“Agosti 17–23. Helamani 1–6: ‘Mwamba wa Mkombozi Wetu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Agosti 17–23. Helamani 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Agosti 17–23.
Helamani 1–6
“Mwamba wa Mkombozi Wetu”
Shughuli katika muhtasari huu zimekusudiwa kuamsha mawazo na msukumo katika moyo na akili yako. Mawazo mazuri zaidi mara nyingi huja wakati kwa sala unapotafakari maandiko na mahitaji ya watoto unaowafundisha.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Ili kuwasaidia watoto katika kujifunza kwao injili nyumbani, waalike baadhi yao kushiriki jambo walilojifunza wiki hii. Elezea jinsi unavyojifunza injili nyumbani, na zungumza kuhusu njia ambazo watoto wangeweza kusaidia familia zao kujifunza kutoka katika Kitabu cha Mormoni.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ninaweza kujenga msingi wangu juu ya Yesu Kristo.
Helamani aliwafundisha wana wake Nefi na Lehi kujenga maisha yao juu ya mwamba wa Mkombozi wetu. Tafakari jinsi unavyoweza kufanya vivyo hivyo kwa watoto unaowafundisha.
Shughuli za Yakini
-
Onyesha picha ya hekalu au jengo jingine, na elezea kwamba majengo hayo yanahitaji msingi imara ili yasianguke kwenye upepo au dhoruba. Ili kuelezea hili kwa mfano, waalike watoto kujaribu kusogeza mwamba kwa kuupuliza. Soma mistari michache ya mwanzo ya Helamani 5:12, na waombe watoto kunyanyua mikono wakati wanaposikia nani ni “mwamba” ambaye anapaswa kuwa msingi wetu.
-
Waalike watoto kufanya matendo unaposoma Helamani 5:12. Kwa mfano, wangeweza kupunga mikono yao wakati ukisoma kuhusu “pepo kali” za shetani na kusimama sehemu moja wakati ukisoma kuhusu “mwamba wa Mkombozi wetu.”
-
Waalike watoto wakusaidie kutengeneza umbo kwa kutumia matofali au zana zingine. Anza kwa kutengeneza “msingi wa uhakika,” na zungumza nao kuhusu jinsi gani Yesu Kristo anapaswa kuwa msingi wa uhakika wa maisha yetu. Waombe watoto washiriki mambo wanayoweza kufanya kumfuata Yesu Kristo, na waruhusu kuongeza tofali kwenye msingi wa umbo kwa kila kitu wanachoshiriki.
-
Waalike watoto kupaka rangi ukurasa wa shughuli, na wasaidie kuukata na kuuondoa. Tunaweza kufanya nini ili kujenga maisha yetu juu ya msingi wa Yesu Kristo? Shiriki baadhi ya njia ambazo umejenga maisha yako juu ya Mwokozi na jinsi kufanya hivyo kulivyobariki maisha yako.
Roho Mtakatifu hunong’oneza kwa sauti ndogo, tulivu.
Maelezo katika Helamani 5:29–30, 45–47 ya sauti ambayo Walamani waliisikia ni sawa na jinsi mara nyingi tunavyoelezea jinsi Roho Mtakatifu anavyozungumza. Unaweza kutumia mistari hii kuwasaidia watoto kutambua sauti ya Roho.
Shughuli za Yakini
-
Shiriki tukio la Nefi na Lehi gerezani. Ungeweza kutumia “Mlango wa 37: Nefi na Lehi Gerezani” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 99–102, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Wakati unapozungumza kuhusu sauti waliyoisikia Walamani, zungumza kwa sauti ya taratibu. Rudia hadithi mara kadhaa, na waalike watoto kunong’ona pamoja nawe. Waambie watoto kuhusu nyakati ambapo Roho Mtakatifu alikunong’oneza na kuimarisha ushuhuda wako.
-
Soma Helamani 5:30, na imba pamoja na watoto wimbo kuhusu Roho Mtakatifu, kama vile “The Still Small Voice” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 106–7 ). Onyesha maneno katika mstari wa maandiko na wimbo unaoelezea jinsi Roho Mtakatifu anavyozungumza nasi (ona pia Helamani 5:45–47). Tumia Helamani 5:29 na uzoefu wako mwenyewe kushiriki pamoja na watoto mifano michache ya mambo mazuri Roho Mtakatifu anayoweza kutupatia msukumo wa kufanya.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninapokuwa mnyenyekevu, Baba wa Mbinguni atanibariki.
