“Agosti 3–9. Alma 43–52: ‘Simama Imara katika Imani ya Kristo,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Agosti 3–9. Alma 43–52,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Agosti 3–9
Alma 43–52
“Simama Imara katika Imani ya Kristo”
Unapopanga shughuli, unaweza kupata mawazo hapa katika mapendekezo kwa ajili ya kufundisha wote watoto wadogo na watoto wakubwa.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waombe watoto kushiriki kile wanachokumbuka kuhusu baadhi ya watu na hadithi katika Alma 43–52, kama vile Kapteni Moroni au bendera ya uhuru. Ili kuwasaidia kukumbuka, onyesha picha kutoka kwenye Hadithi za Kitabu cha Mormoni, Kitabu cha Sanaa ya Injili, au Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Alma 43:17–21; 48:7–8; 49:1–5; 50:1–6
Naweza kupata ulinzi wa kiroho katika injili.
Ili kuwalinda Wanefi dhidi ya Walamani, Moroni aliwaandaa watu wake kwa vazi la vita na kuimarisha. Juhudi zake zinatufundisha jinsi tunavyoweza kupata usalama wa kiroho.
Shughuli za Yakini
-
Wasimulie watoto kidogo kuhusu vita kati ya Wanefi na Walamani (ona Alma 43), ukisisitiza kuwa Wanefi walivaa vazi la vita ili kujilinda. Ungeweza kutumia “Mlango wa 31: Kapteni Moroni Anamshinda Zerahemna” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 85–88, au video inayohusiana katika ChurchofJesusChrist.org). Soma Alma 43:19, na uwaalike watoto kuonyesha sehemu mbalimbali za mwili wao wakati wakisikia zikitajwa katika maandiko.
-
Elezea kwamba kama vile Wanefi walivyokuwa kwenye vita ya kimwili, sisi tuko kwenye vita ya kiroho dhidi ya Shetani, ambaye hataki sisi tutii amri za Mungu. Mchore mtoto ubaoni, na wasaidie watoto kufikiria vitu ambavyo vinatulinda kiroho kama vile vazi la vita linavyolinda miili yetu (kwa mfano, sala, kusoma maandiko, au kutii amri). Kila mara jambo linapotajwa, chora kipande cha vazi la vita kwa mtoto aliyeko ubaoni.
Alma 46:11–16; 48:11–13, 16–17
Ninaweza kuwa mwaminifu kama Kapteni Moroni.
Moroni ni mfano mkuu wa imani, ujasiri, na huduma. Fikiria jinsi unavyoweza kuwapa msukumo watoto kufuata mfano wake.
Shughuli za Yakini
-
Onyesha picha ya Moroni kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia. Wasimulie watoto kuhusu bendera ya uhuru na kile kilichokuwa kimeandikwa juu yake, ukitumia vifungu vya maneno kutoka Alma 46:11–16. Ungeweza kurejelea “Mlango wa 32: Kapteni Moroni na Bendera ya Uhuru” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 89–90, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Waache watoto wasaidie kusimulia hadithi mara nyingi iwezekanavyo. Onyesha kwamba Moroni alitumia bendera ya uhuru kuwasaidia Wanefi kukumbuka kile kilichokuwa muhimu kwao.
-
Wasaidie watoto kutengeneza bendera ya uhuru kwa ajili yao au kwa ajili ya darasa lako. Anza kwa kuwasaidia kufikiria mambo wanayoyaamini au mambo ambayo Baba wa Mbinguni anawataka wakumbuke. Acha wachore picha ya mambo haya kwenye kipande kikubwa cha karatasi, au ungeweza kuleta picha kwa ajili yao kuambatanisha kwenye karatasi.
-
Waombe watoto wakuambie kuhusu baadhi ya watu wanaotaka kufanana nao na kwa nini wanataka kufanana nao. Kisha shiriki pamoja nao baadhi ya maneno kutoka Alma 48:11–13 ambayo yanamuelezea Moroni, na waalike kukisia ni nani ambaye maneno haya yanamuelezea. Onyesha picha ya Moroni, na zungumza kuhusu jinsi tunavyoweza kuwa kama yeye.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Alma 43:17–21; 48:7–8; 49:1–5; 50:1–6
Naweza kupata ulinzi wa kiroho katika injili.
Ulimwengu una hatari nyingi za kiroho, lakini kuna mengi ambayo watoto wanaweza kujifunza kutoka kwa Wanefi kuhusu jinsi ya kujilinda wenyewe.
