Sura ya 54 Mungu na Malaika Februari–Aprili 1843 Siku moja mtu mmoja aliyesema alikuwa amemwona malaika alikuja kumwona Joseph Smith. Mtu huyo alimwambia Joseph jinsi malaika alivyokuwa amevaa. Joseph alisema kuwa mtu huyo hakuwa amemwona malaika kwa sababu malaika hawavai jinsi ambavyo mtu huyo alivyokuwa ameeleza. Mtu huyo alikasirika sana. Aliamuru moto ushuke kutoka mbinguni umchome Nabii na nyumba yake. Lakini mtu huyo hakuwa na nguvu za Mungu, na hakuna moto ulioshuka kutoka mbinguni. Yesu alimpa Joseph Smith ufunuo kuhusu malaika. Yesu alisema kwamba malaika ni watu ambao wameishi duniani, wakafa, na kufufuka. Wana miili ya nyama na mifupa. Mafundisho na Maagano 129:1 Yesu alisema Shetani anajaribu kuwalaghai watu. Wakati mwingine anafanya watu wafikiri kuwa yeye ni malaika. Anajaribu kuwashawishi watu kufanya mambo mabaya. Lakini watu wenye haki wanaweza kujua wakati Shetani anapojaribu kuwalaghai. Mafundisho na Maagano 50:3, 129:8 Baadaye, Joseph Smith aliwaambia Watakatifu kweli zingine kuhusu mbinguni. Alisema kwamba malaika hawaishi katika sayari kama dunia. Badala yake, wanaishi na Mungu. Joseph pia alisema kuwa watu mbinguni watajua kila kitu walichojifunza duniani. Mafundisho na Maagano 130:6–7, 18 Joseph Smith alisema kwamba sheria zote za Mungu zilitengenezwa mbinguni kabla ya kuja kwetu duniani. Kuna baraka kwa kila sheria. Ni lazima tutii sheria ili kupokea baraka. Mafundisho na Maagano 130:20–21 Joseph Smith aliwaambia Watakatifu kuhusu Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni. Yesu anafanana kama mwanadamu na ana mwili wa nyama na mifupa. Mafundisho na Maagano 130:22 Baba wa Mbinguni pia ana mwili wa nyama na mifupa. Yeye anaishi katika sehemu nzuri, na inayong`aa. Mafundisho na Maagano 130:7, 22 Joseph Smith pia alisema Roho Mtakatifu ni roho. Roho Mtakatifu hana mwili wa nyama na mifupa. Mafundisho na Maagano 130:22