Sura ya 39 Hekalu la Kirtland Linawekwa Wakfu Januari–Machi 1836 Bwana alikuwa amewaamuru Watakatifu kujenga hekalu katika Kirtland. Watakatifu walikuwa masikini, lakini walijitolea dhabihu na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga hekalu. Walikuwa na imani kwamba Bwana angewasaidia kufanya kile Alichowataka wafanye. Wakati hekalu lilipokuwa karibia kumalizika, baadhi ya viongozi wa Kanisa walifanya mkutano huko. Kwenye mkutano, baba yake Joseph Smith aliwabariki viongozi wa Kanisa. Baba yake Joseph alikuwa patriaki wa Kanisa. Kisha Joseph Smith alipata ono la kupendeza ambapo aliona ufalme wa selestia wa mbinguni. Ufalme wa selestia ndipo ambapo Mungu anaishi. Joseph aliona jinsi ufalme wa selestia ulivyokuwa mzuri. Aliwaona Baba wa Mbinguni na Yesu. Pia alimuona ndugu yake Alvin, ambaye alikuwa amefariki. Mafundisho na Maagano 137:1–5 Joseph alishangaa kumwona Alvin katika ufalme wa selestia kwa sababu Alvin hakuwa amebatizwa kabla ya kufariki. Yesu alieleza kwamba watu wengi hawakujua kuhusu injili wakati walipoishi duniani. Mafundisho na Maagano 137:7–9 Baadhi ya watu hawa, kama Alvin, waliishi wakati ambapo injili ya kweli ya Yesu Kristo haikuwepo duniani. Baadhi yao waliishi katika maeneo ambapo wamisionari hawakuweza kuwafundisha. Baadhi ya watu hawa wangeamini injili na kubatizwa kama wangelielewa kuhusu hilo walipokuwa wakiishi duniani. Watu hawa watakwenda katika ufalme wa selestia. Mafundisho na Maagano 137:7–9 Katika ono hili, Joseph pia alijifunza kuhusu watoto ambao hufariki kabla ya kufikia umri wa miaka minane. Yesu alisema watoto hawa watakwenda kwenye ufalme wa selestia. Mafundisho na maagano 137:10 Hatimaye Hekalu la Kirtland lilimalizika na kuwa tayari kuwekwa wakfu. Hiyo ina maana hekalu lingetolewa kwa Bwana na kutumiwa tu kwa ajili ya kazi Yake. Watakatifu walikuwa na mkutano maalum wa kuweka wakfu hekalu. Watakatifu wengi walikuja kwenye mkutano. Walikuwa na furaha sana kupata hekalu. Waliimba na kumwomba Baba wa Mbinguni. Waliahidi kumfuata Nabii Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa. Joseph Smith alitoa sala maalum ya kuweka wakfu hekalu. Baada ya sala, Hekalu lilikuwa jengo takatifu. Lilikuwa nyumba ya Bwana. Malaika walikuwepo katika Hekalu la Kirtland siku hiyo. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja na Watakatifu. Ilikuwa ni siku ya kupendeza! Mafundisho na Maagano 109