Sura ya 45 Magenge Zaidi ya watu wenye fujo katika Missouri 1838–1839 Watakatifu wengi walikuwa wakiishi Far West, Missouri, ikiwa ni pamoja na Joseph Smith. Watu walijenga makazi na shule na walikuwa na furaha. Lakini Watakatifu hawakuwa na amani kwa muda mrefu. Tena, watu wengine katika Missouri walianza kuwaletea matatizo. Genge la watu wenye fujo lilikutana ili kupanga njia za kuwaumiza Watakatifu. Genge la watu wenye fujo lilifanya mambo mengi mabaya. Waliwafukuza Watakatifu nje ya makazi yao. Walichoma makazi yao na kuharibu mashamba yao. Waliwapiga wanaume na kuwaweka baadhi yao jela. Magenge ya watu wenye fujo yaliwaumiza baadhi ya wanawake. Watakatifu walimwomba msaada Gavana Boggs wa Missouri. Lakini watu wengine walikuwa wakimwambia gavana uongo kuhusu Watakatifu, na yeye hakuwasaidia. Matatizo kati ya Watakatifu na magenge ya watu wenye fujo yaliendelea kuwa makubwa. Akidhani kuwa Watakatifu walikuwa wa kulaumiwa kwa matatizo haya, Gavana Boggs aliwaambia baadhi ya askari kuwaua Watakatifu kama hawataondoka Missouri. Baadhi ya Watakatifu waliishi katika mji ulioitwa Haun’s Mill. Siku moja genge la watu wenye fujo lilikuja na kuwashambulia. Baadhi ya Watakatifu walikimbilia msituni. Wengine walikimbilia kwenye jengo la magogo kwa ajili ya ulinzi. Genge la watu wenye fujo lilipiga risasi kupitia kwenye nyufa za kuta. Kisha genge la watu wenye fujo liliingia kwenye jengo na kupiga risasi nyingi zaidi. Genge liliwaua watu 17 katika Haun’s Mill na kujeruhi wengine 13. Baadhi ya watoto walipigwa risasi na kuuawa. Kisha genge la watu wenye fujo liliiba kwenye makazi na kwenye magari ya kukokotwa na maksai ya Watakatifu. Baadaye baadhi ya askari walimteka Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa. Askari waliambiwa wampige risasi Joseph na rafiki zake. Lakini kiongozi mmoja wa askari hakutii. Alisema itakuwa ni kosa la jinai kumpiga risasi Joseph na wengine. Kesi ilipangwa dhidi ya Joseph na rafiki zake. Kabla na wakati wa kesi, waliwekwa gerezani katika mji wa Richmond, Missouri. Walinzi waliwafunga kwa minyororo. Joseph na rafiki zake walilala kwenye sakafu yenye baridi. Walinzi walikuwa wakatili sana kwa wafungwa. Waliapa na kusimulia hadithi mbaya. Walisimulia jinsi walivyowaibia na kuwaua Watakatifu. Walisimulia jinsi walivyowaumiza wanawake na watoto. Usiku mmoja walicheka na kujivuna kwa masaa kadhaa. Joseph alichukia kile walichokuwa wakikisema. Hakutaka kusikia lolote zaidi, hivyo alisimama na kuwaamuru kunyamaza. “Kimya,” alisema. “Katika jina la Yesu Kristo … nawaamuru kutulia; sitaishi dakika nyingine na kusikia lugha kama hiyo. Sitisheni maongezi kama hayo, au la ninyi au mimi tufe sasa hivi!” Walinzi waliingiwa na hofu na kumwomba Joseph samahani. Walikaa katika kona na walikuwa kimya usiku wote.