Mafundisho na Maagano 2021
Septemba 27–Oktoba 3. Mafundisho na Maagano 109–110: “Ni Nyumba Yako, Mahali pa Utakatifu Wako”


“Septemba 27–Oktoba 3. Mafundisho na Maagano 109–110: ‘Ni Nyumba Yako, Mahali pa Utakatifu Wako,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Septemba 27–Oktoba 3. Mafundisho na Maagano 109–110,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021

Picha
Hekalu la Kirtland

Hekalu la Kirtland, na Jon McNaughton

Septemba 27–Oktoba 3

Mafundisho na Maagano 109–110

“Ni Nyumba Yako, Mahali pa Utakatifu Wako”

Ili kupata uzoefu wa kiroho unapojifunza Mafundisho na Maagano 109–10 pamoja na watoto katika darasa lako, kwanza tafuta kupata uzoefu wa kiroho wakati unapojifunza maandiko haya wewe mwenyewe.

Andika Misukumo Yako

Picha
ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Onesha picha zitakazowasaidia watoto kukumbuka na kushiriki kitu walichojifunza kuhusu kanuni au matukio katika Mafundisho na Maagano 109–10. Kwa mfano, ungeweza kuonesha picha kutoka kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Mafundisho na Maagano 109:12–13; 110:1–7.

Hekalu ni nyumba ya Bwana.

Tafakari jinsi utakavyowasaidia watoto kuhisi unyenyekevu kwa ajili ya nyumba ya Bwana na kutazamia kwa hamu ile siku wakati watakapoweza kuingia “mahali pa utakatifu [Wake]” (Mafundisho na Maagano 109:13).

Shughuli Yamkini

  • Waombe watoto wakuambie jambo wanalopenda kuhusu nyumba zao. Waoneshe watoto picha ya hekalu la Kirtland, na tumia Mafundisho na Maagano 109:12–13; 110:1–7 ili kuwaambia watoto kuhusu siku ambayo hekalu liliwekwa wakfu na likawa nyumba ya Bwana (ona pia “Sura ya 39: Hekalu la Kirtland Limewekwa Wakfu,” Hadithi za Mafundisho na Maagano, 154). Ili kuonesha kuwa hekalu ni nyumba ya Bwana, soma yafuatayo kutoka katika sala ya kuweka wakfu ambayo Joseph Smith aliitoa: “Ni nyumba yako, mahali pa utakatifu wako” (Mafundisho na Maagano 109:13). Waombe watoto washiriki kitu wanachokipenda kuhusu hekalu.

  • Mpe kila mtoto picha ya hekalu, au waalike wachore hekalu. Imbeni pamoja wimbo kuhusu mahekalu, kama vile “I Love to See the Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95). Waalike watoto kuinua picha zao kila wakati wanapoimba neno “hekalu.” Waoneshe watoto maneno mengine katika wimbo ambayo yanatufundisha kitu fulani muhimu kuhusu hekalu. Waambie watoto jinsi unavyohisi kuhusu hekalu na jinsi gani wewe unavyojua kuwa ni nyumba ya Bwana.

Mafundisho na Maagano 110

Funguo za ukuhani zinazohitajika ili kukamilisha kazi ya Mungu ziko Kanisani leo.

Hekalu la Kirtland ni muhimu katika historia ya Kanisa. Yesu Kristo alijionesha huko, pamoja na manabii wa kale. Manabii hawa walikabidhi funguo za ukuhani kwa Joseph Smith ambazo zinahitajika ili kufanya kazi ya Mungu katika siku za mwisho.

Shughuli Yamkini

  • Tumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii au “Sura ya 40: Maono ndani ya Hekalu la Kirtland” (Hadithi za Mafundisho na Maagano, 155–57) ili kuwaambia watoto kuhusu viumbe wa mbinguni waliotembelea hekaluni. Shiriki vifungu vya maneno kutoka Mafundisho na Maagano 110 ambavyo vinakusaidia wewe na watoto kuelewa utakatifu wa matukio haya.

  • Waoneshe watoto baadhi ya funguo, na ongea nao kuhusu funguo hufanya kazi gani. Waache watoto wafanye zamu kushika funguo hizo na wajifanye wanafungua mlango uliofungwa. Wakati wakifanya hivyo, elezea kwamba Joseph Smith alipokea funguo katika Hekalu la Kirtland. Funguo hizi zinafungua nguvu na baraka ili tuweze kufanya kazi ya Mungu katika Kanisa Lake, kama vile kushiriki injili na kufanya kazi ya hekaluni.

  • Ili kuwasaidia watoto kuelewa funguo ambazo Eliya alizikabidhi kwa Joseph Smith, imbeni pamoja wimbo kuhusu Eliya au historia ya familia, kama vile “Truth from Elijah” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 90–91). Waambie kuhusu uzoefu ambao umekusaidia wewe kugeuza moyo wako kuelekea kwa mababu zako. Waombe watoto kushiriki kitu wanachokijua kuhusu babu au bibi au wahenga wengine.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Mafundisho na Maagano 109; 110:1–10

Hekalu ni nyumba ya Bwana.