Shughuli za Yakini
-
Mwalike kila mtoto kusoma kimya kimya moja ya mistari ifuatayo ambayo huelezea jinsi Wanefi walivyojiandaa kwa vita dhidi ya Walamani: Alma 43:19; 48:8; 49:1–5; na 50:2–4. Waombe watoto kushiriki kile walichojifunza (toa msaada kama itahitajika). Elezea kwamba tuko katika vita ya kiroho dhidi ya Shetani, na tunapaswa kujilinda wenyewe kiroho, kama vile Wanefi walivyojilinda kimwili kutoka kwa Walamani. Ni aina gani ya vazi la vita la kiroho au kuimarisha tunaweza kutengeneza ili kujilinda katika vita vyetu vya kiroho?
-
Wasaidie watoto kutengeneza ngao kwa kutumia kipande kikubwa cha karatasi au kadibodi, na waombe waandike juu yake mambo yanayotulinda kiroho. Mpatie kila mtoto kipande cha karatasi, na waalike watoto kuandika jambo baya ambalo shetani anaweza kutujaribu tufanye (kama vile kudanganya, kuiba, au kutokuwa mkarimu). Waombe wafinyange karatasi na kutengeneza mipira na kuirusha kwenye ngao ili kuonyesha kwa kielelezo jinsi injili inavyoweza kutuweka salama kutokana na Shetani (ona pia Waefeso 6:16).
Alma 46:11–16; 48:11–13, 16–17
Ninaweza kuwa mwaminifu kama Kapteni Moroni.
Moroni alikuwa mfuasi mwaminifu na shujaa wa Yesu Kristo, ambaye aliwapa msukumo Wanefi kuishi injili (ona Alma 48:17). Ni nini watoto katika darasa lako wanaweza kujifunza kutoka kwenye mfano wake?
Shughuli za Yakini
-
Someni pamoja Alma 46:11–16. Ni nini Moroni alitaka Wanefi kukumbuka? (ona mstari wa 12). Ni kwa jinsi gani aliwasaidia kukumbuka mambo haya? Waombe watoto waorodheshe baadhi ya mambo ambayo Baba wa Mbinguni anataka tukumbuke. Acha watoto wabuni “bendera zao za uhuru” kwa vifungu vya maneno au picha ambazo zitawasaidia kukumbuka mambo haya.
-
Muombe mtoto asome Alma 48:17. Ili kuwasaidia watoto kuelewa kwa nini tunaalikwa kuwa kama Moroni, waalike kusoma Alma 48:11–13, 16 Waombe watafute maneno na vifungu vya maneno ambavyo hutusaidia kuelewa kwa nini Moroni alikuwa mfuasi mkuu wa Yesu Kristo. Wakati wakishiriki kile walichopata, wahimize wafikirie mambo mahususi wanayoweza kufanya kuwa zaidi kama Moroni.
Shetani hutujaribu na kutudanganya kidogo kidogo.
Watoto wanapaswa kujua kwamba Shetani atajaribu kutushawishi tufanye dhambi ndogo ili kwamba aweze kutuongoza kwenye dhambi kubwa.
Shughuli za Yakini
-
Someni pamoja mistari iliyopendekezwa kutoka Alma 47:4–19, na waelezee watoto jinsi Amalikia alivyopata udhibiti wa jeshi la Lehonti, japokuwa washiriki wa jeshi walikuwa “wamekata kauli” kwamba wasingelazimishwa kupigana na Wanefi. Nini kingetokea kama Amalikia angemwambia Lehonti kile alichopanga kufanya tangu mwanzo? Mistari hii inafundisha nini kuhusu jinsi Shetani anavyojaribu kutudanganya?
-
Onyesha picha ya nyumba ambayo imetunzwa vizuri na nyumba ambayo imeachwa, au onyesha picha ya bustani iliyositawi na bustani iliyojaa magugu. Waache watoto wazungumzie kile wanachokiona katika picha na jinsi gani mabadiliko haya yangeweza kutokea baada ya muda. Ni nini mwenye nyumba au mwenye bustani angeweza kufanya kuepusha hili. Elezea kwamba watu taratibu wanaweza kuwa watenda dhambi kama hawawezi kushinda majaribu ya Shetani ya kutenda dhambi ndogo (kama vile kutokuwa mwaminifu au kutazama ponografia) na kisha dhambi kubwa. Ni nini baadhi ya mambo mabaya ambayo tunapaswa kuepuka kuyatenda katika maisha yetu?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Muombe kila mtoto kutaja kitu kimoja alichosikia au kuhisi leo na anataka kushiriki na mwana familia. Wahimize kufuatilia mipango yao hiyo.