Mafundisho na Maagano 2021
Machi 29–Aprili 4. Pasaka: “Mimi Ni Yule Aliye Hai, Mimi Ni Yule Aliyeuwawa”


“Machi 29–Aprili 4. Pasaka: ‘Mimi Ni Yule Aliye Hai, Mimi Ni Yule Aliyeuwawa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Machi 29–Aprili 4. Pasaka,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021

Picha
Sanamu ya Christus

Machi 29–Aprili 4

Pasaka

“Mimi Ni Yule Aliye Hai, Mimi Ni Yule Aliyeuwawa”

Darasa la Msingi la Jumapili ya Pasaka ni fursa nzuri zaidi ya kuwasaidia watoto kuimarisha imani yao katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Tafuta mwongozo wa Bwana jinsi ya kufanya hilo. Unaweza kupata baadhi ya mawazo yenye msaada katika muhtasari huu.

Andika Misukumo Yako

Picha
ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Waruhusu watoto kushiriki nawe kile wanachofahamu kuhusu sababu za sisi kusherehekea Pasaka. Waulize ni nini familia zao hufanya ili kusherehekea Ufufuo wa Yesu Kristo wakati wa Pasaka. Au waruhusu kushiriki kile wanachojifunza kuhusu Yesu Kristo nyumbani na kwenye maandiko.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Mafundisho na Maagano 138:11–17

Kwa sababu ya Yesu Kristo, nitafufuka.

Unapowafundisha watoto kuhusu ufufuo wa Yesu Kristo, Mafundisho na Maagano 138:11–17 inaweza kukusaidia kuelezea kile inachomaanisha kufufuka. Mistari hii inaweza pia kujenga imani yao kwamba watafufuka siku moja.

Shughuli za Yakini

  • Onesha picha za kifo, kuzikwa, na Ufufuo wa Mwokozi (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 57, 58, na 59). Waulize watoto ni nini wanachojua kuhusu matukio haya. Shuhudia kwamba Yesu alikufa kwa ajili yetu na kufufuka kutoka wafu ili kwamba sote tuweze kufufuka baada ya kufa.

  • Fikiria juu ya somo la vitendo ambalo linaweza kuwasaidia watoto kuelewa nini kinatokea wakati tunapokufa (roho zetu na miili yetu hutengana) na wakati tunapofufuka (roho zetu na miili yetu huungana tena). Kwa mfano, nini hutokea tunapoondoa betri kutoka kwenye tochi au kopo la wino kutoka kwenye kalamu ya wino? Nini hutokea wakati vitu hivi vinapounganishwa tena?

  • Wasomee watoto kutoka Mafundisho na Maagano 138:17: “Roho na mwili [vitaunganika] kamwe isitengane tena, ili wapate kupokea utimilifu wa shangwe.” Je, ni kwa nini tuna shukrani kwa ajili ya miili yetu? Shiriki shangwe unayohisi kujua kwamba sote tutafufuka na kuwa na miili yetu tena.

  • Imbeni pamoja wimbo kuhusu Ufufuo, kama vile “Did Jesus Really Live Again?” au “Jesus Has Risen” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 64, 70). Wape watoto picha ambazo zinawakilisha maneno au virai katika wimbo (kwa mfano, ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 59, 60, na 61),

Mafundisho na Maagano 76:11–24; 110:1–7; Joseph Smith—Historia ya 1:14–17

Nabii Joseph Smith alimwona Yesu Kristo.

Njia moja ya kuwasaidia watoto kuimarisha imani yao katika Mwokozi ni kushiriki nao ushuhuda wa Joseph Smith: “Yu hai! Kwani tulimwona, hata katika mkono wa kuume wa Mungu”(Mafundisho na Maagano 76:22–23).

Shughuli za Yakini

  • Waoneshe watoto picha ya Ono la Kwanza la Joseph Smith (ona muhtasari wa Januari 4–10 katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia). Waalike watoto wakuambie kile kinachotendeka katika picha, na waombe wamtafute Yesu Kristo. Waulize watoto kama wanajua kuhusu nyakati zingine ambapo Joseph Smith alimwona Mwokozi. Kwa maneno yako mwenyewe, simulia kuhusu uzoefu ulioelezewa katika Mafundisho na Maagano 76:11–24; 110:1–7. Waambie watoto jinsi maandiko haya yanavyojenga imani yako katika Yesu Kristo.

  • Wakati watoto wanapaka rangi ukurasa wa shughuli ya wiki hii, wasomee maandiko yanayourejelea. Onesha maelezo katika picha ambayo yameelezewa katika mistari. Shuhudia kwa watoto kwamba Nabii Joseph Smith alimwona Yesu Kristo, na hii ni sababu moja tunajua kwamba Yesu yu hai.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Mafundisho na Maagano 76:11–24; 110:1–10; Joseph Smith—Historia ya 1:14–17

Nabii Joseph Smith alishuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai.

