Sura ya 34 Mungu Anawaonya Watu wa Sayuni Julai–Agosti 1833 Mungu aliwaamuru Watakatifu zaidi kwenda Jackson County, Missouri. Watu wapya walifika huko karibu kila wiki, na walijenga nyumba, maduka na kiwanda cha uchapishaji. Watakatifu katika Missouri walikuwa na amani na furaha kwa muda. Hata hivyo, ghafla matatizo yakaibuka. Baadhi ya Watakatifu walikuwa wakaidi na wakatili. Baadhi yao walibishana na viongozi wao. Watu wengine walioishi huko walianza kuwa na wasiwasi kuhusu Watakatifu wengi waliokuwa wakihamia katika eneo hilo. Watu hawa waliwataka Watakatifu kuondoka. Genge la watu wenye hasira lilikutana. Walituma baadhi ya watu kuwaambia viongozi wa Kanisa kuwa Watakatifu lazima waondoke Jackson County. Lakini viongozi walijua kwamba Mungu aliwataka kujenga mji wa Sayuni katika Jackson County. Waliwaambia watu kwamba Watakatifu wasingeweza kuondoka. Wanaume katika genge hilo walikuwa na hasira sana. Walivunja na kuingia ndani ya kiwanda cha uchapishaji cha Watakatifu na kukiharibu. Kisha, genge liliwakamata Askofu Partridge na Charles Allen na kuweka lami na manyoya kwenye ngozi zao. Genge pia liliwapiga baadhi ya Watakatifu wengine. Siku tatu baadaye, washiriki wa genge walipita mjini na kufyatua bunduki zao kwenye majengo. Waliwaambia Watakatifu mambo mabaya kwa sauti kubwa na kusema wangemchapa mtu yeyote watakayemshika. Walichoma mazao na kubomoa nyumba, maghala, na maduka. Oliver Cowdery alikuwa mmoja wa viongozi wa Kanisa katika Missouri. Alitumwa kwenda Kirtland kumwona Joseph Smith. Wakati Oliver alipowasili Kirtland, alimwambia Joseph kile kilichokuwa kikitendeka Jackson County. Watakatifu huko walitaka kujua cha kufanya. Joseph alimwambia Oliver kuhusu baadhi ya mafunuo aliyopokea. Bwana alikuwa amefunua kuwa Watakatifu wanapaswa kujenga hekalu katika Sayuni. Hekalu lingelipiwa kutoka kwenye zaka za watu. Yesu alimwambia Joseph kwamba Sayuni ingekuwa kubwa ikiwa Watakatifu wangekuwa watiifu. Lakini Watakatifu wangeadhibiwa ikiwa hawakuwa watiifu. Mafundisho na Maagano 97:10–12, 18, 22–26 Yesu alisema Watakatifu wanapaswa kutii sheria za nchi. Wanapaswa kuwapigia kura watu waadilifu kuwa viongozi wa nchi. Wakati watu waovu wanapokuwa viongozi, watu wanasikitika. Mafundisho na maagano 98:4–10 Bwana aliwaamuru Watakatifu kutii maneno Yake yote. Alisema hawapaswi kuwaogopa maadui zao. Badala yake, Watakatifu wanapaswa kuwasamehe maadui zao. Hawapaswi kupigana na adui zao isipokuwa Mungu amewaamuru kupigana. Bwana alisema ya kwamba Yeye angewaadhibu watu waovu. Mafundisho na Maagano 98:11, 14, 23–29, 33, 39–48 Wiki chache baadaye, Yesu alisema Watakatifu katika Sayuni wangekuwa na matatizo kwa muda kwa sababu hawakutii amri. Hata hivyo, Yesu aliahidi kwamba siku moja angewasaidia Watakatifu kujenga Sayuni. Mafundisho na Maagano 100:13–17