“Septemba 20–26. Mafundisho na Maagano 106–108: ‘Mbingu Kufunuliwa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Septemba 20–26. Mafundisho na Maagano 106–108,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi: 2021
Septemba 20–26
Mafundisho na Maagano 106–108
“Mbingu Kufunuliwa”
Tafakari kile unachojua kuhusu watoto unaowafundisha. Je, ni aina gani ya shughuli zitawasogeza watoto karibu zaidi na Mwokozi? Kumbuka kwamba shughuli kwa ajili ya watoto wadogo katika muhtasari huu zinaweza kutoholewa kwa ajili ya watoto wakubwa, na kinyume chake.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waoneshe watoto picha za viongozi wa Kanisa, kama vile nabii, Mitume, Urais Mkuu wa Msingi, na Viongozi wengine Wakuu wenye Mamlaka na Maofisa Wakuu. Waalike watoto wazungumzie kuhusu nini viongozi hawa wanafanya na kwa nini wanashukuru kuwa nao.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Mafundisho na Maagano 107:18–20, 42–56
Nimebarikiwa kwa sababu ya ukuhani.
Watoto wote wa Baba wa Mbinguni wanaweza kupokea baraka ambazo huja kutokana na ukuhani. Fikiria njia ambazo unaweza kuwasaidia watoto unaowafundisha kuhisi shukrani kwa baraka hizo.
Shughuli Yamkini
-
Chora ubaoni picha inayowakilisha “mbingu [ikiwa] inafunuliwa [kwetu]” (Mafundisho na Maagano 107:19) kwa sababu ya ukuhani (kama vile miale ya mwanga ikiangaza kupitia mawinguni). Wape watoto picha zikiwakilisha baraka ambazo huja kutokana na ukuhani, kama vile ubatizo, sakramenti, na hekalu. Waalike kushiriki ni kwa nini wao wanashukuru kwa ajili ya baraka zilizoko katika picha, na waruhusu waziweke picha zao kwenye miale ya mwangaza iliyopo ubaoni. Toa ushuhuda kwamba tunaweza kuwa na baraka hizi kwa sababu Baba wa Mbinguni amerejesha ukuhani.
-
Tengeneza njia sakafuni, na wape watoto picha za ibada za ukuhani watakazohitaji ili waweze kufuata njia ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 103–8, 119–20). Wasaidie watoto kuweka ibada hizo katika mpangilio sahihi juu ya njia.
-
Onesha picha ya Adamu na Eva pamoja na familia yao (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii au Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 5). Watoto wanapoangalia picha, waulize wanadhani Adamu na Eva wanajisikiaje kuhusu familia yao. Tumia Mafundisho na Maagano 107:53–56 ili kushiriki pamoja na watoto kitu ambacho Adamu alifanya ili kuonesha anaipenda familia yake. Toa ushuhuda wako kuhusu jinsi ambavyo ukuhani umekuwa baraka kwako wewe na kwa familia yako.
-
Taja majina ya wanafamilia wa Adamu aliowatawaza kwenye ukuhani, kulingana na Mafundisho na Maagano 107:42–50, na waombe watoto kuhesabu ni watu wangapi aliwatawaza. Wasaidie kuelewa ni kwa nini Adamu angetaka washiriki wote wa familia yake wawe na ukuhani. Waalike watoto wazungumze kuhusu nyakati ambapo wao au familia zao walipokea baraka kupitia ukuhani.
Mimi ninaweza kuwaimarisha wengine.
Hata watoto wadogo wanaweza kufuata ushauri wa kuwaimarisha wengine “katika mazungumzo yako yote, katika sala zako zote, … na katika matendo yako yote.”
Shughuli Yamkini
-
Chora picha ya mtu ubaoni, na waalike watoto kutaja baadhi ya mambo ambayo mtu huyo angeweza kufanya ili awe imara kimwili. (Unaweza kuchora misuli mikubwa zaidi kwa mtu huyo wakati watoto wakitaja mambo hayo). Soma Mafundisho na Maagano 108:7, na waombe watoto kusikiliza njia tunazoweza “kuwaimarisha kaka [zetu] [na dada zetu].” Fafanua neno lolote ambalo linaweza kuwa gumu.
-
Wasaidie watoto wafikirie juu ya watu wanaowafahamu ambao huenda wakahitaji kuimarishwa. Tunaweza kusema nini kwao au kufanya nini kwa ajili yao? Fanyeni kazi kwa pamoja kuwatengenezea kadi watu hawa, au watie moyo watoto ili wawakumbuke katika sala zao binafsi au sala za familia.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Mafundisho na Maagano 107:1–8, 13–14, 18–20
Ukuhani utanisaidia kurudi kwa Baba wa Mbinguni.
