“Oktoba 25–31. Mafundisho na Maagano 124–125: ‘Nyumba kwa Jina Langu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Oktoba 25–31. Mafundisho na Maagano 124–125,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021
Oktoba 25–31
Mafundisho na Maagano 124–125
“Nyumba kwa Jina Langu”
Je, ni masomo gani kutoka Mafundisho na Maagano 124–25 watoto wanahitaji kujifunza? Tafakari swali hili unapojifunza wiki hii.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Onesha picha ya hekalu lililo jirani na ninyi. Waulize watoto kile wanachojua kuhusu mahekalu. Waruhusu watoto waelezee hisia zao kuhusu kwenda hekaluni.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Mafundisho na Maagano 124:15, 20
Yesu anafurahi wakati ninapojaribu kufanya yaliyo mema.
Katika ufunuo ulioandikwa katika sehemu ya 124, Bwana alielezea kuridhika kwake juu ya Hyrum Smith na George Miller kwa sababu walikuwa wakijitahidi kumfuata Yeye. Utawasaidia vipi watoto kutambua kwamba Bwana amefurahishwa wakati wanapojitahidi kufanya mema?
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto kufikiria juu ya mambo wanayoweza kufanya ambayo ni mema. Onesha picha ili kuwapa mawazo (unaweza kuzipata nyingine katika Kitabu cha Sanaa ya Injili au magazeti ya Kanisa). Waombe watoto kuonesha mambo haya mema. Wasomee watoto, Mafundisho na Maagano 124:15 na waombe kusikiliza jinsi Bwana alivyojisikia wakati Hyrum Smith alipochagua kufanya mema. Je, Yesu anajisikiaje wakati sisi tunapojaribu kufanya mambo mema?
-
Wape watoto mioyo ya karatasi, na waombe kuchora picha za wao wenyewe wakifanya mambo mema. Waombe waelezee kile walichokichora kwa darasa. Je, tunajisikiaje wakati tunapofanya jambo jema? Shuhudia kwamba Yesu anafurahi wakati tunapojaribu kufanya kitu chema.
-
Imbeni wimbo kuhusu kufanya mambo ambayo Yesu Kristo anataka sisi tufanye, kama vile “Jesus Wants Me for a Sunbeam” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 60–61).
Mafundisho na Maagano 124:28–29, 39
Yesu anawaamuru watu Wake kujenga mahekalu.
Mahekalu daima yamekuwa sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake. Kuelewa hili kutawasaidia watoto unaowafundisha kuhisi unyenyekevu mkubwa kwa ajili ya hekalu.
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto kuelewa kwamba Watakatifu walipopata makazi mapya katika Nauvoo, Bwana aliwaambia wamjengee hekalu (ona “sura ya 50: Watakatifu katika Navoo” Hadithi za Mafundisho na Maagano, 183–84, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Waalike watoto kujifanya kuwa wanajenga hekalu.
-
Soma pamoja na watoto kifungu hiki cha maneno: “Nyumba yangu takatifu, ambayo watu wangu daima wameamriwa kuijenga kwa jina langu takatifu” (Mafundisho na Maagano 124:39). Acha watoto washike picha ya hekalu la zamani (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 52 au ukurasa wa shughuli ya wiki hii) na picha ya hekalu katika eneo lenu. Elezea kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo daima wamekuwa wakiwaamuru watu Wao kujenga mahekalu—nyakati za kale na katika siku yetu. Shiriki maneno au vifungu vya maneno kutoka Mafundisho na Maagano 124:28–29 ili kuwasaidia watoto kuelewa ni kwa nini Bwana anataka tujenge mahekalu.
-
Waalike watoto kukamilisha ukurasa wa shughuli ya wiki hii ili iwasaidie wao kuelewa kwamba sisi ni watu wa Mungu na kwamba watu wa Mungu daima wamekuwa wakiamriwa kujenga mahekalu.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Mafundisho na Maagano 124:12–21
Bwana anakuwa na furaha ninapokuwa mwaminifu.