Je, ni kwa jinsi gani utashiriki na watoto upendo wako juu ya nyumba ya Bwana? Zingatia namna wewe utakavyowahamasisha kukubali changamoto ya Mzee Quentin L. Cook “kwa kila mmoja wetu, popote tunapoishi, tujione wenyewe tuko hekaluni” (“Jione Mwenyewe Hekaluni,” Ensign au Liahona, Mei 2016, 98).

Shughuli Yamkini

  • Chagua mistari kutoka sehemu ya 109 au 110 ambayo unahisi inaelezea baraka za hekaluni (mingine imependekezwa katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia). Orodhesha baraka hizi ubaoni, na waalike watoto kupekua mistari uliyochagua ili kupata baraka hizo. Je, ni kwa namna gani sisi tunaweza kumwelezea mtu kwa nini hekalu ni muhimu kwetu?

  • Waambie watoto kwa ukimya wasome Mafundisho na Maagano 110:1–10, na waalike kushiriki kitu wanachojifunza kuhusu Yesu Kristo au hekalu katika mistari hii. Waalike watoto wajichore picha zao wenyewe na Mwokozi wakiwa hekaluni.

  • Waombe watoto wafikirie kuwa rafiki yao anajaribu kuitafuta nyumba yao. Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kumsaidia rafiki yetu kujua nyumba yetu ni ipi? Je, ni kwa jinsi gani tunajua kwamba hekalu ni nyumba ya Bwana? Soma Mafundisho na Maagano 109:12–13 pamoja na watoto, na waambie ni kwa namna gani wewe unajua kwamba hekalu ni nyumba ya Bwana. Onesha picha za mahekalu, na acha watoto washiriki hisia zao kuhusu nyumba ya Bwana.

  • Imba pamoja na watoto “Roho wa Mungu” (Nyimbo za Kanisa na. 2), na waambie kuwa uliimbwa wakati wa kuweka wakfu Hekalu la Kirtland—na katika uwekaji wakfu leo. Kwa nini huu ulikuwa wimbo mzuri kwa ajili ya uwekaji wakfu wa Hekalu la Kirtland?

    Picha
    Hekalu la Kirtland kwa ndani

    Kila mwisho wa Hekalu la Kirtland kuna mimbari kwa ajili ya viongozi wa ukuhani.

Mafundisho na Maagano 110:11–16

Funguo za ukuhani zilizohitajika ili kukamilisha kazi ya Mungu ziko Kanisani leo

Mzee Gary E. Stevenson alisema, “Watoto wote wa Mungu [walikuwa] wamefungiwa nje ya ibada okozi za injili ya Yesu Kristo—hadi urejesho mtukufu ulipofanywa na [Musa, Elia, na Eliya]” (“Ziko Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?Ensign au Liahona, Mei 2016, 30).

Shughuli Yamkini

  • Watake watoto watafute Mafundisho na Maagano 110:11–16 ili kupata majina ya manabii watatu wa kale walioonekana katika Hekalu la Kirtland. Kisha wasaidie kupata maneno katika mistari hii ambayo yanaeleza kile ambacho kila nabii “alikabidhi,” au alimpa, Joseph Smith na Oliver Cowdery. Unaweza kupata maelezo yenye kusaidia katika “Sura ya 40: Maono katika Hekalu la Kirtland” (Hadithi za Mafundisho na Maagano, 156–57).

  • Shiriki maelezo haya ya funguo za ukuhani yaliyotolewa na Rais Russel M. Nelson: “Ndani ya mfuko wako yawezekana kukawa na funguo za nyumba au gari yako. Funguo za ukuhani, kwa upande mwingine, hazishikiki na hazionekani. ‘Zinawasha’ mamlaka ya ukuhani” (“Wajibu Binafsi wa Ukuhani,” Ensign au Liahona, Nov. 2003, 45–46). Ili kufafanua umuhimu wa funguo za ukuhani, jadili pamoja na watoto matatizo ya kupoteza funguo za nyumba au ufunguo wa gari. Je, hii inafananaje na matatizo ya kupotea kwa mamlaka ya ukuhani? Wasaidie watoto kuelewa ni nani anashikilia funguo za ukuhani leo na namna gani funguo hizi zinatumika kufungua baraka kwa ajili ya watoto wote wa Mungu (ona “Priesthood Keys,” True to the Faith, 126–27).

  • Ili kueleza zaidi kuhusu funguo zilizorejeshwa katika Hekalu la Kirtland, onesha video “By the Hand of Elijah the Prophet” (ChurchofJesus Christ.org). Jadili kile tunachoweza kufanya ili kushiriki katika kazi ambayo imewezeshwa na funguo za Eliya. Au onesha video “Gatherers in the Kingdom” (ChurchofJesusChrist.org) na zungumzia kuhusu namna gani sisi tunaweza kusaidia kuwakusanya watoto wa Baba wa Mbinguni ili warudi Kwake.

Picha
ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Waalike watoto kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii au picha walizochora wakati wa darasa ili kuwafundisha watu wa familia zao kitu walichojifunza leo kuhusu mahekalu au funguo za ukuhani.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tengeneza mazingira ya upendo, na unyenyekevu. “Mfano wako una ushawishi mkubwa kwa mitazamo ya [watoto] hawa. … Kwa maneno na matendo yako, waoneshe kuwa unaipenda injili na kwamba unajali ukuaji wao wa kiroho” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 15).

Chapisha