Wito muhimu zaidi wa nabii ni kushuhudia juu ya Yesu Kristo. Wasaidie watoto kujenga imani yao katika Mwokozi kwa kujifunza kutokana na ushuhuda wa Joseph Smith wa Yesu Kristo.

Shughuli za Yakini

  • Vifungu vya maneno vifuatavyo vinaelezea nyakati ambapo Yesu Kristo alimtokea Joseph Smith: Mafundisho na Maagano 76:11–24; 110:1–10; Joseph Smith—Historia ya 1:14–17. Ubaoni, orodhesha baadhi ya kweli tunazojifunza kuhusu Mwokozi kutoka kwenye mistari hii. Waalike watoto kutambua mistari ipi inafundisha kweli zilizoorodheshwa ubaoni. Nini kingine tunajifunza kuhusu Yesu Kristo kutoka kwenye uzoefu wa Joseph Smith?

  • Kwenye ukurasa wa shughuli ya wiki hii, wasaidie watoto kuoanisha picha na mistari ya maandiko. Kwa nini ni baraka kujua kwamba Joseph Smith alimwona Mwokozi aliyefufuka? Shiriki ushuhuda wako kwamba Yesu Kristo yu hai na kwamba Joseph Smith ni nabii.

Mafundisho na Maagano 63:49; 88: 14–17, 27; 138: 11, 14–17

Kwa sababu ya Yesu Kristo, nitafufuka.

Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kuongeza shukrani yao kwa zawadi ya Mwokozi ya ufufuo kwa ajili yetu sote?

Shughuli za Yakini

  • Mpangie kila mtoto mojawapo ya vifungu vifuatavyo vya maandiko: Mafundisho na Maagano 63:49; 88:14–17, 27; 138:11, 14–17. Waalike watoto kupekua mistari yao kupata kirai ambacho wanahisi kinabeba ujumbe wa Pasaka. Waruhusu kushiriki mawazo yao. Kama muda unaruhusu, waache watengeneze kadi ambazo zinabeba virai walivyopata ambazo wanaweza kuwapa wanafamilia au marafiki.

  • Waulize watoto jinsi ambavyo wangeelezea kwa wadogo zao au rafiki kile inachomaanisha kufufuka. Kwa mawazo, someni pamoja Mafundisho na Maagano 138:14–17, na fikiria maswali kama haya: nini hutokea kwenye roho na miili yetu wakati tunapokufa? Nini kinatokea wakati tunapofufuka? Ni kwa jinsi gani Yesu Kristo anafanya ufufuo uwezekane?

  • Onesha video “Because He Lives” (ChurchofJesusChrist.org), na waache watoto kushiriki vile wanavyohisi kuhusu kile Mwokozi alichowatendea.

    Picha
    Yesu Akisali

    Bwana wa Sala, na Yongsung Kim

Mafundisho na Maagano 18:10–13; 19:16–19; 45:3–5; 58:42–43

Kwa sababu ya Yesu Kristo, ninaweza kusamehewa dhambi zangu.

Zaidi ya kutuokoa kutoka kifo cha kimwili, Yesu Kristo alitoa njia kwa ajili yetu kuokolewa kutoka kifo cha kiroho—kwa maneno mengine, kusamehewa dhambi zetu na kurudi kwenye uwepo wa Mungu.

Shughuli za Yakini

  • Andika ubaoni vichwa viwili vya habari vinavyofanana na hivi: Kile Mwokozi alichofanya na Kile ninachopaswa kufanya. Mwalike kila mtoto kupekua mojawapo ya vifungu vifuatavyo ili kupata jambo ambalo linahusika chini ya vichwa hivi vya habari: Mafundisho na Maagano 18:10–13; 19:16–19; 45:3–5; 58:42–43. Shiriki shangwe na shukrani yako kwa ajili ya kile Mwokozi alichofanya kwa ajili yetu.

  • Wasaidie watoto kujifunza makala ya imani ya tatu. Ungeweza kuwasaidia kuikariri kwa kuonesha picha zinazoendana na virai vya msingi.

  • Onesha video “The Shiny Bicycle” (ChurchofJesusChrist.org), au simulia hadithi yako mwenyewe kuhusu mtoto ambaye alifanya uchaguzi mbaya na kisha akatubu. Wasaidie watoto kujadili kile mtoto katika hadithi alichofanya ili kupokea msamaha. Ni kwa jinsi gani Mwokozi alifanya iwezekane kwetu kusamehewa?

Picha
ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Wasaidie watoto kufikiria jambo wanaloweza kufanya ili kuwaambia watu wengine—hasa wanafamilia wao—kile Yesu Kristo amefanya kwa ajili yetu. Mnapokutana wakati ujao, waombe washiriki nawe kile walichofanya.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Watoto wananufaika kutokana na marudio. Usiogope kurudia shughuli mara nyingi, hususani na watoto wadogo. Marudio yatawasaidia watoto kukumbuka kile wanachojifunza.

Picha
ukurasa wa shughuli: Joseph Smith alimwona Yesu Kristo

Chapisha