Katika sehemu ya 124, Bwana aliwapongeza Watakatifu kadhaa kwa sababu ya uaminifu wao. Maneno Yake yanaweza kuwasaidia watoto kutambua sifa wanazopaswa kukuza.
Shughuli Yamkini
-
Chagua baadhi ya sifa nzuri zilizotajwa katika Mafundisho na Maagano 124:12–21, na ziandike ubaoni kuzunguka picha ya Mwokozi. Waombe watoto wachunguze mistari 12–21, wakitafuta maneno haya. Wasaidie kuelewa maneno ambayo yanaweza kuwa hayafahamiki kwao. Kulingana na mistari hii, Bwana anajisikiaje kuhusu watu ambao wanakuza sifa hizi?
Mafundisho na Maagano 124:28–30, 38–41.
Yesu anawaamuru watu Wake kujenga mahekalu.
Watoto unaowafundisha hivi punde watakuwa wakubwa vya kutosha kwenda hekaluni na kushiriki katika ibada za hekaluni. Unaweza kufanya nini ili kuwasaidia kujiandaa?
Shughuli Yamkini
-
Funika picha au picha ya kuchora ya hekalu. Waalike watoto kusoma Mafundisho na Maagano 124:38–41 kwa ajili ya dokezo kuhusu kile kilichoko katika ile picha. Acha watoto wafunue picha na kujadili mistari hii inafundisha nini kuhusu kwa nini Bwana anatutaka sisi tujenge mahekalu.
-
Waalike watoto kusoma Mafundisho na Maagano 124:28–30 ili kutafuta sababu ambazo Bwana alimpa Joseph Smith za kujenga Hekalu la Nauvoo. Shiriki na watoto hisia zako kuhusu hekalu na uzoefu mwingine wowote unaoweza kuwa nao kwa kufanya ubatizo kwa niaba ya wafu. Wasaidie watoto kuamua itakuwa baada ya muda gani kabla ya wao kuwa wakubwa vya kutosha kufanya ubatizo kwa niaba ya wafu hekaluni.
-
Kama unacho kibali cha hekeluni, waoneshe watoto, au mwalike kijana katika kata yako kuwaonesha watoto kibali chake cha kuingia hekaluni. Waambie watoto kwa nini kibali cha hekaluni ni muhimu na kile tunachohitaji kufanya ili kukipata. Wahimize waanze kujiandaa sasa ili kupata kibali chao wenyewe.
Mafundisho na Maagano 124:91–92
Baraka ya patriaki inaweza kunipa mwongozo wa kiungu.
Kama umepokea baraka ya patriaki, ipitie upya kabla ya kuwafundisha watoto kuhusu baraka hizi. Kwa nini una shukrani kwa sababu ya baraka yako ya patriaki? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwashawishi watoto kujiandaa kupokea baraka zao?
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mmoja wa watoto kusoma Mafundisho na Maagano 124:91–92, na alika darasa kusikiliza kile Bwana alichomwita Hyrum Smith kufanya. Je, watoto wanajua nini kuhusu baraka za patriaki? Kama umeshapokea baraka ya patriaki, waoneshe watoto vile inavyoonekana. (Kumbuka kwamba maudhui maalumu ya baraka yako ya patriaki ni matakatifu.) Elezea kwamba baraka za patriaki ni baraka maalumu tunazopata kutoka kwa mapatriaki. Baraka hizi zinaweza kutusaidia sisi kujifunza zaidi kuhusu sisi wenyewe na kile Baba wa Mbinguni anachotaka sisi tufanye.
-
Fikiria kumwalika mzazi au ndugu wa mmoja wa watoto unaowafundisha ili kushiriki na darasa kwa nini wana shukrani kwa ajili ya baraka zao za patriaki. Waombe washiriki ni kwa jinsi gani wao waliamua kuwa wanataka kupata baraka zao hizo. Toa ushuhuda wako juu ya baraka za patriaki.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kushiriki na mwanafamilia wao kitu kimoja walichojifunza kuhusu mahekalu na ni kwa nini wanataka kwenda hekaluni siku moja.