Ukuhani wa Melkizedeki na wa Haruni ulirejeshwa ili kusaidia kuwarudisha watoto wa Mungu Kwake. Wasaidie watoto unaowafundisha kuelewa majukumu tofauti ya ukuhani na namna gani yanatusaidia kurudi kwa Mungu.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kupekua Mafundisho na Maagano 107:1–8, 13–14, 18–20 kwa ajili ya maneno au vifungu muhimu ambavyo huwafundisha kuhusu ukuhani. Je, ni wajibu gani walio nao watu wenye Ukuhani? Je, ni kwa jinsi gani ukuhani unatusaidia kurudi kwa Mungu?
-
Andika maswali ambayo yangeweza kujibiwa katika Mafundisho na Maagano 107:1–8, 13–14, 18–20, kama vile “Je, jina lingine la Ukuhani wa Melkizedeki ni lipi?” Wape watoto dakika chache ili watafute majibu ya maswali mengi kadri wawezavyo katika mistari hiyo. Shiriki na watoto baraka ulizopokea kupitia ukuhani.
-
Soma pamoja na watoto kuhusu Melkizedeki katika Kamusi ya Biblia au Mwongozo kwenye Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Je, tunajifunza nini kutokana na maisha yake kuhusu kile inachomaanisha kutumia mamlaka ya ukuhani?
Mafundisho na Maagano 107:21–26, 33–35, 65–66
Watumishi wateule wa Bwana wanaliongoza Kanisa Lake.
Je, ni uzoefu upi umejenga ushuhuda wako juu ya viongozi wa Kanisa.? Ni kwa jinsi gani utawasaidia watoto kujenga shuhuda zao wenyewe?
Shughuli Yamkini
-
Weka ubaoni picha ya Viongozi Wakuu wenye Mamlaka na Maafisa Wakuu kutoka katika toleo la mkutano mkuu wa hivi karibuni la Ensign au Liahona). Watoto wanaposoma Mafundisho na Magano 107:21–26, 33–35; 65–66, waalike kuandika ubaoni kile wanachojifunza kuhusu majukumu ya baadhi ya viongozi hawa. Je, kwa nini tunashukuru kwa ajili ya mwongozo wao? Shiriki na kila mmoja jinsi ulivyopata ushuhuda wa manabii na mitume.
-
Andika maneno kujiamini, imani, na sala ubaoni. Waulize watoto ni kwa namna gani sisi tunaweza kuwaunga mkono Urais wa Kwanza wa Kanisa kwa kujiamini kwetu, imani na sala (ona Mafundisho na Maagano 107:22. Kwa nini ni muhimu kuwakubali watumishi wateule wa Bwana?
Kuishi maagano yangu kwa uangalifu huleta baraka.
Tafakari jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto unaowafundisha “kuwa waangalifu zaidi … katika kushika viapo [vyao],” au maagano. Je, ni kwa jinsi gani kufanya hili kunawabariki wao sasa na katika siku za baadaye?
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kufanya kitu ambacho kinahitaji wawe waangalifu ili wafanikiwe, kama vile kujaribu kujaza maji kwenye kikombe bila kikombe kufurika na kumwagika. Je, ni kitu gani hutokea wakati tunapokuwa si waangalifu? Waalike watoto wasome Mafundisho na Maagano 108:3 na kutafuta kitu ambacho Lyman Sherman aliambiwa akifanye kwa uangalifu. Orodhesha pamoja na watoto ahadi wanazofanya na Baba wa Mbinguni wakati wanapobatizwa na kula sakramenti. Wasaidie kufikiria juu ya jinsi wanavyoweza kuwa waangalifu kuhusu kuzitunza ahadi hizi.
-
Imba pamoja na watoto wimbo kuhusu kushika maagano, kama vile “I Will Be Valiant” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 162). Wasaidie kutengeneza alama kwa kutumia kifungu cha maneno kutoka kwenye wimbo huo ambacho kinawakumbusha kushika maagano yao, na watie moyo kubandika alama zao nyumbani.
-
Wape watoto sehemu ya hotuba ya Dada Becky Craven “Makini dhidi ya Kawaida” (Ensign au Liahona, Mei 2019, 9–11), na waombe kuelezea kitu ambacho kimewahamasisha wao kuwa waangalifu zaidi kuhusu kuishi maagano yao.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Mara kwa mara wasiliana na wazazi wa watoto unaowafundisha ili kuwatia moyo katika jitihada zao za kufundisha injili nyumbani. Unaweza kuwaambia kuhusu jambo fulani ambalo watoto wao walilishiriki katika darasa la msingi jambo ambalo walijifunza nyumbani.