Kitabu cha Mormoni kina mifano mingi ya madhara ya kiburi na baraka za unyenyekevu, na mifano kadhaa ya haya ipo katika Helamani 1–6 Unaposoma milango hii, tafakari ni kwa jinsi gani unaweza kutumia mifano hii kuwafundisha watoto katika darasa lako.
Shughuli za Yakini
-
Waruhusu watoto wakusaidie kuchora ubaoni mchoro ufuatao wa “mzunguko wa kiburi.” Someni pamoja Helamani 3:24, 33–34 na 4:11–15, na waalike watoto kuonyesha sehemu za mzunguko zinazoelezewa na mistari hii.
-
Andika maneno Nyenyekevu na Enye kiburi ubaoni. Andika mifano kadhaa ya matendo ya unyenyekevu na kiburi kwenye vipande vya karatasi, na waalike watoto kufanya zamu kuchagua karatasi na kuiweka pembeni ya neno ubaoni ambalo huelezea tendo lile. Ni baadhi ya njia zipi tunaweza kuchagua kuwa wanyenyekevu?
Nitajenga msingi wangu juu ya Yesu Kristo.
Helamani 5:12 ina taswira zenye nguvu za kujenga msingi wetu juu ya Yesu Kristo. Unawezaje kutumia taswira hizi ili kuwaelezea watoto kwa mifano kuhusu kanuni hii? Kufanya hivyo kutasaidia kuwaandaa watoto kwa ajili ya majaribu na taabu watakazopata.
Shughuli za Yakini
-
Leta darasani zana kadhaa ambazo zinaweza kuwakilisha misingi dhaifu na imara (kama vile mipira ya pamba au jiwe au kigae lilicho bapa). Waalike watoto wajenge mnara kwa kutumia matofali au zana zingine juu ya aina tofauti za misingi. Nini hufanya baadhi ya misingi kuwa imara kuliko mingine? Someni pamoja Helamani 5:12, na waulize watoto kwa nini wanadhani Yesu Kristo ni “msingi imara” kwa maisha yetu. Ni kwa jinsi gani tunaweza kujenga maisha yetu Kwake? Waalike watafute Helamani 3:27–29, 35 na Makala ya Imani 1:4 ili kupata mawazo.
-
Waalike watoto kupitia kwa haraka Helamani 5:5–14 na kuhesabu ni mara ngapi neno “kumbuka” limetajwa. Ni nini Helamani aliwafunza wanawe ambacho walipaswa kukumbuka? Ni kwa jinsi gani kukumbuka vitu hivi hutusaidia kumfanya Yesu Kristo msingi wa maisha yetu?
Toba hubadilisha giza la kiroho kuwa nuru.
Walamani waliokwenda gerezani kumuua Nefi na Lehi walizungukwa na giza halisi. Tunapotenda dhambi, tunakuwa kwenye giza la kiroho. Helamani 5:20–52 hutufundisha jinsi “wingu letu la giza” linavyoweza kuondolewa (mstari wa 41).
Shughuli za Yakini
-
Fanya darasa liwe giza kadiri iwezekanavyo; kisha soma au fanyia ufupisho maelezo katika Helamani 5:20–40 kwa kutumia tochi ndogo. Ni kwa jini gani Walamani walihisi wakati wakiwa gizani? Waalike watoto kusikiliza kile Aminadabu alichowafundisha watu kufanya ili kwamba giza liweze kuondolewa, na kisha soma mstari wa 41. Kisha washa taa, na someni mstari wa 42–48 kwa pamoja. Mistari hii inatufundisha nini kuhusu baraka ambazo toba huleta kwenye maisha yetu?
-
Waalike watoto kufikiria kwamba wanamfundisha mtoto mdogo kuhusu Roho Mtakatifu. Wangewezaje kutumia Helamani 5:29–33, 44–47 kufundisha vile sauti ya Roho ilivyo na baadhi ya mambo Roho anayotuambia? Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu amekupa msukumo kutubu? Waalike watoto kushiriki uzoefu wakati walipohisi amani na faraja ya Roho Mtakatifu.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kuwauliza wanafamilia kuhusu jinsi walivyojenga maisha yao juu ya Yesu Kristo. Au wangeweza kushiriki pamoja na familia zao jinsi wanavyopanga kujenga maisha yao Kwake.