“Agosti 3–9. Alma 43–52: ‘Simama Imara katika Imani ya Kristo,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Agosti 3–9. Alma 43–52,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Agosti 3–9
Alma 43–52
“Simama Imara Katika Imani ya Kristo”
Yaweza kuonekana kwamba matukio yaliyoelezewa katika Alma 43–52 hayakuhusu mahsusi. Lakini kama katika maandiko yote, Bwana ana ujumbe kwa ajili yako. Kwa maombi utafute ujumbe huo.
Andika Misukumo Yako
Wakati tunaposoma maneno haya mwanzoni mwa Alma sura ya 43—“Na sasa narudia historia ya vita kati ya Wanefi na Walamani”—ni kawaida kustaajabu kwa nini Mormoni alijumuisha historia hizi za vita wakati alikuwa amebakisha nafasi ndogo kwenye mabamba (ona Maneno ya Mormoni 1:5). Ni kweli tuna fungu letu la vita katika siku za mwisho, lakini kuna umuhimu katika maneno yake zaidi ya maelezo ya mkakati na huzuni ya vita. Maneno yake pia yanatutayarisha kwa ajili ya vita ambayo “wote tumeandikishwa” (Nyimbo za Kanisa, na. 250), vita tunavyopigana kila siku dhidi ya nguvu za uovu. Vita hivi ni vya kweli, na matokeo yanaathiri maisha yetu ya milele. Kama Wanefi, sisi “tunatiwa moyo na sababu njema,” ambayo ni “Mungu wetu, dini yetu, na uhuru, na amani yetu, [familia] zetu.” Moroni aliita hii “chanzo cha Wakristo,” chanzo kilekile tunachokipigania siku ya leo (Alma 43:45; 46:12, 16).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Vita katika Kitabu cha Mormoni vinanifundisha kuhusu vita vyangu dhidi ya uovu.
Kusoma kuhusu vita baina ya Wanefi na Walamani kunaweza kuwa na manufaa zaidi kwako kama unatafuta milinganisho kwa vita vyako binafsi vya kiroho. Unaposoma Alma 43–52, tafuta kile ambacho Wanefi walifanya na kusababisha wao kuwa na mafanikio (au kukosa kuwa na mafanikio). Kisha tafakari jinsi unavyoweza kutumia kile unachojifunza kukusaidia kushinda vita vyako vya kiroho. Unapojifunza mistari kama inayofuata, andika mawazo yako kuhusu jinsi unavyoweza kufuata mfano wa Wanefi:
-
Alma 43:19. Wanefi walijiandaa kwa silaha. (Naweza kujitahidi kujitayarisha kwa silaha za kiroho.)
-
Alma 43:23–24. Walitafuta mwongozo wa nabii.
Pia ona jinsi ambavyo Walamani na Wanefi waasi walivyojaribu kuwashinda Wanefi. Vitu hivi vinaweza kukuonya kuhusu jinsi adui anavyoweza kujaribu kukushambulia. Unapojifunza, andika jinsi Shetani anavyoweza kukushambulia katika njia sawa na hizo:
-
Alma 43:8. Zerahemna alitaka kuwakasirisha watu wake ili aweze kuwa na nguvu juu yao . (Wakati ninapokasirishwa na watu wengine, ninampa Shetani nguvu juu yangu.)
-
Alma 43:29. Walamani walitaka kuwaweka Wanefi katika utumwa.
Ninapojitahidi kuwa Mwaminifu kama Moroni, nitakuwa zaidi kama Mwokozi.
Je, ungependa kuwa zaidi kama Mwokozi na kupunguza nguvu za adui katika maisha yako? Njia moja ni kufuata onyo katika Alma 48:17 ili kuwa “kama Moroni.” Zingatia sifa na tabia za Moroni ambazo zimeelezewa kote katika Alma 43–52 lakini hasa katika 46:11–28 na 48:7–17. Kipi kinakuvutia kuhusu “mtu huyu mkuu”? Ni kwa jinsi gani sifa na vitendo kama vyake vina dhoofisha nguvu za ibilisi katika maisha yako? Tafakari kile unachohisi kutiwa moyo kufanya ili kufuata mfano wa Moroni kuwa zaidi kama Mwokozi.
