Alma 13–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Juni 15–21
Alma 13–16
“Ingia katika Pumziko la Bwana”
Uko na watoto katika darasa lako kwa muda mfupi tu kila wiki. Utabariki maisha yao kwa kiasi kikubwa kama unaweza kuwashawishi kuendelea kusoma kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni nje ya darasa—hasa na familia zao.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Wape watoto fursa za kushiriki kile ambacho tayari wanakijua kuhusu hadithi katika Alma 13–16. Kuwasaidia, onyesha picha kama vile zile zilizoko kwenye Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia au “Sura ya 22: Misheni ya Alma huko Amoniha” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 58–63).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ukuhani hunisaida kuja kwa Kristo.
Kwa sala tafakari kile watoto katika darasa lako wanahitaji kuelewa kutoka kwenye kile Alma alichofundisha kuhusu ukuhani katika mistari hii.
Shughuli za Yakini
-
Waombe watoto kurudia pamoja nawe maana rahisi ya ukuhani, kama vile “ukuhani ni nguvu ya Mungu.”
-
Funua maandiko kwenye Alma 13:2, na waambie watoto kwamba Mungu huwaita wenye ukuhani “katika hali ambayo watu wange … kumtumainia Mwana wake.” Kuelezea kwa mfano ni kwa jinsi gani wenye ukuhani hufanya hili, onyesha picha za jinsi wenye ukuhani wanavyotumikia (ona Kitabu cha Picha za Injili, na. 38–41, 103–9), na kisha shiriki hadithi kuhusu jinsi Yesu alivyotumikia (ona Mathayo 26:26–28; Marko 5:22–24, 35–43).
-
Funua kwenye Alma 13:6, na elezea kwamba wenye ukuhani “hufunza amri za [Mungu] kwa watoto wa watu.” Wasaidie watoto kufikiria juu ya wenye ukuhani wanaowafahamu. Ni kwa jinsi gani wao hufunza amri? Waalike watoto kuchora picha ya mwenye ukuhani wanayemfahamu akimfunza mtu amri za Mungu.
Baba wa Mbinguni huniimarisha kulingana na imani yangu.
Tukio la Alma na Amuleki wakikombolewa kutoka gerezani linaweza kuwashawishi watoto kumgeukia Bwana pale wanapohitaji msaada.
Shughuli za Yakini
-
Onyesha michoro ya Alma na Amuleki kwenye ukurasa wa shughuli ya wiki hii unaposimulia hadithi katika Alma 14:18–29. Ungeweza pia kurejelea “Sura ya 22: Misheni ya Alma huko Amoniha” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 58–63, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Acha watoto wafanye zamu kutumia michoro kusimulia hadithi. Sisitiza kwamba Alma na Amuleki walipewa nguvu kutoroka gerezani “kulingana na imani [yao] katika Kristo” (Alma 14:26).
-
Wasaidie watoto kufikiria jinsi Alma na Amuleki walikuwa wamehisi wakati wakiwa gerezani, na waalike kuigiza hisia hizi (ona mstari wa 22). Elezea kwamba Alma alimuomba Bwana kwa ajili ya usaidizi (ona mstari wa 26). Shuhudia kwamba Mungu atatuimarisha pale tunapoomba kwa imani.
-
Tumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kuwafundisha watoto kuhusu baadhi ya njia Mungu hutumia kuwaimarisha wale wenye imani. Wakati watoto wakipaka rangi ukurasa wa shughuli, simulia kuhusu wakati ambapo Mungu alikupa nguvu.
Ninabarikiwa pale ninapomfuata nabii.
Zoramu, kapteni mkuu wa jeshi la Wanefi, alijua kwamba Alma alikuwa nabii na alitafuta mwongozo wake. Kwa sababu ya hili, Zoramu alifanikiwa.
Shughuli za Yakini
-
Shiriki kwa maneno yako mwenyewe tukio katika Alma 16:1–8. Sisitiza kwamba kwa sababu Zoramu na majeshi ya Wanefi walimfuata nabii Alma, Wanefi waliweza kuwaokoa rafiki zao ambao walikuwa wakishikiliwa kama wafungwa na Walamani. Shiriki uzoefu pale ulipobarikiwa kwa sababu ulimfuata nabii.
