Hadithi za Maandiko
Sura ya 57: Nabii Anauawa: Juni 1844


Sura ya 57

Nabii Anauawa

Juni 1844

Hekalu la Nauvoo
jaji akizungumza na Joseph

Maadui wa Kanisa walimlaumu Joseph Smith kwa matatizo katika Nauvoo, na walitaka yeye na viongozi wengine wakamatwe. Lakini baada ya Joseph kukamatwa, jaji alisema hakuwa amefanya kosa lolote na alimwacha aende zake.

Gavana wa Illinois akizungumza na askari

Magenge ya watu wenye fujo yalikuwa na hasira kwamba Joseph Smith alikuwa ameachiliwa. Walitishia kushambulia Nauvoo. Walitishia hata kumpaka lami na kummwagia manyoya mmoja wa majaji. Joseph alimwomba gavana wa Illinois kuyazuia magenge hayo, lakini gavana aliamini uongo wa magenge na hakuyazuia.

Hyrum na Joseph

Joseph Smith alijua angeweza kuwekwa jela tena, na alikuwa na hofu nduguye Hyrum pia angewekwa jela. Joseph alimwambia Hyrum aichukue familia yake na kwenda mji mwingine, lakini Hyrum asingemwacha ndugu yake.

Joseph na Hyrum

Joseph Smith alihisi kwamba kama yeye na Hyrum wakiondoka Nauvoo, magenge ya watu wenye fujo yasingewaumiza Watakatifu. Waliamua kwenda upande mwingine wa mto na kujificha. Kisha wangeweza kwenda magharibi ili kupata sehemu nyingine kwa ajili ya waumini wa Kanisa kuishi.

Joseph akisoma barua

Baadhi ya watu walidhani Joseph Smith alikuwa akikimbia kwa sababu alikuwa anaogopa. Emma Smith, mkewe Joseph, aliwatuma baadhi ya marafiki kumtafuta na kumwomba arudi. Joseph alidhani angeuawa ikiwa angerudi Nauvoo, lakini alifanya kile marafiki zake walichomtaka afanye.

Joseph akichukuliwa na askari

Siku baada ya Joseph na Hyrum kurudi Nauvoo, wao na viongozi wengine wa mji walienda Carthage, mji uliokuwa umbali wa takribani maili 20. Huko Carthage walikamatwa kwa madai ya uongo, na Joseph, Hyrum, na baadhi ya marafiki zao waliwekwa jela hadi pale ambapo kesi itakapoweza kusikilizwa.

Joseph na marafiki ndani ya Jela ya Carthage.

Joseph, Hyrum, na marafiki zao walikuwa jela kwa siku tatu. Wakati huu, magenge ya watu wenye fujo yaliwatishia na kusema mambo mabaya juu yao. Wakiwa jela, Joseph na marafiki zake waliomba na kusoma Kitabu cha Mormoni. John Taylor aliimba moja ya nyimbo pendwa za Joseph juu ya Yesu.

genge la watu wenye fujo likivamia jela

Kufikia mchana wa tarehe 27 Juni 1844, ni Joseph, Hyrum, John Taylor, na Willard Richards pekee ndio waliokuwa bado katika jela ya Carthage. Kama yapata saa kumi na moja, genge la watu wenye fujo la zaidi ya watu 100 lilivamia jela. Baadhi ya washiriki wa genge hilo walipiga risasi kwenye madirisha, na wengine walikimbia mbele na kuwapita walinzi na kupanda juu kwa ngazi mpaka kwenye chumba ambapo Joseph na marafiki zake walikuwemo.

Hyrum akiwa amelala maiti sakafuni

Ndugu hawa walijaribu kufunga mlango, lakini kulikuwa na watu wengi mno kwa wao kuweza kujilinda. Genge lilisukuma mlango na kumpiga risasi Hyrum Smith. Wakati Joseph alipoona kwamba Hyrum amekufa, alipiga kelele, “Ee, mpendwa kaka Hyrum!” Genge pia lilimpiga risasi John Taylor, ambaye alijeruhiwa vibaya lakini hakuuawa. Hawakumpiga risasi Willard Richards.

Joseph akianguka nje ya dirisha

Baada ya Hyrum na John Taylor kupigwa risasi, Joseph Smith alikimbilia dirishani. Alipigwa na risasi mbili zilizorushwa kutoka kwenye mlango wa chumba na risasi ya tatu ilipigwa kutokea nje ya jela. Alilia, “Ee Bwana Mungu wangu!” na kuanguka nje ya dirisha. Nabii alikuwa amekufa. Alikuwa ametoa maisha yake kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo.

Watakatifu wakirudisha mwili wa Joseph

Miili ya Joseph na Hyrum Smith ilipelekwa Nauvoo, ambapo walizikwa. Familia zao na waumini wengine wa Kanisa walihuzunika sana.

kazi ya Joseph Smith

Nabii Joseph Smith alifanya kazi nyingi muhimu. Alitafsiri Kitabu cha Mormoni. Yesu alirejesha Kanisa Lake kupitia yeye. Joseph Smith alituma wamisionari kufundisha injili katika nchi zingine. Aliongoza Watakatifu katika kujenga mji mzuri. Mungu alimpenda Joseph Smith. Watakatifu pia walimpenda. Joseph Smith alifanya mengi kwa ajili ya wokovu wetu wa milele kuliko mtu yeyote isipokuwa Yesu Kristo.