Hadithi za Maandiko
Sura ya 38: Lulu ya Thamani Kuu


Sura ya 38

Lulu ya Thamani Kuu

nyumba ya majira ya baridi
Lulu ya Thamani Kuu

Lulu ya Thamani Kuu ni kitabu cha maandiko kilichoandikwa na manabii. Kuna sehemu tano za Lulu ya Thamani Kuu. Nazo ni kitabu cha Musa, kitabu cha Ibrahimu, Joseph Smith—Mathayo, Joseph Smith—Historia ya, na Makala za Imani.

Kitabu cha Musa

Joseph anapokea ufunuo

Sehemu ya kwanza ya Lulu ya Thamani Kuu ni ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith. Unaitwa kitabu cha Musa. Musa alikuwa nabii aliyeishi hapo kale.

Mungu akimtokea Musa

Kitabu cha Musa kinasimulia kile Mungu alichomwambia Musa juu ya mlima mrefu. Musa alimwona Mungu na kuzungumza Naye. Mungu alisema alikuwa na kazi maalum kwa ajili ya Musa kufanya.

Musa akiona ono

Mungu alimwonyesha Musa ulimwengu na kila kitu ambacho kingetokea ndani yake. Musa pia aliwaona watoto wote wa Mungu ambao wangeishi katika ulumwengu.

Musa akimwambia Shetani aondoke

Mungu alimwacha Musa, na Shetani alikuja na kumwambia Musa amwabudu yeye. Musa hakumwabudu Shetani na alimwambia aondoke. Wakati Shetani alipokataa kuondoka, Musa alimwomba Mungu msaada. Akipokea nguvu kutoka kwa Mungu, Musa tena alimwambia Shetani aondoke. Shetani hatimaye aliondoka, akionyesha hasira kali kwa sababu Musa hakumwabudu.

Yesu akiumba dunia

Musa alijawa na Roho Mtakatifu. Aliomba, na Mungu alikuja na kuzungumza naye tena. Mungu alimwambia Musa kwamba kuna dunia nyingi—zaidi kuliko tunavyoweza kuhesabu. Alisema kuwa Yesu aliumba dunia hizi na ataumba hata zaidi kwa sababu hakuna mwisho kwa kazi za Mungu.

Musa akiandika mafunuo yake

Musa alijifunza kwamba kazi ya Mungu ni kuwasaidia watoto Wake ili waweze kurudi kuishi Naye milele. Kitabu cha Musa pia kinaelezea kuhusu uumbaji wa dunia, Adamu na Hawa na familia yao, nabii Henoko na mji wa Sayuni, na manabii wengine walioishi miaka mingi iliyopita.

Kitabu cha Ibrahimu

mtu akiwasilisha miili iliyokaushwa kwa Joseph

Sehemu ya pili ya Lulu ya Thamani Kuu ni kitabu cha Ibrahimu. Mnamo Julai 1835, mtu mmoja aitwaye Bw. Chandler alikuja Kirtland. Aliwaonyesha Watakatifu baadhi ya miili iliyokaushwa kutoka Misri. Miaka mingi iliyopita, watu katika Misri walitumia nguo kufunika miili ya watu waliokufa. Miili hii iliitwa mummies

Bw. Chandler akiwa ameshikilia mafunjo ya Kimisri

Baadhi ya magombo ya karatasi za zamani sana yalikuwa pamoja na miili hiyo iliyokaushwa. Baadhi ya maandishi ya kigeni yalikuwa kwenye karatasi, na Bw. Chandler alikuwa akitafuta mtu ambaye angeweza kuyasoma. Alikuwa amesikia ya kwamba Joseph Smith angeweza kutafsiri maandishi hayo.

Bw. Chandler akiwasilisha mafunjo kwa Joseph

Joseph aliangalia maandishi. Bwana alimfunulia kile ambacho baadhi yake yalimaanisha, na alimwambia Bw. Chandler. Baadhi ya Watakatifu walileta magombo hayo ya karatasi kutoka kwa Bw. Chandler.

Joseph akitafsiri mafunjo

Joseph Smith alianza kujifunza maandishi hayo, na Mungu alifunua tafsiri kwake. Oliver Cowdery na William Phelps waliandika kile Joseph alichotafsiri. Maandishi yalikuwa ya nabii mkuu Ibrahimu, ambaye alikuwa akiishi Misri miaka mingi iliyopita.

Yesu akizungumza na Ibrahimu

Yesu alikuwa amezungumza na Ibrahimu na kumwambia kuhusu maisha yetu kabla ya kuja duniani. Yesu alisema tuliishi kama watoto wa kiroho pamoja na Baba wa Mbinguni kabla ya kuzaliwa kwetu. Kitabu cha Ibrahimu pia kinaelezea kuhusu uumbaji wa dunia, jua, mwezi, na nyota, vile vile uumbaji wa mimea, wanyama, na watu.

Ibrahimu akitazama mbinguni

Ibrahimu alitaka kupokea baraka ya furaha na amani. Kwa sababu Ibrahimu alikuwa mwaminifu, Yesu alifanya agano pamoja naye. Agano ni ahadi takatifu kati ya Mungu na watoto Wake.

