Njoo, Unifuate
Agosti 24–30. Helamani 7–12: “Mkumbuke Bwana”


“Agosti 24–30. Helamani 7–12: ‘Mkumbuke Bwana,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Agosti 24–30. Helamani 7–12,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Picha
Nefi akisali kwenye mnara ndani ya bustani

Kielelezo cha Nefi kwenye mnara ndani ya bustani na Jerry Thompson

Agosti 24–30

Helamani 7–12

“Mkumbuke Bwana”

Nefi, Lehi, na wengine walikuwa na “mafunuo mengi kila siku” (Helamani 11:23). Ufunuo wa kila mara si tu kwa ajili ya manabii—unapatikana kwa ajili yako, pia. Kuandika misukumo yako kunaweza kukusaidia kupokea ufunuo mara kwa mara .

Andika Misukumo Yako

Baba yake Nefi, Helamani, alikuwa amewasihi wana wake “kumbukeni, kumbukeni”: aliwataka wakumbuke mababu zao, wakumbuke maneno ya manabii, na muhimu kabisa wamkumbuke “Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo” (ona Helamani 5:5–14). Ni wazi kwamba Nefi alikumbuka, kwa sababu huu ujumbe ni sawa na ule aliotangaza miaka mingi baadaye “bila kusita” (Helamani 10:4) kwa watu. “Jinsi gani mmeweza kumsahau Mungu wenu?” (Helamani 7:20), aliuliza. Juhudi zote za Nefi—kuhubiri, kusali, kufanya miujiza, na kumuomba Mungu alete Njaa—zilikuwa juhudi za kuwasaidia watu wamgeukie Mungu na kumkumbuka. Kwa njia nyingi, kumsahau Mungu ni shida kubwa hata kuliko kutomjua, na ni rahisi kumsahau wakati akili zetu zimevutiwa na “vitu vya ulimwengu visivyo vya maana” na kufunikwa na dhambi (Helamani 7:21; ona pia Helamani 12:2). Lakini, kama huduma ya Nefi inavyoonesha, kamwe haujachelewa sana kukumbuka na “[kugeuka] … kwa Bwana Mungu [wako]” (Helamani 7:17).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Helamani 7–11

Manabii hufunua mapenzi ya Mungu.

Kuna manabii wengi walioelezwa kote katika Kitabu cha Mormoni, lakini Helamani 7–11 ni mahali pazuri hasa kujifunza nabii ni nani, kile anachofanya, na jinsi tunapaswa kupokea maneno yake. Unaposoma sura hizi, angalia kwa makini vitendo, mawazo, na mahusiano ya Nefi na Bwana. Ni kwa jinsi gani huduma ya Nefi inakusaidia kuelewa vyema wajibu wa nabii katika siku zetu? Hapa kuna mifano michache. Je, ni nini kingine unapata?

Helamani 7:17–22:Manabii wanahubiri kuhusu toba na kuonya kuhusu matokeo ya dhambi.

Helamani 7:29; 9:21–36:Manabii wanajua kupitia ufunuo kutoka kwa Mungu kile watu wanachohitaji kusikia.

Helamani 10:7:Manabii wamepewa uwezo wa kufunga duniani na mbinguni (ona pia Mathayo 16:19; MM 132:46).

Helamani 10:4–7, 11–12:

Ni kwa jinsi gani mistari hii huathiri jinsi unavyohisi kuhusu nabii wetu aliye hai? Amefundisha nini hivi karibuni? Unafanya nini ili kusikiliza na kufuata mwongozo wake?

Helamani 9–10

Ishara na miujiza ni muhimu lakini hazitoshi kujenga imani ya kudumu.

Kama ishara au miujiza ingekuwa ya kutosha kubadili moyo wa mtu, basi Wanefi wote wangeongolewa kwa ishara za ajabu walizopewa na Nefi katika Helamani 9. Badala yake, “mgawanyiko miongoni mwa watu” (Helamani 10:1) ulitokea kwa sababu wengi wao “bado walishupaza mioyo yao” (Helamani 10:15). Ni kwa jinsi gani waovu mara nyingi hujibu ishara na miujiza? (ona Helamani 10:12–15; ona pia 3 Nefi 2:1–2). Nini hatari ya kufanya ishara kuwa msingi wa ushuhuda? (ona “Ishara,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org).