-
Onyesha picha ya Rais wa Kanisa, na shiriki mambo machache ambayo ametufunza kufanya. Wasaidie watoto kufikiria jinsi wanavyoweza kumfuata Yesu kwa kufanya kile nabii Wake anachotufunza kufanya.
-
Onyesha picha za manabii (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 6–9, 14, 18, 26–27) wakati ukiimba na watoto wimbo kuhusu manabii, kama vile “Follow the Prophet” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 110–11). Sisitiza vifungu vya maneno katika wimbo ambavyo hufundisha kwa nini tunapaswa kumfuata nabii.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ukuhani hunisaida kuja kwa Kristo.
Unaposoma Alma 13:1–19, ni nini unapata ambacho huongeza heshima yako kwa ukuhani? Ni nini unashawishika kushiriki na watoto unaowafundisha? Mawazo yafuatayo yangeweza kusaidia.
Shughuli za Yakini
-
Soma pamoja na watoto Alma 13:10 and 13, mkitafuta sifa mwenye ukuhani anapaswa kuwa nazo. Waombe wawafikirie watu wanaowajua ambao ni mifano bora ya sifa hizi.
-
Wasaidie watoto kutengeneza orodha ya ibada tunazopokea kupitia ukuhani (ona “Ibada” katika Kweli katika Imani, 109–10). Muombe mmoja kusoma Alma 13:16. Ni kwa jinsi gani ibada hizi hutusaidia sisi “kumtazamia mbele [Yesu Kristo] kwa ondoleo la dhambi [zetu]”?
-
Waulize watoto kama wanajua jinsi Ukuhani wa Melkizedeki ulivyopata jina lake. Wasaidie kupata majibu katika Alma 13:14–19 na Mafundisho na Maagano 107:1–4. Ni nini tunajifunza kutoka kwa Melkizedeki kuhusu ni kwa jinsi gani ukuhani unapaswa kutumika?
Baba wa Mbinguni huniimarisha kulingana na imani yangu.
Alma na Amuleki walikuwa gerezani kwa siku nyingi kabla ya Bwana kuwaweka huru. Hadithi hii inaweza kuwasaidia watoto kujifunza kwamba majaribu yao yanaweza yasiwe na suluhisho la haraka na rahisi, lakini Bwana atawaimarisha “kulingana na imani [yao]” (Alma 14:26).
Shughuli za Yakini
-
Andika maswali ubaoni kuwasaidia watoto kutafuta maelezo kutoka Alma 14:18–29, kama vile ni nini mahakimu walifanya kwa Alma na Amuleki gerezani? Au ni kwa jinsi gani walionyesha imani yao katika Yesu Kristo? Mpe kila mtoto mstari mmoja au miwili kusoma, wakitafuta majibu ya maswali.
-
Waalike watoto kuchora picha za matukio kutoka Alma 14:18–29, na kisha waache watumie picha zao kusimulia hadithi. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa kama Alma na Amuleki?
-
Shiriki uzoefu ambapo ulionyesha imani kwa Bwana na akakupa nguvu ya kushinda au kuvumilia jaribu. Wahimize watoto kushiriki uzoefu sawa na huo ambao wamekuwa nao.
Injili inaweza kubadilisha mioyo.
Zeezromu kwa nguvu aliwapinga Alma na Amuleki mwanzoni, lakini shuhuda zao ziligusa moyo wake na kumpa msukumo kutubu. Unapojifunza mistari hii, fikiria jinsi uzoefu wa Zeezromu ungeweza kuwashawishi watoto unaowafundisha.
Shughuli za Yakini
-
Pitia tena pamoja na watoto kile walichojifunza wiki iliyopita kuhusu Zeezromu. Someni pamoja Alma 15:3–12 kugundua jinsi alivyobadilika.
-
Waalike watoto kufikiria wamekutana na Zeezromu kabla hajatubu. Je, ni nini wangesema kumsaidia yeye kuamini injili? Wangeweza kulinganisha kile ambacho wangesema na kile Alma na Amuleki walichomfundisha Zeezromu (ona Alma 11:40–46; 15:6–11). Je, ni kwa nini kujua kweli hizi kungemsaidia mtu kutaka kubadilika?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kufikiria jambo wanaloweza kufanya wiki hii kuonyesha imani yao kwa Bwana. Wahimizi kushiriki mipango na uzoefu wao na familia zao.