Ibrahimu akiandika ufunuo

Katika agano hili, Mungu alimwahidi Ibrahimu kwamba atakuwa na ukuhani na familia kubwa. Mungu pia alimuahidi Ibrahimu kuwa wanafamilia wake wa baadaye watapewa injili na ukuhani ikiwa watakuwa waaminifu. Familia ya Ibrahimu itapeleka injili kwa watu wote wa dunia.

Joseph Smith—Mathayo na Joseph Smith—Historia ya

Joseph akiandika

Joseph Smith—Mathayo ina marekebisho yenye mwongozo wa kiungu ambayo Nabii alifanya kwenye sehemu ya kitabu cha Mathayo katika Biblia. Joseph Smith—Historia ya ina maandishi ya Nabii kuhusu Ono la Kwanza, mabamba ya dhahabu, Kitabu cha Mormoni, na urejesho wa ukuhani.

Makala za Imani

Joseph na mwandishi

Sehemu ya mwisho ya Lulu ya Thamani Kuu ni Makala za Imani. Siku moja mtu ambaye rafiki yake alikuwa akiandika kitabu alikuja kumwona Joseph Smith. Mtu huyu alitaka kitu kuhusu Kanisa kwenye kitabu, hivyo alimwomba Joseph amwelezee jinsi Kanisa lilivyoanzishwa.

Joseph akiandika kuhusu Kanisa

Joseph Smith aliandika kuhusu mwanzo wa Kanisa. Kwa usaidizi kutoka kwa Mungu, aliandika pia kauli 13 muhimu kuhusu kile waumini wa Kanisa wanachoamini. Joseph aliziita kauli hizi Makala za Imani.

Watakatifu wakisoma Makala za Imani

Mnamo tarehe 1 Machi 1842, Makala za Imani zilichapishwa katika gazeti la Kanisa. Watakatifu walisoma Makala za Imani na kuamini kile Joseph alichokuwa ameandika.

Makala za Imani

Joseph Smith

kalamu na karatasi
Joseph Smith

1
Tunaamini
katika Mungu, Baba wa milele, na katika Mwanawe, Yesu Kristo, na katika Roho Mtakatifu.

2
Tunaamini
kwamba wanadamu wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na siyo kwa ajili ya uvunjaji sheria wa Adamu.

3
Tunaamini
kwamba kwa njia ya Upatanisho wa Kristo, wanadamu wote wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili.

4
Tunaamini
kwamba kanuni na ibada za kwanza za Injili ni: kwanza, Imani katika Bwana Yesu Kristo; pili, Toba; tatu, Ubatizo kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi; nne, Kuwekewa mikono kwa ajili ya kipawa cha Roho Mtakatifu.

5
Tunaamini
kwamba mwanadamu ni lazima aitwe na Mungu, kwa unabii, na kwa kuwekewa mikono na wale walio katika mamlaka, ili kuhubiri Injili na kuhudumu katika ibada zake.

6
Tunaamini
katika muundo ule ule ambao ulikuwepo katika Kanisa la Asili, yaani, mitume, manabii, wachungaji, walimu, wainjilisti, na kadhalika.

7
Tunaamini
katika vipawa vya ndimi, unabii, ufunuo, maono, uponyaji, tafsiri za ndimi, na kadhalika.

8
Tunaamini
Biblia kuwa ni neno la Mungu alimradi imetafsiriwa kwa usahihi; pia tunaamini Kitabu cha Mormoni kuwa ni neno la Mungu.

9
Tunaamini
yale yote ambayo Mungu ameyafunua, na ambayo sasa anayafunua, na tunaamini kwamba bado Yeye atayafunua mambo mengi makuu na muhimu yahusuyo Ufalme wa Mungu.

10
Tunaamini
katika kukusanyika kiuhalisi kwa Israeli na katika urejesho wa Makabila kumi; kwamba Sayuni (Yerusalemu Mpya) itajengwa juu ya bara la Amerika; kwamba Kristo atatawala yeye mwenyewe juu ya dunia; na, kwamba dunia itafanywa upya na kupokea utukufu wake wa kipepo.

11
Tunadai
haki ya kumwabudu Mungu Mwenyezi kulingana na mwongozo wa dhamiri zetu sisi wenyewe, na tunawaruhusu watu wote haki hiyo, na waabudu namna, mahali, au chochote watakacho.

12
Tunaamini
katika kuwa chini ya wafalme, marais, watawala, na waamuzi, katika kutii, kuheshimu, na kuzishika sheria.

13
Tunaamini
Tunaamini katika kuwa waaminifu, wakweli, wasafi, wakarimu, wema, na katika kufanya mema kwa watu wote; naam, twaweza kusema kwamba tunafuata maonyo ya Paulo—Tunaamini mambo yote, tunatumaini mambo yote, tumestahimili mambo mengi, na tunatumaini kuwa tutaweza kustahimili mambo yote. Kama kuna kitu chochote kilicho chema, chenye kupendeza, au chenye taarifa njema au chenye kustahili sifa, tunayatafuta mambo haya.