Helamani 10:2–4

Kutafakari hualika ufunuo.

Kama umewahi wakati wowote kuhisi umenyanyaswa, wasiwasi, au kuchanganyikiwa, unaweza kujifunza somo muhimu kutokana na mfano wa Nefi katika Helamani 10:2–4. Alifanya nini wakati alipohisi “kusononeshwa”? (mstari wa 3).

Rais Henry B. Eyring alifundisha, “Tunapotafakari, tunaalika ufunuo wa Roho. Kutafakari, kwangu mimi, ni kufikiria na kuomba ninakoofanya baada ya kusoma na kujifunza maandiko kwa umakini” (“Hudumu pamoja na Roho,” Ensign au Liahona, Nov. 2010, 60). Jinsi gani unaweza kuwa na tabia ya kutafakari? Kusoma kuhusu njia moja ya kutafakari neno la Mungu mara kwa mara, ona ujumbe wa Kaka Devin G. Durrant “Moyo Wangu Huyatafakari Siku Zote” (Ensign au Liahona, Nov. 2015, 112–15).

Ona pia Mithali 4:26; Luka 2:19; 1 Nefi 11:1; 2 Nefi 4:15–16; 3 Nefi 17:3; Moroni 10:3; MM 88:62.

Helamani 12

Bwana ananitaka nimkumbuke Yeye.

Katika Helamani 12, Mormoni, aliyekuwa akifupisha kumbukumbu hiyo, anatoa muhtasari wa baadhi ya masomo tunayoweza kujifunza kutokana na historia ya Nefi kwenye sura za awali. Fikiria kutumia muhtasari wake kama nafasi ya kuuchunguza moyo wako. Unaweza hata kutengeneza orodha ya baadhi ya vitu ambavyo Mormoni anasema vinasababisha watu kumsahau Bwana. Ni nini kinachokusaidia kumkumbuka? Ni mabadiliko gani umetiwa msukumo kufanya kulingana na kile ulichojifunza?

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Helamani 7–9

Ni mifanano gani tunayoona kati ya vitu ambavyo Nefi alifanya na kile manabii wanachofanya siku hizi. Nabii wetu anafundisha nini leo? Pengine unaweza kuchagua ushauri wa hivi karibuni ambao nabii ametoa na kujadiliana kama familia jinsi mnayoweza kuufuata vyema.

Helamani 10:4–5, 11–12

Je, Nefi alionyesha kwa namna gani kwamba alitafuta mapenzi ya Bwana badala ya yake mwenyewe. Ni kwa jinsi gani tunaweza kufuata mfano wake? Ni zipi baadhi ya njia ambazo familia yetu inaweza kutafuta mapenzi ya Bwana?

Helamani 11:1–16

Nefi alitamani nini na alifanya nini kuhusu hilo? Tunajifunza nini kuhusu sala kutokana na mfano wa Nefi?

Helamani 11:17–23

Tunajifunza nini kuhusu kaka yake Nefi, Lehi, katika Helamani 11:17–23? Ni nani tunayemjua ambaye anaishi maisha ya haki bila ya kutambuliwa?

Helamani 12:1–6

Je, unaweza kufikiria somo lolote la vitendo unaloweza kutumia kusaidia familia yako kuelewa maana ya “kutokutetereka”? Kwa mfano, unaweza kumualika mwanafamilia ajaribu kuweka kitu juu ya kichwa bila kuyumba. Kisha unaweza kuwaalika wanafamilia kutafuta katika Helamani 12:1–6 kupata sababu kwa nini watu wanaweza kuwa wasio thabiti katika kumfuata Bwana. Ni kwa jinsi gani tunaweza kubaki imara kiroho?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Pitia upya. Hili ni wazo la kuwasaidia wanafamilia kukumbuka maandiko ambayo wanajifunza: Chagua mstari unaoona una maana, na ubandike mahali ambapo wanafamilia watauona mara kwa mara. Waalike wanafamilia wengine kufanya zamu ya kuchagua andiko la kubandika, na kujadiliana wakati familia inapokutana, kama vile wakati wa mlo au sala ya familia.

Picha
Seantumu anatambulika kuwa muuaji

© Kitabu cha Mormoni kwa ajili ya Wasomaji Wadogo, Seantumu—Muuaji Anatambuliwa, na Briana Shawcroft; kutoa nakala ni marufuku

Chapisha