Sura ya 13 Joseph na Emma Julai 1830 Joseph na Emma Smith waliishi katika shamba dogo huko Pennsylvania. Walipendana na kufanya kazi kwa bidii ili kusaidiana. Joseph na Emma walivumilia magumu mengi. Walikuwa na mtoto wa kiume, lakini alifariki. Walihuzunika sana. Joseph alikuwa na wasiwasi juu ya familia yake. Walikuwa masikini, na alitaka kuwatunza. Alihitaji kupanda mazao ili familia yake iweze kupata chakula. Joseph pia alikuwa na wasiwasi kuhusu Kanisa. Baadhi ya Watu waliendelea kuleta matatizo kwa Watakatifu, na baadhi ya viongozi wa Kanisa iliwabidi wajifiche mbali nao. Wakati mwingine ilimbidi Joseph aondoke nyumbani ili kuwasaidia Watakatifu. Joseph alihuzunika kuondoka, na Emma alikuwa na wasiwasi wakati alipokwenda mbali. Joseph aliomba ili kujua kile alichopaswa kufanya. Yesu alimwambia asiwe na hofu juu ya watu waliokuwa wakijaribu kumdhuru. Yesu alisema Joseph alipaswa kuwa na subira katika mateso yake. Alisema daima angemsaidia Joseph. Mafundisho na Maagano 24:7, 16–17 Yesu alisema Joseph alipaswa kupanda mazao yake na kisha kwenda kuwasaidia Watakatifu katika maeneo mengine. Yesu pia alimwambia asiwe na wasiwasi juu ya chakula, nguo, au fedha. Watakatifu wangempa kile alichohitaji. Mafundisho na Maagano 24:3, 18 Yesu alimpa Joseph Smith ufunuo kwa ajili ya Emma. Yesu alisema Emma Smith alikuwa mwanamke wa kipekee. Alikuwa amemchagua ili afanye kazi muhimu. Mafundisho na Maagano 25:3 Yesu alisema Emma alipaswa kumfariji Joseph wakati alipokuwa na matatizo. Alipaswa kumsaidia kuwa na furaha na si kuwa na wasiwasi. Mafundisho na Maagano 25:5 Yesu alisema Emma alipaswa kuwafundisha Watakatifu na kuwasaidia kujifunza maandiko. Alisema Roho Mtakatifu angemsaidia kujua nini cha kufundisha. Mafundisho na Maagano 25:7–8 Yesu pia alisema Emma alipaswa kutumia muda wake ili kujifunza. Alipaswa kujifunza na kuandika mambo mengi. Mafundisho na Maagano 25:8 Yesu alimwomba Emma kuchagua nyimbo kwa ajili ya Watakatifu kuimba. Nyimbo zingechapishwa katika kitabu cha nyimbo. Mafundisho na Maagano 25:11 Baba wa Mbinguni anapenda kuwasikia watu wenye haki wakiimba. Nyimbo zao ni maombi Kwake, na maombi haya yatajibiwa kwa baraka. Mafundisho na Maagano 25:12 Yesu alimwambia Emma kuwa mnyenyekevu na kumpenda mumewe. Alimwambia awe na furaha kwa sababu ya baraka ambazo zingemjia Joseph. Mafundisho na Maagano 25:14 Yesu alimwaambia Emma kuwa na furaha na kushangilia. Alimwambia pia ashike maagano yake. Ikiwa angefanya hivyo, angepokea baraka kubwa na kuweza kurudi kuishi pamoja Naye mbinguni. Mafundisho na Maagano 25:13, 15 Yesu alisema kwamba mambo aliyomwelezea Emma Smith ni kwa ajili ya watu wote. Mafundisho na Maagano 25:16