Shetani hutujaribu na kutudanganya kidogo kidogo.
Shetani anajua kwamba wengi wetu hatutakubali kutenda dhambi kubwa au kuamini uwongo mkubwa. Kwa hivyo, anatumia uwongo mgumu kutambua na majaribu ili kutuongoza kwenye dhambi zinazoonekana kuwa ndogo—kwa wingi kadiri anavyofikiria tutakubali. Anaendelea kufanya hivi hadi tunapopotea mbali kutoka kwenye usalama wa maisha ya haki.
Unaweza kupata mpangilio huu katika maelezo ya Amalikia akimdanganya Lehonti, unaopatikana katika Alma 47. Unapojifunza, tafakari jinsi Shetani anavyoweza kuwa anajaribu kukudanganya, kama alivyoelezea Mzee Robert D. Hales:
“Msaliti Amalikia alimhimiza Lehonti ‘ashuke chini’ ili akutane naye katika bonde. Lakini wakati Lehonti alipoondoka kwenye uwanda wa juu, alipewa sumu ‘kidogo kidogo’ mpaka akafa, na jeshi lake likabakia mikononi mwa Amalikia (ona Alma 47). Kwa mabishano na mashitaka, baadhi ya watu wanatutega kuondoka kwenye sehemu ya juu. Sehemu ya Juu ndiko nuru iliko. … Ni mahali pa usalama” (“Ujasiri wa Kikristo: Gharama ya Ufuasi ,” Ensign au Liahona, Nov. 2008, 74).
Ona Pia 2 Nefi 26:22; 28:21–22.
Umoja huleta usalama.
Katika hali zilizoandikwa mwanzoni mwa Alma 50, Ilionekana kama Walamani hawakuwa na nafasi yoyote dhidi ya Wanefi. Silaha, ngome, na juhudi za pamoja za Wanefi ziliwafanya waonekane wasioweza kushindwa (ona Alma 49:28–30 na 50:17–20). Lakini baada ya muda Walamani waliteka mingi ya miji yao—ikijumuisha ile ambayo Moroni alikuwa ameimarisha (ona Alma 51:26–27). Ni kwa jinsi gani hili lilitokea? Tafuta majibu unaposoma sura hizi (ona hasa Alma 51:1–12). Tafakari ni maonyo gani maelezo haya yanaweza kuwa nayo kwa ajili yako na kwa familia yako.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
Alma 45:2–8
Kusoma mistari hii pamoja kunaweza kutia familia yako msukumo kuwa na mazungumzo ya injili ya moja kwa moja na wanafamilia, kama Alma alivyofanya na Helamani.
Alma 46:12–22
Bendera ya uhuru iliwatia msukumo Wanefi kutii amri za Mungu na kulinda imani yao. Ni kipi kinachotutia msukumo kufanya vivyo hivyo? Pengine familia yako inaweza kutengeneza bendera yenu ya uhuru—bendera au bango lenye maneno au picha ambazo zinawakumbusha kutii amri za Mungu kila siku.
Alma 48:7–9; 49:1–9; 50:1–6
Familia yako inaposoma kuhusu ngome za Wanefi, mnaweza kujadiliana jinsi mnavyoimarisha nyumba yenu dhidi ya adui. Watoto wanaweza kufurahia kujenga ngome wakitumia vitu kama viti na blanketi, au wanaweza kuchora vile wanavyodhani ngome za Wanefi zilikuwa.
Alma 51:1–12
Mistari hii inafundisha nini kuhusu kile kinachoweza kutokea katika familia yetu wakati tunapobishana? Tunawezaje kuongeza umoja wetu?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.